ad

ad

FUTA MACHOZI MPENZI-33

 
NYEMO CHILONGANI
Moyo wa msichana Cassey ulikuwa kwenye hali mbaya, alikosa amani na kila alipokaa kichwa chake kilimfikiria William. Aliumia kwani alijua kwamba yeye ndiye alikuwa chanzo cha mwanaume huyo kupata ajali hiyo kwani kama asingemwambia kuwa anataka kujiua, basi asingemfuata na hivyo kupata ajali mbaya iliyopoteza kumbukumbu zake.
Alijisikia hukumu moyoni mwake, wakati mwingine alikuwa akikaa peke yake nyumbani kwake na kulia kwa maumivu makali, alikosa raha, akakosa amani maishani mwake, kitu pekee alichokuwa akikifikiria kwa wakati huo ni William tu.
Alikuwa na siri kubwa moyoni mwake, hakutaka mtu yeyote afahamu kitu chochote, si hao tu bali hata William hakutaka afahamu ukweli. Alimwambia kwamba alikuwa na mimba ya mwezi mmoja lakini ukweli ni kwamba hakuwa na mimba, alitaka kumfanya mwanaume huyo awe karibu naye, kwani aliamini kila mwanaume alihitaji mtoto, alidhani kwamba angefurahi lakini mwisho wa siku mwanaume huyo akabadilika na kuhitaji aitoe mimba ile.
Aliumia zaidi moyoni mwake, alijuta kumdanganya William kwani pamoja na ubaya wa sura yake, lakini moyoni mwake alikuwa mwanaume pekee aliyekuwa akimpenda kwa moyo wa dhati.
Hakutaka kubaki nchini Marekani, ilikuwa ni lazima amuone William na ikiwezekana amuombe msamaha kwa kumdanganya kwani ukweli ni kwamba hakuwa na mimba kama alivyomwambia.
Siku mbili zilizofuata, akafanya hatua zote za usafiri na alipopata vibali akaanza safari ya kuelekea nchini Tanzania kwa kutumia ndege yake binafsi. Njiani, mawazo yake yalikuwa kwa William, hakujua angemwambia nini, hakujua kama mwanaume huyo hakuwa na kumbukumbu zake, hakukumbuka kitu chochote kile kilichotokea siku chache zilizopita maishani mwake.
Alipofika Tanzania, akaelekea katika Hoteli ya Serena. Alijua kwamba William alikuwa akijulikana sana, hivyo alichokifanya ni kumuuliza mhudumu ambaye alimwambia kwamba alimfahamu sana William na hakukuwa na Mtanzania ambaye hakumfahamu mtu huyo.
“Everybody knows him. He is a superstar,” (kila mtu anamfahamu! Jamaa ni staa sana,) alisema mhudumu.
“So, you know where he lives?” (kwa hiyo unajua anapoishi?)
“Yeah!”(ndiyo)
Akahitaji kupelekwa huko, alichokifanya ni mhudumu ni kumwambia Cassey kwamba lingekuwa jambo jema kama angezungumza na uongozi wa hoteli hiyo kwa ajili ya ruhusa na hivyo msichana huyo kufanya hivyo.
Mhudumu akaruhusiwa na hatimaye kuanza kwenda Tabata alipokuwa akiishi William. Hawakuchukua muda mrefu sana wakafika, nje kulikuwa na waandishi wa habari ambao walitaka kuingia humo kuzungumza na William lakini mlinzi aliwaambia wasubiri, hivyo wakafanya hivyo.
“Nimemleta mgeni wa William,” alisema kijana yule aliyekuwa mhudumu.
“Siyo mwandishi huyo?”
“Sasa mwandishi kutoka gazeti gani kaka? Au udaku la Marekani!” alihoji mhudumu huyo kiutani.
Wakaruhusiwa na kuingia ndani. Mapigo ya moyo wa Cassey yalikuwa yakidunda mno, walipofika sebuleni, wakakutana na mama yake William aliyekuwa akimbembeleza Linda aliyekuwa akilia huku akiwa na mtoto wake.
Hakujua ni kitu gani kilitokea na kitu cha kwanza kabisa kilichomjia kichwani mwake ni kwamba inawezekana William alikuwa amefariki dunia. Nguvu zikamuisha, akajikuta akisimama palepale mlangoni aliposimama.
