WAKALA WA SHETANI - 09

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
“Sasa ndiyo ujiulize kwa nini mauaji ya watoto albino hamkuletwa, mletewe kwenye mauaji haya?”
“Huoni kama kosa lako linaweza kusababisha kunyongwa?”
“Nilijiandaa mapema toka nilipopata dhamira ya kulipa kisasi, nilikuwa tayari kwa lolote, kifo kitu gani nimempoteza mwanangu na mume wangu nitakuwa mimi,” Ngw’ana Bupilipili alisema kwa hasira huku akilia.
SASA ENDELEA...
Wakiwa katikati ya mazungumzo dawa aliyoweka kwenye vyanzo vya maji bila walinzi kujua ilikuwa imeishafika kwa watu waliochota maji. Miongoni mwao ni baadhi ya askari ambao walioga na kupigia mswaki na kuyameza yale maji.
Walianza kulegea na kutokwa mapovu waliokuwa karibu walipiga kelele kuomba msaada kwa wenzao. Yule askari aliyeonekana mkakamavu alimchukua Ngw’ana Bupilipili mpaka eneo la tukio.
Walipofika walitaharuki kuwakuta askari wenzao wakiwa katika hali mbaya wakitokwa na povu jingi huku wakiwa wameangukia ndani ya maji.
Wawili walikuwa wameisha kufa, kutaharuki kwa askari yule kulimpa nafasi Ngw’ana Bupilipili kuondoka eneo la tukio bila tatizo na alipoingia porini alitimua mbio kama yupo katika mashindano ya marathoni.
Mwendo wa masaa matatu alitumia kwa saa moja na nusu. Kutokana na kwenda mwendo mkali alipofika kambini baada ya kuvuka geti alianguka chini na kupoteza fahamu.
Hali ile iliwashtua na kumkimbiza katika chumba cha mapumziko na kupewa huduma ya kwanza. Vipimo vilionesha msukumo wa damu ulikuwa wa juu sana. Baada ya muda alipata fahamu alijikuta yupo hospitali, kutokana na wasiwasi hata sehemu ile aliiona ngeni kwake.
Alijinyanyua kitandani kupanga mpango wa kutoroka, kabla hajapiga hatua alisikia mlango ukifunguliwa. Alirudi haraka kitandani na kujilaza kama mtu aliyepoteza fahamu.
Daktari Father Joe alipoingia ndani alimkuta Ngw’ana Bupilipili akiwa amejilaza kitandani. Lakini aliamini kabisa mlalo ule si wa mtu kupoteza fahamu bali wa usingizi wa kawaida. Akiwa bado hajapata jibu juu ya kuwa katika hali ile alimgeukia msaidizi wake sister Marry.
“Eti sister nini kilichomtisha na kumfanya akimbie na kuanguka kisha kupoteza fahamu?”
“Kwa kweli mpaka sasa hatujajua ila niliambiwa alitoka mara moja.”
“Alikuwa amekwenda wapi?”
“Mmh, hapo sijui ngoja tumuulize mwenyewe akipata fahamu.”
Ngw’ana Bupilipili sauti zile alizifahamu ya Father Joe na Sister Marry na kumfanya ashushe pumzi kwa kuamini yupo sehemu salama. Alijifanya kujigeuza kitu kilichowafanya wasogee kitandani. Sister Marry alimwita.
“Mama Kusekwa... Mama Kusekwa.”
“Abee,” aliitika na kujinyoosha.
“Vipi unajisikiaje?” Sister Marry alimuuliza kwa sauti ya upole.
“Mmh, sijambo kiasi,” alijibu huku akifungua macho.
“Eti tatizo nini?”
“Nilikuwa natoka kutafuta baadhi ya vitu vyangu niliviacha porini wakati nakuja, ndipo nilipokutana na mnyama mkali aliyeanza kunifukuza kwa kweli nilikimbia kwa nguvu zangu zote. Sikumbuki kilichoendelea na kujikuta nipo hapa,” Ngw’ana Bupilipili alitengeneza uongo unaofanana na ukweli.
“Ooh, pole sana.”
“Asante.”
“Hakuwahi kukujeruhi?” Father Joe aliuliza.
“Sidhani najiona nipo salama ni maumivu madogo madogo ambayo sijui ni ya nini.”
“Unaweza kwenda chumbani kwako, kama utasikia tatizo lolote mwilini mwako utatujulisha.”
