KIFO CHA MTU ASIYE NA HATIA - 03
“Ahsante wifi, ahsante kwa kuja tafadhali utukumbuke!”
“Sawa wifi! Muangalieni sana mama sababu hali yake si nzuri!”
*****************
Belinda alichukuliwa kwa nguvu na kupakiwa ndani ya gari lililompeleka hadi Tabora ambako alisafirishwa kwa ndege ya kukodi hadi Dar es Salaam, alipokelewa na kupelekwa moja kwa moja kituo cha polisi ambako aliwekwa rumande na kukaa kwa siku tatu, alipotolewa aliendelea na adhabu nyingine kali nyumbani kwao.
Pamoja na adhabu hizo bado Belinda hakuwa tayari kueleza ukweli juu ya mahali alikokuwa, aliendelea kudanganya kuwa alikwenda kwao na rafiki yake msichana waliyesoma naye darasa moja!
“Bila kuaga?”
“Nisamehe baba!”
Na kweli Belinda alisamehewa na kuendelea na maisha kama kawaida nyumbani kwao lakini mawazo yake yote yalikuwa kwa Prosper aliyekuwa bado yupo gerezani, alimlilia na alishindwa kula kwa sababu yake! Alitamani kuwa na Prosper tena na hakujua kama katika maisha yake angeweza kumpenda mwanaume mwingine kama alivyompenda Prosper.
Belinda alikonda kwa mawazo na baba yake alimshangaa kwa mabadiliko ya afya ya mwili wake, hakuijua sababu ya tatizo hilo, alijitahidi kumpa mtoto wake kila alichotaka kama njia ya kumbembeleza akiamini Belinda alichukizwa na adhabu alizompa.
Chuo kilipofunguliwa wiki mbili baadaye Belinda alirudi tena Mlimani na kuendelea na masomo yake ya Sheria lakini kitabu kikawa kigumu kwake kwani kila alipomfikiria Prosper akili yake ilizidi kuchanganyika na kupoteza pointi.
Kitu kingine kilichomshangaza zaidi ni mabadiliko ya hali yake ya afya, alianza kujisikia mchovu kupita kiasi hasa nyakati za asubuhi, uchovu ulioambatana na kichefuchefu na alitapika sana asubuhi, matiti yake yalianza kuvimba! Mwanzoni alifikiri ni malaria lakini alipokwenda kupimwa damu yake ilikuwa safi.
Hali yake iliendelea kuwa mbaya na alipitiliza mwezi mmoja katika mpangilio wake wa hedhi! Hilo ndilo lilimchanganya zaidi hatimaye akaamua kupimwa kila kitu ndipo alipogundua kumbe alikuwa tayari ni mjamzito wa mwezi mmoja na nusu!
Belinda alichanganyikiwa, alishindwa kuelewa angemwambia nini mzee Thomson! Kila alipoufikiria ukali wa baba yake alizidi kuingiwa na hofu, alijua mzee yule angemuua, asingemwacha hai hata kidogo kwani hayo ndiyo yalikuwa maongezi yake ya kila siku.
“Mtoto wangu akipata mimba ni lazima nimpige risasi!”
Kila alipoikumbuka kauli hiyo ya baba yake alitetemeka mwili na hakujua ni kitu gani angefanya ili kujiepusha na hasira ya mzazi wake, alipoomba ushauri kwa rafiki zake walimwambia afanye kila alichoweza ili aitoe mimba hiyo kabla mambo hayajaharibika na mimba kuwa kubwa zaidi.
Jambo hilo lilimshinda Belinda, alikuwa na uhakika kabisa Prosper angenyongwa na asingemwona tena, alipenda abaki na ukumbusho wa Prosper mwanaume aliyempenda kuliko wanaume wengine wote duniani na ukumbusho pekee ulikuwa ni mtoto na Mungu alikuwa amelikubali hilo.
“Siwezi kuua mtoto wa Prosper lolote litakalokuwa na liwe!” Alisema Belinda.
Alivumilia na mimba yake chuoni mpaka ikafikisha miezi minne akawa haendi tena nyumbani kwao kila mwisho wa wiki, jambo lililowashtua ndugu zake na kuwafanya kaka zake waende shuleni kumuuliza lipi lilikuwa likimsumbua.
