FUTA MACHOZI MPENZI -10
NYEMO CHILONGANI
Nicolaus alikuwa na furaha tele, kitendo cha msichana Melania kusafiri mpaka nchini Australia kwa ajili ya kwenda kumuomba picha zake kilimfanya kujiona mjanja na kila alipokaa alikuwa akikenua tu.
Moyo wake ulizidiwa kwa furaha kiasi kwamba kila wakati alikuwa akitabasamu tu. Baada ya siku tatu, wakati yupo darasani huku akiangalia simu yake, ghafla ikazima. Hakujua kulikuwa na tatizo gani, hakujua ni kitu kilichokuwa kimetokea.
Harakaharaka akaiwasha lakini haikuwaka, ilikuwa kama imeganda sehemu moja na hakukuwa na batani yoyote iliyokuwa ikifanya kazi. Hakujua ni kitu gani kilichokuwa kimetokea, aliwaambia marafiki zake kuhusu tatizo hilo lakini hakukuwa na mtu aliyemsaidia na hakujua kwamba kipindi hicho ndicho ambacho William alikuwa akifanya yake.
Simu ilibaki katika hali hiyo mpaka ilipokwisha chaji. Aliporudi chumbani na kuiwasha, simu ikakubali, wakati inawaka na kutaka kumuwekea ‘home screen’, picha iliyoonekana ni ya kidole cha kati kikiwa kimenyooshwa.
Alikifahamu kidole hicho kwani jinsi rangi zilivyokuwa zimepakwa, alifahamu kwamba alikuwa Melania. Alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani kilichokuwa kimetokea. Hakutaka kuhangaika, aliona kama msichana huyo alikuwa amejisumbua tu.
Akaiwasha laptop yake ili kuangalia picha zile kitu kilichomshangaza, picha zile alizokuwa amezihifadhi katika kompyuta zake hazikuonekana.
“Mmh! Si niliziweka kwenye hili faili!” alijisemea na kuanza kupitia mafaili yote, moja baada ya jingine lakini hakuweza kuziona picha hizo.
Moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kilichotokea, harakaharaka akakimbilia kwenye barua pepe kwani alizihifadhi huko pia. Alipofungua barua pepe na kuingia, kitu cha kwanza kabisa kilichoonekana ni picha ya kidole cha kati cha msichana Melania.
Alichanganyikiwa zaidi, hakujua ni kitu gani kilitokea. Moyo wake uliuma, hapohapo akajikuta akianza kutokwa na machozi kwani hizo picha ndizo alizokuwa akijitambia nazo, alikuwa na uhakika wa kufanya jambo lolote kwa Melania hasa pale ambapo angemtisha kuzivujisha picha hizo.
Hakuwa na furaha, alionekana kuwa na mawazo mengi. Alipoteza kila kitu, alitamani kumpigia simu msichana huyo na kuzungumza naye lakini hakupata nafasi hiyo tena kwani hata namba yake hakuikariri na mbaya zaidi namba zote kwenye simu yake zilikuwa zimefutwa kama kisasi kwa kile alichokuwa amekifanya.
Kuanzia siku hiyo hakuwa na furaha tena, hakuridhika, aliona ni lazima angefanya jambo lolote lile kulipa kisasi. Kwa kile alichokuwa amefanyiwa kwake kilionekana kuwa ukatili mkubwa, hakutaka kukubali hata kidogo, alijiapiza kwamba ni lazima afanye jambo lolote lile kumkomoa msichana huyo ambaye kipindi hicho hakuwa na taimu naye, aliamua kufanya mambo yake.
****
Moyo wa Melania ukafurahi, hakuamini kuona kile alichokuwa amekitaka kikiwa kimefanikiwa. Moyo wake ukawa na shukrani nyingi kwa William, japokuwa mwanaume huyo alikuwa akitisha kwa ubaya wa sura yake lakini akajiona akitamani sana kuwa karibu naye.
Wakawa wakiwasiliana, hakukuwa na mtu aliyekuwa na hisia zozote za kimapenzi moyoni mwake, walikuwa wakiwasiliana kama marafiki tu. William alikuwa mzungumzaji sana, wakati mwingine alimfanya msichana huyo kuwa na furaha tele kiasi cha kuhisi kwamba kulikuwa na kitu cha tofauti kikianza kuchipuka moyoni mwake.
Alihisi hisia kali za kimapenzi, wakati mwingine alikuwa akikataa, hakuona kama kwa jinsi alivyokuwa mzuri, alivyopendwa na wanaume wengi basi alikuwa anastahili kuwa na mwanaume kama William ambaye sura yake ilikuwa vilevile.
