NYUMA YA MACHOZI - 21

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Moja kwa moja ushahidi wake ulikamilika alijua Jimmy ni mmoja ya watu waliombaka, alijilaumu kwa kuondoka bila siraha ambayo ingemsaidia kumaliza kazi kwani ushahidi wa kutosha kuwa Jimmy ndiye mbaya wake ulikuwa umetimia. Lakini bado aliamini Jimmy alikuwa kiungo muhimu wa kufanikisha mpango wake kabambe utakaomuwezesha kutimiza lengo lake.
SASA ENDELEA...
Baada ya Jimmy kutoka chumbani akiwa amevaa fulana alikaa pembeni kidogo na Kilole.
“Ndiyo sister karibu sana.”
“Asante sana, mbona ndugu yangu umenitupa?” Kilole alijifanya kuchangamka japo moyoni alikuwa na hasira za kuua mtu. “Nikutupe wapi wakati kila kukicha mambo afadhari ya jana.” “Samahani sister unatumia kinywaji gani?” Jimmy aliuliza huku akinyanyuka kuelekea kwenye friji. “Walaa usisumbuke nashukuru.”
Jimmy alirudi kukaa kumsikiliza Kilole aliyeonekana na haraka.
“Sasa ni hivi nahitaji msaada wako wenye malipo mazuri sana.”
“Kazi gani tena sister?”
“Nina imani michongo ya mjini unaiju vizuri nilikuwa nahitaji unga.”
“Unga! Upi?” Jimmy alishindwa kumuelewa. “Kokeni.”
“Ha! Wa nini?” alizidi kushtuka.
“Dada yako najidunga muda mrefu lakini mtu aliyekuwa akiniletea amesafiri hivyo napata shida sana kubembea.”
“Mmh! Wa shilingi ngapi?”
“Kwa vile kuna watu wangu nao wana shida nilikuwa nahitaji wa milioni kumi.”
“Ha! Mbona mwingi?” “Tatizo mwingi au niupate, mbona kila kitu unashangaa.”
“Mmh! Ulikuwa unautaka lini?” “Leo hii na fedha ipo.”
“Na kamishina yangu kiasi gani?” “Wewe unataka shilingi ngapi?”
“Si unajua kazi za hatari hata laki mbili siyo mbaya.”
“Nitakupa milioni.”
“Ooh! Asante sana.” “Samahani Jimmy simu yako ina salio nataka nimpigie mtu wa tigo,” Kilole ambaye siku zote alijengwa uwezo wa kufanya mambo na mumewe Deus hata kumfundisha jinsi ya kutumia siraha kwa utimilifu tena kwa uhakika mkubwa.
Aliamini kupitia simu ya Jimmy ataweza kuipata namba ya mwenzake ambayo ingemsaidia kumfahamu na kuweza kumtia mikononi. Jimmy bila kujua alimpa simu yake, Kilole aliichukua na kujifanya anaingiza namba, kila alilofanya alimuangalia Jimmy ambaye hakuwa na habari naye.
Aliangalia simu iliyoingia jana yake usiku muda ambao yeye alikuwepo pale, baada ya kuiona ili kujiridhisha aliangalia iliyopigwa muda mchache baada ya Jimmy kutoka nje. Jina lilikuwa moja la Rich.
Baada ya kunukuu akilini ile namba alimrudishia simu yake, Jimmy naye bila kuhoji aliipokea simu yake. Kilole alinyanyuka kwenye kochi na kuanza kutoka nje. “Basi twende kwenye gari nikakupe hiyo fedha ili jioni nije niuchukue mzigo.”
Baada ya kusema vile Kilole alitangulia kwenye gari na kumsubiri Jimmy alipokuja alimuhesabia milioni kumi na moja kisha waliagana.
“Jimmy nakutegemea, basi usiniangushe kama zile picha ambazo ninanitia wazimu.”
“Ooh! Ina maana bado wanakusumbua?”
“Hawana lolote shida yao fedha sina jinsi nitawapa.”
“Ooh! Pole sana.”
“Ya kawaida, la muhimu nifanyie kazi yangu vizuri.”
“Hakuna tatizo sister kazi yako nitaifanya vizuri.”