Ngw’ana Bupilipili alinyanyuka kitandani na kutembea kwa kuchechemea kwa muda kisha alitembea kawaida. Alikwenda hadi chumbani kwake na kujilaza bila kumfuata mtoto kwani hakuwa na mawazo ya mwanaye zaidi ya kujifikiria jinsi alivyookoka katika mikono ya askari waliokuwa wakilinda chanzo cha maji.
Wasiwasi wake mkubwa ulikuwa huenda wakafanya msako na kwa vile askari yule ameishaiona sura yake lazima angemtafuta na kumpata. Aliamini katika msako wao lazima wangefika kwenye ile kambi na lazima angemtambua na kumkamata.
Ngw’ana Bupilipili aliamini kabisa kwa upande wake muda ule kwake kuwepo pale kambi hakufai, kwa kuamini wakimkosa porini lazima watamfatuta kwenye kambi ile.
Wazo lake kubwa lilikuwa ikifika usiku atoroke na mwanaye na kutimka sehemu asiyoijua japokuwa alijua ni hatari, lakini aliamini bora akafie mbele kuliko kukamatwa na kuhukumiwa kifo.
Hata shoga yake alipoingia hakumuona kwa vile alikuwa amezama kwenye dimbwi la mawazo.
“Shoga nakuona upo mbali vipi umeumia sana?”
“Walaa, kawaida tu.”
“Mhu, za huko?”
“Shoga mbona yamenikuta leo makubwa.”
“Yapi hayo?”
“Kidogo leo nishikwe na askari waliokuwa wakilinda vyanzo vya maji.”
“Vyanzo vya maji?”
“Eeh, japokuwa nilikuwa sijakueleza ukweli wa safari yangu, kwa vile wewe umekuwa mtu wangu wa karibu na muhimu sana kwangu lazima nikueleze ukweli hata nikishikwa ujue tatizo langu.”
“Ushikwe kwa kosa gani tena?” shoga yake alishtuka.
“Tulia basi nikieleze usiwe na pupa na nitakachokueleza naomba ibakie siri yako.”
“Hakuna tatizo shoga.”
Ngw’ana Bupilipili alimweleza yote aliyoyafanya baada ya kufiwa mume wake na ahadi ya kisasi aliyoiweka ya kukisambaratisha kijiji cha Nyasha.
Siku ile jinsi alivyo kamatwa na askari na kufanikiwa kumtoroka. Shogae Bupe hakuamini alichoelezwa na Ngw’ana Bupilipili na ujasiri aliouonesha wa kutimiza dhamira yake.
“Mmh, nimekusikia pia kukupa hongera ni mwanamke wa shoka kwa yote uliyofanya. Huna kosa shoga kwani ulichokifanya sawa sawa kuwatia adabu mashetani wale.
“Sijui kwa nini hukuniambia na mimi nikusindikize, hata mimi nina kisa changu kizito sikuwahi kukueleza na sababu ya mimi kufika hapa.”
“Kisa gani hicho shoga?”
“Kwa vile wewe umeniamini na kunipa siri yako nzito, nami sina budi kujiweka wazi kwako. Mimi nilikuwa nimeolewa katika kijiji cha Ng’wana Nsimba Shinyanga vijijini na mume aliyekuwa na mali ya wastani.
Kwa bahati mbaya mume wangu alifariki, ndugu walinidhurumu mali yote na kuonekana sina thamani mbele ya watu.
Kwa kweli roho iliniuma kwa vile toka nilipoolewa nilikuta ng’ombe ishirini tu, kwa vile sikutaka mume wangu apate shida katika ng’ombe zangu sabini za mahari nilichukua ngombe zangu 40 na kuzichanganya na za mume wangu.
Kwa miaka minane zizi lilikuwa na ngombe mia nne ishirini. Kwa bahati mbaya mume wangu alifariki ndugu walinifukuza kama mbwa hata nilipoomba ng’ombe zangu 40 walininyima.
Sikutaka kubishana nao niliondoka na kurudi nyumbani na wanangu tu wawili. Nami niliwaapia kuwashikisha adabu japokuwa walinidhihaki na kuniona siwezi kufanya kitu chochote kwa vile waliamini wanawake ni viumbe dhaifu.
