NYUMA YA MACHOZI - 04
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
“Kwa vile alijua una nia nzuri, lakini kama ungetaka kunichezea na kuniacha asingekubali.” “Tuachane na hayo, kwa hiyo amekubali?” “Amekubali.” “Na una uhakika bado msichana?” “Mume wangu hilo swali siwezi kulijibu labda umuulize mwenyewe.” “Si swali la baba kumuuliza mtoto wa kike bali mama yake.” “Basi nitamuuliza, kama hana itakuwaje?” “Tujiandae na aibu au kupimwa kukutwa na wadudu.” “Mungu apishe mbali.” “Basi tulale ili kesho tuwape jibu lao.”
SASA ENDELEA...
*****
Lakini upande wa pili wa Kilole alikosa usingizi kuwaza usaliti wake kwa Kinape mwanaume aliyemuingiza katika katika dunia ya wapendanao. Katika maisha yake aliamini Kinape ndiye mwanaume pekee katika moyo, alijiuliza atamwambia nini akimkuta ameolewa. Akiwa amejilaza chali kalalia mikono kwa nyuma, alijikuta kwenye mtihani mzito wa kuingia katika maisha ya ndoa ya mwanaume asiyekuwepo moyoni mwake. Lakini alikumbuka shoga yake Mariamu mtoto za mzee Sadiki jinsi alivyo ibadili familia yake kimaisha baada ya kuolewa na mwanaume mwenye uwezo aliyekuwa akiishi mjini. Aliufananisha uwezo wa mume wa Mariamu haukuwa mkubwa kama wa Deusi mtoto wa mzee King’ole. Deus alikuwa akimzidi mara mia mume wa Mariamu. Mume wa mariamu pamoja na kuwa amejenga nyumba hakuwa na gari, Deus alikuwa na jumba la kifahari na magari ya kutembelea zaidi ya matatu. Japo moyoni bado alikuwa amemjaza Kinape alijikuta akijisemea moyoni: “Liwalo na liwe.” Alivuta shuka na kujilaza, lakini bado usingizi ulimkimbia na kujikuta akikumbuka ahadi aliyopeana na Kinape. “Kinape nakupenda sana, nakuomba usiniache kumbuka wewe ndiye unayeijua thamani ya usichana wangu, wewe ndiye uliyenionjesha tamu ya dunia. Nakupenda kulicho kitu chochote chini ya jua.” Kilole alikumbuka siku aliyomlilia Kinape baada ya kuzijua raha za dunia. “Kilole naheshimu zawadi uliyonipa, nakuhakikishia wewe pekee ndiye utakaye kuwa mke wangu. Nakuomba usinisaliti.” “Sitakusaliti, nakupenda sana Kinape.” Kilole alipoyakumbuka yale alijikuta akitokwa na machozi kwa kuamini kilichopo mbele yake ni maamuzi mazito kama kumeza mfupa.
********
Siku ya pili familia ya mzee Sikwera ilirudisha majibu kukubali Kilole kuolewa na Deus, taarifa ilipoifikia familia ya mzee King’ole walimfikishia Deus ambaye moyo wake ulijaa furaha baada ya ombi lake la kumuoa Kilole kufanikiwa. Alipata muda wa kuonana na mchumba wake kabla ya kuelekea mjini. Iliandaliwa siku maalumu ambayo ilikuwa kufahamiana na kukubaliana kuunganisha ukoo mbili. Sherehe ndogo ilifanyika nyumbani kwa mzee Sikwera baba yake Kilole. Deus na Kilole waliwekwa sehemu maalumu kwa ajili ya kufahamia kwa karibu. Wakiwa kimya kila mtu akitafakari lake Deus alikuwa wa kwanza kuvunja ukimya. “Kilole,” Deus alianza kwa kumuita jina lake. “Abee,” alijibu huku ameangalia chini. “Naomba unitazame basi.” “Sema tu ninakusikia,” Kilole alijibu huku akiwa ametawaliwa na aibu. Deus alitumia nafasi ile kumchunguza Kilole kwa karibu na kugundua vitu vingi sana, haiba na umbile lililojengeka kike hasa. Moyoni aliona muda aliopanga wa miezi mitatu ni mrefu sana. Mvuto wa Kilole ulikuwa mkubwa baada ya kumsogelea kwa karibu. “Asante sana.” “Asante ya nini?” “Ya kukubali ombi langu.” “Mmh,” Kilole aliguna tu. “Kilole nakuahidi kukupenda kwa moyo wangu wote.” “Asante, nami pia nitakuwa mke mwema.” “Pia nakuahidi kukuendeleza kimasomo.” “Nitashukuru kwa vile kiu yangu ya kutafuta elimu haijaisha.” “Nitakuacha kwa muda kwa vile nawahi kazini, ila kila kitu nimewaachia wazazi. Baada ya miezi mitatu tutakuwa mke na mume.” “Hakuna tatizo nitakusubiri.” “Nashukuru kusikia hivyo.” Baada ya mazungumzo na sherehe iliyochukua saa sita familia mbili ziliagana, Deus aliamini kila kitu duniani hupangwa na Mungu, hakuamini kama kijijini kutakuwa na wanawake wazuri kushinda mjini. Aliapa kumlinda Kilole kwa nguvu zake zote. Upande wa pili Kilole bado mzimu wa Kinape ulimsumbua, ulijikuta akilaumu muda mrefu uliopangwa wa harusi. Wasiwasi wake mkubwa ulikuwa kwa Kinape kutokea kijijini kabla ya ndoa ya kuharibu kila kitu. Moyoni aliomba kila alichokijua ili Kinape asionekane kabla ya ndoa yake ili akikutana naye apate cha kudanganya.
