ad

ad

HADITHI: RAHA YENYE MAUMIVU - 11


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Ilikuwa simulizi iliyoushitua moyo wa mama Gift na kujikuta akitafuta ukweli zaidi kwa kumchimba Tell me.
"Kwa hiyo baba ulipoondoka hukuwaaga wenzako?"
"Sikumuaga yoyote sikupenda mtu ajue mipango yangu, labda rafiki yangu mmoja wa karibu ambaye kwa sasa ni marehemu."
SASA ENDELEA

"Mmh! Unajua baba simulizi yako haina tofauti na ya shoga yangu, pale Arusha hotel na yeye alikutana na kijana mmoja mchoma nyama ambaye alitembea naye na kumuachia pesa laki tano na yeye kuondoka."
"Huyo shoga yako yupo wapi?"
"Ni Muda mrefu tumepotezana."
"Lazima niseme ukweli hili hata mke wangu nilimueleza kuwa pesa za utajiri wangu nilivyozipata. Ni kweli, basi huyo shoga yako ndiye aliyenipa huu utajiri na kama nitamuona leo nitampa zawadi kubwa."
Kauli ile ilikuwa kama mshale moyoni kwa mama Gift kwa mara ya kwanza kauli ya mwanaye inatimia alijikuta akipiga ukulele:
"Ooh! Mungu wangu nimekwisha," baada ya kauli ile walishangaa kumuona mtu akiseleleka kwenye kochi alilokuwa amekaa na kuanguka chini kitu kilicho washtua Gift na mumewe.
"Maskini mama yangu," Gift alipiga kelele baada ya kumuona mama yake amelegea kwenye zuria.
"Hiki nini tena?" Tell me aliuliza.
"Hata sijui tumuwahishe hospitali."
"Ina maana huwa ana matatizo haya?"
"Sijawahi kuyaona."
Tell me alimbeba juujuu hadi kwenye gari na kumuwahisha TMJ Mikocheni. Alipokelewa haraka haraka na kupata huduma ya kwanza ambayo ulimrudisha katika hali yake ya kawaida. Baada ya huduma ya kwanza na kuchukua maelezo na vipimo ilionyesha ni mshtuko tu wala hakukuwa na tatizo kubwa.
Mama gift alipata mapumziko kuangalia hali yake, akiwa katika chumba cha mapumziko alimuomba daktari asimruhusu mtu yoyote aingie ndani kwa sababu hakupenda kuonana na mtu kwa wakati ule.
Daktari alikubali na kuwaeleza Gift na mumewe waliokuwa wakisubiri kujua hali ya mgonjwa
"Samahanini naomba kwa sasa mwende nyumbani mgonjwa atakuwa kwenye mapumziko mafupi kwa hiyo njooni jioni."
"Lakini hali yake inaendeleaje?" Gift aliuliza.
"Ni mshtuko tu lakini yupo sawa ni mapumziko ya matazamio."
"Daktari hebu tueleze ukweli kama amezidiwa usinifiche mimi ndiye mtoto wake wa pekee."
"Kama kungekuwa na tatizo ningekujulisha yupo sawa ni mapumziko ya kawaida tu."
"Sawa daktari tutarudi hiyo jioni, sasa hata hatujui aletewe chakula gani?"
"Suala la chakula lisikusumbueni kila kitu tutamaliza hapahapa jioni njooni tu mumuone na pengine kuondoka naye."
Gift na mumewe waliondoka kurudi nyumbani kila mmoja akiwaza yake juu ya tukio lililotokea la mshtuko wa gafla wa mama Gift.
"Ni nini kilichofanya mama awe kwenye hali ile?"
"Hata mimi sijui la muhimu tumsubiri mwenyewe ndiye anayejua hasa tukizingati ni jana tu amerudi."
"Au labda ni kutokana na ugomvi wa jana?"
"Sidhani lakini si mlisameheana na yakaisha"
"Maskini sijui nini kimemsibu mama yangu," Gift alisema huku akilia.
"La muhimu tumuombee kwa Mungu atoke salama"
*****
Mama gift akiwa chumbani peke yake alijikuta akiyakumbuka maneno ya mwanaye Gift, kuwa tabia ya kutembea ovyo na wanaume ipo siku watatembea na mwanaume mmoja sijui wataangalianaje?
Aliamini mdomo ndio unaonuka ila kauli hainuki, wala si kauli ya mkubwa hata ya mtoto nao usipoifuata lazima yatakukuta ya kukukuta
