NYUMA YA MACHOZI - 03
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’ ILIPOISHIA:
Salome alificha siri ya Kilole kutokana na siku za nyuma kuwa na urafiki wa kimapenzi na Kinape rafiki kipenzi cha kaka yake. Kwa vile Kinape alikuwa na miezi sita toka aende mjini. Hakukuwa na haja ya kumzibia riziki kama kweli kaka yake anampenda. SASA ENDELEA...
“Basi tuachane na hayo,” Deus alibadili mada. “Vipi umempenda, kama umempenda nitafurahi siku moja akiwa wifi yangu.” “Ni haraka sana, kila kitu kizuri kinataka subira.” Kutokana na mazungumzo kupamba moto walijikuta wakifika kwao bila kujua, Deus hakutaka tena mazungumzo aliingia chumbani kwake na kujilaza. Kabla ya kulala mawazo yote yalikuwa kwa Kilole. Aliamini kabisa kama hana mtu basi nafasi ile aitumie vyema mpaka anarudi mjini awe amepata jibu la uhakika. wake kuhamishwa na wazazi wake kwa ajili ya tofauti ya dini. Deus alikuwa na Alikumbuka moyoni mwake kuna chumba hakina mpangaji baada ya mpangaji mpenzi wake anayefanya kazi katika shirika la vifaa vya Electonic kama Series Officer. Uhusiano wao ulianza taratibu, mpaka ulipofikia hatua ya kutambulishwa Deus kwa wazazi wa mpenzi wake Halima. Tatizo lilikuwa dini Halima muislamu na Deus mkiristo, wazazi wa Halima hawakuwa na pingamizi kama Deus atabadili dini kumfuata Halima.
Deus hakuwa tayari wazazi wake walisema kama ni hivyo hakuna ndoa. Deus alibembeleza wafunge ndoa ya serikali, pia hiyo waliikataa. Hakuwa na jinsi zaidi ya kukubali kubwaga manyanga kutokana na kushindwa masharti. Miezi sita ilikatika huku ukaribu wake na Halima ukipungua na mwisho kabisa ulivunjika. Wazo la kutafuta mpenzi mwingine aliliweka kando na kujikita katika kuyatengeneza maisha yake na ya wazazi wake kijijini. Baada ya kukaa kwa muda alijikuta turufu yake ya upendo anaitupa kwa Kilole, baada ya kuwaza sana usingizi ulimpitia. ********** Alishtuka jioni, baada ya kuoga na kupata chakula alikaa na mama yake, katika mazungumzo alimgusia mama yake msichana aliyekutana naye wakati akitoka kwa mzee Solomoni. “Mama wakati narudi toka kwa mzee Solomoni, nimekutana na msichana mtoto wa m.. mmm..ze..ee.ee, eti Salome yule msichana tuliyekutana naye ni mtoto wa mzee nani?” Alimuuliza mdogo wake aliyekuwa amekaa mbali kidogo. “Mmh! Kaka bado unaye, kweli kakugusa.” “Salome hebu tuambie mtoto wa nani?” Mama yao alikuja juu. “Mama si Kilole?” “Kilole huyu mtoto wa mzee Sikwera?” “Ndiye huyo huyo.” “Eeh, amefanya nini?” Mama Deus alishusha sauti na kuzungumza kwa sauti ya chini na mwanaye. “Unamuonaje?” “Kivipi?” “Hata sijui, nimempenda alivyo pia ni mchangafu akiwa ndani nyumba haizubai.” “Kwa hiyo unataka awe mkeo?” “Mama mbona kila kitu kinajieleza.” “Kwa kweli ni mmoja wa wasichana wenye heshima hapa kijijini, mengine siwezi kujua lakini ametulia.” “Mmh! Sawa.” “Vipi? Tufanye mpango?” “Kwa sasa ni maandalizi kama atakuwa tayari, basi tujipange kwa harusi baada ya miezi mitatu tufunge ndoa, vipi kuhusu elimu?” “Mi sijui labda umuulize Salome.” “Eti Salome, shoga amesoma mpaka darasa la ngapi?” “Kidato cha nne.” “Kinatosha ataendelezwa kwa vile elimu haina mwisho.” “Basi kazi hii nitaifanya na baba yako leo usiku tutakwenda kwa wazazi wa Kilole.” ******** Usiku ulipoingia wazazi wa Deus walikwenda kwa wazazi wa Kilole kupeleka ujumbe wa Deus. Walipokelewa vizuri, bila kupoteza muda waliwaeleza kilichowapeleka. “Utani huo mzee mwenzangu, Deus aache wanawake wote mjini aje atafute kijijini?” Baba Kilole alisema baada ya kusikia ombi la mzee mwenzake. “Najua utasema hivyo, kila kitu ni uamuzi wa mtu.” “Wala hatujamshinikiza, sijui kamuona leo,” mama Deus aliongezea. “Jamani kampenda au kamtamani?” “Mzee mwenzangu mpaka kuja hapa tumelijadili jambo hili kwa kina.” “Mmh! Haya, umesikia mke wangu?” Baba Kilole alimuuliza mkewe. “Mimi nafikiri hili ni jambo jema, sifikiri tunatakiwa kuhoji sana,” mama Kilole alijibu. “Mke wangu kuuliza si vibaya japo sisi wenyewe tunajua.” “Ni kweli, lakini mpaka kufunga safari basi hawakuja kufanya utani.” “Wazee wenzetu tumekusikieni tupeni muda tuzungumze naye, majibu mtayapata kesho.” “Hakuna tatizo, jambo lolote zuri linahitaji subira.” “Na kama akikubali harusi mnatazamia iwe lini?” “Amesema baada ya jibu zuri kuna miezi mitatu ya maandalizi.” “Kama ni hivyo itatusaidia nasi kujipanga.” Waliagana na kurudi nyumbani, Deus alikuwa na shauku ya kujua wazazi wake wamerudi na jibu gani. Lakini baba yake alimtuliza kwa kumweleza ujumbe umefika jibu watalipata kesho yake. ******* Baada ya kuondoka wazazi wa Deus, mama Kilole alimwita mwanaye aliyekuwa ndio kwanza ametoka kuoga. “Kilole mwanangu.” “Abee mama.” “Unajijua wewe sasa hivi umeisha vunja ungo?” “Najua mama.” “Unajua huu ni mwaka wa ngapi?” “Mmh! Wa tano sasa.” “Kwa hiyo nina imani upo tayari kwa ndoa.” “Mmh! Nitaweza?” “Kilole kila siku ulikuwa unatoroka usiku kwenda kulala kwa Kinape, bado unajiona mtoto?” “Nani anataka kunioa? Kinape! Vipi amerudi?” Kilole aliuliza kwa mshtuko. “Siyo Kinape.” “Nani?” “Mtoto wa mzee King’ole.” “Yupi?” “Deus” “Yule anayekaa mjini?” “Huyo huyo, nasikia mlionana leo.” “Mmh!” Kilole aliguna. “Mbona unaguna?”
