Rais Magufuli Atengua Uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Dkt. Edward Hoseah kutokana na kutorishwa na namna taasisi hiyo ilivyokua ikitekeleza wajibu wake katika kukabiliana na rushwa hususani kwenye upotevu wa mapato ya serikali katika bandari ya Dar es salaam.
Katibu
Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema kufuatia kutenguliwa kwa
uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa
TAKUKURU Bwana VALENTINO MLOWOLA kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.
Balozi
Sefue amebainisha kuwa, Rais Magufuli amechukua hatua hiyo baada ya
kujiridhisha kuwa utendaji kazi wa TAKUKURU chini ya Dkt. Edward Hoseah
hauwezi kuendana na kazi anayoitaka.
"Eneo
mojawapo la upotevu mkubwa wa mapato ya serikali ni Bandarini na Katika
Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Hivyo Mheshimiwa Rais amesikitishwa na
kitendo cha taarifa za kuwepo kwa vitendo vya rushwa katika eneo hilo
kwa muda mrefu lakini kasi ya TAKUKURU kuchukua hatua haiendani na kasi
anayoitaka" amesisitiza Balozi Sefue
Katika
hatua nyingine Balozi Sefue amesema, Rais Magufuli ameagiza
kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi waandamizi wanne wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU ambao walisafiri nje ya nchi
licha ya Rais Magufuli kupiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa
umma.
Watumishi
hao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas
ambao walisafiri nje ya nchi licha ya kunyimwa kibali cha safari kutoka
kwa Rais ama Katibu Mkuu Kiongozi.
Balozi
Sefue amewataka watumishi wengine wa umma kutii agizo la Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na kuonya kuwa
atakayekiuka atachukuliwa hatua kali.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
16 Desemba, 2015

Post a Comment