Serikali Yatoa Tamko Kali Kuhusu Tiba Asili na Tiba Mbadala
Ndugu Wananchi, Katika nchi yoyote ile uhuru usio na mipaka
ni jambo la hatari; lakini pia hakuna haki isiyo na wajibu. Vivyo
hivyo, katika huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala hapa nchini kuna
Sheria, Kanuni na Taratibu za Maadili zinazoweka masharti, uhuru na
mipaka; pia haki na wajibu wa kila mdau.
Huduma za tiba asili na tiba mbadala ni huduma
zinazotambulika na Jamhuri yetu, watu wake na ina thamani kubwa. Aidha,
ni huduma inayotambuliwa na sayansi ya tiba ya kisasa.
Hata hivyo huduma hizo zimekumbwa na changamoto mbalimbali
ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa watoa huduma wasiozingatia Sheria, Kanuni
na Miongozo mbalimbali.
Kutokana na hali hiyo na kutokana na ziara ya Naibu Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Hamisi
A. Kigwangalla (Mb) kwa Tabibu Juma Mwaka Juma tarehe 14/12/2015 na
kufuatia uchambuzi uliofanywa na Wizara baada ya ziara hii, Wizara
imebaini changamoto zifuatazo:-
1. Huduma za tiba asili na au tiba mbadala zinatolewa na watoa huduma wasiosajiliwa na Mamlaka husika kwa mujibu wa Sheria.
2. Uwepo wa vituo vinavyotoa huduma za Tiba Asili na au Tiba Mbadala bila kusajiliwa kwa mujibu wa Sheria.
3. Kutolewa dawa kwa wagonjwa bila dawa hizo kusajiliwa na mamlaka husika.
4. Uingizaji na matumizi ya vifaa vya uchunguzi ambavyo havijasajiliwa na mamlaka zinazohusika, na
5. Utoaji wa matangazo bila ya kufuatwa kwa matakwa ya
sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo. Aidha baadhi ya matangazo hayo
yamekuwa na taarifa zinazoweza kuleta madhara na kupotosha Umma wa
Watanzania.
Ndugu Wananchi,
Kutokana na hali hiyo, Wizara itahakikisha kuwa huduma za
tiba asili na tiba mbadala zinatolewa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na
Miongozo iliyopo.
Lengo ni kuwezesha huduma za tiba asili na tiba mbadala
zinakuwa huduma rafiki na salama kwa watumiaji. Tunao wajibu wa
kuwalinda wananchi, vile vile tunaowajibu wa kuweka mazingira mazuri kwa
watoa huduma za tiba asili na tiba mbadala ili kufanya shughuli zao
vizuri.
Hivyo kwa upande wetu Wizara itahakikisha kuwa:-
1. Baraza na sehemu inayosimamia huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala inakuwa na watumishi wa kutosha kwa mujibu wa Ikama.
2. Kunakuwa na Mpango Mkakati wa muda mrefu kuwezesha kufanikisha uboreshaji wa huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini.
3. Watoa huduma wote, vituo vyote vya kutolea huduma, dawa na vifaa na vifaa tiba vinavyotumika vinasajiliwa.
4. Utaandaliwa mwongozo wa mafunzo kwa watoa huduma wote
nchini, kuhusu namna ya kuweka kumbukumbu za wagonjwa, kutoa rufaa kwa
wagonjwa na kutengeneza dawa zilizo bora.
5. Kunakuwa na mawasiliano na Wizara zinazohusika na habari
na mawasiliano ili kuboresha utoaji matangazo yanayohusu Tiba Asili na
Tiba Mbadala.
6. Kunakuwa na mawasiliano na Ofisi ya Rais TAMISEMI na
Taasisi za Utafiti ili kuboresha huduma za tiba asili na tiba mbadala
nchini.
7. Tutafanya mabadiliko ya Sheria ili kuongeza kiwango cha
adhabu kwa watakaokiuka, na pia tunakusudia kuondoa Kanuni inayoruhusu
matangazo kwa idhini ya Baraza kwa sababu inaweka mianya ya matumizi
mabaya ya fursa ndogo ya matangazo inayotolewa.
Ndugu Wananchi, Katika kufanikisha hayo, Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatoa maelekezo yafuatayo
kwa watoa huduma na jamii:-
1. Hairuhusiwi kwa mtu yeyote kutoa huduma za tiba asili na au tiba mbadala bila kusajiliwa.
Ninalielekeza Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kuhakikisha kuwa watoaji huduma wote wanasajiliwa kwa mujibu wa Sheria:
(a) Mijini, (Majiji, Manispaa na Miji) – usajili wao ukamilike katika kipindi cha miezi mitatu; kuanzia Januari 15, 2016 na
(b) Vijijini, Halmashauri zote zilizobaki – usajili wao ukamilike katika kipindi cha miezi sita kuanzia Januari 15, 2016. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakaye puuza kujisajili katika kipindi hicho
(b) Vijijini, Halmashauri zote zilizobaki – usajili wao ukamilike katika kipindi cha miezi sita kuanzia Januari 15, 2016. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakaye puuza kujisajili katika kipindi hicho
2. Hairuhusiwi kuuza na au kugawa dawa yoyote ile ya tiba
asili au tiba mbadala mpaka iwe imesajiliwa na Baraza baada ya
kuchunguzwa na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa ni
salama na kupewa kibali na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
3. Hairuhusiwi kuendesha kituo cha kutolea huduma za tiba asili na au tiba mbadala bila kukisajili.
4. Wizara inapiga marufuku kwa mtu binafsi au taasisi
yoyote ile kutumia kifaa au kifaa tiba chochote bila kukisajili TFDA na
kupewa kibali; na 5. Matangazo yote yanayohusu Tiba Asili na Tiba
Mbadala ambayo hayajapitishwa na Baraza yamezuiliwa kuanzia leo tarehe
15/1/2016.
Wizara inavitaka vyombo vya Habari hasa Televisheni, Radio
na Magazeti kuzingatia Sheria na Kanuni za Tiba Asili na Tiba Mbadala
inayozuia matangazo ambayo hayajachunguzwa na Baraza. Ni wajibu wa
vyombo vya habari kujiridhisha na Mamlaka husika yaani Baraza kabla ya
kutoa tangazo lolote linalohusu Tiba Asili na Tiba Mbadala.
Wizara itashirikiana na Mamlaka zinazohusika na habari na
mawasiliano kutekeleza agizo hili. Vile vile, hairuhusiwi kutoa elimu
kwa umma kupitia vyombo vya habari na mikutano ya hadhara kuhusu tiba
asili na tiba mbadala.
Ndugu Wananchi, Katika kuwezesha ulinzi wa afya za
wananchi, kila mmoja wote alinde afya yake kwa kuhakikisha kuwa huduma
anayopata ya tiba asili na tiba mbadala ni kwa mujibu wa Sheria, Kanuni
na Miongozo inayotolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto.
Ni uhakika uliowazi kuwa kwa pamoja tukiboresha huduma za
tiba asili siyo tu tutaboresha afya zetu bali pia tutaweza kuuza dawa na
huduma hizo nje ya nchi na kupata fedha za kigeni kupitia na hivyo
kuboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja, jamii na nchi kwa ujumla.
Kwa pamoja tushirikiane kuboresha huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini.
INAWEZEKANA.
Ummy A. Mwalimu (Mb) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO 15 Januari, 2016
Post a Comment