NYUMA YA MACHOZI SEHEMU: 16

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Deus baada ya kupata uhakika kwa Kinape alimgeukia Teddy aliyekuwa akiendelea kunywa juisi taratibu bila wasi kama hakuna kitu cha hatari kilikuwa mbele yake.
“Teddy,” alimwita.
“Abee.” “Nafikiri kila kitu kimekwenda vizuri.”
“Hakuna tatizo, naheshimu sana kazi yako pia muda wako.”
“Asante lakini kumbuka umeniweka katika wakati mgumu sana.”
“Kawaida tu kaka yangu, nakuapia ulichokifanya leo hutakijutia maishani kwako, huenda leo usione umuhimu wake lakini ipo siku utayakumbuka maneno yangu.”
SASA ENDELEA...
“Basi wacha nikutoe ili ukapumzike na safari.”
“Na kweli muda huu ningekuwa nimelala, hata chakula ningekula jioni baada ya kuamka.”
“Pole sana ni harakati za maisha.”
“Tunaweza kwenda,” Deus alisema huku akinyanyuka na kuweka vitu vyake sawa kwenye meza. Teddy alinyanyuka na kuchukua mkoba wake wenye dawa za kulevya na kuuweka begani kisha alitangulia kutoka, alipofika kwenye korido la kutokea nje alisimama kumsubiri Deus kuogopa maswali kwa baadhi ya watu ambao angekutana nao njiani.
Baada ya kuweka ofisi yake sawa Deus alitoka na kumpitia Teddy kwa kumshika mkono, kwa mtu angewaona kwa mara ya kwanza angeamini wale ni marafiki wanaojuana muda mrefu.
Lakini kumbe muda mfupi walikuwa chui na paka. Walikwenda kwenye gari na kuondoka kumrudisha sehemu aliyofikia, lakini Teddy aliomba aachwe sehemu ambako ataingia kwenye gari litakalomfuata na kwenda kwake. Wakiwa njiani Teddy alianzisha mazungumzo.
“Nashukuru kwa ukarimu wako.”
“Japo unanishukuru, lakini kumbuka nimenilazimisha nimeisaliti nchi yangu kwa damana waliyonipa ya kulinda nchi yangu.”
“Huenda leo huijui faida yake lakini narudia kukuapia msaada wako hautakwenda bure, ila nilikuwa na wazo moja.” “Wazo gani?”
“Najua kazi hii umepewa na taifa lakini kuna maisha badala ya kazi.”
“Hayo najua, ulikuwa na maana gani?”
“Hivi ukistaafu utalipwa kiasi gani?”
“Kiasi cha kawaida.”
“Nina imani hakitaweza kuyaendesha maisha yako?” “Ni kweli kabisa.”
“Sasa unaona unafanya kazi ya mamilioni lakini mwisho wa siku unakufa maskini.”
“Ni kweli, lakini kazi yetu inalenga kujitolea na si kujitajirisha.”
“Wewe unasema hivyo wakati wakubwa zako wanaokutisha usichukue rushwa, wao ndiyo wanaongoza kuwa na utajiri wa kutisha.”
“Sasa wewe ulikuwa unanishauri nini?” “Nataka kupitia kazi yako uweze kufaidika ili mwisho wa siku ulie kivulini.”
“Kwa hiyo unanishauri nile rushwa.”
“Kula rushwa siwezi kukushauri nina imani hii si rushwa ya kwanza inawezekana umeisha kula nyingi, inaonesha kabisa unakula za kawaida mimi nilitaka tufanye biashara kwa muda mwaka mmoja uwe trionea.”
“Kazi hii ukiifanyia tamaa huchelewi kushtukiwa na mwisho wa siku unapigwa chini au unategewa mtego na ukinasa unafia gerezani.”
“Biashara hiyo nataka tufanye sisi wawili.”
“Kumbuka biashara hii mwisho wake mbaya kwa mfano ungekutana na mtu aliyekunywa maji ya bendera ya taifa si ungepotelea gerezani?” “Kabla ya kupotelea gerezani yeye kabla ya jioni jina lake lingebakia historia midomoni mwa watu.”
“Una maana ungemuua?”
“Siku zote kazi na dawa.”
“Nani angemuua wakati wewe umo ndani?”
“Mtandao ni mkubwa, miongoni mwenu kuna mtu angemuua.”
“Kwa nini mnamuua?”
“Kifo chake ni kupoteza ushahidi ili wakubwa wako wapate nafasi ya kunitoa kwa urahisi.” “Kama kuna wakubwa wanaweza kukutoa kwa njia hiyo, kwa nini hukuitumia kuliko kutoa fedha nyingi kiasi hicho?”
“Hii ni biashara kati yako na mimi hivyo lazima tukubaliane tukishindani lazima nitumie ya upande wa pili ambayo huwa sipendi kuitumia kwa kuamini kila mwanadamu ni muelewa wote tunatafuta kwa njia ya halali na haramu.”
