Maelezo ya Mtatiro kuhusu kesi ya kupinga ushindi wa CCM Segerea
Napenda kutoa taarifa hii rasmi na ya awali kwa wananchi wa Segerea na watanzania wote ambao walipigana kufa na kupona ili kuhakikisha UKAWA tunashinda madiwani, mbunge na kuongoza kura za Rais hapa jimboni. Kwa bahati mbaya tulifanikiwa kushinda madiwani wote, kuongoza kura za Rais lakini tukashindwa kwenye Ubunge.
Baada ya jimbo letu kwenda CCM
nilishauriwa nisisaini kukubali matokeo na nikatekeleza ushauri huo,
lengo lilikuwa ni kuwapa muda wanasheria wetu na mawakili waweze
kushauri ikiwa kuna kesi ya kufungua kupinga ushindi wa CCM.
Baada ya mashauriano ya wiki kadhaa yaliyohusisha mawakili na wataalam
wa sheria wa ngazi mbalimbali, tumejiridhisha na kushauriwa kwamba
hatutakuwa na kesi ya kufungua, na kwamba tukiifungua kwa kulazimisha au
"kwa kusukumwa na upepo wa wananchi" tutashindwa mahakamani mapema.
Wanasiasa wengi hukimbilia mahakamani wanaposhindwa uchaguzi si kwa
sababu wana kesi zenye ushahidi wenye mashiko, bali huogopa maneno na
tuhuma wanazoweza kupewa kuwa "wamenunuliwa na wagombea wa CCM", mimi
kwa bahati nzuri sijakumbwa na upepo huo na natambua wananchi wa Segerea
wananiamini kiasi cha kutosha.
Baada ya wiki moja kutoka sasa,
ntatoa taarifa rasmi na ya kina juu ya hoja na sababu zilizopelekea
wanasheria na mawakili wetu washauri tusihangaike kufungua kesi na
kupoteza muda wa matumaini ya wananchi.
Mtatiro Julius,
Segerea.
Post a Comment