ad

ad

HADITHI : NYUMA YA MACHOZI - 01


SI KILA CHOZI LIDONDOKALO, hudondoka kwa huruma au maumivu, mengine nyuma yake yamebeba siri nzito. Siku zote siraha ya mnafiki huwa machozi, unaweza kuona anakuonea huruma kumbe kikulacho kinguoni mwako, anakutafuna taratibu ukishtuka amekumaliza. Deusi aliamini wote waliomlilia siku ya hukumu yake hasa mkewe na rafiki yake kipenzi walikuwa na uchungu wa kweli, lakini kumbe ilikuwa siri nyuma ya machozi. Ukitaka kujua yote naomba twende pamoja katika hadithi hii tamu. TWENDE SASA….

Gari aina ya Toyota Land cruser GX lilionekana likitembea taratibu mbele ya lango kuu la gereza la Segerea. Askari magereza wa zamu alilifuatilia lile gari huku moyoni akiamini kazi anayofanya na mshahara anaopata kununua gari lile ingebaki ndoto ya mchana.
Aliliona gari lile likisimama na kutulia kwa muda bila kufunguliwa mlango, kutokana na uzuri wake aliendelea kulitazama kwa matanio huku akijisemea moyoni’ Wenye fedha wanafaidi.” Baada ya dakika kumi mlango wa gari ulifunguliwa na kuteremka mwanamke mmoja aliyeonekana mjamzito, maisha yake mazuri, akiwa na kitoto kidogo cha kike cha miaka mitatu. Baada ya kutoka nje ya gari, yule mama alichuchumaa kuzungumza na kile kitoto. Baada ya muda yule mwanamke aliingia kwenye gari na kuondoka akimuacha mtoto amesimama peke yake. Alikuwa na boksi la biskuti ameshikilia sambamba na bahasha iliyofungwa kwa uzi mkononi. Kitendo kile kiliacha maswali mengi kwa askari , mbona kitoto kidogo kimeachwa pale. Wazo la haraka lilimjia huenda amekwenda sehemu mara moja atarudi kumchukua mwanaye. Lakini muda uliendelea kukatika bila kuonekana, na kitoto kile kiliendelea kusimama palepale kilipoachwa bila kujitikisa. Wakati huo wingu zito lilitanda na mvua ilianza kunyesha kitoto kile kikiwa pale pale huku kikiangua kilio cha kutaka msaada. Askari magereza alitoka kwenye lindo lake na kukifuata ili kukiondoa kwenye mvua. Alikibeba mpaka kwenye kibanda chake na kukiketisha kwenye benchi, ilibidi aingie kazi ya ziada kukimbembeleza kutokana na kumlilia mama yake. Jicho la askari lilitua kwenye bahasha aliyofungiwa mkononi yenye maandishi makubwa, MKUU WA GEREZA. Alishtuka na kujawa na mawazo mengi juu ya barua ile, alijiuliza kwa nini haikupelekwa moja kwa moja kwa mhusika au kulikuwa na ajenda gani kuachiwa mtoto mdogo barua ya mkuu wa gereza. Wasiwasi wake mkubwa alifikiria labda yule ni mtoto wa pembeni wa mkuu wa gereza hivyo aliletwa pale ili kumsusia. Hakutaka kumpeleka moja kwa moja kwa mkuu wa gereza, kuhofia kuleta mtafaruku ndani ya ndoa yake. Alimuita askari mwenzake aliyekuwa akipita. “John hebu njoo.” “Okote umeamua kuingia lindo na mwanao?” “Kaka wee acha, kuna gari moja la kifahari limesimama mbele ya lango kuu na kumuacha mtoto huyu.” “Halafu waliomuacha walikueleza nini?” “ Lilisimama kule, nilijua labda wamemwacha watamrudia, lakini mpaka mvua inateremka sikuona gari wala mtu. Ilibidi nikamchukue na kumuhifadhi hapa, kilichonichanganya na kutaka msaada wako ni barua aliyokuwa amefungwa mkononi , imeandikwa mkuu wa gereza.” “Eti?” “Imeandikwa mkuu wa gereza,” Okote alirudia kusema. “Sasa mkuu wa gereza na mtoto huyu wanahusiana