KIFO CHA MTU ASIYE NA HATIA - 04

“Naam daktari!”
“Nafikiri sasa hivi hali yako ni nzuri kidogo inabidi urudi nyumbani uje baada ya mwezi mmoja ili tuone kama tutaweza kukufanyia operesheni!”
“Sawa daktari lakini......!”
“Kwani vipi Belinda?”
“Wifi zangu hawajaja kuniangalia tena, nina wasiwasi wanaweza wakawa hawataki niende tena kwao!”
“Sasa tufanye nini?”
“Daktari ungeniacha tu nikae hapa wodini!”
“Belinda haiwezekani kukaa wodini siku zote hatuna vitanda kabisa! Nakuomba tu uende nyumbani na urudi baada ya muda huo, hali yako inaendelea vizuri!” Alimaliza daktari na kuhamia kitanda cha mgonjwa mwingine.
Belinda alijikunja kitandani na kumkumbatia mtoto wake Alikuwa ni mtoto mzuri aliyefanana na baba yake Prosper kwa kila kitu.
Belinda alishindwa kuelewa angepokelewa vipi nyumbani na watu ambao walimfikisha tu hospitali na kuondoka zao! Lakini hakuwa na mahali pengine kwa kwenda mkoani Tabora zaidi ya kurudi Tutuo, siku ya Jumatatu asubuhi alimbeba mtoto wake mgongoni na kuondoka hospitali.
Alikuwa akichechemea kwa sababu mguu wake bado ulikuwa hauna fahamu vizuri pamoja na kufanya mazoezi kwa muda mrefu, hakuwa na nauli alichechemea hadi kituo cha mabasi ambako badala ya kupanda basi la kwenda Tutuo aliomba msaada katika basi la kwenda Isanga gerezani, hakuwa mvumilivu siku hiyo ipite bila kumwona Prosper! Alikuwa amemkumbuka mno na alitaka Prosper amwone mtoto wao.
“Mh! Jamani humu ndani kuna mtu amebeba samaki waliooza nini?” Mmoja wa abiria aliuliza, hali ya hewa ndani ya basi alilopanda ilikuwa nzito sababu ya harufu.
Belinda alijua harufu hiyo ilitokanana na nini lakini hakutaka kuwaeleza ukweli, swali hilo la abiria lilimuumiza sana moyo wake akajikuta akilia! Nguo zake zote zililowa mkojo uliotoka bila fahamu zake sababu ya tundu alilotoboka wakati wa kujifungua.
Aliposhushwa kituo cha gerezani Isanga abiria wote waligundua kuwa harufu ile ilitokana na yeye, kwani waliona nguo zake zikiwa zimelowa mkojo.
“Hiloooo! Kubwa zima linajikojolea!” mpiga debe wa gari alimzomea.
Belinda aliumia sana moyo wake na kujikuta akilia machozi, hakupenda kuwa alivyokuwa ilikuwa ni bahati mbaya katika maisha, alikuwa ni mtoto wa tajiri kuliko mpiga debe aliyemzomea.
Alichechemea hadi gerezani ambako alijitambulisha kwa maaskari kama mke wa mfungwa Prosper, maaskari walimwambia siku hiyo ilikuwa si ya kuwaona wafungwa lakini alipowaeleza hali halisi iliyotokea na kwamba alikuwa akitokea hospitali maaskari walimwonea huruma na kumwingiza katika chumba alichokutana na Prosper mara kwa mara kabla ya kuugua na kulazwa hospitalini!
“Subiri tumwite!”
“Ahsante nasubiri!” Belinda alijibu.
Dakika chache baadaye Prosper aliingia chumbani akiongozana na mwanaume mwembamba mrefu aliyekuwa amemshika kiunoni, mtu huyo alionekana mgonjwa! Alikohoa mfululizo na nywele zake zilikuwa nyepesi sana kichwani, alionekana ni kama mgonjwa wa Ukimwi, Belinda alipomwangalia vizuri mtu huyo alimtambua alikuwa ni Savimbi!
Belinda alishindwa kuelewa ni kwanini Savimbi alikuwa amekonda kiasi kile lakini hakutaka kuuliza, yeye na Prosper walikumbatiana na kusalimiana kwa furaha! Ulikuwa umepita muda mrefu sana bila kuonana.
“Huyu ndiye mtoto wako nimemleta umwone! Ila alitaka kunitoa roho, nashukuru Mungu leo niko hai!”
