ad

ad

NYUMA YA MACHOZI - 05


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Sasa kama hivyo hatujui ulikuwa wapi tungeweza vipi kukusubiri mtu tusiyejua upo wapi na utarudi lini. Kuolewa ni bahati tusingeipoteza bahati ile ambayo msichana yoyote kijijini asingekubali kuipoteza” “Sawa, lakini kumbukeni wewe na mwanao mmenifanyia ukatiri mkubwa.” “Utatulaumu bure makosa umeyafanya mwenyewe.” Kinape aliaga na kuondoka huku moyo ukiwa na majonzi ya kuolewa mpenzi wake Kilole mwanamke ambaye aliamini ndiye aliyemuonesha raha ya mapenzi. Lakini hakuwa na jinsi kwa kujua siku zote mwenye kisu kikali ndiye hula nyama.
SASA ENDELEA... MIAKA MIWILI BAADAYE Maisha mjini yaliendelea vizuri kwa Kilole kuzidi kupendeza baada ya kupata mtoto wa kike kwenye ndoa yake. Kijijini kwao nako hakukusahau kwa kupeleka misaada ikiwemo kubadili paa la nyasi na kuweka bati. Mabadiliko yale yalifanya mama Kilole aamini kama mwanaye angeolewa na Kinape angempoteza. Maisha ya Kinape aliyajua mwenyewe kazi yake kubwa kijijini ilikuwa kulima shamba la wazazi wake na mashamba ya watu na kulipwa fedha kidogo. Ugumu wa maisha ulimfanya akate tamaa ya maisha na kuamua kuwa mvuta bangi na mlevi wa pombe za kienyeji. Matumizi yale yalimchakaza na kuoneka amechoka kama alirudishwa gerezani, wazazi wake walisikitika kwa hatua aliyofikia. Hata jina lake alilibadili na kujiita Marehemu mtalajiwa kwa vile aliamini kuwa maisha mazuri ni sawa na ngamia kupita katika tundu la sindano yeye ni wa kusubiri kufa. Kama ilivyokuwa kawaida ya Deus kila baada ya miezi sita alikwenda kijijini kuwatembelea wazazi wake, taarifa za kuwepo rafiki yake Kinape zilimfikia. Baada ya kufika kijijini alikwenda moja kwa moja nyumbani kwao na Kinape ili aonane naye, alipofika alimkuta mama Kinape aliyempokea kwa furaha na bashasha. “Karibu mwanangu.” “Asante mama, za hapa?” “Nzuri kiasi.” “Shikamoo.” “Marabaha.” “Unasema kiasi kivipi?” “Ukimuona Kinape utamtambua?” “Kivipi?” “Kinape anajiita Marehemu mtalajiwa.” “Kwa nini?”
”Amekwisha kata tamaa ya maisha.” “Kwa nini?” “Maisha ya kijijini yamekuwa magumu kwake hata huko mjini alikokutegemea anapaogopa kama kuzimu.” “Yupo wapi?” “Akitoka asubuhi kurudi jioni.” “Mmh, sasa sijajua hiyo jioni itakuwa saa ngapi? Maana nategemea kuondoka saa kumi na mbili jioni.” “Baba wala usisumbuke kumsubiri, hiyo jioni bahati lakini muda wake kabisa ni saa mbili usiku akiwa amelewa.” “Sasa mama, nataka kufufua matumaini yaliyopotea ya Kinape.” “Yapi tena hayo baba?” “Nitamchukua, nina imani kwa muda mfupi atakuwa tegemeo la familia.” “Tutashukuru, kwani tumekwisha kata tamaa na kumuachia Mungu.” “Basi mama mwambie jumapili nitamfuata au kama nitakuwa na kazi nyingi nitamtuma mtu amfuate.” “Sijui baba nikushukuru vipi.” “Wala hakuna cha kunishukuru, Kinape ni ndugu yangu wa damu siwezi kukubali kumuona akiadhirika wakati ndugu yake nina uwezo wa kumsaidia.” “Nitashukuru baba,” mama Kinape alisema huku akitaka kupigia magoti, Deus alimuwahi asifanye vile. Waliagana huku akimsisitiza asisahau kumweleza Kinape siku hiyo asitoke, jioni ilipofika Deus alirudi mjini bila kuonana na rafiki yake kipenzi. **** Kinape aliporudi alikuta salamu kwa mama yake. “Kinape, Deus alikuja.” “Shida yake nini?” “Swali gani hilo mwanangu, Deus si rafiki yako?” “Deus si rafiki yangu ni adui yangu namba moja.” “Kwa nini unasema hivyo?” “Atamuoaje Kilole akijua ni mchumba wangu.” “Kinape, maisha