Kauli ya Freeman Mbowe Baada ya Makonda Kumtaja kwenye Orodha ya Wahusika wa Madawa ya Kulevya
Muda
mfupi baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwaita
polisi kuhojiwa kwa tuhuma mbalimbali, baadhi ya walioitwa wamelaani
hatua hiyo wakisema inalenga kuwachafulia majina na heshima mbele ya
jamii.
Miongoni mwa waliotwa ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye amezungumza na kueleza kutofurahishwa na hatua hiyo.
Mbowe aliyekuwa safarini kwenda bungeni Dodoma, alisema ameshangazwa kutuhumiwa kwa jambo asilolijua.
“Kama amemtaja mbunge wa Hai anajulikana ni mmoja, hata kama asingesema Freeman, Mbunge wa Hai anajulikana ni Freeman Mbowe.
“The
only thing (kitu pekee) ninaweza kusema nchi haiendeshwi hivyo.
Yametajwa majina mengi ambayo sijui Makonda ana evidence (ushahidi)
gani!
“Anasema
tukiwaita tukiridhika na maelezo yao tutawaachia. Huwezi kusema tu,
yaani kwa kusema ni Mbowe... mimi ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, mimi ni mbunge, mimi ni mzazi, nina wanachama, maaskofu,
mapadri, mashehe na viongozi mbalimbali.
“Unapokuwa
unamhusisha kiongozi na ‘drug trafficking au drug business’
(usafirishaji wa dawa au biashara ya dawa za kulevya), sijui ana
ushahidi gani hadi akanihusisha na jambo hilo, mimi sielewi, kwa hivyo
siwezi kusema kwa kitu ambacho sielewi,” alisisitiza Mbowe.
Mbowe
aliendelea kusema kuwa kesi za dawa za kulevya hazina dhamana, hivyo
alimtaka Makonda awe na ushahidi wa kutosha anapowataja watuhumiwa.
“Tuache
habari ya kuitwa, wewe umepata tuhuma, hujafanya uchunguzi, hakuna mtu
aliye juu ya sheria, lakini unatakiwa kufanya uchunguzi ili ukimkamata
mtu unamshtaki, siyo unataja mtu unachafua hadhi yake. Halafu ukija
kusema hatuna ushahidi juu yako umeshaharibu jina lake,” alisema na kuongeza:
“Mimi
sijui kama jeshi la polisi linafanya kazi hii au ni Makonda amejipa
kazi ya kuwa mpelelezi. Au labda yeye kwa kuwa ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Ulinzi na Usalama ndiyo amejipa kazi ya kutaja majina kwenye mambo
yenye kashfa kama haya? Sielewi. This is very wrong precedence (Hii ni
rejea mbaya) kwa utawala wa sheria.”
Mbowe alisema inawezekana ni mikakati ya Serikali kuendelea kukandamiza upinzani kwa kuwakamata viongozi wake.
“Sijui
kama kuna watu wanaolengwa, lakini tumeona viongozi wetu wanakamatwa
hawapewi dhamana, (Tundu) Lissu amekamatwa, (Godbless) Lema amekamatwa
... mtu anakaa miezi minne, kwa hiyo wanaweza kufanya lolote.
Inawezekana ni mkakati wa kutesa wapinzani. Wamenitafuta kwenye biashara
wameona haitoshi... sina uhakika lakini sioni kama wana nia njema na
sisi,” alisema Mbowe.
Alipoulizwa kama ataitikia wito wa Makonda, Mbowe alisema bado anawasiliana na wanasheria wake kabla ya kuchukua hatua.
Post a Comment