“Pole sana Belinda, ninajua unateseka sana kwa ajili yangu Mungu atakulipia!”
Waliongea mengi yaliyopita katikati yao, wakati Savimbi aliendelea kukohoa mfululizo na jasho jingi likimtoka! Hatimaye aliamua kutoka nje kwenda kupunga upepo.
“Kipenzi changu Pros, nipo nje napunga upepo mama!” Savimbi alisema na kunyanyuka kisha akampiga busu Prosper usoni na kutoka nje.
Belinda alipata uhakika wa kilichokuwa kikiendelea kati ya Prosper na Savimbi, alishindwa kujizuia na kuanza kulia mbele ya Prosper.
“Prosper tafadhali niambie ukweli nini kinaendelea kati yako na Savimbi nimejiuliza maswali mengi sana leo naomba unipe majibu!”
Prosper alimwangalia Belinda kwa macho ya huruma, alionekana mnyonge, alionekana kuwa na kitu moyoni alichotaka kukisema lakini alishindwa aanzie wapi.
“Tafadhali niambie Prosper vinginevyo mimi nakuacha narudi Dar es Salaam kwa baba yangu!”
“Usifanye hivyo Belinda!”
“Basi niambie!”
“Ninaweza kukuambia lakini tafadhali niahidi kitu kimoja!”
“Kitu gani?”
“Kwamba utanifichia siri na hutaniacha!”
“Itategemea Prosper! Lakini ni lazima unieleze vinginevyo naondoka nina wasiwasi kuna uhusiano mbaya kati yako na Savimbi kweli sio kweli?”
“Ni kw...eli Beli...nda! Nisa..mehe Beli..nda, Savi..mbi alinis..hawishi, alijifanya msamaria kwangu akawa ananipa chakula kizuri chenye mafuta, sukari nikafikiri ni mtu mwema lakini siku moja usiku niliamka na kukuta.....!”
Prosper aliingia gerezani kwa kosa la mauaji ambalo hakulifanya! Ni mama yake aliyemuua baba yake lakini ili kumtoa mama yake kifungoni, prosper alikwenda polisi na kusema ni yeye aliyemuua baba yake ingawa wakati wa tukio hakuwepo.
Prosper yuko gerezani ambako amekutana na jambazi Savimbi na kufundishwa mchezo usiostahili, Belinda mpenzi wa prosper waliyezaa naye mtoto mmoja ameligundua hilo la kumuomba Prosper aeleze ukweli! Prosper anakubali kueleza ukweli kwa sharti la kutoachwa na Belinda, je Belinda atachukua hatua gani? Fuatilia...
Huku akilia machozi Prosper aliendelea kumsimulia Belinda kila kitu kilichotokea kati yake na Savimbi ndani ya gereza, lilikuwa jambo la aibu lakini alilazimika kuliweka wazi kwa sababu Belinda alitoka kufahamu.
“Ni kweli Belinda nisam...ehe mwenz’...angu, nisamehe mke wangu mtarajiwa, ni kweli Savimbi ananifanyia kitendo hiki! Alijifanya mweka kwangu tulipoingia gerezani akawa ananipa chakula kizuri, sukari, maji ya kunywa na kila nilipotaka kupigwa na wafungwa alinikingia kifua kwani mie ndiye nilikuwa mfungwa mdogo kuliko wote kwa wakati huo! Kumbe alikuwa na nia mbaya ambayo mimi sikuifahamu tangu awali, hakuacha kunisifia eti nilikuwa na sura na umbile zuri, lakini mimi sikujali nilichukulia kitu cha kawaida kumbe alinitamani kimapenzi!”
“Halafu ikawaje?”Aliuliza Belinda kwa mshangao.
“SIku moja usiku nilizinduka usingizini na kumkuta akinipapasa mwili wangu, nilinyanyuka na kukaa huku nikimuuliza ni kitu gani alichotaka kufanya ndipo aliponieleza wazi kuwa alinitaka mapenzi mimi mwanaume mwenzake!”
Belinda alibubujikwa na machozi ya uchungu wakati akisikiliza maelezo ya Prosper jambo alilokuwa akilisikiliza haikuwa mara yake ya kwanza kulisikia alishalisikia kabla na alihisi lingekuwepo kati ya Prosper na Savimbi.
