ad

ad

FUTA MACHOZI MPENZI-11

 
NYEMO CHILONGANI

“Mkuu! Hakuna intaneti chuoni,” alisikika mwanachuo mmoja.
“Haiwezekani!”
“Hakuna intaneti mkuu! Tumejaribu kila mbinu lakini hakuna intaneti. Modem zinafanya kazi, lakini intaneti haipatikani, wireless ipo wazi lakini napo intaneti hakuna,” alisema mwanachuo huyo.
Hilo lilimshangaza kila mmoja, hawakuamini kile walichokuwa wamesikia kwamba huduma ya intaneti haikuwa ikipatikana katika maeneo ya chuo hicho. Hilo lilikuwa jambo lisilowezekana hata mara moja kwani tangu huduma ya intaneti iwekwe chuoni hapo hakukuwa na siku yoyote ambayo kulionekana kuwa na tatizo kama hilo.
Maprofesa walichanganyikiwa, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea, kwa kutumia wanachuo waliokuwa chuoni hapo, wakawaaambia wafanikishe suala hilo lakini walipohangaika nayo, kwa zaidi ya saa saba hakukuwa na majibu yoyote yale.
Mambo mengi yalidorora, kila kona chuoni hapo kulikuwa na malalamiko kwamba intaneti haikupatikana lakini walipokuwa nje ya eneo hilo ilikuwa ikipatikana kama kawaida.
Hilo likawafanya maprofesa kuwasiliana na wataalamu waliobobea kutoka katika mashirika mengi lakini nao walipofika chuoni hapo walishangaa, tatizo ambalo walilikuta chuoni hapo hawakuwahi kulipata kabla.
Siku hiyo ikakatika huku mafundi wakihangaika, hawakulala, waliingiza codes na kuangalia tatizo lilikuwa nini lakini hawakugundua kitu chochote kile. Mpaka inafika asubuhi, hakukuwa na huduma ya intaneti na hapo ndipo walipoamua kuwasiliana na watu wa NASA kwa kuona kwamba wangeweza kuwasaidia katika hilo kwani mambo yao ya anga walioyokuwa wakishughulika nayo yangerahisisha kile kilichokuwa kimetokea.
Wataalamu wawili kutoka NASA (NASA - National Aeronautics and Space Administration) wakafika chuoni hapo. Wanachuo walipowaona, mioyo yao ilikuwa na faraja kwamba hatimaye tatizo hilo lingekwisha.
Gari lililokuwa na maneno makubwa yaliyosomeka NASA ubavuni likaegeshwa na wataalamu hao kuteremka na kuelekea ndani ya ofisi ya professa Turnbull ambapo baadaye wakapelekwa katika chumba cha kompyuta ambapo huko wakawakuta wataalamu wengine wakiendelea na kazi zao za kuhakikisha intaneti inapatikana haraka iwezekanavyo.
“What is going on?” (nini kinaendelea) aliuliza jamaa mmoja wa NASA, huyu aliitwa Fredrick.
“We are still working on it?” (bado tunaendelea nayo)
Alichokifanya Fredrick na mwenzake ni kuwaambia watu hao wakae pembeni na wao kufanya kazi yao. Walihisi kwamba ilikuwa kazi nyepesi mno, wakaanza kufanya kazi, walitumia ufundi wao, waliingiza codes zao kwenye kila kompyuta lakini hazikuweza kufanya kazi hata kidogo.
“Kuna virusi vimeingia,” alisema Fredrick baada ya saa tatu kupita na hakukuwa na mafanikio yoyote yale.
“Virusi gani?”
“Hatuvijui, ila vimefuta codes zote ambazo zilitakiwa ziwe zinaonekana ili zibadilishwe,” alisema Fredrick.
“Lakini tuna anti virus!”
“Nayo imeshambuliwa. Mungu wangu! Sijawahi kuona virusi hatari kama hivi! Imekuwaje? Vimetoka wapi? Nani kavitengeneza?” alijiuliza maswali mengi lakini hakukuwa na mtu aliyekuwa na majibu.
Siku ya pili ikakatika hakukuwa na huduma ya intaneti chuoni hapo. Kila mmoja alichanganyikiwa, wanafunzi hawakuingia darasani waliamua kugomea masomo kwani yasingeweza kuendelea pasipo huduma ya intaneti chuoni hapo.
Waandishi wa habari wakazipata taarifa hizo na kufika chuoni hapo, wakaulizia kilichokuwa kikiendelea, ilikuwaje mpaka intaneti ishindwe kupatikana chuoni hapo. Maprofesa hawakuwa na jibu zaidi ya kujiumauma.
“Tutawaambia. Bado tunalishughulikia,” alisema Profesa Turnbull huku akionekana wazi kuchanganyikiwa.
“Lini litakuwa tayari?” aliuliza mwandishi wa Daily Mail.
“Nimesema bado tunalishughulikia,” alisema profesa huyo kwa ukali uliomaanisha kwamba hakutaka maswali mengine. Baada ya kuhangaika kwa muda wa siku nne ndipo wakakubaliana kwamba ilikuwa ni lazima wampigie simu mtaalamu Vint Cerf.
Huyu alikuwa mtu aliyeigundua intaneti mwaka 1983 na kuwa hewani mwaka 1993 kwa kupewa kitu kiitwacho World Wide Web yaani www na kupewa jina la heshima la Father Of The Internet, yaani Baba wa Intaneti.