Ni hao ndio waliomgundua Belinda na mimba yake na bila hata kusita walizipeleka taarifa moja kwa moja kwa mzee Thomson! Belinda alihisi hilo lingetokea ni asubuhi ya siku iliyofuata tu alipopanda basi kwenda Tabora nyumbani kwao na Prosper kujificha mpaka azae mtoto wake.
******************
Belinda aliingia Tabora jioni ya saa kumi akiwa amechoka hoi bin taaban, hakutaka kupoteza muda hata kidogo mjini alipanda basi la mwisho kumpeleka hadi kijijini Tutuo! Hakuwa na mzigo mwingine zaidi ya begi lililojaa nguo zake mwenyewe, hakuwa na pesa zaidi ya shilingi elfu kumi aliyokuwa amebakiza.
Alijua wazi kuwa alikokuwa anakwenda kulikuwa na taabu kubwa na nzito ikimsubiri, alijua tangu siku hiyo asingepata msaada wowote kutoka kwa baba yake sababu alikuwa amemuudhi kupita kiasi! Isitoshe alijua wazi kuwa mama yake wa kambo na ndugu zake wangemjaza chuki baba yake ili azidi kumchukia.
“Lolote na liwe lakini sipo tayari kumuua mtoto wangu! Ni bora mimi niteseke lakini kiumbe hiki kizaliwe kama ni masomo nitaendelea nayo baadaye ingawa sina uhakika ni nani atanilipia ada!” Aliwaza Belinda wakati akitembea kuelekea nyumbani kwao na Prosper.
Alishangazwa na umati mkubwa wa watu aliouona alipokaribia nyumba yao, wanaume wengi walikuwa wamekaa katika miduara wakiota moto na wengine walionekana kula chakula! Belinda alishindwa kuelewa ni nini kilikuwa kimetokea.
Alipofika kwenye uwanja wa nyumba alishangaa kuwaona wifi zake wakija mbio huku wakilia machozi! Wote walimkumbatia huku wakimtaarifa kuwa mama yao alikuwa amefariki asubuhi ya siku hiyo.
“Mama amefariki leo! Na hapa tulipo hata pesa ya sanda tumekosa!” Nyamizi alimwambia Belinda baada ya kuketi chini huku akilia na kujifuta machozi.
“Ni heri umekufa wifi maana hapa ndani hatuna hata senti, nafikiri utatusaidia pesa kidogo tukanunue sanda na kuchonga jeneza!”
Belinda alipofikiria pesa aliyokuwa nayo mfukoni ilikuwa ni shilingi elfu kumi peke yake, hiyo ndiyo ilikuwa maisha yake hakuwa na tegemeo la kupata pesa mahali pengine mpaka wakati wa kujifungua! Hakuwa na jinsi ilikuwa ni lazima asaidie, alichukua pochi yake na kuifungua akatoa noti ya shilingi elfu kumi na kumkabidhi Nyamizi ambaye naye aliwakabidhi wazee wa kijiji ili waende kununua sanda.
Huo ndio ulikuwa mwisho wa Belinda kuwa na pesa, alielewa mbele kulikuwa na shida kubwa kwa sababu nyumbani kwao na prosper asingeweza kupata msaada wowote!
Pamoja na hayo yote hakuwa tayari kumuua mtoto wake.
Belinda alishindwa kuelewa maisha yangeendeleaje bila pesa, pesa pekee aliyokuwa amebaki nayo ilikuwa shilingi elfu kumi ambayo aliitumia kununua sanda ya mama yake Prosper! Hakuwa na jibu la jinsi gani angeitunza mimba yake mpaka kujifungua, aliielewa hali ya uchumi kijijini Tutuo, alijua dada zake na prosper waliobaki wangehitaji msaada kutoka kwake.
Aliona giza kubwa mbele yake lakini yote alimwachia Mungu, alikuwa tayari kwa lolote lakini si kurudi tena Dar es Salaam kwa baba yake, aliamini maisha yalikuwa yamembadilikia na hayo ndiyo yalikuwa maisha yake! Kulikuwa ni kuporomoka kwa aina yake lakini hakuwa na jinsi ya kuubadilisha ukweli huo hiyo ndiyo ilikuwa hali halisi.
