ad

ad

NYUMA YA MACHOZI -17


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Kilole alijisemea moyoni kuwa asali ile aliyomlambisha ni chambo cha kumuingiza kwenye mtego wamlipue hakuwa na mapenzi tena na mumewe na kumuona shetani wa roho yake aliyetamani afe wakati wowote ili afaidi penzi tamu la Kinape.
SASA ENDELEA...
***
Siku ya pili Kinape alichelewa kutoka kwenda kazini kutokana na ishara aliyooneshwa na Kilole kuwa asiondoke ili wazungumze. Deusi aliondoka peke yake kuwahi kazini huku akijiona alichelewa kupata dili kubwa kama zile. Alipofika ofisini aliwasiliana moja kwa moja na Teddy mwanamke muuza unga. “Haloo Teddy.”
“Ooh! Brother za asubuhi?”
“Nzuri.”
“Nina imani una habari njema asubuhi hii?”
“Ni kweli, mimi nipo tayari kuifanya ile kazi.”
“Ooh! Vizuri sana, tena una bahati washirika wangu wote wapo hapa.”
“Kwa hiyo?”
“Basi jioni tukutane ili tuzungumze jinsi ya kufanya.”
“Hakuna tatizo.”
“Nakutakia kazi njema kaka yangu.”
Deus baada ya kukata simu alitabasamu kidogo kabla ya kuanza kazi. Wakati yeye anapanga mipango ya utajiri, nyumbani kwake pia kulikuwa na mipango ya kummaliza. Kinape baada ya kujiandaa kwenda kazini kabla ya kutoka chumbani Kilole alimfuata.
“Vipi mpenzi?”
“Safi.”
“Naona jana jamaa alikuita chemba alikuambia nini, au ndiyo anataka uwahi kumuoa Happy?”
“Walaa.”
“Alikuitia nini?”
“Jamaa anataka kututajirisha.”
“Kututajilisha una maana gani?” Kinape alimueleza yote aliyoelezwa na Deus pamoja na kukatazwa kuitoa siri ile nje. Pamoja na kusikia mpango ule wa mabiloni ya shilingi bado Kilole aliona wanamchelewesha.
“Kinape hiyo fedha itapatikana lini huoni kama tunachelewa, tuachane na mpango wake tummalize tufikiri mambo mengine.”
“Kilole zile ni fedha nyingi zitakazo tufanya tuishi kama peponi, tutakula mpaka tunakufa bila kufanya kazi.”
“Kwani huo mpango mwezi gani?”
“Wanamsubiri yeye tu watu waingine unga wakati wowote.”
“Mmh! Nitavumilia lakini kwa upande wangu naona zilizopo zinatutosha.”
“Ni kweli lakini tutafanya kosa kumbwa kuacha mabilioni ya fedha.”
“Mmh! Sawa.”
****
Wakati Kilole na Kinape wanapanga mipango ya kummaliza Deus, Jimmy mpiga picha naye alikuwa akipanga yake. Aliamini kupitia picha zile atajipatia fedha na penzi toka kwa Kilole mwanamke aliyempenda kupindukia. Aliamua kumtumia rafiki yake kumtisha ili wapate fedha. Kilole akiwa katika usafi wa kawaida wa nyumba simu yake iliita, namba ilikuwa ngeni kwake. Alibofya cha kupokelea na kusema:
“Haloo.”
“Haloo, nazungumza na Kilole.” “Ndiyo, nani mwenzangu?”
“Naitwa Simon, kumeokota picha zako ambazo zinaonesha unafanya uchafu kwa hiyo ili nisizisambaze nataka milioni tano.”
“Picha zangu?” Kilole alishtuka.
“Eeh, tena unafanya uchafu na ndugu wa mumeo, kabla picha hazijamfikia mumeo tunaomba huo mzigo.”
“Na..na..omba unipigie baada ya dakika tano,” Kilole alichanganyikiwa na kuona Jimmy amemgeuka. Kwa haraka alimpigia simu Jimmy kutaka kujua picha zake zimemfikiaje mtu mwingine. Alipopiga simu iliita kwa muda bila kupokelewa, hakukoma alirudia tena na kupokewa upande wa pili.
“Haloo Sister,” Jiimy alipokea upande wa pili. “Nazungumza na Jimmy?”
“Ndiyo Sister, lete stori.”
“Jimmy nilikueleza nini?”
“Kuhusu nini?”
“Kuhusu picha.”
“Kwani vipi?” “Kuna mtu kanipigia simu anasema ameokota picha zangu kwa hiyo anataka milioni tano la sivyo atazisambaza au kumpelekea mume wangu.”
“Ha!” Jimmy alijifanya kushtuka.
“Jimmy tulizungumza nini na umefanya nini?”
“Samahani Sister, wiki mbili zilizopita nilivamiwa ndani na kuibiwa vitu vingi, nina siku mbili tangu nitoke hospitali.”
“Taarifa ulifikisha polisi?”
“Niliogopa kwa vile kulikuwa na picha zako.” “Jimmy kwa nini umekaa na picha zangu, kama pesa yako nilikulipa yote?”
“Sister niliamini picha zile ulikuwa na umuhimu sana kwako hivyo ungeweza kuzipoteza ndiyo nikaamua kuzihifadhi nyingine kwangu.”
“Sasa umeona umenitia hasara?”
“Sikujua ingekuwa hivyo.”
“Sasa nitafanyaje, utawezaje kunisaidia?”
“Dada yangu kama fedha unayo ungempa kwa kweli picha zile siyo nzuri kuonwa na mumeo.” “Nampa lakini kumbuka umenifanyia kitu kibaya sana.”