Kilole baada ya kuondoka njiani aliwaza mengi huku hasira zikumpanda kichwani na kutamani kuwafanyia kitu kibaya. Lakini alikumbuka upumbavu wote anaoufanya ni kwa ajili ya kutetea penzi lake kwa Kinape. Hivyo alitakiwa kuwa makini kutekeleza mipango yake bila kumshirikisha mtu moja kwa moja hasa ya mauaji.
Kilole alirudi nyumbani kujipanga kuhakikisha kazi yake ya usiku wa siku ile anaifanya kwa umakini mkubwa japo moyo mwingine ulimshauri aachane na mpango ule wa hatari. Lakini upande wingine aliamini maji kaisha yavulia nguo lazima ayaoge na liwalo na liwe.
***
Wakati Kilole akipanga mkakati wa kummaliza Happy mchumba wa Kinape ili kuhakikisha haendi kijijini. Kinape naye alikuwa na mazungumzo na mpenzi wake sehemu tulivu waliyochagua, ambaye alikuwa akiteseka na mabadiliko ya mpenzi wake yaliyoonekana kutishia uhusiano wao.
Kinape pamoja na kujitahidi kuwa karibu na Happy lakini muda mwingi alibanwa na Kilole ambaye nia yake ilikuwa kuuvunja uhusiano ule.
“Kinape pamoja na kusema kesho unakwenda kunitambulisha kwenu bado siamini najua ni kunipoza moyo lakini hunipendi tena.”
“Happy kama kusingekuwa na umuhimu wa kwenda kukutambulisha kwetu ningekaa kimya usingejua nini kinaendelea?”
“Kinape lakini umegeuka kiasi hiki, nini nimekukosea?” Happy aliuliza kwa sauti ya kilio.
“Mambo yameingiliana tu lakini muda si mrefu kila kitu kitakuwa sawa,” Kinape alijitetea.
“Kuna kitu unanificha, Kinape una mwanamke mwingine.”
“Sina mwanamke mwingine zaidi yako.”
Kinape alijitetea japo alijua ana mtihani mzito kwa Kilole, moyoni mwake hakuwa tayari kumsaliti Deus rafiki yake kwa ajili ya mpenzi wake wa zamani.
Kilichomuumiza kichwa kilikuwa ni picha za kufanya mapenzi na Kilole ambazo kwake aliamini zilikuwa bomu ambalo kama lingepasuka kusingekuwa na usalama. Moyo alijipanga kuhakikisha anamfahamu aliyefanya mchezo ule, akiwa katikati ya mawazo Happy alimshtua.
“Ha..ha..lafu mbona simuelewi shemeji yako?”
“Umuelewi kivipi? Kinape alishtuka kidogo.
“Asingekuwa mke wa kaka yako ningesema mwanamke wako.” “Kwa nini unasema hivyo?”
“Kuna kila dalili za kuwepo siri nisiyojua kuhusu mustakabali wa penzi langu kwako. Mimi si wa kukatazwa kuingia ndani kwenu, hata kama haupo bado nina haki ya kuja kwenu.”
“Nimekuelewa lakini kila kitu kitakwenda vizuri, naomba uniamini na kesho ndiyo siku yako ya kuamini kuwa penzi letu lipo hai.”
“Mmh! Nitaamini mpaka nitakapokuwa mbele ya wazazi wako na kunitambulisha kuwa mimi ni mpenzi wako mkeo mtalajiwa.”
“Tena tumepewa lile lexus kwenda nayo kwa raha zetu.” “Usiniambie!” Happy alifurahi kwa kumkumbatia Kinape na kujisahau kama muda mfupi alikuwa akilaumu.
“Hii yote kukuonesha jinsi gani ninavyo kujali na ahadi niliyokuahidi ni ya kweli.” “Asante sana mpenzi wangu.”
“Si hilo tu, brother amenipa jana milioni 50 kwa ajili ya maandalizi ya harusi yetu.” “Jamani yaani matamani siku ifike niwe nisimame pembeni yako nikiulizwa: Happy Kinape unakubali kuolewa na Kinape kama mumeo?”
“Mmh! Utajibu nini?”
“Ndiyooooooo, tena mara mia.”
“Basi nikuache akajiandae na safari, kesho alfajiri nakupitia.”
“Sawa mpenzi wangu, katika siku ambayo nitakula chakula kiteremke sehemu zake ni leo, na siku tukifunga ndoa sijui itakuwaje bado naona ndoto ya mchana.”
