BOBAN, KASEJA MGUU NDANI, MGUU NJE MBEYA CITY, WATASUBIRI UAMUZI WA PHIRI
Kocha
wa Mbeya City, Kinnah Phiri, amesema msimu huu amelazimika kuwa na
lundo la wachezaji wakongwe kwani aliipokea timu hiyo katikati ya msimu,
lakini msimu ujao anataka ‘mafaza’ wasiozidi watatu tu.
Phiri, raia wa Malawi, amesema anataka kujaza wachezaji vijana kikosini mwake msimu ujao akiamini wanaweza kumletea mafanikio.
Kocha
huyo wa zamani wa Free States ya Afrika Kusini, amekwenda mbali kwa
kusema anataka robo tatu ya kikosi kizima kiwe ni vijana, tofauti na
sasa ilivyo na wakongwe hawatazidi watatu.
Mbeya
City inayoshika nafasi ya nane katika Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 34,
ina wakongwe kama Juma Kaseja, Them Felix, Hassan Mwasapili, Anthony
Kalyesubira, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Haruna Moshi ‘Boban’ na Steven
Mazanda.
“Msimu
huu nimekuta timu imeshasajili, lakini msimu ujao lazima nisimamie
falsafa yangu. Ninataka robo tatu ya kikosi changu kiwe na wachezaji
vijana.
“Nitabaki
na wakongwe watatu tu, ila siwezi kuwataja sasa kwa kuwa ligi bado
inaendelea, nataka kuwatumia vijana kwani naamini nitafanikiwa nao,”
alisema Phiri.
Wakati
Phiri akisema hayo, taarifa zinasema Mbeya City ipo katika harakati za
kumsajili straika wa Ndanda FC, Atupele Green. Mbeya City kesho Jumapili
inamaliza ligi kuu kwa kucheza na Ndanda kwenye Uwanja wa Sokoine,
Mbeya.
SOURCE: CHAMPIONI
Post a Comment