Siyo gari wala pesa, Global sasa kutoa zawadi ya nyumba
Na Mwandishi Wetu
SIYO runinga,
pikipiki, pesa wala gari, safari hii msomaji wa Magazeti ya Global
Publishers Ltd ya Uwazi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Risasi, Amani na
Championi, atamiliki nyumba.
Ataimiliki nyumba hiyo kwa utaratibu
uleule wa kununua magazeti yanayochapishwa na kampuni hiyo katika
promosheni inayotarajiwa kuanza Desemba 11, 2015, ikiwa ni mara ya
kwanza kwa zawadi ya nyumba kutolewa na kampuni inayomiliki vyombo vya
habari.
Tangu mwaka 2000 Kampuni ya Global
Publishers, imekuwa ikijihusisha na shughuli mbalimbali za kijamii
ikiwemo kutoa misaada ya kiutu na zawadi mbalimbali kupitia mashindano
na promosheni.
Kumbukumbu zinaonesha kuwa, michezo ya
kubahatisha imekuwa ikichezeshwa na kampuni mbalimbali za habari, lakini
hakuna yoyote iliyowahi kutoa zawadi ya nyumba. Zawadi kubwa zaidi
kuwahi kutolewa ni magari.
Meneja mkuu wa kampuni hiyo, Abdallah
Mrisho, amesema wameamua kutoa zawadi hiyo ya nyumba kwa nia ya
kuwarudishia wasomaji wao faida, huku wakiamini shindano hilo litabadili
maisha yao hasa kwa atakayebahatika kushinda, ili kuwa na makazi bora.
“Tunaamini maisha bora ni pamoja na
nyumba bora, sasa promosheni hii ni changamoto kwa wasomaji wetu lakini
lengo kubwa ni kuwarudishia faida kwa sababu tunaamini nao ni sehemu
yetu,” alisema.
Mbali ya kutoa misaada kwa jamii, lakini
pia kampuni hiyo imekuwa ikienzi mchango wa wasomaji wake kwa kutoa
zawadi mbalimbali kupitia mashindano kama hayo.
“Sisi siyo matajiri na hatuna fedha za
kutosha, lakini tunaguswa na maisha ya Watanzania wenzetu ndiyo maana
tuko tayari kugawana hata kile kidogo tunachopata,” anasema Eric
Shigongo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo.
Post a Comment