ad

ad

NYUMA YA MACHOZI - 06


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
...ILIPOISHIA:
Deus aliondoka na kumwacha mkewe akimsindikiza kwa macho mpaka alipopotea ndipo alipogeuka kurudi ndani. Alirudi taratibu huku akiwa na mawazo mengi juu ya kuwepo Kinape pale, hakutaka hata siku moja katika maisha yake baada ya kuolewa na mtu mwingine kwa kuvunja ahadi yao asikae karibu na Kinape.
SASA ENDELEA...
Kilole hata alipokwenda kijijini baada ya ndoa hakutaka kuonana na Kinape, aliingia kimya kimya mpaka anaondoka Kinape hakujua. Alijiuliza akimtaka mumewe amuondoe Kinape na kumtafutia sehemu nyingine atamuelewa. Jambo lingine alilojifikiria lilikuwa kama hilo litashindikana basi atatafuta mbinu nyingine kuhakikisha anauvunja urafiki wa Deus na Kinape. Baada ya kuingia ndani alifanya usafi wote muhimu, akiwa jikoni akiandaa kifungua kinywa, Kinape aliamka na kwenda hadi sebuleni. Sebule ilikuwa tupu ila runinga ilikuwa wazi, alikaa kwenye sofa viti ambavyo toka azaliwe hakuwahi kukalia. Taratibu alitembeza macho kuangalia uzuri wa nyumba ambayo ilikuwa na kila kitu, akiwa bado anashangaa alisikia sauti ya vyombo. Aliamini Kilole anaosha vyombo, alinyanyuka na kuelekea jikoni. Alimkuta akikaanga mayai huku amempa mgongo, alimsogelea taratibu bila kumshtua alipomkaribia alimsalimia. “Za asubuhi shemeji,” sauti ile ilimshtua sana Kilole na kumfanya ashike mkono kifuani. “Kilole usishtuke maji yamekwisha mwagika jione huru,” Kinape alimtoa hofu. “Sio hivyo Kinape ni wazazi si mimi,” Kilole alijitetea. “Najua, ndiyo maana nikasema jisikie huru, tupo sehemu ya watu tusije kosa mwana na maji ya moto.” “Nisamehe Kinape bado nakupenda nipo hapa kwa shinikizo, lakini mimi nilikuwa radhi kukusubiri mpaka atakaporudi,” Kilole alijikuta akiomba msamaha huku akibubujikwa machozi ya aibu. “Si kweli Kilole, kwa nini hukuwaeleza ukweli, ina maana mama yako hajui uhusiano wetu. Au ndiyo sababu ya pesa?” “Mama alikuwa anajua lakini alimuogopa baba ambaye hakuujua uhusiano wetu.” “Kilole muongo, baba yake alitufuma mara ngapi asijue?” “Kama alikuona alijua ni mzowezi si muoaji.” “Si kweli kwa nini hukumwambia kuwa mimi ndiye mumeo mtarajiwa au kwa vile sina kitu. Kumbuka Kilole mateso yote niliyoyapata mjini ni kwa ajili yako, nimefungwa kwa ajili yako kutafuta maisha mazuri ili tuje tuishi maisha mazuri. Lakini mwisho wa siku umeamua kunisaliti.” “Niamini Kinape si mimi ni wazazi wangu.” “Kwa nini hukukataa?” “Nilik...,” Kilole alinyamaza baada ya kusikia sauti ya gari, kweli alikuwa mumewe amerudi mara moja. Aliingia ndani haraka na kukutana na Kinape anatoka jikoni, alishtuka kumuona Kinape akitokwa na machozi. Hakumuuliza kitu alikwenda moja kwa moja jikoni, alishtuka kumkuta mkewe anafuta machozi alishtuka sana na kuhoji. “Vipi mbona mnalia, kuna usalama?” Kilole alishtushwa na swali la mume wake na kujilaumu kusahau kufuta machozi. “Mke wangu kuna nini mbona wote mnalia?” Kilole alikosa jibu la kumjibu mumewe alibakia ameinama huku akijiuliza mumewe kama atajua kuwa alikuwa na mahusiano na Kinape ndoa yake itakuwa