Alivumilia lakini kitu cha ajabu kabisa kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo alivyochanganyikiwa na penzi la William. Mwanaume huyo hakuwa na taimu naye, yeye alikuwa bize na mambo yake.
Alikuwa mchangamfu kila alipopigiwa simu lakini simu zilipokatwa, hakuwa akimtafuta msichana huyo kwani alikuwa na mambo mengi ya kufanya mbali na mapenzi. Hakutaka kuendelea kuishi nchini Tanzania, alijiamini kwamba aliifahamu sana kompyuta hivyo aliona kwamba hiyo ilikuwa nafasi pekee ya kuondoka nchini Tanzania na kuelekea Marekani kwa ajili ya kusoma katika Chuo Kikuu cha Harvard.
Alijua kwamba malipo yote ya ada yalikuwa yakilipwa katika akaunti ambazo ziliwekwa wazi, kitendo cha kushirikisha benki na kompyuta kilimfanya kuwa na uhakika wa kufanikiwa katika kile alichotaka kukifanya.
Akaingia mtandaoni, akaangalia sifa za wanafunzi waliotakiwa kusoma katika chuo hicho. Walihitajika wanafunzi waliokuwa na akili sana na mbali na hao, pia walihitajika wanafunzi waliokuwa na fedha nyingi kwani malipo ya masomo katika chuo hicho yalikuwa makubwa mno.
Hilo halikuwa tatizo, alikuwa na fedha za kutosha lakini pia hakutaka kulipia masomo hayo, alitaka kusoma bure kabisa kuonyesha kwamba alikuwa mtundu katika mambo ya kompyuta kwa ujumla.
Alichokifanya ni kucheza na codes za kompyuta tu. Kuingia katika codes za kompyuta za chuo hicho haikuwa kazi kubwa, kompyuta zao zilifungwa na watu waliobobea katika ‘programing’, wenye digrii zao lakini kwa William hakuona kama kulikuwa na tatizo kwani aliamini kwamba kwenye kila code, kama alikuwa na nafasi ya kuviingiza virusi vyake vya Wirus basi angefanikiwa katika kila kitu.
Akaingia katika kompyuta zao na kuanza kuzipitia codes zao, zilikuwa ngumu, zilizojifunga ambazo zilimpa wakati mgumu mno kupambana nazo. Alitumia kila njia, alizichambua moja baada ya nyingine lakini alishindwa kabisa.
Alichokifanya ni kuvitumia virusi vyake lakini kitu cha ajabu kabisa, virusi hivyo havikuweza kufua dafu kwani anti virusi waliyokuwa wakiitumia ilikuwa kali na ilitengenezwa moja kwa moja kutoka Microsoft maalumu kwa ajili yao.
“Wamejitahidi sana, ila nitapambana. Ngoja niwatumie barua ya maombi kwanza,” alisema William na kufanya hivyo.
Akatuma barua hiyo ya maombi ya kutaka kujiunga na chuo hicho. Hakuwa na sifa za kutosha lakini kwenye barua hiyo aliwaambia kwamba alitaka kujiunga nao kwa kuwa alikuwa genius ambaye alikuwa na uwezo wa kufanya chochote kile katika masuala ya kompyuta.
“How genius are you?” (una akili kiasi gani?) lilikuwa swali aliloulizwa katika maelezo marefu aliyopewa.
“I can change impossible to possible,” (naweza kufanya visivyowezekana viwezekane) alijibu.
Walichomwambia ni kwamba wakihitaji kuzungumza naye kwa ajili ya kuhakikisha kama kweli alikuwa genius au la. Kwa kuwa chuo hicho kilithamini sana watu waliokuwa na uwezo huo, wakampigia simu na kumwambia kwamba alitakiwa kusafiri mpaka nchini Marekani kwa ajili ya kuzungumza naye kwani kama alisema kuwa alikuwa genius kwenye masuala ya kompyuta, walitaka kuangalia uwezo wake.
“I will be there,” (nitakuwa huko)
Akamwambia mama yake kile alichoambiwa kwamba alitakiwa kwenda nchini Marekani kwa ajili ya kuwaonyesha ni kwa jinsi gani alikuwa na akili. Mama yake alikuwa na hofu, alizungumza naye na kumwambia kwamba kama walihitaji fedha kama ada, awalipe lakini alikataa katakata.
“Huwezi kulipia kitu ambacho una uhakika wa kukipata bure,” alisema William.
“Kwa hiyo utahakikisha unasoma bure?”
“Hiyo ndiyo maana yangu!”
Wakati akizungumza hayo bado alikuwa akihangaika kuingia katika kompyuta za chuo hicho. Alijitahidi kwa nguvu zote, alipambana usiku na mchana lakini bado kompyuta hizo zilionekana kuwa ulinzi mkali sana.
