WAKALA WA SHETANI - 10

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
“Hapana shoga, niamuapo kitu siwezi kukisitisha, niache niondoke nitarudi baada ya siku mbili. Nina imani huenda asubuhi ya kesho wakaingia hapa.”
“Mmh sawa, nakuombea safari njema na Mungu akutangulie kwa jambo lolote.”
“Amen.”
Bupe alimuacha Ng’wana Bupilipili apumzike kwa ajili ya safari yake ya usiku wa manane.
SASA ENDELEA...
****
Baada ya tukio la kushtukiza la vifo vya askari watatu waliokuwa wakilinda na kutoroka kwa mtuhumiwa. Jeshi lilijipanga upya kumsaka mtuhumiwa kwa kuagizwa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kumsaka muuaji ambaye alionekana ni mzoefu tena mtu hatari.
Baada ya kupatikana siraha na askari wa kutosha msako mkali ulipangwa kuanza siku ya pili alfajiri kwa kusaka pori lote na maeneo ya karibu na pori. Kila kitu kilikwenda kama kilivyopangwa watu nao walijipanga kwa kuamini adui yao ni mzoefu wa kutumia siraha za moto.
Msako ulianza saa kumi na moja Alfajili wakiwa wamekosana robo saa na muda aliopanga Ngw’ana Bupilipili kutoka kambini. Wao walikuwa nyuma kwa nusu saa Ngw’ana Bupilipili aliondoka majira ya saa kumi na nusu.
Ngw’ana Bupilipili aliondoka kambini majira ya saa kumi na nusu akiwa amembeba mwanaye mgongoni kwa kumfunga madhubuti na kitenge. Kwa ujasiri mkubwa aliingia ndani ya pori lenye kiza kinene. Akiwa amejitolea kwa lolote litakalo tokea mbele yake.
Alianza safari yake kwa kupita kwenye mbuga iliyokuwa ikitisha huku milio ya wanyama na wadudu watembeao usiku ikitawala. Hali ya hewa ilikuwa ya baridi kali lakini hiyo haikumsumbua. Alitembea huku akimuomba Mungu amfikishe salama na kumlinda na vitu vibaya japokuwa hakujua anakwenda wapi usiku mzito kama ule.
Baada ya mwendo wa robo saa wingu zito lilitanda na kuongeza kuimeza nuru ndogo ya nyota na kuzidi kuongeza hofu kwa Ngw’ana Bupilipili. Alimuomba Mungu amuokoe na mvua ile kwa vile sehemu aliyokuwa akienda hakukuwa na sehemu ya kujikinga na mvua hiyo.
Dua yake haikufua dafu baada ya dakika tano mvua nzito ilishuka. Alijikuta akipata wazo la kurudi kambini, kwani sehemu aliyokuwa akielekea ilikuwa haionekani vizuri kutokana na kiza kizito.
Hivyo hakujua ajifiche wapi, alisimama akiwa amemkumbatia mwanaye aliyemtoa mgongoni na kumweka kifuani. Alijikuta yupo kwenye maamuzi mazito. Mvua ikiendelea kuwanyeshea ikiambatana na upepo mkali. Aliamini kabisa kurudi ni kujitia ndani ya kitanzi alipiga moyo konde na kuamua kuendelea na safari. Lakini kwa upende mwingine aliona kama ataendelea na safari itakuwa sawa na kuhatarisha maisha ya mwanaye kwa mvua na baridi kali la usiku ule.
Hakuwa akijua mvua ile itakatika saa ngapi, hivyo lazima mwanaye angepata matatizo ya baridi ambalo litamfanya uwe katika wakati mgumu wa kumhudumia pia kujificha na maadui zake.
Alijikuta akipiga moyo konde na kuamua kuendelea na safari yake kwa kuamini haitanyesha muda wote uliobakia kufika asubuhi. Alitembea huku amemkumbatia mwanaye ambaye kwa baridi lile alimpatia joto kupitia kwake mwenyewe kwa kumkumbatia.