“Kwa nini usiokoe fedha nyingi kuliko kutoa bila sababu.”
“Njia ya pili ina faida na hasara zake, faida ni kutoka salama lakini hasara zake kwanza kutoa uhai wa mtu ambao kwa kupitia uwezo wangu wa kifedha huwa sipendi kuutumia.
“Pili mara nyingi unaweza kutoka salama lakini mzigo wako ukapotea mikononi mwa dola, mara nyingi ukikamatwa kwanza taarifa zako zinafika katika vyombo vya habari hata kama ukitoka unakuwa umechafuka. Na mzigo nao unakuwa katika stoo kabla ya kuteketezwa hivyo inakuwa vigumu kuupata. Kama nitatumia njia ya kutoa fedha nyingi lakini ukiuza unarudisha faida japo kidogo.”
“Inaonesha una fedha nyingi, kwa nini usiachane na kazi hatari kama hii?”
“Hakuna mwanadamu anayetosheka fedha kila kukicha matajiri wanabuni miradi kuongeza kipato.”
“Lakini si kwa kazi kama hii.”
“Basi kwa taarifa yako kuwa watu wana fedha kufuru kwa kazi hii, kutokana na uwezo wao wamekuwa wakiwatuliza wenye viherehere. Hebu tuachana na hayo naomba tufanye kazi niliyokueleza awali, kwa muda mfupi nimeamini wewe ni mtu muhimu sana kwangu.”
“Kazi gani?”
“Kwa vile upo kwenye kitengo hiki naomba utumie cheo chako kufanikisha biashara hii. Nakuahidi kila safari yangu ikivuka salama una milioni 250.”
“Una sema?” Deus aliuliza kama hakusikia. “Nitakapopita salama, nikifika nyumbani nakukabidhi milioni 250 hata kabla sijafanya biashara.”
“Kwa mwezi utakuja mara ngapi?”
“Itategemea mara moja au mara moja kwa miezi miwili.”
“Naomba unipe muda wa kufikiria jambo hili.”
“Kama ningekuwa mimi wala nisingesubiri kwani kijua ndicho hiki, ila napenda kukuonya kitu kimoja.”
“Kitu gani?”
“Kama utakubali kuufanya mpango huu ambao nakuhakikishia kwa mwezi kupitia mtandao wangu utatengeneza bilioni moja.”
“Bilioni moja?”
“Ndiyo, watu wanne wakiingia kwa mwezi mmoja utakuwa na kiasi gani?”
“Nimekuelewa na nini ulichotaka kunionya?”
“Nakuomba chonde chonde mpango hatari kama huu usimshirikishe mkeo.”
“Kwa nini?”
“Wanawake nawajua mvizuri si waficha siri kwenye wakati mgumu, kosa lolote litalotokea kwenye ndoa anaweza kutumia kukuangamiza.”
Kauli ile ilimshtua Deus kwani mipango yote ya awali aliyofanya, mkewe ndiye aliyekuwa msiri wake. Lakini alikuwa mstari wa mbele kumshauri mambo ya kimaendeleo hata baadhi ya fedha za rushwa aliziweka kwenye akaunti ya mkewe.
“Deus najua kabisa ulimshirikisha mkeo mambo yako ya nyuma, lakini kwa hili naomba iwe siri yako. Watu wengi wanaocheza michezo michafu kama hii huwaua hata wake zao pale wanapoona wamegundua kazi zao za hatari zinazoweza kuwapotezea maisha.
Lakini sikushauri umuue mkeo, ila nakuomba ili uweze kuwa tirionea kwa muda mfupi kwani mtando una watu zaidi ya kumi mwezi mmoja wote wakipitia katika mikono yako salama utajikuta ukitengeneza bilioni mbili na nusu kwa mwezi, unataka Mungu akupe nini?”
“Nimekuelewa nina imani ukiwa tayari nijulishe, tutaifanya kazi.”
“Nashukuru kuwa muelewa, huwezi kuamini wewe ni mtu wa kwanza kumueleza mpango huu wa hatari. Naomba usinigeuke unaweza kunishangaa pamoja na umbile langu dogo lakini nitakachokufanya hutasahau maisha yako yote.”
“Ondoa wasiwasi kazi itafanyika.”
“Niteremshe hapa watu wangu wamenifuata, mambo mengine tumia namba yangu hii ya simu ambayo ni watu muhimu tu wanayoijua.
” Deus alimteremsha Teddy ambaye aliingia kwenye gari lenye tinted na kutoweka kwa mwendo wa kasi na kumwacha Deus akilisindikiza kwa macho huku akiuona utajiri mbele yake.
Baada ya Teddy mwanamke hatari katika kuuza dawa za kulevya kuondoka, Deus alijikuta akipoteza ujasiri wa kulitumikia taifa na kujikuta akiota ndoto ya utajiri kwa kujiingiza kwenye biashara ya madawa ya kulevya. Aliamua kurudi ofisini kumalizia kazi zake ili jioni akakutane na Kinape akiamini kabisa rafiki yake hawezi kumweleza mtu yeyote siri ile kama livyomkataza.
