Diego Costa: Silizimii Soka la England

MSHAMBULIAJI wa Chelsea, Diego Costa, ameonyesha kuwa anaweza kuondoka
kwenye timu hiyo wakati wowote, aliposema kuwa analichukia soka la
England.
Kocha wa timu hiyo Antonio Conte, alimuondoa mshambuliaji huyo kwenye
kikosi chake kilichovaana na Leicester City wikiendi iliyopita kwa kile
kilichodaiwa kuwa alikorofishana na mmoja kati ya makocha wa timu hiyo.
Costa, 28, yupo kwenye mkataba na timu hiyo hadi mwaka 2019 na Chelsea
waligoma kumuuza kwenye usajili wa majira ya joto yaliyopita, lakini
sasa inaonekana kuwa anaweza kuondoka.
Taarifa zinasema kuwa Conte atakuwa na kikao na mchezaji huyo kesho kujadili kuhusu sakata hilo.
“Diego alifanya mazoezi Jumanne na kusikia maumivu kwenye nyama za
miguu, hakufanya mazoezi tena na kwa sababu hiyo akakosekana kwenye
mchezo uliopita,” alisema kocha huyo.
Gazeti la SunSport limeripoti kuwa linajua mchezaji huyo alikorofishana
na kocha wa viungo mazoezini na wakala wake amekuwa akipambana sasa
kuhakikisha kuwa anamtafutia timu nchini China.
Inaelezwa kuwa aliwaambia wenzake kuwa atafanya kila linalowezekana ili
aondoke kwenye timu hiyo kwa kuwa analichukia soka la England pamoja na
Chama cha Soka England (FA).
Chanzo kutoka nchini China kimesema: “Costa ni chaguo la kwanza hapa, tunajua kuwa anataka kuja kucheza huku.”
Post a Comment