“Nina imani kuanzia kesho utakula na kunywa kwa furaha baada ya kukuvisha pete ya milioni kumi.” “Haaaa!” Happy alishika mikono kifuani asiamini masikio yake.
“Nataka uamini ile ahadi niliyokuahidi inatimia.” “Kinape amini usiamini mabadiko yako kama yangeendelea kidogo nilikuwa nimewaza kufanya kitu kibaya.”
“Kipi tena mpenzi wangu?”
“Haki ya nani, leo isingepita salama nilipanga kunywa sumu nifilie mbali.”
“Aah! Happy mawazo gani tena hayo mpenzi wangu?”
“Hujui tu, nimeteseka sana, nimeumia sana, hebu nitezame mimi ndiye Happy unayemfahamu nimekuwa kama mti uliokauka.”
Happy alizungumza huku akiangua kilio ambacho kilikuwa sawa na kukamua uchungu wa moyo kutokana kuteswa na penzi la Kinape baada ya kutekwa na Kilole.
“Happy mpenzi wangu yote hayo yatakwisha hata mimi najua kosa langu lilikuwa wapi.” “Naomba usinitende nakupenda sana Kinape, sioni sisikii juu yako, bila wewe mimi sipo,” Happy aliendelea kusema huku akibubujikwa na machozi. “Basi mpenzi nimekuelewa nina imani nilikuumiza lakini nakuahidi kutuliza maumivu yako yote.”
Kinape alimpeleka Happy kwao na kuamua kwenda club ili aingie nyumbani usiku sana asionane na Kilole na alfajiri awahi kuamka na kuondoka ili kumkwepa.
****
Majira ya jioni akiwa amejipumzisha nyumbani kwake alipokea simu ikiulizia mzigo wao.
“Vipi umefikia wapi?” “Kila kitu kipo sawa ila sasa hivi nina wageni muhimu naomba univumilie kidogo.”
“Mpaka saa ngapi?”
“Sijajua ila lazima usiku huu nikupe mzigo wako wote kwa vile nimekwisha uandaa kabisa.” “Sasa tuambie saa ngapi?”
“Nimepanga baada ya mume wangu kulala nitoke mara moja, ila nilikuwa naomba uje karibu na nyumbani ili nikikukabidhi nirudi haraka kabla mume wangu hajashtuka kama nimetoka.”
“Kwa hiyo saa ngapi?” “Kuanzia saa sita usiku ila uhakika saa saba.”
“Hakikisha muda huo unatupa mzigo wetu ukifanya ujanja wowote picha zako zitasambaa kila kona ya jiji.” “Walaa usitie hofu nilichowaeleza kitakwenda kama nilivyopanga, naomba usikae mbali na simu yako ili nikikupigia utokee na kuchukua.”
“Nimekuelewa baadaye.”
Kilole baada ya kukata simu alicheka na kuuapia moyo wake usiku wa siku ile utabakia historia nzito moyoni mwake. Majira ya saa moja na nusu usiku Kilole alipigiwa simu ya Jimmy kumjulisha kupatikana kwa mzigo, walielekezana pa kuonana.
Alikwenda eneo la tukio na kupewa unga wake wa shilingi milioni moja. Baada ya kuupata aliamini kabisa utamsaidia kuifanya kazi yake kwa uhakika mkubwa. Aliagana na Jimmy na kurudi zake nyumbani na kuuficha sehemu ambayo mumewe hawezi kuiona.
Baada ya kuweka mzigo vizuri alichukua bastola ya mumewe na kuichunguza kama risasi, alikuta za kutosha aliamini zitafanya kazi yake ya usiku ule aliiweka vizuri kwa kazi ya usiku ule. Alichota unga kidogo na kuuweka kwenye chakula cha mumewe ili akila alale na yeye aweze kutoka usiku ili akafanye kazi yake nzito ambayo ilimpa mtihani mzito. Baada ya kuipanga mipango yake vizuri, alitulia kusubiri muda. Mumewe baada ya kutoka kazini alimuandalia chakula.
Baada ya kula alimuomba waende wakazungumzie chumbani. Waliingia chumbani huku Deus akikisikia kichwa kizito. Hata wakuwahi kuzungumza usingizi mzito ulimpitia. **** Ndani ya jiji Sicily nchini Italia, jiji linalosifika kwa uuzwaji wa dawa za kulevywa,Teddy bado alikuwa na hasira baada ya kugundua shemeji yake ndiye aliyemchoma kwa kitengo cha kuzuia dawa za kulevya Tanzania. Kwake alimuona ni adui mkubwa asiyefaa kuendelea kuishi.
