Serikali Yatoa Masharti Kwa Watumishi wa Umma Kusafiri Nje ya Nchi
Ofisi
ya Rais imesambaza mwongozo unaoweka masharti ambayo watumishi wa umma
wanaotaka kusafiri nje ya nchi watatakiwa kutimiza ili wapewe kibali,
ikiwa ni mkakati wa kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kudhibiti
safari holela za nje.
Rais
alitoa agizo hilo baada ya kikao baina yake na makatibu wa wizara
kilichofanyika Ikulu siku chache baada ya kuapishwa, akisema ofisi yake
ndiyo itakayotoa kibali kwa watumishi ambao wana safari za nje.
Kwa mujibu wa waraka huo, sharti la kwanza linalotakiwa kuzingatiwa na watumishi hao ni kuomba kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Pili,
kwa mujibu wa mwongozo huo, maombi yawasilishwe kwa msajili wa hazina
kabla ya kwenda kwa katibu ili aweze kujenga hoja kwa kuzingatia umuhimu
wake na tija itakayopatikana kutokana na safari hiyo.
Tatu,
mtendaji mkuu wa shirika au taasisi lipime maombi ya safari husika ili
kuona kama yana tija na yana umuhimu wa kuombewa kibali kwa katibu mkuu
kiongozi, kabla ya kuwasilishwa kwa msajili wa hazina, kwa mujibu wa
mwongozo huo.
Sharti la nne, lina vipengele vitano ambavyo vinatakiwa kuzingatiwa wakati wa kuwasilisha hoja ya safari.
Kipengele
cha kwanza ni chanzo cha safari husika, cha pili ni faida yake, tatu
kwa nini ni muhimu kwa safari hiyo kufanyika na isipofanyika itaathiri
vipi.
Kipengele
cha nne kinachambua gharama za safari, kikiweka masharti yanayomtaka
mwombaji aainishe gharama ya tiketi ya ndege, posho za safari husika,
mlipaji wa gharama za safari na uwezo wa taasisi kifedha.
Kipengele
cha tano cha sharti la nne kinamtaka mwombaji aeleze manufaa ya safari
hiyo kwa taasisi na Taifa kama imewahi kufanyika huko nyuma.
Akizungumzia
hilo, Balozi Sefue alisema ni kweli ofisi ya Rais ilituma taarifa ya
kupiga marufuku safari za nje na kinachofanywa na ofisi za umma ni
taratibu za safari hizo zisizoepukika.
Alisema
tangu Rais Magufuli apige marufuku safari za nje, ofisi hiyo imesambaza
agizo hilo katika ofisi za umma kuwa ni marufuku mtumishi wa umma
kusafiri isipokuwa kwa kibali, kiwe cha Rais au cha Katibu Mkuu
Kiongozi.
Alisema
miongozo ya safari hizo inazitaka ofisi za umma kuhakikisha kuwa ombi
la kila anayetaka kusafiri, lichujwe na kuhakikisha safari yake
haiepukiki.
“Ofisi
inapoleta maombi kwetu ijiridhishe kuwa haiepukiki. Maombi mengi
yataishia kwenye ofisi zao, ikija kwetu inatakiwa ionyeshe wazi kuwa
haiepukiki na tukipima vigezo vyake na kuona haviridhishi, tunaweza
kuikataa vile vile,” alisema.
Alisema
miongozo iliyobandikwa katika ofisi za umma kuhusu safari za nje ni
taratibu ambazo zinafuatwa na taasisi baada ya agizo hilo kutoka ofisi
ya Rais.
Ofisi
za umma zilipokea barua kutoka kwa msajili wa hazina, yenye kumbukumbu
namba CEA.111/372/01 iliyowasilishwa Novemba 12 mwaka huu ikielekeza
kuwa Rais Magufuli ametoa zuio la jumla la safari za nje ya nchi katika
utumishi wote wa umma na mihimili yake.
Zuio
hilo linayagusa mashirika na taasisi zote za umma. Barua hiyo ya
msajili ilieleza kuwa zuio hilo litadumu hadi pale itakavyoelekezwa
vinginevyo.
Post a Comment