BAADA YA MIEZI MITATU
Muda ulipotimu Deus alirudi mjini huku akiacha maandalizi ya harusi yake yakianza taratibu ikiwemo kuwekwa ndani kwa ajili ya mafunzo kabla ya ndoa. Deus baada ya kufika mjini aliendelea na shuhuli zake huku watu wake wa karibu akiwapa majukumu ya kufanikisha harusi yake. Muda ulipotimu Deus alimuoa rasmi Kilole na kuwa mke wake wa kufa na kuzikana. Ndoa yao ilijaa kila aina ya furaha huku Kilole ajilaumu kwa uamuzi wake wa kutaka kuikataa ndoa yake na Deus kwa ajili ya Kinape. Maisha aliyoishi kwa Deus hakuyawaza kuishi siku moja. Kwake aliamini maisha yale ni ya ndotoni kumbe yapo kweli.
KINAPE MJINI
Kinape naye baada ya kuingia mjini akiwa na shauku ya kupata maisha mazuri, lakini haikuwa kama alivyodhani. Maisha yalikuwa magumu sana kiasi cha kujiuliza maisha mazuri watu wanayapata vipi. Alijikuta akifanya kazi ngumu mshahara mdogo uliomtosha kula siku moja tu na siku ya pili alipoamka alianza upya. Alijikuta akiingia katika makundi ya wahuni ili aweze kuihimili kasi ya ugumu wa maisha kwa kulala nje ya soko kuu. Kila siku asubuhi walipo amka na kugombea kushusha mazao yaliyoingia sokoni, wazo la kuendelea kuishi mjini aliliona alifai kutokana na mateso ya kukamatwa na askari kila kukicha. Siku aliyopanga kesho yake arudi kijijini ndiyo usiku uliyokuwa mbaya kwake baada ya msako wa wazurulaji kukamatwa na kufunguliwa mashitaka. Kinape alikosa dhamana na kujikuta akihukumiwa miezi mitatu jela. Maisha aliyoishi gerezani yalimfanya kuuchukia mji. Siku alipotoka hakuwa na hamu ya kukaa mjini alirudi moja kwa moja kijijini kwao, hakutaka kuingia mchana kuhofia kuonekana na watu jinsi alivyo konda na mwili kuwa na upele na ukurutu. Aliingia kwao usiku hakuna aliyemuona. Alipofika wazazi wake walishtuka kumuona mtoto wao amedhoofu mwili. Walitaka kujua nini kimemsibu aliwaeleza: “Wazazi wangu nimekoma, kweli kiburi si maungwana jiji limeninyoosha.” Aliwaeleza yote yaliyomsibu mpaka kuingia gerezani. Wazazi wake hawakuwa na neno zaidi ya kumpokea. “Pole mwenetu hayo ndiyo maisha, tumshukuru Mungu umerudi salama, basi tusaidiane kwenye kilimo.” Kinape baada ya kurudi nyumbani kwao hakutaka kuonekana na mtu, aliishi maisha ya kujificha mpaka atakapopona upele na ukurutu. Hakuwa na hamu tena ya kusikia neno mjini, aliapa kwenda mjini kwa kazi maalumu na si kwenda kubahatisha. Kutokana na hali yake ya kukonda na ukurutu hakutaka kuonana hata na mpenzi Kilole. Alipanga hali yake itakapo imalika afya yake ndipo angeweza kujitokeza hadharani, pamoja na kuwa ndani taarifa za kuolewa kwa Kilole zilimshtua sana. Ili kupata ukweli alimuuliza mdogo wake wa kike. “Eti Eliza Kilole ameolewa kweli?” “Ndiyo kaka.” “Nasikia na rafiki yangu Deus.” “Ndiyo kaka.” “Siamini mpaka