Mwezi mmoja baadaye:
Maisha yalikuwa magumu sana kwa Belinda na familia nzima ya akina Prosper iliyotegemea yeye angetoa msaada, mara nyingi walilala na kushinda na njaa sababu ya kukosa chakula!Afya ya Belinda ilizidi kudhoofika, akakonda na alionyesha dhahiri dalili za kupungukiwa damu jambo alilokabiliana nalo kwa kula mboga za majani chukuchuku ambazo gharama yake ilikuwa ni kuzichuma tu na kuzipika.
Mara nyingi alikumbuka maisha ya starehe aliyoishi nyumbani kwao, maisha hayo hayakuwepo tena ilimlazimu azoee hali aliyokuwa nayo.
Chakula chao kikuu kilikuwa mihogo na karanga, ambacho walikila mara moja kwa siku! Mihogo hiyo ilipatikana baada ya kufanya vibarua katika mashamba ya watu ya mihogo na ujira wao ulikuwa ni hiyohiyo mihogo waliyoitumia kula, Belinda alikuwa na mimba lakini alilazimika kwenda kufanya vibarua kwenye mashamba ya watu asubuhi mpaka saa kumi jioni.
Kwa mwanamke mjamzito ilikuwa ni kazi ngumu lakini alilazimika kuifanya ili aishi, ili kupata pesa ya kumwezesha kwenda kumwona Prosper gerezani kila jumapili,Belinda alilazimika kutafuta kazi ya kusomba maji na kupasua kuni nyumbani kwa mwarabu mmoja tajiri kijijini hapo! Kwa pipa moja la ndoo kumi na mbili Belinda alilipwa shilingi mia tatu, ilikuwa ni pesa kidogo sana lakini alilazimika kuikubali! Alitunza shilingi mia mbili na kutumia shilingi mia.
Akiba aliyojiwekea kwa kufanya kazi hiyo ndiyo ilimwezesha kuwalipia nauli wifi zake pamoja na yeye mwenyewe kwenda gerezani kumwona Prosper! Yalikuwa ni maisha ya huzuni kubwa kwa Belinda aliyekulia katika familia ya kitajiri na yenye fahari kubwa lakini alilazimika kuyakubali.
Belinda alikonda na kukondeana, akabaki mifupa tupu ni mimba tu iliyoonekana mbele yake, nywele zilizotiwa dawa kichwani mwake zilichakaa na kulazimika kuzikata, pamoja na shida zote hizo bado Belinda hakuwaza kurudi kwa baba yake ambako alijua baba yake angemtoa roho.
“Nitafia hukuhuku Tutuo kamwe sitathubutu kurudi kwa baba nina uhakika atanichinja! Ninajua ameshaambiwa mambo mengi ya ajabu na mama na ndugu zangu wa kambo ili anichukie!” Aliwaza Belinda.
**************
Belinda aliendelea kuishi na kuitunza mimba yake katika mazingira hayo magumu! Akipasua kuni na kusomba maji nyumbani kwa mzee Mohamed, zilikuwa ni kazi ngumu sana kwa mama mjamzito lakini hakuwa na chaguo jingine ilibidi azifanye hivyohiyo vinginevyo asingepata pesa ya kumpa mahitaji muhimu pamoja na nauli ya kumpeleka gerezani kila mwisho wa wiki.
Belinda alikuwa na uwezo wa kuamua kurudi Dar es Salaam na kuanguka miguuni mwa baba yake akiomba msamaha, aliamini pengine angeweza kusamehewa ingawa hakuwa na uhakika sana, alishindwa kufikia uamuzi huo kwa sababu alimpenda mno Prosper na hakuwa tayari kumwacha peke yake.
Alifanya kazi ngumu za kupasua kuni na kusomba maji kwa muda wa miezi minane ya mimba yake, hakukumbuka hata siku moja kwenda kliniki kupimwa maendeleo ya mimba yake, alichofanya ni kununua vifaa muhimu alivyoambiwa na akinamama wazoefu wa mambo ya uzazi kijijini kama vile mipira ya kuvaa mikononi,khanga za kutosha, wembe na nepi za mtoto wake.
Watu wote kijijini walimshangaa kwa jinsi alivyofanya kazi ngumu akiwa na mimba kubwa ya kujifungua wakati wowote, mwezi wa tisa wa mimba yake ulipoingia Belinda alizidiwa na kuishiwa na nguvu kabisa, alianguka siku moja wakati akipasua kuni chini ya jua kali na kuzimia, walimtoa juani na kummwagia maji akazinduka.