Akakaribishwa, akakaa kochini na kuanza kujitambulisha. Linda alimfahamu, alikwishawahi kutambulishwa mara kadhaa na William hivyo hakushtuka kumuona msichana huyo amefika mahali hapo.
“What the hell is going on?” (kitu gani kinaendelea?)
Linda akaanza kumwambia kila kitu kilichotokea kwamba ajali mbaya aliyoipata William ilimsababishia kupoteza kumbukumbu zake. Cassey hakutaka kuliamini hilo, alichomwambia ni kwamba alitaka kuonana na William ili kuzungumza naye.
Hilo halikuwa tatizo, mama yake William, Bi Sophia akamchukua na kumpeka chumbani alipokuwa William ambaye alikuwa amelala. Akaamshwa na macho yake yalipotua kwa Cassey alibaki akimshangaa, hakumfahamu msichana huyo na hakujua kama katika maisha yake aliwahi kuonana naye.
“Wewe ni nani?” aliuliza William huku akionekana kushangaa.
“Umenisahau?”
“Sijakusahau, bali sikujui kabisa,” alijibu William.
“Naitwa Cassey!”
“Ndiye nani na unahitaji nini?” aliuliza William huku akimwangalia msichana huyo.
Cassey akabaki kimya kwa muda, hakuamini kwamba William alimsahau hata yeye mwenyewe. Kwa jinsi walivyokuwa na majibu ya William yalivyotoka ilionekana kama walikuwa wakiigiza lakini mwenzake alikuwa akimaanisha, hakumkumbuka na hakujua alifika mahali hapo kufanya nini.
“Mimi ni mpenzi wako! Kumbuka nilikwambia nina mimba yako,” alisema Cassey na kumfanya William kushtuka.
“Una mimba yangu?”
“Ndivyo nilivyokwambia!”
“Mbona sikufahamu! Tulishawahi kukutana kabla?”
“Ndiyo!”
“Wapi?”
“New York!”
William hakujibu kitu, alibaki akimwangalia Cassey, hakumkumbuka kabisa, alimshangaa kwa sababu mpaka kipindi hicho hakuwahi kuwa na rafiki Mzungu, sasa ilikuwaje mtu kama Cassey amfuate na kumwambia maneno hayo na wakati hakuwahi kuwa karibu na Mzungu?
Akamfukuza kwani alimuona muongo na kulikuwa na kitu alichokihitaji. Cassey hakuamini, alikuwa akifukuzwa na mwanaume ambae kila siku alimwambia kuwa alikuwa mwanamke wake wa ndoto. Moyo wake uliumia lakini hakuwa na jinsi, akaondoka zake kurudi nchini Marekani.
Hali ya William haikubadilika, bado aliendelea kuwa na mawazo kila siku, mambo yaliyokuwa yakitokea hakuamini, kila alipokaa, alifuatwa na waandishi wa habari na kuambiwa maneno mengi kuhusu umaarufu wake.
Hakujua sababu ya waandishi kumuuliza hivyo kwani kitu alichokikumbuka, hakuwa maarufu bali mtu wa kawaida sana. Kwenye mitandao ya kijamii, alikuwa akizungumziwa yeye tu.
Ukiachana na tovuti ya Global Publishers, Jamii Forum na nyingine nyingi, pia alikuwa akizungumziwa mpaka katika tovuti za nchini Marekani, Uingereza na nchi nyingine.
Alishangaa, watu hao walimjuaje, na kama alikuwa maarufu, umaarufu wa nini kwani aliyakumbuka maisha yake yote, hakuwahi kuona kama kuna siku aliwahi kuwa mtu maarufu.
“Mimi ni maarufu? Eti nina mtandao! Sasa mtandao gani tena?” alijiuliza William pasipo kupata jibu.
Linda hakutaka kuendelea kubaki nchini Tanzania, kama kuumia, aliumia sana, kama kulia alilia sana lakini hakukuwa na kitu kilichobadilika. Alichokifanya baada ya siku mbili ni kurudi nchini Marekani huku akiwa na majonzi tele. Alisimiamia biashara za mpenzi wake, akaunti zake zote kwa kuamini kwamba kuna siku angerudiwa na kumbukumbu na kukumbuka kila kitu kilichotokea.
