Malaika ‘Nguo zangu za ndani simpi dada anifulie’
KAMA kawa, kama dawa! Makachero wa Mpaka Home wiki hii walimuibukia,
mtoto mzuri anayetamba na Wimbo wa Zogo, Diana Exavery Clavery
‘Malaika’. Nyumbani kwake Kunduchi jijini Dar anaishi na mpenzi wake
aitwaye Steven lakini mara nyingi anakuwa peke yake kwani bebi wake huyo
ni mtu wa kusafirisafiri- mfanyabishara.
Mbali na wimbo huo wa Zogo kufanya
vizuri katika vituo mbalimbali vya redio Bongo, msanii huyo ameshatamba
na Wimbo wa Naenda, Mwantumu na Sare…
Yafuatayo ni mahojiano kati ya Mpaka Home Next Level na Malaika:
Mpaka Home: Habari yako
mrembo na hongera kwa usafi maana nyumba yako inapendeza na moja kwa
moja tunaomba utupe ratiba yako ya kila siku uamkapo.
Malaika: Asante. Mimi
bwana nikiamka kitu cha kwanza kabisa ni kuangalia simu. Naperuzi
mitandao kujua kama kuna kitu kipya nimetumiwa. Maana usiku huwa nazima
simu na mimi kila kitu nafanya kwenye simu. Kuanzia muziki wangu na hata
biashara zangu.
Mpaka Home: Biashara utazizungumzia baadaye, hebu tuambie baada kuangalia simu huwa unafanya nini?
Malaika: Naenda kuoga,
nasafisha uso na baada ya hapo nafanya usafi chumbani kwangu kisha dada
anakuwa ameshatengeneza chai lakini mara nyingi mimi sinywi chai,
nakunywa juisi peke yake, biashara ya asubuhi inakuwa imeisha.
Mpaka Home: Enhe, baada ya chai?
Malaika: Namwita dada,
tunapanga vitu vya kupika mchana kisha nakwenda zangu benki kufanya
miamala ya kibiashara. Nauza pochi ambazo tunaziuza pia kwa njia ya
mtandao, pia tunatengeneza bidhaa mbalimbali ambazo zinakuwa na picha ya
mhusika kama vikombe na vitu vinginevyo kwa oda maalum.
Mpaka Home: Usafi wa nguo zako hususan za ndani huwa anakufulia dada au wewe mwenyewe?
Malaika: Wee, za ndani huwa simpi dada. Atafua nyingine zote lakini si za ndani.
Mpaka Home: Shemeji akiwepo anapendelea kupikiwa na dada au wewe?
Malaika: Akiwepo huwa
nampikia mwenyewe. Anapenda tambi, alikuwa hapendi ugali lakini kwa kuwa
mimi ni fundi wa kupika, nimemshawishi sasa hivi anakula.
Mpaka Home: Uborekapo nyumbani, huwa unafanya nini?
Malaika: Napenda kutazama muvi za katuni. Mara nyingine nakunywa wine kidogo ili kuuchangamsha mwili.
Mpaka Home: Tukushukuru kwa muda wako, tukutakie siku njema.
Malaika: Karibuni tena na tena! Asanteni.

Post a Comment