Mzee Mohamed mwarabu tajiri aliyekuwa akifanya kazi kwake alipopata taarifa hizo alimfukuza kazi sababu ya kuogopa angeweza kufia nyumbani kwake.
“Belinda iko wewe acha kazi sababu wewe uko na mimba kuba sasa!” Mzee Mohamed alimwita Belinda na kumwambia
“Hapana mzee ninaweza tu ile ilikuwa ni bahati mbaya kwani nilikanyaga mti nikaanguka chini, tafadhali niache nifanye kazi sina pesa ya chakula wala nauli ya kwenda kumwona mume wangu gerezani!” Belinda alimbembeleza mzee Mohamed lakini haikusaidia kitu amri ilishatolewa afukuzwe kazi na hivyo ndivyo ilivyokuwa.
Belinda aliondoka nyumbani kwa mzee Mohamed akilia machozi kwani pesa aliyokuwa nayo ilikuwa haitoshi kumkamilishia kila kitu wakati wa kujifungua, alijua wangeitumia kwa chakula kabla miezi tisa kamili haijakamilika.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani mpaka Belinda anapatwa uchungu saa moja na nusu ya jioni siku ya Ijumaa ya mwezi huo wa tisa hakuwa na pesa yoyote kama akiba yake, pesa yote alishaitumia kuwatunza dada zake na Prosper, Nyamizi na Kasanda ambao hawakujishughulisha na kazi yoyote pamoja na kuwa afya zao zilikuwa njema.
Hapakuwa na pesa ya kumpeleka hospitalini usiku ule ilibidi ateseke na uchungu mpaka asubuhi lakini bado hakujifungua, aliendelea mpaka saa tano asubuhi hali ilikuwa bado ileile mtoto hakuwa tayari kutoka, Belinda aliishiwa na nguvu sababu ya kusukuma mtoto kwa muda mrefu bila mafanikio na mguu wake mmoja ulipoteza kabisa hisia.
Saa sita mchana Kasanda na Nyamizi walishtukia badala ya kichwa kutokeza katika njia ya uzazi mkono wa mtoto ulichungulia! Wote waliogopa na kulazimika kutafuta baiskeli na kukimbia hadi kijiji cha jirani kuchukua mkunga wa Jadi, naye alipokuja na kuiona hali aliyokuwa nayo Belinda alishtuka.
“Huyu alikuwa anakwenda Kliniki kweli?”
“Hapana!”
“Mh!” Mkunga aliguna.
“Tusaidie mama!”
“Sina uwezo wa kuwasaidia kama mna pesa tukodisheni gari tumpeleke hospitali!”
“Hatuna hata senti tano!”
“Sasa tutafanya nini?”
“Labda niende kwa mzee Mohamed nikaombe msaada!” Kasanda alisema kwa sauti ya upole.
“Wifi nisaidieni nitakufa!” Belinda alisema akiwa katika maumivu makali.
“Ngoja niende!” Alisema Kasanda na kutoka mbio kwenda kwa mzee Mohamed kuomba msaada wa gari. Aliporudi alikuwa na trekta lenye tela na Belinda alipakiwa mara moja ndani ya tela na safari ya kwenda hospitali ya mkoa, Kitete ilianza.
***************
Njia nzima Belinda aliendelea kusukuma lakini mtoto hakutoka, damu peke yake ndiyo zilivuja kwa wingi na kulichafua tela la trekta, hakuna mtu aliyekuwa na uhakika kuwa Belinda angepona katika tatizo hilo, walipofika hospitali walipokelewa na daktari alipopima alithibitisha kuwa mtoto aliyekuwepo tumboni alikuwa bado yuko hai ila mapigo yake yalikuwa yakiendelea kufifia.
“Daktari huyu mama ana tatizo gani sasa?”
“Ah! Ana Malpresentation, nafikiri alikuwa haendi kliniki kupimwa mlalo wa mtoto!” Alisema daktari Kaniki bingwa wa magonjwa ya wanawake katika hospitali ya Kitete akimaanisha mtoto wa Belinda alikuwa amelala vibaya na kutanguliza mkono.
“Sasa tutafanya nini?”