Alitembea bila kupumzika kwa zaidi ya saa moja huku mvua ikipungua na kumfanya aendelee na safari yake kwa kuingia ndani ya vidimbwi vya maji bila kujua kwa vile kiza kilikuwa kizito hasa kutokana na wingu zito lililokuwa limetanda.
Baada ya mwendo mfupi alijikuta akipita kwenye njia ambayo ilikuwa na shimo na kumfanya akiteleze na kutumbukia kwenye shimo lililokuwa limejaa maji.
Alipiga kelele za woga na kujikuta akizama mpaka chini na mwanaye, alianza kuhangaika ndani ya maji kuokoa maisha yake na ya mwanaye.
Alibahatika kushika mzizi uliokuwa ndani ya maji, kwa nguvu zake zote aliufuata ule mzizi hadi kufanikiwa kutoa kichwa chake nje na cha mwanaye.
Aliung’ang’ania ule mzizi huku akichezesha miguu na kufanikiwa kukanyaga jiwe lililokuwa pembeni ndani ya maji mule shimoni.
Alijisogeza hadi juu ya jiwe na kusimama juu yake. Mikono yake ikiwa bado imeshikilia ule mzizi ambao ulikuwa kama nguzo yake mule ndani ya maji.
Baada ya kusimama ndani ya maji aliweza kujitoa kwenye maji mpaka sehemu za kifua, sehemu iliyobaki ilibakia ndani ya maji. Bado hakuona nje wala kujua urefu wa shimo lile. Alimuomba Mungu amuokoe mwanaye kama kifo basi kimkute yeye.
****
Kikosi maalumu kiliendelea na msako wa nguvu katika pori lile kwa kumtafuta Ngw’ana Bupilpili kila kona bila mafanikio, kwa kupita pori kwa pori.
Watu wote walitawanyika na kuziba njia zote za kutokea kusubiri kupambazuke ili msako kamili uanze. Wakati kunapambazuka Ngw’ana Bupilipili alijikuta yupo ndani ya shimo ambalo pembeni yake kulikuwa na mti mkubwa ulioingiza mizizi yake ndani ya shimo.
Ilikuwa ajabu muda wote wa misukosuko mwanaye hakupiga kelele, alikuwa kimya na kutulia kwa mama yake. Ilifika hatua ya Ngw’ana Bupilipili kufikiri mwanaye huenda amefariki kutokana na ukimya wake. Alipomuita aliitikia kumuonesha mama yake yupo salama.
Baada ya kuhakikisha mwanaye yupo salama alishika mizizi ya ule mti na kupanda hadi juu. Alifanikiwa kutoka ndani ya shimo salama, kwa vile alikuwa amechoka na maji ya mvua alijilaza pembeni ya mti na mwanaye ambaye alimuachia ziwa anyonye.
Akiwa katikati ya usingizi alisikia sauti za watu wakibishana.
“Sidhani kama atakuwa amefika huku.”
“Bwana wee kwani nani alikuambia adui huwa ana mpaka wa sehemu ya kukimbilia.”
“Kwa hiyo tuendelee kumtafuta, nina uhakika tutampata.”
“Haya jamani safari iendelee mvua ya leo inatisha tumekesha nayo na kuamka nayo, nguo zote zimetota maji.”
“Hii ndio kazi ya jeshi.”
“Haya jamani nataka mpaka saa sita mchana tuwe na jibu tumempata au la.”
“Haya jamani tunaweza kuendelea tumepumzika vya kutosha.”
Ngw’ana Bupilipili alijua amekwisha, lazima wangemuona hakuwa na sehemu ya kukimbilia. Sauti za askari zilizidi kumsogelea hakuwa na ujanja zaidi ya kumchukua mwanaye bila kufikiria anafanya kitu nini na kujitupa naye ndani ya shimo la maji ili kujificha.
Kama mwanzo aliporomoka ndani ya maji na kwenda hadi chini ya maji kisha alirudi juu na kufanikiwa kuishika mizizi ya mti ambayo ilimsaidia kumpandisha juu.
Aliwasikia watu wale wakizungumza huku wakisogea kwenye lile shimo. Ngw’ana Bupilipili alizama chini ya maji na mwanaye kwa muda ili watu wale wasimuone.