William aliendelea na maisha yake nchini Tanzania, hakujua sababu ya waandishi kumtafuta sana, kila alipokaa, alifuatwa na watu na kuhitaji kupiga naye picha. Alishangaa, aliambiwa kwamba alikuwa mtu maarufu kitu ambacho kila siku alipingana nacho.
Baada ya kukaa Tanzania kwa wiki mbili, akaalikwa ikulu kwa ajili ya kuonana na rais, alishangaa, hakuwahi kufikiria kitu kama hicho. Alijiona kuwa mtu wa kawaida, sasa ilikuwaje mpaka aitwe na rais na wakati hakuwa amefanya jambo lolote lile.
Mualiko huo ulitakiwa kufanywa baada ya siku mbili, alikuwa kwenye presha kubwa, kila alipokuwa akilifikiria jambo hilo, mapigo yake ya moyo yalimdunda kupita kawaida.
Siku hizo zilipotimia, akaelekea huko huku akiwa na mama yake. Akakutana na waandishi wa habari wengi, wote walikuwa wamealikwa, alipoteremka kwenye gari, akaanza kupigwa picha mfululizo.
Kila kitu kilichokuwa kikiendelea kilimshangaza sana, hakujua sababu, aliambiwa kwamba alikuwa mtu maarufu lakini hakujua umaarufu wake ulikuwa ni wa nini.
“Au ndiyo natengenezwa kuwa mrithi wa Kanumba? Au labda natengenezwa kuchukua mikoba ya Diamond Platnumz. Lakini mbona sijui kuimba wala kuigiza! Kwa nini wanataka niwe mtu maarufu?” alijiuliza lakini akakosa jibu.
Akakaribishwa ikulu kwa heshima kubwa, hakuamini kama ingetokea siku ambayo angeingia ndani ya ikulu hiyo. Alikaa kwenye kochi kubwa huku akionekana kutokujiamini kabisa. Alitetemeka, hiyo ndiyo ilikuwa siku yake ya kwanza kufika humo.
“Mama! Sijiamini kabisa,” alisema William huku wakiwa sebuleni wakimsubiri rais.
“Jiamini mwanangu! Nilishakwambia kwamba wewe ni mtu maarufu!” alisema mama yake.
“Umaarufu gani?”
“Umetengeneza mtandao!”
“Mtandao? Mama! Sijawahi na wala kufikiria kutengeneza mtandao hata siku moja. Sasa iweje niwe nimetengeneza mtandao? Mimi ni mtaalamu wa kompyuta ila si mtaalamu wa kutengeneza mtandao,” alijibu William, walikuwa kama wakinong’ona.
Baada ya dakika kadhaa, rais akafika sebuleni hapo, kitu cha kwanza akamuonyeshea tabasamu pana William na kisha kumsogelea na kumkumbatia.
Kwa muonekano aliouonyesha rais huyo ulionyesha kabisa kwamba alikuwa akimfahamu kabla kitu kilichomfanya William kumshangaa kwani hakujua kama rais huyo alikuwa akimfahamu hata kidogo.
“Kumbe unanifahamu?” aliuliza William.
“Yeah! Nakujua sana. Kwa nini umeniuliza hivyo?” aliuliza rais, alionekana kutokujua tatizo alilokuwa nalo William.
“Siamini kama unanijua kwani sijawahi kulifanyia taifa kitu chochote kile.”
“Hahah! William! Umeibadilisha dunia, kila mtu anakishangaa kichwa chako, hivi kina uwezo gani?” aliuliza rais.
“Kawaida. Ila...daah! Mbona mnanichanganya sana,” alisema William.
Rais mwenyewe alikuwa akishangaa mpaka pale alipoambiwa kwamba William alipata ajali na alipoteza kumbukumbu zake hivyo hakuwa akikumbuka kitu chochote kile.
Alipoambiwa hivyo, kidogo hata mazungumzo yake yakabadilika na kuanza kuzungumzia habari nyingine kabisa. Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake, mpaka mwaka mmoja unapita, hakuwa amekumbuka kitu chochote kile, hakujua mpenzi wake, Linda alikuwa katika hali gani, hakujua kuhusu mtandao wake, kila kitu kilichokuwa kikiendelea, kwake yalikuwa maisha mapya.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumamosi hapahapa.

No comments

Powered by Blogger.