“Hakuna la kufanya zaidi ya kumpeleka chumba cha upasuaji tukamfanyie Ceasserian section, tujaribu kuokoa maisha yake pamoja na ya mtoto!” Alijibu daktari akimaanisha ilikuwa ni lazima Belinda apelekwe chumba cha upasuaji kufanyiwa operesheni ya uzazi.
“Amekula kitu chochote tangu jana?”
“Hapana!” Kasanda na Nyamizi waliitikia.
“Safi sana!”
Kwa haraka bila kuchelewa Belinda alibebwa kwenye machela na kukimbizwa chumba cha upasuaji ambako aliandaliwa na operesheni kufanyika, madaktari walifanikiwa kumtoa mtoto katika dakika zake za mwisho, rangi yake ya ngozi ilikuwa bluu sababu ya kukosa hewa ya oksijeni na alionekana kutohema na ikalazimika afungiwe mashine ya oksijeni ili mapafu yake yafanye kazi.
“Amepata Cynosis!” Alisema daktari akiiongelea rangi ya bluu iliyokuwa katika mwili wa mtoto.
******************
Baada ya operesheni hiyo Belinda akiwa hajitambui alirudishwa moja kwa moja wodini ambako aliendelea kupata matibabu, mtoto wake alitunzwa katika chumba maalum ambako aliendelea kupewa matunzo ya kumsaidia apumue vizuri.
“Daktari mgonjwa wetu atapona kweli?” Nyamizi alimuuliza daktari Kaniki.
“Atapona ila atakuwa na matatizo kidogo yaliyosababishwa na kuchelewa kufika hospitali!”
“Matatizo gani daktari?”
“Belinda ametoboka tundu kati ya mfuko wa mkojo na njia ya uzazi! Hali hii sisi kitaalamu tunaiita Vaginal vesco fistula au kwa kifupi VVF kwa hiyo mkojo utakuwa unatoka tu wenyewe na wakati mwingine utatokea ukeni! Ni hali ngumu kidogo kuishughulikia itabidi Belinda abaki hapa hospitali kwa muda mrefu kidogo!”
“Matibabu yake ni nini?”
“Matibabu yake ni mpaka operesheni tu na hii itafanyika baada ya miezi mitatu hadi sita katika muda huu wote mkojo utakuwa unatoka peke yake!”
“Kuna tatizo jingine lililojitokeza daktari?”
“Ndiyo mguu wake wa kushoto umepoteza hisia kwa sababu mshipa wa fahamu unaoshughulika na mguu huo uligandamizwa na mtoto! Lakini hili si tatizo kubwa sana baada ya muda akifanya mazoezi hali yake itakuwa nzuri!” Alimaliza daktari na kuwaaga Nyamizi na Kasanda.
Walibaki katika masikitiko makubwa na hawakujua nini wangefanya kumsaidia Belinda katika tatizo alilokuwa nalo na hawakuwa na uhakika kama mtoto angepona.
Miezi miwili baadaye:
Belinda alikuwa bado yuko hospitali akisubiri siku tisini zitimie ili afanyiwe operesheni, muda wote huo alimkumbuka Prosper gerezani, hakuna siku hata moja iliyopita bila kumfikiria na alitamani atoke hospitalini na kwenda gerezani Isanga kumwona lakini haikuwezekana.
Hali aliyoambiwa na daktari ilikuwepo! Mkojo ulivuja wenyewe na kulowanisha nguo zake, alitoa harufu mbaya kiasi kwamba wagonjwa wenzake hawakupenda kabisa kukaa naye!
Alishangaa mpaka muda huo baba yake alikuwa bado hajamtafuta, hilo lilimuumiza sana moyo wake na zaidi ya hilo wifi zake walikomea siku moja aliishi kwa kutegemea misaada ya ndugu wa wagonjwa wengine waliomhurumia walipokuja wodini kusalimia ndugu zao na kusikia habari yake.
Ilikuwa ni siku ya Jumamosi asubuhi daktari Kaniki alipokuwa akipita raundi wodini, alipokifikia kitanda cha Belinda alianza kutabasamu na kumwita Belinda kwa jina.
“Naam daktari!”
“Nafikiri sasa hivi hali yako ni nzuri kidogo inabidi urudi nyumbani uje baada ya mwezi mmoja ili tuone kama tutaweza kukufanyia operesheni!”
“Sawa daktari lakini......!”
“Kwani vipi Belinda?”
Post a Comment