FUTA MACHOZI MPENZI-09
NYEMO CHILONGANI.
Maisha ya kimasikini aliyokuwa akiishi na mama yake ndiyo yaliyomfanya kuanza kuiba fedha katika benki moja na kuziweka kwenye simu yake. Moyo wake ulifurahi, ndani ya simu hiyo kulikuwa na shilingi milioni mia tano, kiasi kikubwa ambacho angeamua kufanya kitu chochote kile.
Hakumwambia mama yake, alichokifanya ni kuzitoa fedha hizo na kuziweka katika akaunti yake ya benki. Katika kila kitu kilichokuwa kikiendelea kilifanyika kwa kuzichezea codes za benki hiyo ambapo hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akiufahamu mchezo huo.
Maisha yakaanza kubadilika, akaanza kununua nguo na vitu vingine, yalikuwa ni mabadiliko ya haraka sana, mama yake hakujua kilichokuwa kikiendelea, alishangaa tu kuona mtoto wake akianza kubadilika, kuwa na muonekano mpya ambao aliushangaa.
Kila alipokuwa akimuuliza, William hakuwa akijibu kama ilivyokuwa ikitakiwa. Kisiri sana akaanza kutafuta nyumba ya kununua, kwa bahati nzuri akaipata maeneo ya Tabata Kimanga ambapo huko akaiona na kuinunua kwa kiasi cha shilingi milioni mia moja.
Ilikuwa nyumba kubwa, yenye kila kitu ambayo ilitakiwa kukaliwa na mtu mwenye fedha. Hakumwambia mama yake, iliendelea kuwa siri huku akiendelea kuzitumia fedha zile. Ndani ya nyumba hiyo akatenga chumba kimoja kwa ajili ya kompyuta tu, humo ndani ndipo kulipokuwa kukitumika mambo yake yote ya kompyuta huku akinunua laptop kwa ajili ya kupiga madili yake.
Alikuwa kijana mdogo lakini alionekana kuwa na mafanikio makubwa. Baada ya kupita kipindi cha miezi mitatu, akamtafuta mzee mmoja ambaye alimtaka kuzungumza na mama yake ili ajue kilichokuwa kimetokea.
“Habari yako mama,” ilisikika sauti kwenye simu.
“Salama tu!”
“Una mtoto anaitwa William?” aliuliza mwanaume huyo.
“Ndiyo! Amefanyaja mwanangu?”
“Ni kwamba alicheza bahati nasibu yetu ya shinda nyumba na amefanikiwa kushinda nyumba yenye kila kitu ndani iliyopo huku Tabata Kimanga,” ilisikika sauti ya mwanaume huyo.
“Unasemaje?”
“Ndiyo hivyo! Aliandika namba yako ya simu kwenye tiketi yake na ndiyo maana tumekupigia wewe kumpa taarifa ya ushindi wake,” alisikika mwanaume huyo.
Bi Sophia hakuamini alichokisikia, machozi yakaanza kumtiririka mashavuni mwake, moyo wake ulikuwa na furaha tele. Siku hiyo hata biashara ya genge haikufanyika tena, alimsubiri mwanaye kwa hamu kubwa kwa ajili ya kumpa taarifa juu ya kilichotokea.
Saa kumi jioni William akarudi nyumbani, alipomuona tu, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumkumbatia huku machozi yakimtiririka mashavuni mwake. Hakuamini kama mtoto wake alishinda nyumba hiyo, hakuamini kama kipindi hicho kilikuwa ni cha kuhama huko Tandale na kuhamia Tabata.
“Willy! Ulicheza bahati nasibu ya nyumba?” aliuliza Bi Sophia huku akimwangalia William.
“Ndiyo! Kuna nini mama?”
“Umeshinda nyumba.”
“Unasemaje?”
“Umeshinda nyumba mwanangu! Nimepigiwa simu,” alisema Bi Sophia na kumkumbatia tena mtoto wake.
William akashindwa kuvumilia, kwa jinsi mama yake alivyokuwa akibubujikwa na machozi, hata naye akajikuta akibubujikwa na machozi ya uchungu kwani umasikini uliwatesa kwa kipindi kirefu.
Siku iliyofuata William akawasiliana na mwanaume huyo na kumwambia awafuate na gari na kuwachukua, hilo halikuwa tatizo kwani muda waliopanga mwanaume huyo na mwenzake wakafika mahali hapo, wakawachukua na kuelekea huko Tabata.
Kila kitu kilikuwa ndani, nyumba kubwa, Bi Sophia alipoiona, hakuamini, alijikuta akianza kulia tena na kupiga magoti. Moyo wake ulikuwa na furaha kubwa, isiyosimulika, hakuamini kama walikuwa wametoka Tandale na kuhamia Tabata tena kwenye nyumba yao.