”Lakini mama si unajua kila kitu.” “Kuhusu Kinape?” “Ndiyo.” “Wee mtoto hebu acha ujinga, Kinape atakusaidia nini?” “Mama, siwezi kuvunja ahadi yangu na Kinape, ameniahidi anakwenda mjini kutafuta maisha na akirudi anakuja kunichukua.” “Mwanangu haya si ya kuyasema kwa baba yako, ile ilikuwa siri yetu. Baba yako akijua atatuua.” “Mama mimi siwezi kuolewa na mume nisiyempenda.” “Haya maneno yaishie hapa, chonde mwanangu usiangushe, nakuomba ukubali.” “Mama kama nitaolewa nitakuwa sikuolewa kwa hiyari yangu.” “Najua mwanangu, ila nakuomba unifichie aibu hii.” “Mama Kinape nitamueleza nini? Kumbuka nilimuahidi, kuendelea kumsubiri mpaka atakapo rudi na ahadi ni deni.” “Mwanangu, sivyo vyote vinavyo ahidiwa hutimia, kumbuka Deus ni mtu mwenye uwezo mkubwa kimaisha, huoni itatusaidia hata sisi wazazi wako? Hebu ona Mariamu mumewe ana uwezo mdogo, lakini wazazi wake wanaishi maisha mazuri. Deusi amejenga nasikia mshahara wake mkubwa ana gari zaidi ya matatu tofauti na hili alilokuja nalo kama la mbunge, tena ni mtu tunayemfahamu.” “Mama nakubali kwa shingo upande, bado nampenda Kinape,” Kilole alisema huku akibubujikwa na machozi. “Najua mwanangu, lakini inaonesha Deus naye mtu mzuri, si unaona familia yetu, hebu tutoe kwenye dimbwi la umaskini nafasi hii asije pata mwingine tukaijutia.” mama yake alisema huku akiwa amemkumbatia na kumpigapiga mgongoni taratibu. “Sawa mama, sina jinsi lazima nikubali.” “Asante mwanangu.” Mama Kilole aliagana na mwanaye aliyeingia chumbani kwake kulala, alishukuru Mungu mwanaye kukubali kuolewa na Deus. Alipoingia ndani alikutana na mumewe akimsubiri. “Vipi imekuwaje?” “Hakuna tatizo.” “Amekubali?” “Ndiyo.” “Lakini kuna kitu nina wasiwasi nacho,” kauli ile ilimshtua mama Kilole. “Kitu gani?” “Kuhusu uhusiano wa Kilole na Kinape.” “Uhusiano upi?” Mama Kilole alijifanya hajui kitu.
”Wewe ndiye ulitakiwa kunifafanulia na sio kuniuliza.” “Mume wangu, ungeweka wazi ili nielewe unalenga nini.” “Ukaribu waliokuwa nao.” “Ni wa kawaida, Kinape si alikuwa kama mtoto wa familia.” “Mbona nilisikia wana uhusiano wa kimapenzi, sio tumuoze aje atutie aibu.” “Kwa kweli hilo mwenzangu nilikuwa silijui, mbona hukunieleza mapema ili nilifanyie kazi.” “Nikueleze nini wakati siku zote siri za watoto wa kike wanajua mama zao.” “Mume wangu kumbukeni mmekuwa mkitutia lawama wazazi wa kike, kuna mzazi anayetaka mtoto wake wa kike aharibike?” “Mbona mama yako ndiye aliyekuwa akinipa wepesi wa kuzungumza na wewe?” “Kwa vile alijua una nia nzuri, lakini kama ungetaka kunichezea na kuniacha asingekubali.” “Tuachane na hayo, kwa hiyo amekubali?” “Amekubali.” “Na una uhakika bado msichana?” “Mume wangu hilo swali siwezi kulijibu labda umuulize mwenyewe.” “Si swali la baba kumuuliza mtoto wa kike bali mama yake.” “Basi nitamuuliza, kama hana itakuwaje?” “Tujiandae na aibu au kupimwa kukutwa na wadudu.” “Mungu apishe mbali.” “Basi tulale ili kesho tuwape jibu lao.”
Itaendelea Jumatatu
Post a Comment