ad

ad

Hafahamiki saana... Ila ndiye mkali wa Beyonce


BEYONCE Knowles ni jina la msanii marufu wa R&B, umri wake ni miaka 34, umaarufu wake umetokana na fani yake ya kuimba, umaarufu huo uliongezeka mara baada ya kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na rapa Shawn Carter ‘Jay Z’ ambaye kwa sasa ndiye mumewe.

Beyonce amefanya mengi huku ikikumbukwa mwaka 2008 aliingia kwenye Jarida la Forbes akiwa msanii wa kike anayeingiza mkwanja fedha nyingi duniani kiasi kikiwa ni dola milioni 80 (Sh bilioni 160).

Hiyo ilimfanya awafunike wakongwe katika fani yake, Madonna na Celine Dion ambao walikuwa kwenye ‘pick’ wakati huo. Baada ya hapo akaendelea kufanya mengi makubwa na hakuwahi kushuka kisanii, moja ni lile la mwaka 2014, MTV kumtaja kuwa msanii wa kike mweusi kuingiza fedha nyingi zaidi katika historia ya muziki.

Mei, mwaka huu (2015) Forbes walimtaja tena kuwa msanii wa kike anayeingiza fedha nyingi zaidi ambazo ni dola milioni 250 (Sh bilioni 525).

Unafahamu kuwa yupo mkali wake?
Jibu ni kuwa yupo, naye ni Adele Adkins ‘Adele’, staa wa R&B kutoka Uingereza, ukali wake unatokana na rekodi zilizoandikwa mwezi uliopita katika kitabu cha rekodi cha Guinness kutokana na mauzo ya albamu yaliyovunja rekodi alizoweka Beyonce.

Iko hivi!
Awali kitabu hicho kilionyesha Beyonce ndiye msanii wa kike anayeongoza kwa mauzo, rekodi hiyo aliiweka mwaka 2013 kutokana na albamu yake iliyopewa jina la Beyonce.

Saa tatu baada ya albamu kuingia sokoni iliuza nakala 80,000, ndani ya saa 24 zikawa zimeuzwa nakala 400,000, siku tatu baadaye nakala 617,223 zilikuwa zimeuzwa Marekani pekee na duniani kwa jumla ziliuzwa 828, 773.

Wakati huohuo, kwenye mtandao wa iTunes, albamu hiyo ilinunuliwa na watu 750,000, hivyo ndani ya wiki moja Beyonce aliandika rekodi ya kuwa msanii wa kwanza wa kike mweusi kuuza zaidi ya nakala milioni moja ndani ya wiki moja.

Adele vipi?
Maajabu ya mauzo ya albamu ya Beyonce yanabaki kuwa historia iliyovunjwa na Adele kupitia albamu yake iliyopewa jina la 25.

Rekodi zinaonyesha wiki moja tu tangu albamu hiyo ilipoingia sokoni Novemba 20, mwaka huu, iliuza zaidi ya nakala 800,000 kwa Uingereza na kuuza nakala milioni 3.38 nchini Marekani kwa wiki ya kwanza.

Mwanzoni mwa mwezi huu albamu hiyo yenye nyimbo 11 kwa upande wa iTunes, ilikuwa imeshafanya mauzo ya nakala 500,000, jambo linaloonyesha huenda mauzo yake yakazidi kuongezeka maradufu.

Wimbo wa Hello unaopatikana kwenye albamu hiyo umefanya maajabu baada ya mauzo ya peke yake kwa Marekani tu kufikia milioni 1.1 ndani ya wiki moja. Hiyo imevunja rekodi iliyowahi kuwekwa na Elton John kupitia wimbo wake wa Candle In The Wind uliouza nakala milioni 1 ndani ya wiki moja mwaka 1997.

Adele amefunga mwaka kwa kuuza zaidi ya nakala milioni 5 za wimbo wake wa Hello huku video yake ikiwa imetazamwa zaidi ya mara milioni 700 kwenye Youtube.

Akizungumzia mauzo hayo ambayo hasa yamefanyika nchini Marekani, anasema: “Hata mimi imenishangaza kidogo na kunishtua. Ukizingatia mimi siyo Mmarekani, labda wanafikiri nina undugu na Malkia…”

Hivi karibuni tetesi zilienea kuwa Beyonce aliomba kufanya ‘kolabo’ na Adele lakini alikataliwa, Adele alikana taarifa hizo akisema ni za uwongo. Pamoja na hivyo bado umaarufu wa Beyonce ni mkubwa lakini kama atalegeza kamba basi Adele anaweza kuchukua utawala wake mdogo-mdogo.

Beyonce Knowles
Raia: Marekani
Miaka: 34
Mume: Shown Carter ‘Jay Z’
Mtoto: Blue Ivy Carter
Utajiri: Dola 250m


Adele Adkins
Raia: Uingereza
Miaka: 27
Mpenzi: Simon Konecki
Mtoto: Angelo Konecki
Utajiri: Dola 76.5m

Powered by Blogger.