“Siku alipofanya hivyo ilikuwa ni usiku na wafungwa wote walikuwa usingizini, hakuna mtu aliyesikia kitu chochote, nilinyanyuka na kuanza kukimbia kwenda nje ambako Savimbi alinifuata na kuendelea kunishika ili aniingilie kwa nguvu.
“Aliweza?”Belinda hakuwa mvumilivu, alitaka kujua ni kitu gani kilitokea ingawa hakutaka kabisa mwisho wa habari hiyo uwe Prosper kufanya kitendo hicho.
“Hapana!”
“Afadhali, ulifanya kitu gani kujiokoa?”
“Nilichukua ubao mkubwa uliokuwepo na kumpiga nao usoni akaanguka chini na damu nyingi zikamtoka!”
“Kwa hiyo hakukufanya kitu?”
“Siku hiyo ndiyo! Lakini asubuhi kulipokucha Savimbi alikuwa amenichukia sana hakusema na mimi kitu chochote na aliniambia kuwa ningekiona cha mtema kuni! Asubuhi hiyo sikupata chai aliyokuwa akinipa kila siku pia sikupata chakula wala maji! Usiku ulipoingia nililala sakafuni kwani alininyang’anya godoro lake, hiyo haikutosha siku iliyofuata alitoa taarifa kwa mkuu wa gereza kuwa mimi nilimpiga kichwani na ubao baada ya kugoma kupasua kuni kitu ambacho hakikuwa kweli, kwa sababu yeye Savimbi alikuwa nyampara alisikilizwa zaidi na mkuu wa gereza kuliko mimi!
“Walikufanya nini baada ya hapo?”
“Nikaadhibiwa kwa kupigwa viboko ishirini na ni Savimbi huyohuyo aliyenichapa., niliumia sana!”Alisema Prosper kwa sauti ya upole.
“Pole sana Prosper sikujua kama ulipata mateso hayo yote sasa kwa nini hukuniambia?”
“Hukuwepo darling wakati huo wewe ulikuwa bado upo shule ulikuwa hujaja hapa Tabora!”
“Kiliendelea kitu gani baada ya hapo?”
“Gereza liligeuka Jehamanu kwangu! Nilifanyishwa kazi ngumu, niliteswa kwa kunyimwa chakula na hata maji ya kunywa na katika muda wote wa mateso hayo Savimbi akawa anamhudumia kijana mwingine mwenye umri sawa na wangu ambaye aliingizwa gerezani muda mfupi baada ya mimi kukataa.Kila mara Savimbi alinifuata na kuniambia kuwa nikitaka kuishi vizuri gerezani ilikuwa ni lazima tu nikubaliane na matakwa yake, bado nilikataa!”
“Hongera sana Prosper!”
“Ahsante lakini ngoja kwanza nimalizie kukusimulia kila kitu Darling!”
“Haya endelea?”
“Mwezi mmoja tu baadaye nilishangaa kuona savimbi akirejesha huduma zake kwangu tena! Nilishindwa kukataa kwa sababu ya shida na nikawa nakula chakula kizuri tena, akanipa godoro na kunipunguzia kazi gerezani, maisha yakawa mazuri, hakunieleza tena juu ya kufanya kitendo hicho lakini siku moja alinipa chai ya rangi jioni, baada ya kuinywa chai hiyo mwili ulilegea na nikapitiwa na usingizi na kumkuta Savimbi akinifanyia viba......!” Prosper alishindwa kumalizia sentensi yake na kuanza kulia, belinda nae alishindwa kuvumilia na kuanza kulia akiwa na mtoto wake mkononi!
“Nisamehe sana mke wangu! Nisamehe Belinda! Nililazimika kufanya hivyo kwa sababu ya shida, yalikuwa ni mateso makali mno!”Alisema prosper akiwa ameinamisha kichwa chini.
“Nini kilifuata?”
“Na baada ya hapo tuliendelea kufanya hivyo mara kwa mara, nisamehe belinda lakini pamoja na hayo yote bado nakupenda wewe pamoja na mtoto wangu na nitabadilika!”
“Prosper! Prosper! Ulishindwa nini kuvumilia mpenzi? Huwezi kuwa mwanaume wa kawaida tena!”Alisema Belinda huku akilia.
“Hapana Belinda nipo kawaida na ninakuahidi kubadilika na kama ikatokea nikatoka gerezani tuendelee na maisha yetu!”