yako yanakushinda ungeweza vipi kukaa na mwanamke?” “Hii haikuwa juu yenu.” “Basi kwa taarifa yako huyo adui yako ndiye anayetaka kuyabadili maisha yako kwa kukurudisha mjini.” “Kufanya nini?” “Deus ni mtu mkubwa sana, siku hizi ana gari kama la mbunge, kweli duniani hakuna mtu mwembamba. Deus kanenepa huyo na kitambi juu, kaacha maagizo kuwa jumapili atakufuata uende mjini.” “Ni umaskini ndiyo utakaonifanya niende kwake, lakini niliapa sitamsamehe mpaka nakufa.” “Lakini unamlaumu bure, nina imani alikuwa hajui, kama angejua sidhani angekubali kumuoa Kilole.” “Kwa nini hakuuliza kabla ya kuoa?” “Ni wazi alifichwa.” “Kama ni hivyo familia ya kina Kilole kimenitendea unyama.” “Kwa hiyo mwanangu nakuomba usiipoteze nafasi hii, nina imani ndoto zako huenda zikatimia.” “Sawa mama nitajiandaa na safari.” “Basi acha kunywa mipombe yako ili kidogo mwili upendeze kwa siku mbili” “Nitafanya hivyo mama.” ******* Siku ya jumapili Kinape alijiandaa na safari ya kwenda mjini kwa ajili ya safari. Saa nne asubuhi gari aina ya Toyota land cruser Vx ilisimama mbele ya nyumba ya mzee Solomoni baba yake Kinape. Kinape alikuwa wa kwanza kutoka nje ili aonane na rafiki yake kipenzi Deusi. Baada ya mlango kufunguliwa, kwanza kuteremka alikuwa Salome mdogo wake Deus, alipomuona tu alipaza sauti: “Kaka Kinape mwenyewe huyo hapo,” alisema huku akigeuza shingo kumuangalia mtu aliyefuatana naye. Alikuwa kijana mmoja mtanashati alisogea hadi alipokuwa amesimama Kinape. “Habari ndugu?” “Nzuri tu, karibu.” “Nina imani wewe ndiye Kinape?” “Hujakosea ndiyo mimi.”
”Vipi wazazi wamo ndani?” “Yupo mama, baba ametoka kidogo.” “Naomba nionane naye.” “Karibu kwenye kigoda nimwite,” Kinape alimkaribisha mgeni kwenye kigoda kisha aliingia ndani kumwita mama yake. Baada ya muda mama Kinape alitoka alipomuona mgeni alimkaribisha. “Karibu baba.” “Asante, shikamoo mama. “ “Marahaba, karibu.” “Asante, mama mimi si mkaaji nimetumwa hapa na brother Deus nimfuate Kinape.” “Hakuna tatizo baba, ndugu yenu mwenyewe huyo hapo.” “Nashukuru nilipofika tu Salome kanionesha, kwa hiyo nilikuwa naomba ruhusa niwahi kuondoka.” “Hakuna tatizo hata yeye mwenyewe amekwisha jiandaa” “Basi tunaweza kwenda.” Kabla ya kuondoka mama Kinape alimwita ndani mwanaye na kumpa maneno ya mwisho. “Kinape mwanangu najua wazi ulikuwa na urafiki wa karibu na Kilole, nakuomba chondechonde achana naye, fuata kilichokupeleka. Kumbuka kosa lako moja linaweza kuwa majuto ya milele. Muogope Kilole kama ukoma muone ni shemeji yako.” “Sawa mama nimekuelewa.” Kinape na Dereva aliyetumwaamfuate aliongozana hadi kwenye gari na kuondoka pamoja. ****** Dereva aliyemfuata Kinape alimjulisha Deus kuwa wamekaribia nyumbani, Deus alimjulisha tayari yupo nyumbani kwa ajili ya kumsubiri mgeni. Sauti ya gari ilimfanya Deus asogee mlangoni kusubiri kumpokea rafiki yake kipenzi waliopotezana muda mrefu. Gari liliposimama dereva alimfungulia mlango Kinape ambaye aliteremka kwenye gari, Deus alipomuona akipaza sauti huku akitoka mbio kwenda kumpokea rafiki yake kwa kumwita jina alilolizoea. “Keiii Piii.” “Dewuuuu.” Wote walikutana na kukumbatiana kwa furaha. “Ooh, karibu sana rafiki yangu.” “Asante nimekaribia” Walishikana mikono na kuiingia ndani pamoja, wakati wanaingia Kilole alikuwa anatoka kwenye friji kuchukua juisi ya mtoto. Macho yake yalipatwa na mshtuko baada ya kumuona Kinape ndani ya nyumba yake mwanaume aliyemkimbia