Mwambusi avujisha siri za Mbeya City
Dar es Salaam
KOCHA wa Yanga, Hans van Der Pluijm, kwa siku mbili mfululizo alionekana kuvalia njuga programu ya soka la kutibua na soka la nguvu huku mashambulizi yakipitia wingi zote.
Kikosi hicho kinaendelea na mazoezi yake kwenye Uwanja wa Boko Veterani, kujiweka tayari kumenyana na Wagonga Nyundo wa Mbeya City, timu ya zamani ya Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi.
Si kawaida ya Pluijm kukomaa na programu ya ‘fiziki’ na alipoulizwa, alikiri kufanya vile kutokana na aina ya soka la wapinzani wao kuwa la ‘minguvu’ tu.
Mdachi huyo aliongeza kuwa tayari amejua jinsi ya kuwamaliza kwani anajivunia uwepo wa Mwambusi ambaye anaijua fika Mbeya City, hivyo kwa kiasi kikubwa ni msaada wa kuwakabili pasipo shaka.
“Kweli nilitaka kujaribu mfumo wa soka la nguvu kutokana na upinzani wenyewe. Nimekutana nao kama mara tatu, lakini mfumo wao ni uleule (nguvu), hivyo tumeona kuna kila sababu ya kulifanyia kazi.
“Itakuwa mechi ngumu kutokana na mfumo wao, lakini kwa upande mwingine najivunia kuwa nina mtu ambaye anawafahamu vizuri (Mwambusi) nafikiri haitakuwa shida sana,” alifunguka Mdachi huyo kwa furaha.
Post a Comment