Hilo likaendelea kuwa siri, William aliendelea kuziibia benki mbalimbali. Hakuwa akitoka nyumbani lakini kila siku alikuwa akiingiza kiasi kikubwa cha fedha. Maisha yake yalibadilika, alinunua magari na kufungua biashara kubwa.
“Kuna kitu unanificha,” alisema Bi Sophia.
“Hakuna kitu!”
“Hapana! Kuna kitu unanificha...”
“Sawa. Basi ngoja niwe muwazi. Nimepata kazi!” alijibu William.
“Kazi gani?”
“Bandarini!”
“Ndiyo uwe na magari namna hiyo!”
“Ujanjaujanja tu mama!”
“Hapana niambie ukweli,” alisisitiza Bi Sophia.
Baada ya kubanwa sana huku mama yake akionekana kutaka kufahamu ukweli ndipo akaamua kumuelezea kila kitu tangu siku ya kwanza mpaka hapo alipofikia. Mwanamke huyo alikuwa kimya, hakuamini kile alichokizungumza mtoto wake, wakati mwingine aliona kama alikuwa ndotoni, iweje mtoto wake awe na kiasi kikubwa cha fedha namna hiyo na asigundulike na mtu yeyote?
“Samahani kwa kukuficha mama! Ila ukweli ni kwamba nina bilioni mbili kwenye akaunti!” alisema William maneno ambayo yalimshtua mwanamke huyo.
“Na siku ukikamatwa?”
“Hakuna kitu kama hicho mama! Niliwachukulia fedha kiakili sana. Ninataka kwenda kuongeza elimu yangu, mwezi ujao nataka niende kusoma katika Chuo cha Harvard nchini Marekani,” alisema William, mama yake akashtuka.
“Kusoma Marekani?”
“Ndiyo!”
“Na ada?”
“Nina hela nyingi mama! Uwezo wa kulia ada upo ila sitotaka kulipia, nitasoma bure kabisa,” alisema William.
“Unanichanganya!”
“Mama ulimwengu umebadilika. Siku hizi ada hupeleki mkono kwa mkono, unalipia benki na ndiyo maana nakwambia nitasoma bure huko Marekani! Nitataka niwe mtu mwenye heshima kubwa hapo baadaye, watu walitudharau, walikuzomea kwa sababu ya sura yangu! Mama! Mungu hakunyimi kila kitu, ameninyima sura nzuri ila ameupa ubongo wangu uwezo mkubwa wa kufanya kitu chochote kile,” alisema William huku akiachia tabasamu ambalo liliufanya uso wake kuwa mbaya zaidi.
Baada ya siku kadhaa, akatembelea na mtu aliyemfahamu sana, huyu aliitwa Michael. Alimfuata nyumbani kwao huku akiongozana na msichana aliyekuwa na sura nzuri aliyejitambulisha kwa jina la Melania.
Kwa jinsi alivyokuwa akimwangalia msichana huyo, alikiri kwamba alikutana na mtu mwenye sura nzuri kuliko wasichana wote aliowahi kuwatia machoni.
Melania alionekana kuogopa, kila alipomwangalia William alitamani kukimbia. Mwanaume huyo alitisha, sura yake ilifanana na nyani na kilichowatofautisha ni kwamba hakuwa na manyoya mengi kama nyani.
Alimwangalia kwa hofu, wakati mwingine alitamani kuondoka mahali hapo kwani kila alipoyatua macho yake kwa mwanaume huyo, alihisi mapigo yake ya moyo yakidunda kwa nguvu kupita kawaida.
Michael akaanza kumtambulisha Melania na kile kilichomfanya kuwa mahali hapo na kumuhadithia juu ya kile kilichokuwa kimemtokea msichana huyo. William alitoa tabasamu pana, Melania akazidi kuogopa, hakuamini kama mtu huyo alikuwa binadamu.
“Pole sana mrembo,” alisema William huku akimwangalia Melania.
“Nashukuru!”
“Kwa hiyo tatizo ni hizo picha tu?”
“Ndiyo!”
“Basi haina shida! Unataka tuzifanye nini?”
“Zifutwe kwenye kompyuta yake, hilo tu!”
“Aliziweka kwenye barua pepe tu au hadi kwenye kompyuta yake kwenye mafaili?” aliuliza William.
“Sijajua. Ila nahisi kotekote!”