hatiani. Alitamani kuomba radhi na kumweleza ukweli juu ya uhusiano wake na Kinape na kumhakikishia hawezi tena kuwa na uhusiano naye. Deus bado alikuwa yupo kwenye kizungumkuti asijue nini kimetokea muda mfupi baada ya kuondoka kwenda kazini na kumuacha Kinape amelala na mkewe akirudi ndani. Lakini amerudi na kukuta mabadiliko na mkewe kushindwa kumjibu. “Mke wangu kuna habari za msiba?” “Hapana.” “Sasa kuna nini?” Kilole aliendelea kukosa jibu kwa mumewe, Deus alimwacha mkewe jikoni na kumfuata Kinape aliyekuwa amesimama sebuleni akifuatilia jibu la Kilole ambalo alijua linaweza kuharibu ndoto yake kwa mara ya pili. “Kinape.” “Naam.” “Kuna nini mbona mnaniacha njia panda kuna kitu gani kimetokea muda mfupi baada ya kuondoka?” “Ni jambo la kijijini.” “Jambo gani lililowatoeni machozi?” “Ni kweli, sikutegemea shemeji kuniuliza swali kama lile.” “Swali gani?” Kilole mapigo ya moyo yalimwenda mbio miguu ilianza kumwisha nguvu kwa kuamini kosa moja la Kinape litayagharimu maisha yake yote. Alitamani kumuomba Kinape asiseme ukweli ambao ungemgharimu maisha yake. Alipotaka kumuomba Kinape anyamaze ili akayazungumze na mumewe ndani mdomo ulikuwa mizito alibakia akimuomba Mungu amuepushe na balaa lile. “Shemeji aliniulizia habari za rafiki yake kijijini.” “Sasa habari za rafiki yake na machozi yenu yanahusiana vipi?” Swali lile lilizidi kumuweka katika hali mbaya Kilole kwa kujiuliza yeye alimuuliza swali gani kuhusu rafiki yake lililosababisha watokwe na machozi. “Aliniulizia shoga yake aliyesoma naye ambaye alikuwa rafiki yangu wa kike, mwezi jana tumemzika baada ya kufa kwa uzazi. Kwa kweli kwangu ilikuwa sawa na kutonesha kidonda kilichoanza kupona, nilipomweleza habari zile shemeji alianza kulia kitu kilichonikumbusha maumivu ya moyo ya kumpoteza kipenzi changu aliyekufa na kiumbe changu tumboni.” “Ooh! Poleni sana, sikujua rafiki yangu kama ulipata msiba mzito kiasi hicho, Mungu atakulipia hiyo yote ni mitihani ya maisha.” Deus alimvutia kifuani rafiki yake na kumpigapiga taratibu huku akiendelea kumfariji. “Pole sana rafiki yangu Mungu atakulipia mara mbili.” “Asante.” Alimwacha Kinape na kwenda kumkumbatia mkewe aliyekuwa bado akitokwa na machozi ya hofu. “Pole mke wangu kwa kuondokewa na rafiki yako kipenzi.” “Asante mume wangu.” “Nakuombeni msahau yaliyopita kwani kuendelea kuumia ni kuingilia kazi ya Mungu na kuona kama mmeonewa lakini kumbe hiyo ni njia yetu sote tatizo kutangulia.” “Tumekuelewa, kwangu ulikuwa mshtuko ambao sikuutegemea,” Kilole alijikuta akipata nguvu za kuongeza uongo baada ya Kinape kumuokoa kwenye swali lililokuwa kama kaa la moto mdomoni mwake. “Basi jamani mimi si mkaaji nimerudia flash disic yangu niliisahau juu ya droo ya kitanda.” Deus alielekea chumbani na kumuacha mkewe akiwa bado amesimama, Kilole naye aliamua kumfuata mumewe chumbani. Alipofika alimkumbatia kwa nyuma na kusema kwa sauti ya chini. “Samahani sweet.” “Samahani ya nini tena mpenzi?” “Kwa hali uliyonikuta nayo, sikupenda upatwe na mshtuko kama ule.” “Aah, kumbe hilo mbona la kawaida, si ujajua nakupenda kiasi