ad

ad

FUTA MACHOZI MPENZI-31

 

Watu waliendelea kumiminika hospitalini hapo huku kila mmoja akitaka kujua undani juu ya ajali iliyokuwa imetokea. Wapo waliohisi kwamba kulikuwa na mchezo ulifanyika, kuna baadhi ya mabilionea walitaka kumpoteza William kwa kuwa tu alikuwa mtu aliyekuja juu kifedha na kulikuwa na kila dalili za kuwapiku katika utajiri wao.
Hospitalini hapo, hakukuwa na aliyecheka, kila mmoja alionekana kuwa na uso uliokuwa na huzuni tele. Wengi walipata taarifa kwamba William alikufa hivyo walitaka kupata ufafanuzi juu ya mahali ambapo mazishi hayo yangefanyika na hata kanisa ambalo wangelitumia kumuaga sura ya mwisho.
Dunia ilikuwa kimya, kila mmoja aliyeisikia taarifa hiyo hakuamini kama kweli William alikuwa hai, na kama alikuwa hai hakukuwa na mtu aliyehisi kama mwanaume huyo angeinuka tena kitandani alipolala.
Madaktari walihangaika mno, walijaribu kuyaokoa maisha yake kwani kadiri dakika zilipokuwa zikienda mbele, mapigo yake ya moyo yalikuwa yakishuka sana hivyo kumuwekea dripu iliyokuwa na dawa ya kushtua zaidi mapigo yake ya moyo.
Walipambana, aliumia zaidi kichwani, alikuwa ametoka damu lakini kwa wakati huo hawakutaka kushughulika na kichwa, kitu muhimu kilikuwa ni kuhakikisha mapigo yake ya moyo yanarudi na kuwa katika hali ya kawaida kabisa.
Baada ya kumuwekea dripu zaidi ya nne zilizokuwa na dawa Melphonilyze ambayo ilitumika kushtulia mapigo ya moyo ndiyo kidogo ikamsaidia na hatimaye kuanza kurudi katika hali yake ya kawaida, kilichotakiwa kufanyika ni upasuaji wa kichwa chake tu kuangalia tatizo lilikuwa nini.
“We must perfom craniotomy surgery,” (ni lazima tumfanyie upasuaji wa kichwa) alisema daktari mmoja aliyekuwa na kibati kilichoandikwa Dr. Pham.
Hakukuwa na kuchelewa, ili kufanikisha kile walichotaka kukiangalia ilikuwa ni lazima wamfanyie upasuaji wa kichwa kwani walihisi kwamba damu ziliweza kuvilia kwenye ubongo kitu ambacho kingemletea tatizo kubwa zaidi.
“Play the music,” (washa muziki) alisema Dk. Pham.
“Which one?” (upi?)
“Abba’s 1977 While the Music still Goes On,” (While the Music Still Goes On wa Abba wa mwaka 1977) alisema Dk. Pham na daktari mmoja kuwasha muziki.
Ilikuwa ni kawaida yao katika kila wakati walipokuwa wakikutana na upasuaji mkubwa ilikuwa ni lazima kuwasha muziki na kusikiliza huku wakiendelea kufanya upasuaji huo.
Muziki huo ukawashwa na kuanza kufanya upasuaji huo. Walikuwa wakizungumza, wakicheka kwani waliamini kwamba upasuaji haukutakiwa kuwa siriazi sana kwa kuogopa kuingiwa na hofu, hivyo hali hiyo ingewafanya kuona kile kilichokuwa kikitokea kuwa cha kawaida sana.
Upasuaji ukaanza, baada ya kukichana kichwa cha William, wakaanza kutoa kipande cha fuvu ambacho kitaalamu huitwa Bone Flap na kisha kukiweka pembeni kwa ajili ya kuangalia ndani ya ubongo kuona kulikuwa na nini.
Wakati wakiendelea kufanya upasuaji huo bado walikuwa wakizungumza huku wakikiangalia kichwa hicho kwa makini kabisa ambapo huko wakaliona donge la damu likiwa limeganda katika ubongo wake, tena kwa kujificha ndani ya ubongo kwa mbali.
“Ooh my God!” (Ohh Mungu wangu) alisema Dk. Pham huku akionekana kushangaa.
“What is it?” (kuna nini?) aliuliza nesi mmoja.
“This is brain hemorrhage,” (damu imevuja kwenye ubongo) alijibu Dk. Pham.
Kila mmoja alishtuka, hawakuamini kusikia kwamba damu ilikuwa imevilia katika ubongo wa William. Hilo lilikuwa tatizo kubwa ambalo kwa watu wengi waliokuwa wakipata tatizo hilo, asilimia themanini walikuwa wakifa kwani damu huwa na kawaida ya kusambaa kwa haraka sana katika ubongo kuliko sehemu nyingine yoyote ile.
