ad

ad

FUTA MACHOZI MPENZI-30

NYEMO CHILONGAN
Vijana wa Nicholaus hawakuacha kufika hospitalini hapo, walikuwa wakienda na kujifanya kwamba walikuwa na wagonjwa kumbe nyuma ya pazia walikuwa wakifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Kila kona, watu walizungumzia tukio lililotokea kwamba kulikuwa na daktari aliyetaka kumuua mgonjwa kitandani kitu kilichowafanya wagonjwa wengi kuhisi kwamba hawakuwa sehemu salama, hasa katika hospitali hiyo ambayo ilikuwa ikijulikana kila kona kutokana na huduma zake nzuri.
Madaktari walichukia, walimwambia polisi aliyekuwa akilinda alinde kiuhakika na mwisho wa siku mgonjwa huyo apone na kurudishwa nyumbani huku akiwa salama kabisa.
Ulinzi uliendelea kama kawaida. Kitu walichokifanya Kibra na vijana wenzake ni kutafuta mavazi ya kipolisi, yaliyofanana na polisi yule aliyekuwa akilinda katika chumba kile ili mmoja aende na kulinda yeye ili iwe rahisi kuingia ndani ya chumba kile.
Baada ya siku mbili, tayari walipata mavazi ya polisi. Alitakiwa kuvaa kijana mmoja, walichokifanya kilikuwa ni kupanga dili kwamba ni lazima wamchukue msichana mmoja na kwenda kule hospitalini ambapo baada ya kufika ajifanye ameanguka na kuchukuwa na polisi yule.
Hilo halikuwa tatizo hata kidogo, siku hiyohiyo wakampata msichana huyo na kumpanga na hivyo kuelekea hospitalini huku yule aliyetakiwa kuvaa kama polisi akiwa ameziweka nguo hizo katika mfuko wa plastiki na kuelekea chooni huku akifuatilia kwa kutumia masikio yake.
Wakati msichana yule akipiga hatua kuelekea katika wodi moja, alipofika karibu na polisi yule akajifanya kuanguka kwa kuzidiwa na ugonjwa kitu kilichowafanya watu wote kushtuka. Haraka sana Melania, mama yake na polisi yule wakamsogelea pale alipoangukia na kisha kumuinua, hakuyafumbua macho yake, akajifanya kuzidiwa hivyo kuanza kumpeleka katika chumba kingine huku wakiongozwa na nesi mmoja.
Kwa haraka sana jamaa aliyekuwa chooni ambaye tayari alikuwa na mavazi ya kipolisi akatoka chooni kule na harakaharaka kuanza kutembea kuelekea katika chumba kile.
Watu walimuona lakini walipuuzia kwani kila mmoja aliamini kwamba huyo alikuwa polisi yule aliyekuwa ametoka. Hakutaka kuchelewa, kwa haraka sana akaingia ndani ya chumba kile, akayapeleka macho yake, yakatua kitandani, akamuona Godson akiwa amelala huku amejifunika shuka mwili mzima, hakutaka kuchelewa, akachukua sindano yake na kuanza kumsogelea pale kitandani alipokuwa tayari kwa kumuua.
“Ni muda wake wa kufa,” alisema mwanaume huyo, harakaharaka akaitoa sindano tayari kwa kumchoma Godson kitandani pale.
****
Ilikuwa ni ajali mbaya, kila aliyeiona alishika kichwa kwa mshtuko mkubwa, hawakuwahi kuliona gari likibingilika kwenye bonde kiasi kile zaidi ya kuangalia kwenye filamu tu.
Waliokuwa wakipita na magari yao, wakayasimamisha na kisha kuteremka, waliliangalia gari lile lililokuwa bongeni kulipokuwa na miti mingi. Hawakujua kama dereva wa gari hilo alikuwa mzima au la.
“Mungu wangu!” alisema mwanamke mmoja.
Wanaume wawili wakaanza kuteremka kule bondeni huku wakimwambia mwanamke yule apige simu katika hospitali iliyokuwa karibu na mahali hapo na kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea.
Wanaume wale walipofika chini, wakavunja mlango na kumtoa William. Hakukuwa na aliyejua kama mtu huyo alikuwa William kwa jinsi alivyokuwa. Kichwa kilikuwa kinatoa damu, alikuwa ametulia tuli na kitu kilichowafanya kugundua kwamba alikuwa hai ni mapigo yake ya moyo yaliyokuwa yakidunda kwa mbali sana.
Wakambeba na kumpeleka juu barabarani. Hakuwa akijitambua, walipomfikisha huko, wakamuingiza katika gari la wagonjwa ambalo lilifika mahali hapo kwa haraka sana na kuanza safari ya kuelekea hospitali.
“Atapona kweli?” alisikika mwanaume mmoja akiuliza, zaidi ya magari kumi yalikuwa mahali hapo.
“Inawezekana! Ila ameumia sana, yaani mpaka tumeshindwa kumtambua,” alisema mwanaume mmoja ambaye naye alimuona William alivyokuwa akipelekwa kule barabarani lakini hakujua kama alikuwa William kwa jinsi uso wake ulivyochakazwa kwa damu.
Akapelekwa mpaka katika Hospitali ya Apostal Medical Centre iliyokuwa hapohapo Manhtattan. Walipofika, akateremshwa, akawekwa kwenye machela na kuanza kusukumwa kuelekea katika chumba cha upasuaji.
