ad

ad

FUTA MACHOZI MPENZI-04

 
NYEMO CHILONGANI
ILIPOISHIA
Msiba ukafanyika, mzee huyo alihuzunika na kulia, katika kipindi chote alichoishi na mke wake, waliishi kwa upendo mkubwa, alimpenda na kumthamini na kwake alikuwa kila kitu katika maisha yake. Wakamzika katika makaburi ya Kinondoni na baadaye kuamua kuishi na Pamela kitu kilichompa amani na furaha msichana huyo.
SONGA NAYO

“Oya! Umemuona yule mtoto?” aliuliza jamaa mmoja aliyekuwa kwenye daladala, alikuwa akizungumza kwa sauti ya chini kuhakikisha abiria wengine hawasikii.
“Mtoto gani?”
“Yule aliyebebwa na yule mwanamke!”
“Duuh! Huyu binadamu au nyani?” aliuliza jamaa huyo aliyeambiwa amwangalie mtoto huyo.
“Shiiiiii....atasikia..” alisema jamaa huyo.
Mwanamke mmoja masikini aliyevalia kitenge kilichochakaa kilichokuwa juu ya dela kuukuu alikuwa ndani ya daladala moja iliyokuwa ikitoka Gongo la Mboto kuelekea Makumbusho.
Mwanamke huyo aliyeonekana kupigwa na maisha alikuwa amembeba mtoto wake ambaye alikuwa gumzo ndani ya daladala hiyo kutokana na ubaya wa sura yake. Kila abiria alimshangaa, alitisha, watu wengi walihisi mwanamke huyo alimbeba nyani mpaka pale mtoto alipoanza kulia na kugundua kwamba alikuwa binadamu.
Aliwashangaza watu wengi, hawakujua tatizo lilikuwa nini mpaka mtoto huyo kuwa na sura mbaya namna ile. Wapo waliokuwa wakicheka na wengine kujisikia vibaya, japokuwa mara nyingine aliwasikia abiria wakimcheka mtoto wake, alinyamza lakini moyo wake ulikuwa na maumuvu makubwa mno.
Hilo ndilo lililomtesa, tangu alipomzaa mtoto huyo, kila kitu kilionekana kubadilika. Mumewe ambaye naye alikuwa masikini alipoona mkewe amezaa mtoto mbaya namna ile, akaamua kumkimbia na kumuacha peke yake akiteseka.
Maisha yalimpiga, hakuwa na kazi yoyote zaidi ya kuuza genge katika Mtaa wa Tandale kwa Tumbo alipokuwa akiishi. Mtoto wake alikuwa gumzo kila kona, wengi walipenda kumwangalia na kumcheka kwa jinsi alivyokuwa na sura mbaya.
Watoto na watu wazima mitaani walimtumia mtoto huyo kuwa tusi kwa wengine kwani kila aliyeambiwa ana sura mbaya kama mtoto huyo alichukia na kupigana. Mama wa mtoto huyo alidharaulika, na si kwa sababu alikuwa masikini, pia kwa sababu ya ubaya wa sura ya mtoto wake.
Mpaka anateremka katika kituo cha Tandale Kwa Tumbo, watu walikuwa wakimwangalia, gumzo humo ndani lilikuwa ubaya wa sura ya mtoto yule ambaye kila alipokuwa akilia, ubaya wake uliongezeka na kumtisha kila mmoja.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake, yalimuumiza lakini hakuwa na jinsi. Wakati mwingine alikuwa akimuuliza Mungu kwa nini aliamua kumpa mtoto wake sura mbaya kiasi kile lakini hakupata jibu lolote lile.
Ilipombidi kulia, alilia sana lakini kamwe hakutaka kumtelekeza mtoto wake, aliamini kwamba Mungu alikuwa na makusudi yake, kwa nini mtoto huyo asingepewa Bakhresa? Kwa nini mtoto huyo asingepewa Mengi? Kwa nini Mungu aliamua kumpa yeye mtoto huyo na wakati alijua kwamba alikuwa masikini? Alijua Mungu alikuwa na sababu ambayo ndiyo iliyomfanya kusubiri na kuona ni kitu gani kingetokea.
Maisha yaliendelea kumpiga kila siku, alipambana, alikuwa radhi kukosa chakula lakini si kwa mtoto wake ambaye aliendelea kukua zaidi na zaidi na alipofikisha umri wa miaka mitatu, akamuanzisha shule ya chekechea.