“Basi itabidi nikutane naye, kama sitokutana naye nitahitaji mambo kadhaa! Nitahitaji nijue kompyuta yake ni ya aina gani, ina namba zipi, nataka nifahamu kila kitu kuhusu hiyo kompyuta,” alisema William.
“Mmh!”
“Ni kazi ngumu kupata vielelezo hivyo?”
“Nitajaribu! Ila nikivipata matatizo yatakuwa yamekwisha?” aliuliza Melania, William hakujibu chochote, akaachia tabasamu pana lililojibu swali lake kwamba ingewezekana kwa asilimia mia moja.
“Ila nyingine anaweza kuwa nazo kwenye simu!”
“Napo si tatizo! Nitaizima simu yake. Una namba yake?”
“Ninayo!”
“Naiomba!” alisema William na kupewa namba hiyo.
Akaondoka kuelekea chumbani kwake. Melania akabaki sebuleni, hakujua kitu gani kingeendelea, wakati yote yakiendelea, Michael alikuwa kimya tu, uso wake ulikuwa na tabasamu na aliamini kwa kitendo chake cha kumpeleka msichana huyo kwa William basi kila kitu kingefanikiwa kwa kuwa alimuamini sana.
“Ila ataweza!” aliuliza Melania huku akionekana kuwa na hofu.
“Huyu jamaa ni balaa! Utaona, kwanza anaanza kuizima hiyo simu!” alisema Michael.
Baada ya dakika kadhaa William akarudi sebuleni hapo, alipofika, akaiweka laptop yake mezani na kuwaita watu hao na kukaa nao. Akaiwasha na kisha kuziingiza namba ya simu ya Nicolaus kwenye kompyuta yake.
Hawakujua alifanya nini, walimuona akiichezea kompyuta yake kwa kuingia huku na kule, zilitokea namba zilizokuwa zikipata juu, zilikuwa zaidi ya milioni moja na zilikuwa zikibadilika kwa haraka sana.
Hizo zilikuwa codes na alikuwa akitaka kuingia kwenye simu ya Nicolaus kilazima. Alipoona kwamba nayo simu ilikuwa na ulinzi mkali, akachukua virusi vyake vya Wirus na kuviingiza, vilipoingia tu, codes zikabomolewa na kuingia kwenye simu hiyo.
“Simu yake si ndiyo hii?” aliuliza William huku akiwaonyeshea. Melania alipoangalia majina yaliyokuwepo na vitu vingine, aligundua kwamba ilikuwa ya Nicolaus.
“Ndiyo!”
“Tupo ndani ya simu yake! Unataka tufanye nini?”
“Zitafute zile picha, kama zipo, zifute!”
“Sawa.”
Hiyo haikuwa kazi hata kidogo, akaanza kuzitafuta picha hizo, mbali na picha hizo, akazipata picha ambazo Nicolaus alipiga na laptop yake, kwa sababu alihitaji sana kuijua laptop ya Nicolaus na ndiyo ilimfanya kutaka kusafiri kwenda huko alipokuwa, alichokifanya ni kuzichukua picha hizo ambazo akazipeleka Google na kuhitaji kufahamu aina ya laptop hiyo, ikaletwa na kugundua kwamba ilikuwa Acer Chromebook 14 CW10.
“Safi sana! Kazi nyepesi mno!”
Akazichukua namba hizo na kuziingiza katika kompyuta yake na hapohapo kuingia kwenye laptop ya Nicolaus. Kazi ilikuwa nyepesi, hakuhitaji kuhack akaunti yake ya Google kwani aliingia kwa kupitia kompyuta ileile ambapo huko akazikuta zile picha, akazihamisha, kule akazikata kabisa na kuyafunga mafaili.
Alipomaliza akahamia kwenye kompyuta yenyewe, akazihamisha picha hizo kwa kuzifuta kabisa, hakuridhika, akaingia kwenye simu na kisha kuzifuta picha zote, mbaya zaidi akaviingiza virusi vyake vya Wirus ambavyo pia vilifuta majina yote kwenye simu hiyo.
“Hivi virusi vitaendana na picha. Melania nyoosha mkono, kiweke kidole cha kati juu nikipige picha,” alisema William na hapohapo Melania kufanya kama alivyoambiwa, picha ikapigwa na kisha kutumwa kwenye simu ya Nicolaus na kwenye barua pepe yake ili pale atakapofungua, kitu cha kwanza kabisa kukiona kilikuwa ni kidole cha kati cha Melania kilichokuwa kimesimama dede.
“It is done,” (Kazi imekwisha) alisema William na kuweka miguu juu ya meza huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumamosi mahali hapa.
KuSHARE kwako kunaweza kukufanya ukapata sehemu ijayo kabla ya siku husika.
Post a Comment