gani, sipendi kukuona kwenye matatizo, heri niteseke mimi si wewe kipenzi changu.” “Najua, ndiyo maana nikakuomba samahani mpenzi wangu, hata mimi sitaki nikuone unaumia kwa ajili yangu.” “Nashukuru kwa kulifahamu hilo.” “Basi mpenzi nisikucheleweshe, mke mwema ni yule anayemhimiza mumewe katika kazi zake na si yule anayemuacha akiharibikiwa.” “Asante sana mke wangu, lazima nimshukuru Mungu kunipa mke mwema.” Baada ya kuchukua Flash disc Deus alimuaga tena mkewe na kuwahi ofisini. ******** Baada ya kuondoka Kilole alishindwa amshukuru vipi Kinape kwa kumuokoa kwa mumewe kwa kuamini kama angejibu yeye lazima angejichanganya. Wakiwa wanapata kifungua kinywa, Kilole alimshukuru Kinape. “Kinape sikuwezi wewe kiboko sikutegemea ungejibu vile.” “Hiyo mbona kazi ndogo hata kama angenifumania natoka chumbani kwako bado ningeweza kujitetea na yeye angekubali kwa kukiamini nitakacho mweleza.” “Basi nilikuwa na wasiwasi na kujua talaka ipo usoni mwangu.” “Kama nilivyokueleza maji yameisha mwagika hayawezi kuzoleka.” “Usiseme hivyo Kinape, sipendi uumie kiasi hicho.” “Nimeishaumia kinachotakiwa kutuliza maumivu.” “Nitakusaidia kuhakikisha maisha yako yanakuwa mazuri.” “Sawa, lakini naomba tuishi kama mtu na shemeji yake tuondoe mazoea ya karibu yatakayo muondoa wasiwasi mumeo.” “Nashukuru Kinape kuwa muelewa, nakuhakikishia kuyasahau mateso yote ya kijijini na kuyaanza maisha mapya.” MWAKA MMOJA BAADAYE Maisha ya Kinape yalibadilika kutokana na kazi aliyokuwa akifanya, hata hali ya mwili ilikuwa ya mvuto kutokana na maisha aliyokuwa akiishi. Kilole alijikuta akivutiwa na Kinape kila alipopita au alipokuwa amekaa alimwangalia sana. Tofauti ya Deus na Kinape ilikuwa katika mavazi, Deus siku zote alivaa nguo za heshima muda wote tofauti na Kinape alivaa nguo zinazokwenda na wakati kama jeans tisheti na raba za bei mbaya kutokana na pesa aliyokuwa akipata. Kinape alijipenda kwa kujipulizia manukato ya bei mbaya kifuani alikuwa na mkufu mkubwa wa dhahabu. Kila mwanamke alitaka awe wake, lakini alichagua msichana mmoja ambaye aliamini ndiye anayefaa kuwa mkewe baada ya kila kitu kwenda vizuri. Hakuisahau familia yake kitu ambacho siku zote alisisitizwa na rafiki yake ahakikishe kipato anachokipata aikumbuke familia yake kijijini pamoja na kufanya marekebisha ya makazi ya wazazi wake. Kinape alikuwa makini sana katika maisha yake hakutaka mchezo kabisa. Mvuto wake machoni kwa wanawake ulikuwa mateso mazito kwa Kilole na kujikuta akimuona Kinape kama mwanaume pekee mwenye mvuto na uwezo wa kitandani tofauti na Deus, ambaye hakuwa mtundu sana kitandani zaidi ya upendo wa dhati. Kilole alijiuliza atawezaje kumsogeza karibu Kinape ambaye tayari ameisha jitangaza kuwa ana rafiki wa kike ambaye wakati wowote atatambulishwa kwao. Kila alipokuwa Kinape peke yake alitamani kuzungumza naye ili kumweleza jinsi gani anavyoteseka juu yake. Japo hakutaka kuachana na mumewe lakini shida yake wawe karibu ili kukumbushia mapenzi yao ya zamani ambayo aliamini hakuna mwanaume mwingine wenye kumpa raha kama Kinape.
Itaendelea Jumatatu
Powered by Blogger.