ad

ad

EFM Radio yaibuka mshindi wa tuzo ya kituo bora cha redio kwa mwaka 2015

Meneja Mahusiano wa E-fm Dennis Ssebo (kulia) akikabidhi tuzo kwa Mkurugenzi wa kituo hicho bwana Francis Ciza (kushoto).
Kwa mara ya kwanza nchini Tanzania, tarehe 11/12/2015, siku ya Ijumaa ni siku ambayo haiwezi kusahaulika kwa radio changa na bora kama EFM ambayo inatangaza kutoka jijini Dar Es Salaam.

Mkurugenzi wa kituo hicho bwana Francis Ciza (kushoto) akiwa na tuzo baada ya kukabidhiwa.

Ilikuwa katika Hoteli ya Hyatt Regency ambayo zamani ilijulikana kama Kilimanjaro Hotel  ambako  waandaaji wa Tuzo hiyo Tanzania Leadership Awards  chini ya usimamizi wa Taasisi maarufu ya Kimataifa  – Purple Cow waliweza kuiandika historia ya Efm nchini Tanzania.

Waandaaji  wa Tuzo hiyo Tanzania Leadership Awards walitumia vigezo sahihi vya utoaji tuzo kwa kila mtu au kampuni ambazo zilifanya vizuri katika biashara kwa mwaka 2015

Katika Kampuni zote za biashara zilizoingizwa kwenye kinyang’anyiro hicho, EFM iliibuka kidedea ikiwa na miezi 18 tu tangu kuanzishwa kwake na imeonesha mafanikio makubwa kutokana na jitihada zake katika utendaji kazi hali ambayo haikushangaza wengi na  hivyo ikafanya kuwa ya kwanza ikifuatiwa na TBC Taifa.

Baada ya kamati kuu kukaa na kutathmini, pamoja na kura zilizopigwa na watu walioshiriki, 93.7 EFM radio ilichaguliwa kuwa kituo bora cha redio cha mwaka. Hatimaye majira ya saa mbili usiku ikatangazwa kuwa mshindi wa Kituo Bora cha Redio mwaka 2015.

Meneja Mawasiliano na Mahusiano wa EFM Dennis Ssebo ambaye aliipokea tuzo hiyo kwa niaba ya EFM, anasema pamoja na kujipongeza wao wenyewe, wafanyakazi wote wa Kituo hicho, lakini kwakutambua umuhimu na mchango wa Wasikilizaji na wadau wote wa Efm,  Tuzo hiyo  wanaitoa kwao na kuwakaribisha wadau wengine nao kushirikiana na kituo hiki bora cha Radio ili kiweze kusonga mbele.

Akizungumza baada ya ushindi huo Ssebo alisema, “Sina wasiwasi kwa mafanikio haya kwasababu juhudi zetu zinajidhihirisha wazi na hatuna hata miaka miwili katika biashara hii lakini kwa kipindi hiki kifupi tumekuwa miongoni mwa  redio bora na zenye wasikilizaji wengi jijini  Dar Es Salaam, na hata kuvifanya vituo vingine  Vikubwa na vikongwe vya radio kuvutiwa na aina ya utangazaji wetu. Hivyo, kwa mtazamo wangu  mafanikio haya sio madogo”.

Tunaipongeza sana  EFM kwa mafanikio hayo makubwa ambayo yanatokana na juhudi za uongozi na wafanyakazi wote wa kituo hicho, huu ni mwanzo tu, lakini tunaamini kwamba mkiendelea kwa kasi hii mliyoanza nayo mtafika mbali .
Ushindi wenu huu,  ni changamoto kwa Vituo vingine vya Radio nchini ambavyo vinapaswa kuwa makini na kutambua  uwepo wenu katika Soko.
Powered by Blogger.