nini?” “Kuna kitu kimenitisha.” “Kipi hicho?” “Huenda mkuu alimpa mimba mwanamke, leo ameamua kumletea mtoto hapa.” “Mmh! Inawezekana, kwani si yupo ofisini kwake?” “Sijui, nilikuwa naomba msaada niangalizie kama yupo tumpeleke mtoto na barua” “Gari lake sijaliona kupita atakuwa yupo.” “Basi naomba unipelekee na kumpa maelezo haya.” Alikubali kumpeleka, alimbeba na kuelekea naye kwenye ofisi ya mkuu wa gereza, mlango ulikuwa umefungwa, mlinzi wake alimuuliza. “Vipi John mbona na mtoto ofisini?” “Nina shida na mkuu.” “Shida gani?” “Sefu, shida ya mkuu nikueleze wewe?” “Ok, ingia.” John aliingia hadi mapokezi, sekretari naye alishtuka kumuona John amembeba mtoto. “John, vipi mtoto anaumwa mbona hivyo?” “Hapana nina shida na mkuu.” “Sasa hivi amesema hataki kuonana na mtu ana kazi nyingi.” “Najua lakini kuna mzigo wake.” “Huyo mtoto?” “Ndiyo na barua,” alimkabidhi barua ambayo aliisoma na kukutana na jina la Mkuu wa gereza. “Umemtoa wapi?” “Kuna mwanamke kamtelekeza hapo nje na kuondoka.” “Mmh, isiwe nyumba ndogo?” Suzy alisema kwa sauti ya chini. “Hata mimi ndiyo wasiwasi wangu.” “Hebu ngoja nimpigie simu nimsikie anasemaje, unajua John hii kashfa.” “Tena inabidi tusijichanganye tutakimbia kazi.” Suzy alimpigia bosi wake simu. “Halo Afande kuna ugeni wako mzito.” “Nani?” “Kuna mtoto katelekezwa nje ya gereza mkononi ana barua yako.” “Barua yangu! Inasemaje?’
”Hatujaisoma afande ila kuna jina la mkuu wa gereza.” “Mmh! Hebu mlete ofisini haraka.” John alimbeba mtoto na kuingia naye ofisi kwa mkuu wake, baada ya kupiga saruti alimtua mtoto . Mkuu wa gereza alimuangalia yule mtoto lakini hakugundua kitu chochote katika uso wa mtoto. “Nipe hiyo barua,” John alimkabidhi na kusubiri maelekezo. Mkuu wa Gereza Mzee Sikamtu aliifungua ile barua na kuisoma kwa muda kisha alishusha pumzi na kusema: “John.” “Naam afande.” “Nenda gerezani kaniletee mfungwa Deusi Ndonga njoo naye mara moja,” alisema huku akiweka barua juu ya meza. Baada ya maelekezo John alipiga saruti na kugeuka kisha aliondoka kwa mwendo wa ukakamavu.
********
Ndani ya gereza Deusi Ndonga alikuwa amejiegemeza kwenye ukuta huku maumivu ya moyo wake yalikuwa makubwa zaidi ya yale ya kufungwa gerezani miaka saba. Lakini kitendo cha usaliti wa mkewe Mwaka mmoja toka aingie gerezani kwa kosa la kukamatwa na dawa za kulevya ambazo aliamini kabisa ule ulikuwa mtego alitegewa na bosi wake. Kila dakika aliiona kama njozi ya mchana isiyo na ukweli wa kumuona mkewe akiwa mjamzito, mimba ambayo haikuwa yake. Akiwa katikati ya mawazo jina lake liliitwa. Alinyanyuka na kusogea mlangoni. “Deus unaitwa na mkuu wa gereza.” Deusi alitoka chumba cha gereza na kufuatana askari aliyetumwa na mkuu wa gereza. Akiwa nyuma yake, alijawa na mawazo na kujiuliza mkuu wa gereza anamuitia nini. Na kwa nini amuite ofisini kwake. Alipofika nje ya ofisi John alimweleza Deusi asubiri na yeye kuingia ofisini kwa mkuu wa gereza. Baada ya muda alitoka na kumweleza aingie, alipoingia moyo wake ulishtuka kumuona mtoto pale ofisini. Lakini hakutaka kuhoji kitu kwa vile aliitikia wito si kuuliza swali. “Deusi,” mkuu wa gereza alimuita baada ya kuketi kwenye kiti. “Naam mkuu.”