“Najua lakini nia yangu ilikuwa nzuri tu.”
“Okay, imekwisha tokea sina jinsi, ila baadaye nitakupa kazi ya kunifanyia.”
“Hakuna tatizo dada yangu ila pole sana.”
“Bado sijapoa mpaka uifanye kazi yangu kwa asilimia mia.”
“Hakuna tatizo.”
“Basi baadaye.”
Kilole alikata simu na kumpigia aliyempa taarifa ya kuokotwa kwa picha zake. Baada ya kuita ilipokelewa upande wa pili.
“Ndiyo, sema.”
”Ulisema?” Kilole aliuliza.
“Kuhusu nini?”
“Si umesema una picha zangu?”
“Ndiyo.”
“Samahani kaka angu.”
“Samahani ya nini, fedha haipungui hata senti tano kama huna niifanye kazi yangu,” upande wa pili ulimtisha.
“Kaka yangu mbona unanifanyia ukatili kama huo, nimekukosea nini mpaka kushindwa kunisikiliza?” “Dada eeh, niambie utatoa mzigo au hutoi nijue moja sikuja kubembelezana.”
“Sio kwanza sitoi, nitatoa hata zaidi lakini nilitaka kujua hizo picha umeziokota wapi na zilikuwa kwenye nini?”
“Dada yangu eeh, sipo mahakamani kama mshiko upo nijulishe nina mambo mengi, hivi unafikiri nikimweleza mumeo kuwa nina picha hizo ningepata hata mara tatu ya fedha yako.”
“Basi naomba unielekeze nizilete wapi hizo fedha?”
“Unazo sasa hivi?”
“Hapana nakwenda kwenye mashine ya kutolea fedha.”
“Basi ukiisha kuwa nazo nijulishe nikuelekeze.”
“Nielekeze wala haichuki hata nusu saa.”
“Nitakujulisha baada ya dakika tano.” Jamaa baada ya kukata simu alimgeukia Jimmy aliyekuwa pembeni yake.
”Sasa mkuu fedha ndiyo hiyo atuletee wapi?”
“Mwambie Sea Green view hotel.”
“Poa.”
“Yule mwanamke anaonekana ana fedha za kuchezea lazima tumtumie kutengeneza maisha.” “Hakuna noma mkuu.”
Baada ya mazungumzo alimpigia simu Kilole. “Haloo Sister tukutane Sea Green view hotel.”
“Nje au ndani?”
“Aah! Jambo hili si la kitoto tunatakiwa tukabidhiane ndani.”
“Mmh! Sawa.”
“Mbona unaguna?”
”Si unajua mimi mke wa mtu naweza kuingia kwenye matatizo nikionekana katika mazingira ya kutatanisha.”
“Kuachika na kuonekana kipi kibaya?”
”Mmh! Sina jinsi kisu kimegusa mfupa.”
“Nikupe dakika ngapi?”
“Sidhani itachukua nusu saa, naomba basi nikukute kwani nina haraka.”
“Hakuna tatizo.”
Kilole alijikuta akiingia katika matatizo ambayo hakuyategemea, moyoni aliapa kumfanyia kitu kibaya Jimmy ambacho hatakisahau maishani mwake. Baada ya kutoka kwenye mashine ya kutolea fedha, alielekea Sea Green view hotel. Alipofika nje ya hoteli alimpigia simu mwenye picha zake.
“Haloo nimeisha fika upo wapi?”
“Njoo ndani ghorofa ya pili chumba namba 112.”
“Mmh! Mbona makabidhiano ndani ya chumba cha hotel?”
“Kwa vile wewe ni mke wa mtu.”
“Mmh! Sawa nakuja.
” Haikumpa shida kuingia ndani bila kujulikana kutokana na kujitanda kanga iliyomfunika kichwa na kujiziba na miwani nyeusi. Aliingia hadi ndani ya hoteli na kwenda moja kwa moja kwenye chumba namba 112, kabla ya kuingia alipumua kidogo na kugonga mlango.
“Pita mlango upo wazi,” sauti toka ndani ilimjibu.
Alizungusha kitasa na kusukuma mlango, mlango ulifunguka na kuingia ndani. Alimkuta kijana mmoja aliyekuwa amekaa kwenye sofa akinywa maji yaliyokuwa juu ya meza ndogo.
“Karibu,” alimkaribisha huku akitabasamu.
“Asante,” Kilole alijibu huku akikaa pembeni yake akiwa hajiamini. “Karibu soda.”
”Hapana nina haraka fedha hii hapa nipe picha zangu niondoke.” “Sikiliza dada yangu kufanya mambo yako kwa pupa utajikuta kila siku unarudia makosa.”
“Nimekuelewa kaka yangu ila naomba unipe kwanza hizo picha mambo mengine tutapanga siku nyingine.”
“Basi kunywa soda kidogo.”
“Hapana kaka yangu nina haraka.”
“Ina maana mimi ni mjinga kukununulia soda?” Jamaa alionesha kukasilishwa na kauli ya Kilole. “Basi wacha ninywe kidogo,“ Kilole alisema huku akichukua chupa ya soda iliyokuwa imekwisha funguliwa kabisa.
Alikunywa kidogo bila kujua alikuwa amepangiwa mchezo mwingine katika soda, aliona kama inamchelewesha alikunywa yote ili awahi kuondoka. Lakini hakufanya lolote baada ya kupatwa na kuzunguzungu na kujilaza kwenye kochi bila kujua. Joe alimpigia simu Jimmy aliyekuwa nje ya hoteli.
Itaendelea

No comments

Powered by Blogger.