*******
Wakati akiwaza yale rafiki yake Kinape alikuwa na furaha ya ajabu moyoni mwake, alipofika nyumbani Kilole alitaka kujua furaha yake inatokana na nini.
“Vipi mwenzangu leo mbona una furaha umeongezwa mshahara nini?”
“Sasa hivi mimi ni milionea.”
“Una maana gani kusema hivyo?” Kilole alihoji. Alimpa picha yote ilivyokwenda, Kilole baada ya kusikiliza taarifa ile alimweleza kitu Kinape. “Mungu mkubwa.”
“Una maana gani kusema hivyo?” “Sasa mpango wetu utakamilika.”
“Una maana gani?”
“Sasa hivi ni wakati muzuri wa kumpotezea mbali Deus.”
“Tusifanye hivyo.” “Shauri yako akigundua atakumaliza wewe.”
“Kwa hiyo unanishauri nini?”
“Kwa vile benki kuna milioni 75 zinatutosha kwangu nina milioni 24 huoni milioni 99 zitatusaidia kufanya mambo mazuri baada ya kumuua tutauza majumba yake mawili na magari kisha tutafungua mradi wowote wa kutuendeleza kimaisha na kuuhama mji huu.”
“Hapana tusimuue.”
“Lazima Deus afe, ikiwezekana kazi ifanyike leo usiku.”
“Hapana tusifanye pupa tunaweza kuozea gerezani au hata kunyongwa kama ikigundulika sisi ndiye tuliyehusika na kifo chake.”
“Sasa tufanye nini?” “Hebu nipe muda.”
“Muda gani Kinape, mchicha umeisha kolea nazi fedha za kutosha tunazo tunasubiri nini?”
“Japo lolote zuri halihitaji haraka,” Kinape alimtuliza Kilole aliyekuwa na pupa. “Mpaka lini?”
“Nipe siku mbili.”
“Na ziwe siku hizo mbili, ukizidisha utakuta mzoga wa mtu ndani.”
“Unataka kujiua?”
“Nani afe, nitamnyongelea mbali Deus.”
“Punguza pupa kila kitu kitakwenda vizuri.”
“Lazima nikueleze ukweli Kinape hakuna mwanaume chini ya jua ninaye mpenda kama wewe.”
“Hilo nalijua lakini yote uliyataka wewe.”
“Lakini kukubali kwangu kuolewa na Deus huoni faida leo hii akaunti yako kuna milioni 75 hukuwahi kuota kuingiza fedha kama hizi.”
“Mmh! Na kweli.”
***
Deus baada ya kazi alirudi nyumbani na kupokewa kwa furaha na mkewe huku Kilole akionesha mapenzi mazito kwa mumewe ili kumfumba macho kabla kumtendea unyama. Baada ya chakula cha usiku Deus alimtoa nje rafiki yake ili ampe taarifa za utajiri wa ajabu unaokuja mbele yake.
“Unataka kuniambia kwa mwezi utakuwa unaingiza milioni 1000?”
“Ndio maana yake, nataka baada ya muda nipabadilishe kijijini kwetu pawe kama peponi.”
“Mmh! Mshiko mzito kauli ya yule dada kwa miaka mitano dunia utaishika mkononi.”
“Yaani naona kama ndoto.”
“Ungekuwa mnoko ungeishia na virushwa vya milioni kumi.”
“Basi naomba siri hii isimpe mtu mwingine, nimekupa wewe mtu wa karibu hata mke wangu sitamwambia ni siri ya hatari sana.”
“Hii ni siri nzito siwezi kumwambia mtu.”
“Hujui dhamira yangu kwako, katika kila fedha itakayo ingia asilimia kumi nitachukua wewe.”
“Unataka kuniambia katika milioni 1000 zangu ngapi?”
“Milioni 100.”
“Wachaaa, usinitie uchizi kwa furaha.”
“Lazima nikujali nataka nawe kijiji upabadilishe wajue kweli watoto wao tumekuja kutafuta maisha.” “Kweli nimeamini wewe ni zaidi ya ndugu.”
“Nathamini urafiki wetu tumetoka mbali kumbuka ndoto zetu tulipanga kufanya nini?” Baada ya mazungumzo walirudi ndani, Kilole hakuwa na haraka ya kujua walichokuwa wakizungumza kwa kuamini yote angeyajua kupitia kwa Kinape. Usiku nao ulikuwa wa raha kwa Kilole kuendelea kuonesha kumjali mumewe kwa kumpa penzi tamu ambalo lilimpagawisha Deus na kujikuta akimuahidi mkewe gari la milioni 20.
Kilole alijisemea moyoni kuwa asali ile aliyomlambisha ni chambo cha kumuingiza kwenye mtego wamlipue hakuwa na mapenzi tena na mumewe na kumuona shetani wa roho yake aliyetamani afe wakati wowote ili afaidi penzi tamu la Kinape.
Itaendelea
Post a Comment