”Unamfahamu huyu?” alimuuliza huku akinyoosha mkono kwa mtoto mdogo aliyekuwa ameketi kwenye kochi. “Ndiyo mkuu.” “Unamfahamu vipi?” “Ni mwanangu,” Deusi alijibu kwa utulivu. “Shika barua hii usome,” aliipokea na kuanza kusoma taratibu. Alitembeza macho taratibu kusoma herufi moja baada ya nyingine, kila alichosoma kilikuwa sawa na kuupasua moyo wake kwa kisu butu bila ganzi. Mkuu wa gereza alimfuatilia Deusi alipokuwa akisoma barua huku akishuhudia michirizi ya machozi ikiteremka kwenye mashavu yake. Mishipa ya kichwa ilimsimama na macho kuzidi kuwa mekundu ikifuatiwa na kamasi nyepesi, baada ya kuimaliza kuisoma barua alimwangalia mwanaye aliyekuwa amekaa kwenye kochi akishangaa picha ya mkuu wa nchi iliyokuwa ofisini huku akiendelea kutafuna biskuti zake. Baada ya kumwangalia mwanaye aliyemuonea huruma huku moyo wake ukiongezeka maumivu mara dufu. Katika maisha yake kitendo cha yeye kufungwa gerezani hakikumuumiza moyo wake kwa kuamini ile ni mitihani ya maisha, mwanadamu anatakiwa kupambana nayo. Lakini pigo zito la kwanza lilikuwa kumuona mkewe akiwa na ujauzito usio wake, akiwa bado katika maumivu ya mkewe kukosa uaminifu mwaka mmoja baada ya kifungo chake. Pigo zito zaidi ya bomu la kilo 1000 lililousambalatisha moyo wake lilikuwa kwenye ile barua. Barua ilikuwa imeandikwa hivi: Dear zilipendwa, mume wangu wa zamani, najua kidonda cha kuona mwanaume mwenzako kunijaza tumbo bado hakijapona, lakini sina jinsi, siku zote punda unaweza kumlazimisha kumpeleka mtoni, lakini huwezi kumlazimisha kunywa maji. Hii ilikuwa sawa na tamaa ya wazazi wangu kunilazimisha niolewe na wewe, mwanaume asiye chaguo langu. Walijua kabisa chaguo la moyo wangu ni Kinape. Kuolewa nawe ilikuwa sawa na punda kumlazimisha kuingia mtoni lakini ilikuwa vigumu kuendelea kuwa na wewe kwa vile si chaguo langu. Baada ya kufungwa kwako ilikuwa ni nafasi yetu ya kujinafasi kufanya mapenzi kwa uhuru mkubwa. Kwa muda mrefu tulikuwa tukifanya kwa wizi, najua itakuuma sana na kuupasua moyo wako kwa kisu butu bila ganzi. Lakini ukweli unabaki palepale nilikuwa sikupendi na sitakupenda milele. Kama Kinape angekuja mapema hata huu uchafu wako usingeingia tumboni mwangu, nilipanga kukinyongea mbali. Lakini moyo wa huruma ulinijia wa kuidhuru damu yangu ilinishika. Nimeamua kukuletea mtoto wako ili ukae naye gerezani. Siwezi kumtunza mtoto wa mwanaume nisiye mpenda, siwezi kuchanganya mtoto wa njiwa na bundi. Mimi kuolewa na Kinape sawa na mshare umerudi porini haukupotea, sasa hivi mimi ni mke mtarajiwawa Kinape. Nakutakia maisha marefu yenye furaha na mwanao gerezani. Ni mimi dear zilipendwa Kilole. Mkuu wa gereza alimshuhudia Deusi akiwa naye kimwili lakini kiakili alikuwa mbali sana, alimuita. “Deusi...Deusi.” “Haiwezekani... haiwezekani, kwa nini lakini, kwa nini mke wangu unanitendea unyama kama huu. Nimekukosea nini? Kwa nini unamtesa mtoto asiye na hatia, kwa nini unanisaliti na rafiki yangu. Eee Mungu kosa langu nini, haya huyu mtoto mdogo nitamweka wapi, anajua nimefungwa anakuja kuniterekezea mtoto. ” Deusi alishindwa kujizuia aliangua kilio cha sauti ya chini. “Deusi pole,” Afande John alimtuliza. “John,” Mkuu wa gereza alimuita. “Naam afande.” “Nipe nafasi nizungumze machache na Deusi.” Baada ya John kutoka, alitulia kwa muda akimwangalia Deusi aliyekuwa akitoa kamasi kwa mkono na kufuta kwenye shati lake. Alinyanyuka na kwenda kwenye friji ndogo ya ofisini na kutoa chupa kubwa ya maji yaliyokuwa nusu na kummiminia kwenye glasi kisha alimpa Deusi. “Pole sana Deusi, naomba unywe maji haya kwanza.” Deusi aliipokea glasi na kuyanywa maji yote kwa mkupuo kisha aliiweka glasi juu ya meza. “Deusi.” “Naam mkuu.” “Kwanza pole sana.” “Sijapoa mkuu.” “Kuna siri gani kati yako na mkeo?”
Powered by Blogger.