Kila mtu aliyemuona, alimuonea huruma kwani kwa hali aliyokuwa nayo, kila mmoja alijua kwamba mtu huyo alikuwa akienda kufa. Walipofika katika chumba hicho, harakaharaka manesi wengine wakaingia na kuanza kumsafisha, walipomaliza, ndipo wakagundua kwamba mtu huyo alikuwa William.
“Ni William,” alisema nesi mmoja huku akionekana kushtuka.
“Unasemaje?”
“Ni William,” nesi huyo alisikia hivyo, harakaharaka akayapeleka macho yake kwa mgonjwa huyo na kumwangalia, kweli alikuwa William.
Huruma walizokuwa nazo zikaongezeka mioyoni mwao, hawakutegemea kumuona mtu huyo akiletwa hospitalini hapo baada ya kuumia vibaya katika ajali iliyotokea.
Manesi hayo ndiyo waliosambaza taarifa hiyo kwa watu wengine na ndani ya dakika ishirini tu tayari waandishi wa habari walifika hapo na kutaka kujua ukweli kwani wao waliona kwenye mitandao ya kijamii kwamba mwanaume huyo alikuwa amepata ajali mbaya ya gari.
“Sisi si wasemaji wa hospitali,” alisema nesi mmoja.
“Basi sawa. Tunahitaji kuonana na wasemaji,” alisema mwandishi mmoja.
Wakachukuliwa na kupelekwa katika ofisi ya daktari huyo ambaye aliwapa taarifa kamili kwamba ni kweli William alikuwa amepata ajali mbaya ya gari na hali yake haikuwa nzuri kabisa. Aliwaambia kila kitu huku wakionekana kuwa na hofu kwamba inawezekana mwanaume huyo alikuwa amekufa kwenye ajali hiyo ila walifichwa.
“Ila taarifa zinasema kwamba amekufa!” alisema mwandishi mmoja.
“Hiyo ni taarifa ya mitandaoni. Mmekuja kwangu kwa kuwa mnataka kupata taarifa ya hospitali, kwa hiyo nawaambieni hajafa na hatokufa kwa kuwa yupo kwenye mikono salama,” alisema daktari huyo huku akionekana kumaanisha alichokuwa akikizungumza.
Taarifa hizo ziliendelea kusambazwa na baada ya dakika kadhaa, Linda akapigiwa simu na wazazi wake ambao walitaka kuonana naye.
“Upo wapi?” aliuliza mama yake.
“Nyumbani!”
“Tunakuja!”
Hawakutaka kumwambia kwenye simu, walijua hali aliyokuwa nayo, kama wangempa taarifa juu ya kilichokuwa kimetokea basi wangeweza kusababisha matatizo mengine.
Baada ya dakika kadhaa wakafika nyumbani hapo. Kwa jinsi alivyoonekana, Linda hakujua kilichokuwa kimetokea, aliwakaribisha huku akiwa na furaha tele na hivyo kuanza kuzungumza naye huku wakimkazia macho.
“William alikupigia simu lakini hakuwa amekupata,” alisema mama yake.
“Mbona simu ipo hewani!”
“Hatujajua kwa sababu gani. Alitupigia na kutuambia kwamba alijisikia kuumwa kichwa hivyo alipitia hospitali,” alisema mama yake, kidogo Linda akashtuka.
“Mbona hakuja nyumbani au kumpigia simu dokta wa familia?” aliuliza Linda.
“Hatujajua! Ila hali yake si nzuri, alisema kichwa kinamsumbua sana,” alisema baba yake.
Linda alihuzunika, aliwaamini wazazi wake, hakugundua kama alikuwa akidanganywa, walichokifanya ni kuondoka nyumbani hapo na kwenda hospitalini. Hakuwa na mawazo sana, kitu alichokifikiria ni kwamba mume wake alikuwa akiumwa kichwa kweli.
Hawakuchukua dakika nyingi wakafika hapo hospitalini. Hali aliyokutana nayo ikaanza kumtisha, kulikuwa na idadi kubwa ya watu huku kukiwa na waandishi wengi waliomtia hofu na kuhisi kulikuwa na kitu. Kitendo cha kuteremka kutoka garini, waandishi wakamfuata kwa lengo la kumuhoji.
“Unajisikiahe?” alimuuliza mwandishi mmoja.
“Kuhusu?”
“Kifo cha mume wako,” alijibu mwandishi huyo.
Hakufuata miiko ya kazi, aliuliza swali ambalo hakuwa na uhakika nalo hata kidogo. Linda akashtuka, hakuamini kile alichokuwa ameulizwa, hakujibu kitu, alibaki amepigwa na butwaa, alimwangalia vizuri mwandishi huyo na ndipo alipopata jibu la watu wengi kukusanyika mahali hapo kwa wingi namna ile.
Huku akiwa kwenye hali hiyo, mama yake akamvuta na kisha kuondoka naye huku waandishi wa habari wakitaka kuzungumza naye ka kumuhoji baadhi ya maswali kitu ambacho wazazi hao hawakutaka kuona kikitokea.
Bila kutarajia, machozi yakaanza kumtoka mashavuni mwake, hakuamini kama kweli mpenzi wake, William alifariki dunia. Hakutembea kwa mwendo mrefu ndani ya jengo la hospitali hiyo, akasimama, akaona miguu kuwa mizito, akataka kuanguka, baba yake akamuwahi, akamdaka na kumpeleka kwenye benchi ambapo hapo, Linda akaanza kulia mfululizo huku akilitaja jina la mume wake. Kwa kifupi, alichanganyikiwa.

Je, nini kitaendelea?
JE, William atakufa?
Vipi kuhusu Godson?

No comments

Powered by Blogger.