Waliogopa, waliuona mwisho wa William ukiwa mikononi mwao kwani hata kama angepona ilikuwa ni lazima kupata matatizo mawili, iwe ugonjwa wa kusahau kila kitu kilichotokea katika maisha yake yote au nusu ya maisha lakini pia ilikuwa ni kupata ugonjwa wa kupooza ambao ungeyatesa maisha yake kitandani.
Japokuwa walikuwa wakiimba lakini baada ya kugundua hilo, kila mmoja akabaki kimya, wakaanza kuangalia, damu ilikuwa kwenye ubongo na kwa bahati nzuri sana kwa William ni kwamba ilikuwa kama donge moja la damu na si kwamba ilisambaa.
“We have to remove it without soring a brain,” (ni lazima tuiotoe damu pasipo kuutonesha ubongo) alisema Dk. Pham huku akiliangalia donge lile la damu.
“We have ten hours to perfom this craniotomy,” (tuna saa kumi za kufanya upasuaji huu wa kichwa) alisema Dk. Pham, na mpaka kipindi hicho, tayari yalikuwa yamepita msaa mawili.
Upasuaji ulikuwa ukiendelea, Dk. Pham na wenzake hawakutoka ndani ya chumba kile, walijua kwamba nje kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakisubiri kuona ni kitu gani ambacho kingetokea ndani ya chumba kile.
Donge la damu halikutoka kirahisi, kila walipoligusa kwa maana ya kulitoa, lilihama na kuhamia sehemu nyingine kitu kilichowapa usumbufu mkubwa kwani mpaka wanakamilisha kulitoa, tayari walitumia saa sita na hivyo kuanza kurudishia fuvu taratibu.
Mpaka wanamaliza, walichukua saa kumi na mbili, walichoka, hawakuwa na matumaini kama William angepona kwani kila walipokuwa wakiangalia mashine ya Mult Parameter Monitor mapigo yake ya moyo yalionyesha kushuka kwa ghafla na kupanda.
“We have to pray for him,” (inabidi tumuombee) alisema Dk. Pham.
Hawakuwa na jinsi, kadiri walivyomwangalia William kitandani pale walikiri kwamba mwanaume huyo alikuwa akienda kufa. Hali yake ilitisha na kila walipomwangalia, mioyo yao iliwaambia kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa William kuvuta pumzi ya dunia hii.
Baada ya kumaliza kusali, wakatoka na moja kwa moja Dk. Pham kuwaita wazazi na Linda ofisini kwake kwa ajili ya kuzungumza nao. Hakuwaficha, aliwaambia ukweli juu ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea kwamba kijana wao alikuwa kwenye hali mbaya na kama wasingemuomba Mungu basi angeweza kufariki dunia kitandani hapo.
“Hatuna ujanja zaidi ya kusali sana, tukishindwa, basi atakufa kwani nisingependa kuwaficha, watu wanaopata tatizo hili, wengi hufa japokuwa kwa William tunajaribu kupambana,” alisema Dk. Pham japokuwa alikuwa akizuiliwa kuwaambia ndugu wa wagonjwa maneno kama hayo lakini hakuwa na jinsi.
Linda alikuwa akilia, moyo wake ulikuwa ukimuuma mno na alikuwa amebakiza wiki moja kabla ya kujifungua lakini mumewe alikuwa hoi kitandani. Hakutaka kumwangalia hapo alipolala kwani alihisi angeumia zaidi, angelia na hatimaye mimba yake kuharibika.
****
“Mandy! I want to see you,” (nataka nikuone Mandy) alisema Cassey kwenye simu, alikuwa akizungumza na rafiki yake kipenzi.
“Is there something wrong?” (kuna tatizo huko?)
Cassey alitaka kuzungumza na rafiki yake kipenzi na ndiyo maana alimpigia simu kwa lengo la kukutana naye na kuzungumza naye mambo mawili matatu.
Moyo wake ulikuwa ukimuuma, kila alipokuwa akiiona habari ya William kwenye mitandao ya kijamii na televisheni, alijiona kuwa mkosaji kwa kuwa alijua fika kuwa mwanaume huyo alipata ajali baada ya kumwambia kwamba alitaka kujiua.
Mandy hakuchelewa, ndani ya nusu saa alikuwa ndani ya nyumba ya rafiki yake, Cassey na kuanza kuzungumza naye. Hakutaka kumficha, alimwambia jinsi alivyokuwa akijuta kwa kile kilichotokea na wakati mwingine alijiona kuwa mkosaji mkubwa. Alimwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea, tangu siku aliyomwambia William kwamba alikuwa na mimba yake mpaka siku hiyo.