Baada ya muda alitokeza kwa juu kuvuta hewa. Aliwaona wakiwa wamempa mgongo, aliweza kuwaona askari waliokuwa wamebeba siraha kali za kisasa kama walikuwa wakimsaka Osama.
Moyoni alijiuliza kama watamkamata watamfanya nini. Pembeni ya shimo lile kulikuwa na majani ambayo angeweza kusimama chini yake na mtu wa juu asimuone.
Alijisogeza chini ya yale majani ambayo yalimficha. Aliendele kumuomba Mungu wale watu waondoke haraka kwani maji ya mule shimoni yalikuwa ya baridi tena machafu.
Wasiwasi wake mkubwa uchafu na baridi lile ni hatari kwa afya ya mwanaye. Wakiwa bado akimuomba Mungu alimsikia mtu mmoja akisema.
“Ngoja nikojoe shimoni.”
Haikupita muda mkojo ulitua kichwani kwa Ngw’ana Bupilipili. Ilibidi atulie na kuuacha mkojo ule umnyeshee kichwani. Baada ya jamaa kumaliza aliwasikia wakishauriana kuhusiana na msako uliokuwa ukiendelea bila mafanikio.
“Jamani kwa nini tuendelee kumtafuta porini kwa nini tusiende hata kwenye kile kituo cha kiroho labda atakuwa amekimbilia kule, “ mmoja alitoa wazo.
“Wazo zuri, wengine watakwenda kule na tuliobaki tutaendelea kumtafuta.”
“Kwa hiyo?”
“Muda huu tupumzikeni kidogo kama nusu saa kisha tunaendelea na msako, tuhakikishe mpaka jioni kila kitu kiwe kimeeleweka,” aliagiza mkuu wa msako ule.
“Hakuna tatizo.”
Baada ya muda Ngw’ana Bupilipili alisikia kimya sehemu ile, hakuwa na haraka aliongeza dakika tano kuthibitisha kweli wameondoka.
Baada ya dakika tano kupita alishika mizizi na kujipandisha juu, alipofika juu alishukuru Mungu hakukuwa na mtu yoyote.
Taratibu kama komandoo wa kivita aliyekuwa akiwatoroka maadui, alifanikiwa kuwatoroka baada ya kuwaona kwa mbali.
Alielekea upande wa mashariki kuwakimbia adui zake. Baada ya mwendo mfupi aliamua kupumzika kwani mwanaye alianza kutetemeka kwa baridi.
Alijitahidi kumkumbatia lakini haikusaidia kwa vile naye mwili wake kwa baridi la muda ule na ubaridi wa maji uliufanya mwili wake uanze kufa ganzi.
Kila dakika hali ya mwanaye ilibadilika na kuonesha kupoteza uwezo wake wa kawaida. Hali ile ilimfanya Ngw’ana Bupilipili kuchanganyikiwa na kuona jinsi alivyokuwa akimpoteza mwanaye huku akimuona.
Baada ya kuanza kuhema kwa shida. Alijilaumu kwa kukaidi ombi la shoga yake Bupe la kumuacha mtoto kambini. Aliamini kama mwanaye atakufa yeye ndiye atakayebeba lawama kwa vile hali ile isingemtokea kama angemuacha mtoto kambini.
Moyoni alijuta na kuona kama mwanaye atakufa, basi kwake yeye hakuwa na sababu yoyote ya kupoteza maisha ya mume wake kupoteza maisha ya wanakijiji na sababu ya yeye kuteseka vile.
Hali ya mwanaye ilizidi kuwa mbaya hata akawa haoneshi kupumua. Aliamini kabisa njia iliyokuwepo ya kumsaidia mtoto wake ni kujisalimisha kwa wale askari ambao wangeweza kuokoa maisha ya mwanaye kama wakifanikiwa.
Kwake hakuona hatari yoyote kama atafungwa au kunyongwa na mwanaye kubakia salama japokuwa hakujua mtoto wake ataishi maisha gani.