“Prosper umeniumiza sana! Na kwa heri ya kuonana!”Alisema Belinda na kuanza kusimama wima alitembea hadi nje bila kugeuka nyuma, machozi yaliendelea kumbubujika na kulowanisha nguo zake, alikuwa ameumia kupita kiasi, hakutegemea kama mwanaume aliyempenda angeweza kutenda jambo hilo! Aliumia kiasi cha kuusahau hata ugonjwa uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu!
“Belinda! Belinda! Belinda! Tafadhali rudi mpenzi nisamehe sitafanya tena jambo hili!” Alimsikia Prosper akisema wakati akitoka nje ya gereza lakini hakutaka hata kuangalia nyuma! Kila alipoikumbuka picha ya Savimbi amemkumbatia mume wake alizidi kupata uchungu zaidi.
“Narudi kwa baba yangu siwezi tena kukaa hapa kama tu anayenisababishia mimi shida hizi ndiye aliyenifanyia ukatili huu!” Alisema Belinda wakati akitoka gerezani.
Hakuwa na nauli ya kulipia usafiri wa gari kutoka gerezani Isanga hadi Tabora mjini na isitoshe hakutaka kusababisha usumbufu kwa abiria kwa harufu aliyokuwa nayo hivyo aliamua kutembea kwa miguu mpaka mjini ulikuwa ni umbali mrefu lakini Belinda hakujali.
Maisha ya Belinda wakati huo yalikuwa tofauti sana na alivyokulia, hakuwahi hata siku moja kutegemea angekuja kuishi maisha ya taabu kiasi hicho wakati nyumbani kwa baba kulikuwa na kila kitu, lakini hiyo ndiyo hali aliyokuwa nayo.
Alitembea kama kilometa tano katika barabara ya vumbi mtoto wake akiwa mgongoni na mfuko wa rambo uliojaa nguo zake ukiwa mkono wake wa kushoto! Miguuni hakuwa na kiatu na miguu yake ilichanika ilikuwa si rahisi hata kidogo kufahamu kuwa Belinda alikuwa ni miongoni mwa watoto wa matajiri nchini Tanzania.
“Piiii! Piiii!Piii!” ilikuwa ni honi ya gari ikipigwa nyuma yake Belinda alikuwa akitembea katikati ya barabara bila kufahamu aliruka na kuangukia pembeni mwa barabara, dereva wa gari lile aliyempakia mwanamke aliyeonekana kuwa mkewe alimuonea huruma Belinda na kulazimika kukanyaga breki gari likasimama ghafla.
“Pole binti!”Alisema dereva baada ya kugundua kuwa alimshtua Belinda.
“Ahsante sana na samahani dereva!” Alisema belinda huku akijaribu kunyanyuka ardhini.
“Unakwenda wapi binti?”
“Nakwenda mjini Tabora!”
“Basi twende!”
“Hapana nyie nendeni tu mimi nitatembea kwani nina matatio!”
Belinda alikataa katakata kupanda ndani ya gari pamoja na dereva aliyeonekana kuwa mzee wa makamo kuendelea kumsisitia Belinda apande kitu cha nyuma cha gari na alipoona Belinda hataki kusikia aliteremka akachukua mzigo wake na kuuingiza ndani kisha akafungua mlango na kumwomba Belinda aingie, alifanya hivyo kwa shingo upande na safari ikaanza.
“Jamani samahani kama hali ya hewa itachafuka kidogo hapa ndani nina tatizo nililolipata wakati nilipojifungua!”
“Tatizo gani?”
“Nilitoboka tundu!”
“Aha! Una VVF siyo?”Mwanamke aliyekaa upande wa kushoto kwa dereva aliuliza.
“Ndiyo!”
“Usijali hili ni tatizo la kawaida tu kwa mwanamke hata mimi linaweza kunipata jisikie vizuri binti mimi naitwa Dk. Zubeda Katunzi ninafanya kazi hospitali ya Kitete wodi ya watoto na huyu ni mume wangu anaitwa Bwana Katunzi Katagile yeye ni afisa mifugo wa mkoa wa Tabora! Pole sana!”
“Ahsante mama!”
“Huyu ndiye mtoto wako wa kwanza?’
“Ndiyo!”
“Alikuwa mkubwa sana wakati wa kujifungua eeh ndiyo sababu akakusababishia tatizo?”
“Hapana alitanguliza mkono!”
“Mkono? hukuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito wako?”
“Sikuwahi kwenda hata siku moja!”
“Pole sana na huku umetoka wapi?”
