ad

ad

Shoo ya kifalme... Diamond ndani ya DAR LIVE leo


MWANDISHI WETU
Dar es Salaam
SIKUKUU ya Krismasi si ndiyo leo? Jibu ni ‘ndiyooooo!’, sasa habari kamili ni kuwa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani, wote wanatarajiwa kukutana kwenye Ukumbi wa Dar Live, Mbagala-Zakhem ambapo Simba wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ atakuwa akifanya makamuzi.
Diamond, staa ambaye anasadikika kupata umaarufu mkubwa nje ya mipaka ya nchi zaidi ya wasanii wengi wa Bongo Fleva katika historia ya muziki huo, atakuwa akitambulisha kwa mara ya kwanza wimbo wake wa Utanipenda?
Meneja wa Dar Live, Juma Mbizo amefunguka kuwa burudani itaanza rasmi asubuhi maalum kwa watoto ambapo kutakuwa na michezo mingi ikiwemo kuteleza, kubembea, kupanda ndege maalum, kuogelea kwenye bwawa kubwa la kisasa na mingine mingi.
“Watoto wote wanaruhusiwa kuja kwa kiingilio kidogo cha shilingi 2,000 tu na kupata burudani zote hizo hadi saa kumi na mbili jioni kisha itafunguliwa rasmi shoo ya wakubwa,” anasema Mbizo.

Diamond:
Nitakamua shoo live
Kuelekea shoo yake ya leo pale Dar Live, Diamond anasema: “Kwanza nitatoa zawadi kwa mashabiki wote watakaotoka bomba siku ya shoo ikiwa ni pamoja na kupiga nao picha na kuzungumza nao mawili matatu kabla sijapanda jukwaani.
“Pia nitafanya shoo ya ‘live’, ambapo nitakuwa pamoja na timu yangu nzima ya Wasafi Classic Baby (WCB). Ngoma zangu zote kali nitaziimba zikiwemo Mbagala, Mdogomdogo, Nasema Nawe, Nana, Nitarejea, Nataka Kulewa, Kesho, Moyo Wangu na huu ambao ni wimbo wa taifa kwa sasa, Utanipenda?”

Msagasumu, Diamond uso kwa uso
Bingwa wa muziki wa Singeli, Msagasumu naye atakuwepo jukwaani kupiga shoo kali.
Unajua amesemaje jamaa? Ah ah ah ah ana mbwembwe balaa, msikie hapa. “Siku zote nikiwa Dar Live huwa sikosei, nitapiga ngoma zote kuanzia Shemeji Unanitega, Huyu Mtoto, Inaniuma Sana na Naipenda Simba, yaani kwa ufupi nitafunikaaa!”
Wakali Dancers kudansi 100%
Kuthibitisha kuwa Sikukuu ya Krismasi inakwenda vizuri, mashabiki pia wategemee kuliona kundi linalobamba Afrika Mashariki upande wa kudansi, Wakali Dancers nao watakuwa jukwaani kufanya kweli.

Mshindi Ijumaa Sexiest Girl huyu hapa
Wafuatiliaji wa shindano la mwanamke mwenye mvuto (Ijumaa Sexiest Girl 2015) linaloendeshwa na Gazeti la Ijumaa kwa mara nyingine watapata fursa ya kuwashuhudia live washiriki wote walioshiriki shindano hili sambamba na kutangazwa mshindi.
Shindano hili ambalo limedhaminiwa na Hamadombe Distributor limebakiwa na washiriki watatu walioingia fainali ambao ni Asha Salum ‘Kidoa’, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na Vanessa Mdee ‘Vee Money’, leo usiku mshindi atajulikana.
Miongoni mwa zawadi atakazoibuka nazo mshindi wa shindano hili ni fedha taslim, tuzo, cheti, ofa ya bure ya kufanya shopping ya nguo na kutengenezwa nywele kwa kipindi cha miezi sita.

Unaingiaje Dar Live? Soma hapa
Burudani yote hiyo itakuwa ni kwa kiingilio cha shilingi 15,000 (kawaida) huku V.I.P ikiwa ni shilingi 30,000 tu.
Mbali na kiwango hicho, wadhamini wakuu wa shoo hii ambao ni Kampuni ya Mawasiliano ya Simu za Mkononi Airtel, kupitia huduma yao ya kijanja kimawasiliano ya Airtel Money Tap Tap watatoa punguzo la kiingilio kwa tiketi 1,000 za awali endapo utakata kwa kutumia huduma hiyo mpya.
Unachopaswa ni kuwa na kadi yako ya Airtel Money Tap Tap ambayo inapatikana kwa mawakala wote wa Airtel waliopo Temeke na Ilala na ukifika nayo Dar Live utapata punguzo la Sh 5,000 yaani tiketi ya Sh 15,000 utapata kwa Sh 10,000 na ya Sh 30,000 itakuwa Sh 25,000.

Powered by Blogger.