na hakutaka hata siku moja aonane naye na kujibu maswali ambayo aliaminbi kwake ni magumu. Kinape hakushtuka sana kwa vile alijua Kilole yupo wapi na ni mke wa mtu, Kilole glasi ya juisi ilimponyoka na kuanguka chini. “Mke wangu vipi mbona hivyo?” “Ha..ha..pana.” “Kinape, karibu sana hapa ndipo ninapoishi.” “Asante kupafahamu.” “Nina imani nilikueleza tutakuwa na ugeni, naomba basi apatiwe huduma zote muhimu kisha aoneshwe chumba chake,” Deusi alimwambia mkewe. “Ha..ha..kuna ta..ta..tizo.” Kilole alisahau kuokota glasi iliyoangukia juu ya zuria, aligeuka na kuelekea chumba cha mgeni kuangalia kama matayarisho ya mwisho kabla ya kumkaribisha chumba mgeni. Alijikuta akikosa raha kwa kitendo cha mumewe kumwingiza ndani ya nyumba yake mwanaume ambaye lazima atataka majibu ya usaliti wa ahadi yao. Alijikuta akimlaumu mumewe kwa kitendo cha kutomjulisha ni mgeni gani anayekuja. Kwa upande wa Kinape alibakia na siri moyoni hakutaka kumueleza rafiki yake uhusiano wake na Kilole. Pia alikumbuka wosia wa mama yake juu ya kuwa karibu na mke wa mtu japo alikuwa mpenzi wake. ******* Baada ya Kinape kuoga na kubadili nguo Deus alimtambulisha rasmi rafiki yake kwa mkewe Kilole. “Mke wangu, huyu ni rafiki yangu kipenzi Kinape nina imani si mgeni kwako.” “Ni kweli, lakini sikuwa na mazoea naye,” Kilole alimjibu mumewe akiwa ameangalia chini. “Kinape huyu ndiye mke wangu Kilole ambaye ni shemeji yako.” “Nashukuru kumfahamu shemeji.” “Mke wangu, Kinape atakuwepo hapa kwa muda mpaka nitakapomtafutia kazi na yeye kuanza maisha yake.” “Hakuna tatizo, karibu shemeji,” Kilole alimkaribisha Kinape kwa sauti ya chini. Baada ya utambulisho ule, Deus na Kinape walizungumza mengi wakikumbushia mambo ya miaka mingi. Deus alikuwa na furaha tofauti na Kinape aliyejifikiria atatazamana vipi na Kilole mwanamke aliyemsaliti. Usiku ulipoingia waliagana kuonana kesho asubuhi. Chumbani aliyelala usingizi uzuri alikuwa Deus peke yake lakini Kinape na Kilole kila mmoja aliwaza lake. Kilole aliamini kabisa kuolewa na Deus kumeweza kuyabadili maisha yake, alijiuliza kama Kinape ameletwa na mumewe ili amsaidie, angeweza vipi kumtimizia mahitaji yake muhimu. Aliamini Kinape pamoja na kuahidiana kuoana angempotezea muda tu na si kumtengenezea maisha yake. Alijikuta akiondoa hofu moyoni na kuwa tayari kukabiliana na maswali atakayo ulizwa na Kinape. Naye Kinape alijikuta akiumia kwa usaliti wa mpenzi wake wa kuolewa na mtu mwingine. Kilichomuuma sana kilikuwa kuolewa na mtu wa karibu na kibaya zaidi kukaa nyumba moja huku wote wakilishwa na mtu mmoja. Siku ya pili Deus baada ya kujiandaa kwenda kazini alimfuata rafiki yake Kinape chumbani kwake kumuaga. “Best mimi nawahi kazini tutaonana jioni.” “Hakuna tatizo.” “Kila kitu nimemuachia maagizo shemeji yako, nakuomba uwe huru au siyo Keiiii Piii,” Deus alikumbushia enzi zao. ‘Hakuna tatizo Dewuuuu.” Walicheka pamoja na kuagana Deus alitoka chumbani kwa Kinape na kumpitia mkewe aliyembusu kisha walisindikizana hadi kwenye gari. “Bai Bebi.” “Bai honey safari njema, kazi njema.” “Asante mke wangu.” Deus aliondoka na kumwacha mkewe akimsindikiza kwa macho mpaka alipopotea ndipo alipogeuka kurudi ndani. Alirudi taratibu huku akiwa na mawazo mengi juu ya kuwepo Kinape pale, hakutaka hata siku moja katika maisha yake baada ya kuolewa na mtu mwingine kwa kuvunja ahadi yao asikae karibu na Kinape.
Itaendelea Ijumaa
Powered by Blogger.