Alipanga usiku wa siku ile amuulie mbali na yeye kutimka zake kwenda mji mwingine wa Turin kuanzisha maisha mapya kwa kuamini uwezo wa kifedha ungemwezesha kuishi sehemu yoyote duniani bila tatizo.
Baada ya kugundua kuwa shemeji yake ndiye mbaya wake hakutaka kumuonesha kukasilishwa na kitendo kile. Ili kumvuta adui yake alijifanya kubadilisha msimamo kuwa amemkubali kimapenzi. Asubuhi ya siku ile baada ya kifungua kinywa alimwita Mose na kumweleza kitu:
“Mose my sweet.”
“Teddy kauli hiyo imeanza lini?” Mose alishtuka kusikia anaitwa vile.
“Leo mpenzi, nimetafakari na kuona hakuna umuhimu wa kulikataa penzi lako kwa vile wewe ni mwanaume kama wanaume wengine pia kuwa na wewe sawa na kuwa na marehemu kaka yako.”
“Umeona eeeh,” Mose alifurahi kusikia vile bila kujua aliyekuwa anazungumza naye si Teddy aliyemzoea bali malaika wa kifo.
“Unajua Mose nimekuwa sipati jibu kila nilipojiuliza kwa nini nisikukubalie uwe mpenzi wangu, lakini ujio wa safari yangu Italy ilikuwa kuja kukueleza nimekufungulia moyo wangu kwako.”
“Ooh! Asante sana, siamini kwa kweli lazima nikueleze ukweli Teddy nimeteseka kwa muda mrefu juu yako. Nina imani sasa hivi moyo wangu utapoa.”
“Najua umeumia kwa muda mrefu, nina imani kama uliteseka juu yangu basi penzi letu litakuwa lenye upendo wa dhati. Mose mpenzi naomba usinitende.”
“Teddy amini nitakupa mapenzi zaidi ya kaka, hutajutia kunikubali kuwa mpenzi wako.”
Siku ile ilikuwa yenye furaha kwa Mose lakini moyoni kwa Teddy ilikuwa ngumu sana kwake kwa kujipanga kuhakikisha kujirahisi kule kutamlahisishia kummaliza kwa urahisi. Teddy hakuona hiyana kuutoa mwili wake kwa Mose japo alikwisha muapia labda atafanya naye mapenzi akiwa marehemu asiye na fahamu.
Siku ile alijitoa ili kumvuta karibu na kuamini kabisa anachokitafuta muda mrefu atakipata. Majira ya mchana Teddy alibuku tiketi ya ndege ya kuelekea Turin saa tatu usiku, baada ya kurudishiwa taarifa ya kupatikana kwa nafasi katika ndege ya usiku ule.
Alijipanga kuhakikisha mipango yake inakwenda kama alivyopanga na saa tatu awe kwenye kiti cha ndege akihamia jiji wa Turin kuanza maisha mapya baada ya kummalizia mbali shemeji yake Mose aliyetaka kumpoteza kwenye ramani ya dunia.
Baada ya mambo yake kwenda alivyopanga alirudi kwa Mose na kuendelea kunywa katika mahaba mazito. Mose baada ya kulewa sana Teddy alitumia nafasi ile kumpeleleza kupata ukweli. “Mose mpenzi wangu kwa nini ulinichoma?” Teddy alijifanya kulalamika katika mahaba mazito.
“Teddy ulinichanganya kimapenzi kwa kweli nilichokifanya hata sielewi nilifanya nini, nilikuwa sawa na mfa maji.”
“Lakini usirudie tena, ona sasa kama ningefungwa penzi tamu kama hili ungelipata wapi?”
“Nisamehe mpenzi wangu.”
Kauli ya Mose ilizidisha machungu moyoni kwa Teddy na kuamini wazo lake na ushahidi aliopata lilikuwa sahihi.
Alijitahidi kutengeneza tabasamu la uongo ili kuvuta muda wa kummaliza Mose. Muda wote alionesha mapenzi mazito yaliyomziba masikio asijue nini kilichokuwa kikiendelea.
Itaendelea
Post a Comment