Kila mtu alimheshimu mwanasayansi huyo wa kompyuta ambaye alijinyakulia tuzo nyingi mpaka kipindi hicho alichokuwa na miaka sabini na tatu.
Haraka sana wakaitafuta namba yake, wakampigia huku wakitaka kuzungumza naye kwa kuamini kwamba alikuwa nyumbani kwake alipozaliwa, New Haven, Connecticut hukohuko nchini Marekani.
Simu yake haikuwa ikipatikana, hilo liliwachanganya sana, walihangaika kumtafuta mpaka baadaye walipowasiliana na wanasayansi wengine na kuambiwa kwamba mtu huyo alikuwa amekwenda Paris nchini Ufaransa kwa mambo yake binafsi, wakapewa namba aliyokuwa akiitumia huko na kuwasiliana naye.
Alipopokea simu, wakamwambia kuhusu kile kilichokuwa kikiendelea. Alishangaa, hakuwahi kusikia kitu kama hicho na mshangao wake zaidi ni pale aliposikia hata watu wa NASA walichemka kwani wao walikuwa na uwezo mkubwa wa kuweka sawa kitu kama hicho kutokana na kutumia satalaiti zilizotumia sana intaneti wakati wote.
“Sidhani kama ni kweli,” alisikika kwenye simu.
“Ni kweli mkuu! Hapa tumechanganyikiwa!”
“Basi nakuja!”
“Leo au?”
“Kwa sababu ni jambo la kushtukiza, nikodieni ndege, nakuja!” alisema na kukata simu.
Hilo halikuwa na tatizo, chuo hicho ambacho kilikuwa chini ya serikali kikalipia ndege na kisha kumchukua mtu huyo na kumpeleka nchini Marekani ambapo baada ya kufika tu, akapelekwa mpaka chuoni.
Alihisi kulikuwa na tatizo kwani kipindi ambacho alikuwa aligundua intaneti kulikuwa na siri ambazo hakuwa ameziweka wazi wala kuziweka katika vitabu vyake. Baada ya kufika chuoni hapo, hakutaka kushughulika na kompyuta zao, alichokifanya ni kuchukua laptop yake na kuiweka mapajani kisha kuanza kushughulika nayo.
Haikuwa kazi nyepesi, ilikuwa ni kazi kubwa iliyofanya kijasho chembamba kuanza kuonekana. Kilichokuwa kikimtatiza ni virusi vilivyoitwa kwa jina la Winirus, vilikuwa hatari na vilificha codes nyingi, hasa zile muhimu ambazo kama zingeonekana kurekebishika kwa tatizo hilo kusingekuwa na tatizo lolote lile.
Alikaa na laptop yake, hakukubali kula, hakuwahi kushindwa hivyo ilikuwa ni lazima afanikishe kile alichotakiwa kufanya. Alichukua saa zaidi ya nne, baadaye akaonekana kama kuanza kufanikiwa.
Alishughulika nayo na baada ya saa tano, huduma ya intaneti ikaanza kurudi taratibu, yaani ilikuwa ikirudi na kukata.
“Inakuja na kukata!” alisema Profesa Turnbull.
“Usijali! Itarudi moja kwa moja!”
Aliendelea kuhangaika nayo. Ilipofika saa mbili usiku, kwa tabu sana hatimaye akafanikiwa kuirudisha intaneti chuoni hapo kitu kilichomfanya kila mtu kuwa na furaha.
“Imerudi!” alisikika Profesa Turnbull kwa sauti kubwa.
“Imerudi!” alidakika profesa mwingine.
Hiyo ilikuwa ni furaha ya kila mmoja, Vint akachukua glasi ya maji na kunywa kama kupoza kiu kwani mwili wake ulikuwa umechemka kwa kiasi kikubwa kutokana na kazi kubwa ambayo aliifanya, kazi ambayo hakuwahi kukutana nayo tangu alipoanza kutumia kompyuta.
“Tatizo lilikuwa nini?” aliuliza profesa.
“Ni tatizo kubwa ambalo halielezeki!”
Wakati kila mmoja akionekana kuwa na furaha tele, hawakujua ni kitu gani kilitokea, mara intaneti ikakata tena. Hilo ndilo lililowachanganya zaidi, harakaharaka Vint akachukua laptop yake na kuiwasha, alitaka kujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea. Alipoiwasha tu, kitu cha kwanza akakutana na maneno makubwa yaliyosomeka ‘I GET YOU BACK TO WORK’ yakimaanisha NAKURUDISHA TENA KAZINI. Baada ya maneno hayo, picha kubwa ya William ikatokea katika kompyuta yake.
Profesa Macleash akashtuka kwani sura aliyoiona, aliifahamu. Ilikuwa ya William, mtu aliyemwambia kwamba alikuwa genius kutoka Tanzania na alitaka kujiunga na chuo hicho, aliikumbuka barua pepe yake ya mwisho kumtumia kwamba alitakiwa kufika nchini Marekani ili kuonyesha huo ugenius wake, kumbe kuizima intaneti ya chuo hicho ndiyo ilikuwa njia mojawapo ya kuonyesha ni kwa namna gani alikuwa genius.
“He is the one,” (ndiye yeye) alijikuta akisema Profesa Macleash kwa sauti iliyowafanya wenzake wote kushtuka, Vint akatoa miwani na kumwangalia profesa huyo.

Je, nini kitaendelea?

No comments

Powered by Blogger.