Siku ya kwanza kufikishwa shuleni hapo, watoto wengine wakaanza kulia, walimuogopa, walimkimbia kitu kilichomfanya kumuumiza mno moyoni mwake. Machozi yalimtoka mbele ya mwalimu, kwa sababu watoto wengine walikuwa wakiogopa, akaamua kuondoka naye, hakutaka kumpeleka shule tena, aliona ni bora angekaa naye nyumbani tu.
Mtaani, mtoto huyo aliyeitwa William alionekana kuwa kituko, watoto wenzake hawakutaka kucheza naye kwa sababu walimuogopa mno. Yeye mwenyewe hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea, hakujua kama sura yake ndiyo iliyokuwa ikiwatisha watoto wengine.
Siku zikaendelea kukatika, miezi ikasonga mbele na alipofikisha umri wa miaka minne, mama yake, Sophia akakutana na mwanaume mmoja, hakumfahamu, ilikuwa mara yake ya kwanza kumtia machoni.
Mwanaume huyo alikuwa akipita mtaani kwao, alikuwa ameshika brifukesi, alionekana kuwa na haraka mno ya kuelekea ofisini kwake. Alipokaribia na genge la Sophia, akamwangalia mwanamke huyo na mtoto aliyekuwa pembeni yake, ghafla akasimama na kugeuka na kumfuata mwanamke huyo.
Sophia alishangaa, hakumjua lakini kwa jinsi alivyokuwa akimfuata, uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana kana kwamba alikuwa akimfahamu mwanamke huyo, alipomfikia, akamsalimia na kisha kuinama na kumwangalia William.
“Huyu ni mtoto wako?” aliuliza mwanaume huyo aliyevalia nadhifu.
“Ndiyo!”
“Aisee! Una bahati sana,” alisema mwanaume huyo.
“Nina bahati! Ya nini?” aliuliza Sophia huku akimshangaa mwanaume huyo.
“Una mtoto mzuri sana,” alisema mwanaume huyo huku akiachia tabasamu.
Alichokuwa akikisema, alimaanisha kutoka moyoni, uso wake ulikuwa na tabasamu pana na kila Sophia alipomwangalia mwanaume huyo, aliona tabasamu lile ambalo lilitoka kwa dhati kutoka moyoni mwake.
“Unamaanisha nini?”
“Huyu mtoto ni mzuri! Ana akili sana!” alisema mwanaume huyo.
“Ana akili?”
“Ndiyo! Ni mtoto mwenye uwezo wa ajabu sana. Unalijua hilo?” aliuliza mwanaume huyo huku akiendelea kumwangalia William, kwake, mtoto huyo alionekana wa tofauti.
“Unamaanisha nini!”
“Mtoto wako ni mzuri, ana akili sana, nahisi Mungu aliamua kukupa huyu mtoto kwa makusudi yake, usimlalamikie Mungu. Hajawahi kuumba mtu mbaya, kila anapokaa na kumwangalia mtoto wako, anajisifia kwamba ametengeneza kitu kizuri sana kiasi kwamba anaweza kuwa sehemu na kujisifia kwamba miongoni mwa watu aliopatia kuwaumba, wa kwanza huyu mtoto,” alisema mwanaume huyo maneno yaliyomchanganya sana Sophia.
“Sijajua unamaanisha nini?”
“Kuna siku utajua namaanisha nini! Ninachotaka ujue ni kwamba Mungu kila anapomwangalia mtoto wako, anajivunia kwa kufanya kazi nzuri,” alisema mwanaume huyo, alipomaliza, akasimama, akachukua shilingi elfu kumi kutoka mfukoni mwake na kumkabishi Sophia kisha kuondoka mahali hapo.
Moyo wake ukawa na furaha, hakuamini kile alichokisikia kutoka kwa mwanaume huyo. Moyo wake ulikata tamaa, kila alipomwangalia mtoto wake, alimlaumu Mungu kwa kumpa mtoto mwenye sura mbaya kama aliyokuwa nayo.
Akamuinamia William na kumkumbatia. Moyo wake ulikuwa na faraja ambayo hakuwahi kuisikia tangu alipomzaa mtoto huyo. Mume wake alimkimbia kwa sababu ya William, alipoteza ndugu zake kwa sababu ya mtoto huyo, kwake, ndiye alikuwa faraja yake na hakujua sababu iliyomfanya Mungu kumchagua mto to huyo na kuwa uzao wake.