“Nitaingiaje? Ni lazima nipate njia za kuingia humu! Ngoja nitengeneze virusi vingine,” alisema William, hakutaka kuona akishindwa, alihitaji kuwaonyeshea Wamarekani kwamba alikuwa mtu hatari. Akatengeneza virusi vingine alivyovipa jina la Winirus ambavyo aliamini kwamba vingekuwa na nguvu zaidi.
Utengenezaji wake haukuwa mwepesi, alihangaika kwa nguvu zote, alijitahidi kufanya kila liwezekanalo kupambana na kompyuta za chuo hizo. Ilikuwa vigumu sana kuingia kwenye kompyuta hizo na kuchanganya codes hizo, alipoona kwamba ameshindwa, akapata wazo jingine kabisa.
“Ni lazima niondoe huduma ya internet katika eneo la chuo hicho halafu ndiyo niingize virusi hivi,” alisema William, baada ya hapo akatabasamu. Harakaharaka akaivuta kompyuta yake kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
****
Hicho kilikuwa kipindi kipya cha kuanza masomo katika Chuo Kikuu cha Harvard kilichokuwa Cambridge, Massachuesetts nchini Marekani. Wanafunzi wengi wenye akili na wale waliotoka katika familia za kitajiri walikuwa wakifika hapo kwa ajili ya kuanza masomo chuoni hapo.
Watu wengi duniani, wasomi walikuwa wakitamani kuingia chuoni hapo kwani mbali na Oxford kilichokuwa nchini Uingereza, hiki kilikuwa chuo kimojawapo miongoni mwa vile vikubwa duniani ambacho pia watu maarufu kama Barack Obama, rais John F Kennedy na watu wengine maarufu na wakubwa walisoma hapo.
Professa John Macleash ndiye aliyekuwa akihusika na watu wote waliokuwa wakitaka kujiunga na chuo hicho, yeye ndiye aliyekuwa akimtumia barua pepe William na kumwambia kila kitu alichotakiwa kukifanya.
Siku ambayo kijana huyo alimwambia kwamba alikuwa na akili sana, akaichukua barua pepe hiyo na kuwapelekea maprofesa wenzake ambao walikaa chini na kuanza kuisoma. Walimpuuzia kwa sababu walijua kwamba hakukuwa na mtu aliyekuwa na akili kubwa ambaye alikuwa nje ya chuo hicho.
Waliamini kwamba mtu yeyote ambaye alikuwa na akili nyingi, kabla ya kwenda katika vyuo vingine ilikuwa ni lazima apitie kwao. Walijiuliza kuhusu William, kilichowafanya kumshangaa zaidi ni kwamba alitokea barani Afrika, katika nchi masikini kama Tanzania.
“Kwa hiyo?” aliuliza Profesa Macleash.
“Achana naye! Watu wote wenye akili wapo humu! Yeye atakuwaje na akili akiwa nje ya chuo hiki? Kuna wataalamu wa hesabu hapa, kuna wataalamu mbalimbali, hivi kweli unaamini mtu mwenye akili nyingi anaweza kuwa Afrika?” aliuliza profesa mwingine, huyu aliitwa Thomson.
“Hata mimi nilishangaa ila tunatakiwa tumpe nafasi!”
“Haiwezekani! Watu weusi ni wataalamu wa kuzungumza na si mambo ya kompyuta au hesabu. Mwangalie Martin Luther Jr, Obama na wengineo, wote ni wataalamu wa kuzungumza ila si mambo ya hesabu kama haya, si mambo ya kompyuta,” alisema profesa mwingine, huyu aliitwa Turnbell.
Walikuwa wakizungumza yale waliyokuwa wakiyafahamu wao lakini kwa Profesa Macleash alikuwa akifikiria yake kabisa. Alipenda kuona watu wengi waliokuwa na vipaji wakiendelea kumiminika katika chuo hicho, aliamini kwamba huyo mtu aliyejitambulisha kwa jina la William alikuwa genius na ndiyo maana hakutaka kuficha, alimwambia ukweli juu ya maisha yake.
Hakukubaliwa lakini alichokifanya ni kumtumia barua pepe William na kumwambia kwamba alikuwa akihitajika chuoni hapo kwa ajili ya kudhihirisha kile kipaji alichokuwa nacho.
Barua pepe hiyo ilipopokelewa, ikajibiwa kwamba angefika baada ya wiki moja hivyo profesa huyo kumtumia tiketi, kumuombea viza na kumfanyia taratibu nyingine zote za safari wa kwenda huko pasipo kuwaambia wenzake kwamba alikuwa amemkubalia mwanafunzi huyo afike chuoni hapo kwa ajili ya kuonyesha uwezo wake.
Je, nini kitaendelea?
Post a Comment