“Kwa hiyo alipopata ajali alikuwa akikukimbilia wewe?” aliuliza Mandy!”
“Ndiyo!”
“Na ulitaka kweli kujiua?”
“Hapana! Nisingeweza, nilitaka kuona kama anajali. Nimefanya upumbavu mkubwa sana Mandy! Ninajuta, ninajuta kuufanya utoto kama huo,” alisema Cassey huku akilia kama mtoto.
“Pole sana rafiki yangu!”
Cassey hakutaka kubaki nyumbani, ilikuwa ni lazima kwenda hospitali kumuona William. Alipokwenda huko na kuteremka, waandishi wa habari wakamsogelea na kisha kuanza kumpiga picha.
Alikuwa msichana maarufu na ujio wake mahali pale uliwafanya waandishi wa habari kutokutulia na hivyo kutaka kumuhoji maswali machache. Hakujibu kitu, kwa jinsi alivyoonekana tu alionyesha ni jinsi gani alikuwa na mawazo tele na moyo uliojaza maumivu makubwa.
Alikwenda mpaka ndani ya hospitali hiyo. Alipomuona Linda, moyo wake ulizidi kuchoma kwani alijiona mkosaji kwa kuona kabisa kwamba kile kilichokuwa kimetokea, yeye ndiye alisababisha hali hiyo. Akawafuata pale alipokuwa na kuwapa pole.
Cassey alikuwa msichana wa kwanza maarufu kufika hospitalini hapo lakini baada ya siku mbili, zaidi ya masupastaa ishirini walifika mahali hapo kwa ajili ya kumpa pole Linda na wazazi kwa kile kilichokuwa kimetokea.
William aliendelea kuwa kimya kitandani, siku ya kwanza ikapita, hakuzinduka, ya pili ikaingia na hatimaye wiki nzima kukatika lakini bado alikuwa kimya tu.
Mpenzi wake Linda akajifungua huku akiendelea kuwa kitandani hapo. Hakujua kama alikuwa baba, aliendelea kuteseka huku akiendelea kupumulia mashine ya oksijeni kwani vinginevyo angeweza kufa palepale.
Baada ya miezi miwili kupita ndipo William akaamka kitandani, akayafumbua macho yake, alipona, kichwani kulikuwa sawa na mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kawaida, na hata lile bega lililokuwa limeumia, kidogo alijisikia nafuu.
“William ameamka,” alisema nesi mmoja baada ya kumuona akifumbua macho, aliamua kumwambia Dk. Pham ambaye alikwenda katika chumba kile, kweli William alikuwa amefumbua macho lakini hakuzungumza kitu chochote kile.
Wazazi walipopewa taarifa, hawakuamini, hata Linda aliposikia, alitaka kujionea hivyo Dk. Pham kuwaruhusu kumuona mgonjwa huyo aliyekaa kitandani kwa miezi miwili pasipo kuzungumza kitu chochote.
Walipoingia ndani na kumuona, wakaachia tabasamu pana lakini kwa William alionekana kuwa tofauti kabisa. Alibaki akiwaangalia huku akiwakodolea macho.
“My husband....”(mume wangu!) aliita Linda, akamsogelea pale kitandani na kumkumbatia.
“Who are you? Do we know each other?” (wewe ni nani? Tunafahamiana?) aliuliza William huku akimwangalia Linda machoni kwani alionekana kuwa mgeni, mtu ambaye hakuwahi kumuona katika maisha yake. Kwa kifupi, kitendo cha damu kuingia kwenye ubongo wake, ukafuta kumbukumbu zake za miezi kadhaa nyuma kabla ya kuelekea nchini Marekani.
“Mwanangu....” aliita mama yake.
“Mama! Huyu ni nani? Nipo wapi? Mbona nipo na Wazungu? Kuna nini mama?” aliuliza William.
“Mwanangu....”
“Mama! Ninahitaji kumuona Melania! Nilipanga kuonana naye. Mungu wangu! Nilimkataa Melania, ameumia sana, kwa nini nimemuumiza msichana wa watu! Mama, Melania yupo wapi? Mama nataka nimuone Melania nimuombe msamaha,” alisema William huku akianza kulia. Hakukumbuka kitu chochote kile, hakukumbuka kama alikwenda nchini Marekani kusoma chuo, kitu alichokikumbuka ni mama yake na msichana Melania tu.

Je, nini kitaendelea?

No comments

Powered by Blogger.