“Ninakupenda mwanangu! Nakupenda sana,” alisema Sophia na kumkumbatia mtoto wake huku machozi ya furaha yakimtoka machoni na kutiririka katika mashavu yake.
Maneno yale yakamtia nguvu ya kusonga mbele, alimuona mtu huyo kama malaika ambaye aliyatabiri maisha ya mtoto wake hapo baadaye. Nguvu yake ya utafutaji ikaongezeka na kila siku alihakikisha anakuwa karibu na mtoto wake huyo.
Miaka ikakatika na alipofikisha miaka saba akaamua kwenda kumuanzisha Shule ya Msingi ya Hekima iliyokuwa hapohapo Tandale. Japokuwa hakuwa amesoma chekechea lakini aliamini kwamba Mungu angempa nguvu mtoto wake kusonga mbele na kufanya vizuri shuleni hapo.
Wanafunzi wengi walimshangaa, mbele ya macho yao alionekana kuwa kituko kiasi kwamba wanafunzi wa darasa la saba wakaamua kumuita jina la Zinjathropus, jina ambalo kwa kipindi hicho hakujua lilikuwa na maana gani.
Kila kona, aliitwa kwa jina hilo, hakujua wanafunzi hao walimaanisha nini, alilipenda kwa sababu lilionekana kuwa jina zuri la Kiingereza au Kigiriki, hivyo kwake ikawa sifa kubwa.
Hakuwa amesoma chekechea lakini yeye ndiye alikuwa mwanafunzi wa kwanza kujua kusoma vizuri na kuandika. Walimu walimshangaa mno, hakuonekana kuwa mwanafunzi wa kawaida.
Alipenda hesabu, alipenda kuzifanya kila wakati, uwezo wake haukuishia kwenye hesabu tu, alifanya vizuri katika masomo yote kitu kilichomfanya Sophia kusikia faraja kila siku katika maisha yake.
Miaka ikakatika, ikasonga mbele, akaingia darasa la saba. Mpaka kufikia hapo, alijulikana na wanafunzi wote wa shule za msingi zilizokuwa katika Wilaya ya Kinondoni. Alikuwa ndiye kichwa chao, katika mitihani yote iliyokuwa ikijumlisha shule zote za Wilaya ya Kinondoni, yeye ndiye alikuwa akifanya vizuri.
Hakuliacha jina la Zinjathropus, alitambua kwamba alikuwa mbaya wa sura, alilipenda jina hilo ambalo aliendelea kukua nalo huku kwenye kila daftari lake akiliandika jina hilo kwa ukubwa zaidi na kuonekana.
“Kwa nini umelipenda jina hili?” alimuuliza rafiki yake, Omari.
“Kwa sababu ni zuri na linaendana nami! Si unaona nilivyo mbaya,” alisema William huku akitoa tabasamu lililoufanya ubaya wake kuongezeka maradufu.
“Hapana! Huendani nalo! Unatakiwa kuitwa Bill Gates!”
“Kwa nini?”
“Kwa sababu wewe ni genius sana! Badilisha jina, jiite Bill Gates,” alisema Omari.
“Hapana! Nalitaka jina hilihili,” alisema William huku akimwangalia Omari.
Siku zikaendelea kukatika, japokuwa alikuwa na sura mbaya shuleni hapo lakini wanafunzi wengi walikuwa wakimfuata wakitaka kufundishwa masomo mbalimbali. Kwa William hilo halikuwa tatizo, alikuwa mtu wa kujitolea kiasi kwamba aliwafanya wanafunzi wengi kumpenda kwa kile alichokuwa akikifanya shuleni hapo.
Walimu walimpenda, walimtaka kila mwanafunzi kuiga kile alichokuwa akikifanya, uwezo wake uliendelea kuwashangaza watu wengi na kulifanya jina la Zinjathropus kukua kila siku na hata kulifunika jina lake la William.
Baada ya kukaa kwa miezi kadhaa na kuingia darasa la saba, mitihani ya taifa ikafanyika, hakuonekana kuwa na hofu, aliamini kabisa kwamba alikuwa akienda kufanya vizuri katika mitihani hiyo.
“Zinjathropus aongoza Tanzania...” aliisikia sauti hiyo kichwani mwake, sauti ililolifanya tabasamu pana kuonekana usoni mwake.

Je, nini kiliendelea?
Je, nini kitatokea katika maisha ya William na Melania?

No comments

Powered by Blogger.