“Nimetoka gerezani ambako baba wa mtoto huyu ameshinikiliwa!”
“Pole sana na alifanya nini?”Mzee Katunzi Kategile aliuliza.
“Wanasema alimuua ma..ma ya....ke!”Belinda alishindwa kujizuia na kuanza kulia tena.
Mzee Katunzi na mke wake waliendelea kumbembeleza wakati gari likiendelea na safari mpaka Belind aliponyamaza. walimuomba awaeleze zaidi juu ya kilichotokea!
“Kwa hiyo wewe ni mtoto wa mzee Thomson.
“Ndiyo!Mimi ndiye mtoto wake wa kwana!”
“Oh my God! Why did Thomson do this?(Oh Mungu wangu kwanini Thomson alifanya jambo hili?) Alisema Dk. Katunzi.
“Hata mimi mwenyewe sifahamu!”
“Tunamfahamu baba yako sana na mara kwa mara huwa tunaonana naye Dar es salaam unataka tukusaidie nini binti?”
“Nataka kurudi kwa baba sitaki kitu kingine tena, nisaidie nauli ya treni ili niondoke siku yoyote kurudi Dar es Salaam!”Aliendelea kusema Belinda huku akilia machozi.
Gari lilikuwa likiingia mjini Tabora mzee Katunzi na mkewe walikuwa kimya gari liliendeshwa hadi nyumbani kwao eneo la Kanyenye mjini Tabora kitu cha kwanza walichofanya baada ya kuuingia ndani ni kumpigia simu mzee Thomson nyumbani kwake Dar es Salaam ili kumuuliza kama alikuwa na mtoot aliyeitwa Belinda.
“Belinda?”
“Ndiyo na tena ana mjukuu wako?”
“Hakuna mtoto mwenye jina hilo hapa kwangu, mzee Thomson alikata simu kwa makusudi ingawa alimfahamu Belinda alikuwa bado na hasira kali kwa Belinda baada ya kupata mimba na alijazwa maneno mengi ya chuki kutoka kwa mama wa kambo wa Belinda.
“Wewe msichana umetudanganya siyo?”
“Kwanini?”
“Mbona mzee Thomson anakataa?”
“Hapana huyo ni baba yangu kabisa!”
“Wewe ni tapeli?”
‘Hapana kama hamuamini nipeni simu mimi niongee naye!”Belinda alisema lakini hakuruhusiwa kuigusa simu.
“Tunasikitika hatuwezi kukusaidia kitu chochote binti!”
“Baba nisaidie tafadhali, nisaidieni kama mtoto wenu!”Alisema Belinda.
Mzee Katunzi na mkewe walimuonea huruma Belinda na kuamua kumsaidia pesa ya nauli kumrudisha Dar es Salaam peke yake na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani siku iliyofuata Belinda alikuwa ndani ya behewa daraja la tatu akielekea Dar njia nzima alilia machozi, aliumia sana kusikia baba yake alimkataa, pamoja na hayo bado alikuwa ameamua kwenda kuonana naye na kuomba msamaha!
Alijingia Dar saa 12 ya jioni na treni la abiria, kwa pesa kidogo iliyokuwa imebaki alikodisha teksi na kwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwao.
“Niteremshe hapa hapa!” Alimwambia dereva teksi na kisha akamlipa pesa yake.
Baada ya teksi kuondoka alinyoosha moja kwa moja hadi getini ambako aliingia hadi ndani, watu wa kwanza kukutana nao walikuwa ni kaka zake wa kambo, walimwangalia kwa mshangao, alipowaamkia hakuitikia, waliendelea kucheza mpira wa kikapu katika kiwanja kilichokuwemo ndani ya ngome ya nyumba yao.
“Na wewe hicho kitoto chako unakipeleka wapi?” Walimuuliza Belinda kwa kejeli lakini hakuwajibu kitu alizidi kusonga mbele kuelekea nyumba kubwa waliyoishi.
Alikuwa nyumbani kwao kwa mara nyingine baada ya kukaa na kuteseka nje kwa muda mrefu, hakujua ni kitu gani kingetokea baada ya kukutana na baba yake lakini hilo hakulipa nafasi sana, alichotaka ni kukutana na baba yake na kumuomba msamaha basi!
Kabla hajaingia ndani mlango ulifunguliwa na baba yake alitoka nje na kumkuta, palepale sura yake ilibadilika.
ITAENDELEA
Post a Comment