niende kwa mama Kilole anieleze ukweli, itakuwaje amuoze Kilolo akiujua ni mchumba wangu.” Kinape alijikuta akitoka ndani japo hali yake ilikuwa haijatengemaa vizuri na kwenda moja kwa moja nyumbani kwao Kilelo kupata ukweli wa kuolewa mpenzi wake ambaye ndiye aliyepanga kuwa mkewe. Njiani alijawa na mawazo juu ya usaliti wa Kilole aliyemuhakikisha kumsubiri mpaka atakaporudi. Alipofika nyumbani kwao Kilole alimkuta mama Kilole akianika mpunga, alipomuona alishtuka kwa mambo mawili. Kwanza kumuona Kinape aliyepotea miezi zaidi ya saba iliyopita, pili hali yake iliyodhoofika. Badala ya kumkaribisha alimshangaa. “Shikamoo mama,” Kinape alianza kumsalimia baada ya kugundua mama Kilole alikuwa akimshangaa. “Kinape!” Badala ya kuitikia alizidi kumshangaa. “Naam mama.” “Ni wewe?” “Ndiyo mama.” “Ulikuwa unaumwa?” “Hapana.” “Nini kimekusibu mwanangu?” “Ni habari ndefu mama.” “Hebu karibu ndani,” aliacha kazi zake na kumkaribisha ndani. Baada ya kuingia ndani alimkaribisha kwenye kigoda. “Karibu.” “Asante mama.” “Haya niambie nini kimekufanya uwe hivi wakati unasema ulikuwa huumwi?” Kinape alimueleza yote yaliyomkuta na kumfanya aishie gerezani badala ya kupata kazi. “Ooh, pole sana mwanangu.” “Asante mama.” “Inaonekana ulipoondoka hukuaga, baba yako kila siku alikuwa akilalamika, safari kubwa kama hizo unatakiwa kupata baraka za wazazi.” “Mama tuachane na hayo, kuna kitu kimoja muhimu ndicho kilichonileta hapa.” “Kipi hicho?” “Kuhusu Kilole.” “Kilole kafanya nini?” “Nasikia ameolewa?” “Ndiyo.” “Nani aliyetoa idhini ya kuolewa?” “Kwa nini unaliza swali kama hilo?” “Mama si unafahamu Kilole ni mchumba wangu?” “Najua.” “Sasa kwa nini mmemuoza kwa Deus?” “Uchumba wako na Kilole tulikuwa tunajua sisi lakini baba yake alikuwa hajui lolote, na penzi lenu lilikuwa la wizi halikuwa wazi.” “Hata hivyo lakini si mnajua mimi na mwanao tulikuwa na marengo gani katika maisha yetu?” “Nimekueleza idhini ya kuolewa kaitoa baba yake siyo mimi.” “Kwa nini hukumwambia amechumbiwa?” “Ningeanzia wapi wakati hatukujua upo wapi, ulikuja kutuaga kuwa unasafiri?” “Sikufanya hivyo, kutokana na dharula iliyojitokeza kwa hilo naomba mnisamehe.” “Sasa kama hivyo hatujui ulikuwa wapi tungeweza vipi kukusubiri mtu tusiyejua upo wapi na utarudi lini. Kuolewa ni bahati tusingeipoteza bahati ile ambayo msichana yoyote kijijini asingekubali kuipoteza” “Sawa, lakini kumbukeni wewe na mwanao mmenifanyia ukatiri mkubwa.” “Utatulaumu bure makosa umeyafanya mwenyewe.” Kinape aliaga na kuondoka huku moyo ukiwa na majonzi ya kuolewa mpenzi wake Kilole mwanamke ambaye aliamini ndiye aliyemuonesha raha ya mapenzi. Lakini hakuwa na jinsi kwa kujua siku zote mwenye kisu kikali ndiye hula nyama.
Itaendelea Jumatano
Post a Comment