Moyoni nilipanga pigo zito, ndipo siku moja niliwavizia wamelala na kutia moto nyumba zao za majani kwa kuanzia mlangoni. Kwa vile nyumba nyingi za vijijini za majani madirisha yake madogo walikosa pa kutokea na kuiteketeza familia yote ya marehemu mume wangu.
Siku ya pili taarifa zilizagaa za vifo vya familia ya mume wangu, sikutaka kuitwa kutoa ushahidi kutokana na vifo vya familia ya mume wangu kutokana na kutoa maneno makali siku waliyonidhurumu mali zangu.
Niliamini mtu wa kwanza nitakuwa mimi, basi nilitoroka bila mtu kujua na kutembea kwa miguu mdogo wangu kwa muda wa siku tatu usiku nililala na asubuhi niliendelea na safari zangu.
Ndipo siku moja nilipotokea mbele ya kambi hii nikiwa nimevimba miguu kwa kutembea. Kwa kweli watu wa hapa kwa ukarimu waliniokota na kunitibu kisha walinitunza mpaka leo hii.
Najua walinitafuta nami nilijificha huku sijui nitatoka lini, kwa vile najua nikionekana kijijini kwetu nina kesi ya mauaji. Basi mdogo wangu matatizo yetu yanafafana na kisasi chetu kinafanana japo wewe ulidhamilia kufyeka kijiji kizima mimi nilitimiza nadhiri yangu ya kuipoteza familia yote.
Japo dhambi lakini namshukuru Mungu kuweza kuniwezesha kulipa kisasi, hata leo nikifa nitakuwa nimekufa bila kinyongo. Kwa kweli sikushangai kwa hatua uliyochukua, kisasi ni hapahapa dunia kwa Mungu hesabu. Naamini hata uliowaua umelipa kisasi kwa kiasi kikubwa.” Bupe alisema kwa hisia kali zilizochubua donda la maumivu ya moyo.
“Mmh! Umeona dada watu walivyo na roho za kikatiri kuliko wanyama. Ni kweli kabisa kisasi duniani kwa Mungu kwenda hesabu,” alisema Ngw’ana Bupilipili.
“Umeona eeh!”
“Ila shoga kuna kitu kinanichanganya akili sana.”
“Kitu gani tena?”
“Wasi wasi wangu huenda wale askari wakaendesha msako mkali, wakinikosa porini lazima huku watafika. Heri ningekuwa nimewaua wanakijiji tu msako wake usingekuwa makali lakini nimewaua baadhi ya askari waliopiga mswaki asubuhi kwenye mto ule.
“Hawawezi kukubali kirahisi lazima watanisaka kwa udi na uvumba, wakinikosa porini watakuja kunitafuta hapa na lazima watanikamata,” Ngw’ana Bupilipili aliingia mchecheto.
“Sasa ulikuwa na wazo gani?”
“Nitoroke.”
“Uende wapi?”
“Nitokemee zangu mbele kwa mbele huku nikimkinda mwanangu na wanyama wakali.”
“Kwa nini usibakie ili siku wakija ujifiche usijitokeze?”
“Mmh, hiyo itakuwa yumkini, hujui wana ujuzi gani katika kumsaka wahalifu, wanaweza kunikamata kama kuku wa mdondo, shoga niache nitokomee zangu lililo mbele yangu Mungu anajua majaliwa yangu na mwanangu.”
“Sema tu wasiwasi wako, basi wakipita hao watu urudi sidhani kama watarudi mara mbili.”
“Sawa shoga.”
“Sasa kwa nini usimuache Kusekwa ili uende pake yako si unajua jinsi pori linavyotisha hasa usiku huu.”
“Hapana shoga huenda hii ni safari yangu ya mwisho, hivyo siwezi kumuacha mwanangu japokuwa kiza cha nje kinatisha pia hatufahamu tunakwenda wapi. Ila tuombee kwa Mungu atulinde ili tuonane tena.”
“Yaani huwezi amini moyo wangu umekuwa mzito kwa nini usiahirishe kuondoka usiku huu, uondoke asubuhi.”
“Hapana shoga, niamuapo kitu siwezi kukisitisha, niache niondoke nitarudi baada ya siku mbili. Nina imani huenda asubuhi ya kesho wakaingia hapa.”
“Mmh sawa, nakuombea safari njema na Mungu akutangulie kwa jambo lolote.”
“Amen.”
Bupe alimuacha Ng’wana Bupilipili apumzike kwa ajili ya safari yake ya usiku wa manane.
Itaendelea
Post a Comment