Alimchukua mtoto wake na kumweka begani na kuwafuata wale askari waliokuwa wakimsaka huku akitokwa na machozi kwa uchungu wa mwanaye. Askari waliokuwa wamejipumzisha walishtuka kumuona mwanamke akiwa amembeba mtoto begani huku akionekana ametota kwa maji.
Wote walimtazama na kujiuliza anatoka wapi. Alipofika mbele yao alimbwaga mtoto wake mbele yao huku akisema.
“Haya mleni nyama sasa,” alisema huku akifoka kwa sauti ya kilio.
“Mbona hatukuelewi, tumle nyama kivipi?” Askari mmoja alimshangaa.
“Si mlikuwa mnataka kuona mwanangu anakufa haya amekufa furahini, haya nipelekeni mkaninyonge sasa.”
Mkuu wa oparesheni ile alimchukua haraka yule mtoto na kugundua tatizo lake ni yabisi, kwa haraka walitengeneza joto ambalo lilimsaidia mtoto yule kurudi katika hali ya kawaida kisha alichukuliwa na kupelekwa kwenye kituo chao cha huduma ya kwanza kabla ya kumpeleka hospitali kwa matibabu zaidi.
Wakati huo Ngw’ana Bupilpili alikuwa amekwishawekwa chini uya ulinzi baada ya kugundulika ndiye adui aliyekuwa akitafutwa, naye hakutaka kuwabishia.
Walimshangaa mtu ambaye walikuwa na wasiwasi huenda ni mkakamavu tena mwenye mafunzo ya kijasusi. Mkuu wa oparesheni ile alishtuka na kuuliza mara mbili.
“Ndiye huyu?”
“Ndio mkuu,” alijibu askari aliyekimbiwa na Ngw’ana Bupilipili.
“Sasa mbona anaonekana tofauti na sifa nilizosikia.”
“Mkuu usimtazame kwa macho, ni zaidi ya gaidi, mwanamke huyu kama alivyoniahidi alipania kukimaliza kijiji kizima.”
“Eti mama ni kweli?” Mkuu alimuuliza kwa upole.
“Maswali ya nini, si mmeisha nikamata ninyongeni basi au niueni kwa risasi si mmekuja na bunduki kuniua, niueeeeni?”
“Hatuwezi kukunyonga kwa vile sisi si mahakama, la muhimu maelezo yako wanaweza kukusababisha sisi tukuache huru.”
“Hayatasaidia kitu kwa vile maelezo ya awali nimweleza huyu kaka, lakini mliamua kunisaka kama gaidi. Mmefanikiwa kunikamata nipelekeni nikanyongwe ili mfurahi. Lakini naapa Mungu atalipa kwa kila roho zisiyo na hatia,” Ngw’ana Bupilipili alizungumza kwa uchungu huku akiwaga machozi.
“Serikali haipo kwa ajili ya kumuonea mtu bali kuhakikisha kila mwanadamu anaishi kwa uhuru na amani bila kuvunja sheria,” mkuu alionesha ustaarabu.
“Kwa vile wao wamekufa ndio serikali imeliona hilo, na sisi tuliopoteza roho za watoto wetu na waume zetu serikali yetu ni ipi?”
”Mmepotezaje hizo roho?”
Ngw’ana Bupilipili alirudia maelezo ya mauaji ya albino kijiji cha Nyasha na kifo cha mumewe, ikiwemo kuporwa mali zao na wanakijiji cha Nyasa.
Baada ya kumsikiliza mkuu alisema:
“Bado hukutakiwa kuchukua sheria mkononi kwa vile kuna vyombo vya sheria.”
“Mmh! Vyombo vya sheria kwa vile wamekufa wao, mbona vifo vya watoto albino hamkuwahi kuja hata siku moja ila hivi ndio mmetengeneza mtego wa kuninasa, ndio maana nikasema nipelekeni mkani.ni..ni..ni.. Haaa!”
Ngwana Bupilipili alishika chini ya titi la mkono wa kushoto baada ya kusikia mchomo mkali kwa ndani kama kumepasulika.
Maumivu yalikuwa makali na kuhisi kama mbavu zinagusana. Alipiga kelele za maumivu na kuanguka chini akiwa amepoteza fahamu.
Itaendelea
Post a Comment