"Maskini mie nitaiweka wapi sura yangu, heri ningetembea na mwanaume mmoja na mwanangu, lazima hii itakuwa laana ya mume wangu baba Gift ya kumtelekeza....Sijui mwanangu atamwitaje Tell me why na dada yake? Mbona nimeleta kitendawili cha mwaka sijui nani wa kukitegua.
“Hii aibu nitauweka wapi uso wangu, najua wanangu wanataka kujua nini kilichonisibu, lakini sina jinsi lazima niwe muwazi sijui mkwe na wanangu watanitazama vipi na akikuwa nitamueleza nini pia jamii itanielewa vipi.
“Hakuna njia nyingine ni kuuacha ukweli na mimi nitangulie mbele ya Mungu ili nisubiri hukumu yangu," mama Gift alikuwa akiongea huku machozi yakimtoka kama maji, alikuwa amepiga magoti pembeni ya kitanda na kuendelea kulia kilio cha majuto.
"Kweli Mungu akitaka kukuumbua hukuumbua kwa dhalilisho zito, mbona nimefanya kioja cha mwaka, sistahili kuishi bora nife."
Mama Gift alifuta machozi na kutoka mpaka nje ya wodi na kuagiza kalamu na kalatasi, baada ya kuletewa. Akiwa amepiga magoti kalatasi ilikuwa juu ya kitanda, aliandika ujumbe ambao alitaka apewe mwanaye atayekuja jioni.
Machozi yakiwa yanamwagika kama maji alianza kuandika ujumbe kwa mwanaye Gift:
Mwanangu Gift, najua uamuzi wangu utakushtua na kukuumiza kwa namna moja au nyingine. Lakini siyo mapenzi yangu, sina jinsi lazima nifanye hivi.
Kauli yako mwanangu haikwenda mbali, siku zote malipo ya ubaya huwa hapa hapa duniani. Ulilosema ambalo uliliogopa katika maisha yako limetimia, nashindwa sijui nitauweka wapi uso wangu, wewe na mumeo mtanielewaje. Mdogo wako nitamueleza nini anielewe na jamii itanielewaje. Nakubaliana na usemi wako, japo niliuona wa kitoto wa mtu asiye jua lolote, lakini leo umenifanya nijute na kuijutia nafsi yangu. Kweli pesa iliyonipa sifa lakini leo imenidhalilisha na kunifanya niwe kituko mbele ya jamii.
Najua nimezunguka sana kuusema ukweli, lazima nikuweke wazi wewe na mumeo. Kama ulikuwa ukifuatilia mazungumzo yangu na mumeo najua hakuna aliyejua kuna kitu gani kimepatikana kwenye yale mazungumzo si wewe wala mumeo.
Huu ndio ukweli, mdogo wako Malon baba yake mzazi ni Tell me why ambaye wakati ule alikuwa akitumia jina la Tamilway na ndiye niliyetembea naye pale Arusha hotel. Na ndiye niliyempa laki tano ambazo anadai ndizo zilizompa utajiri.
Hebu angalia ni aibu gani uliyoingia kwenye familia, mdogo wako atakuitaje ikiwa lazima Tell me amwite baba mzazi. Hiki ni kitendawili sijui kama kitapata mfumbuzi. Mwanao ambaye ni mgeni mtalajiwa atamwitaje Malon, mbona mwanangu nimefanya vioja vya mwaka na kufanya simulizi midomoni mwa watu.
Uamuzi niliochukua ndio haki yangu sina njia nyingine, nimeamua kujiua ili kujiepusha na aibu hii ambayo haina tofauti na kujipaka mavi mbele ya kadamnasi. Najua nimekukosea, najua nimemkosea baba yako najua nimemkosea mwanangu Malon.
Lakini naomba wote mnisamehe naomba uniombee msamaha kwa baba yako nimemkwaza kwa mambo mengi. Mwisho naomba mnilelee mwanangu Malon Mungu akipenda tutaonana. Nakuombeeni maisha marefu yenye upendo na furaha.
Buriani mwanangu nakupendeni sana mimi mama yako Thereza.

Aliirudia ile barua zaidi ya mara mbili huku machozi yakimmiminika kama maji. Alijifuta machozi kisha alitoka mpaka kwenye ofisi ya wauguzi na kuwakabidhi ile bahasha aliyokuwa ameiandika jina la mwanae Gift.
"Samahanini naomba akija mwanangu kama nitakuwa nimepitiwa na usingizi mumpe. Ila sipendi nionane naye kwa leo, akija mwambie tuonane kesho."
"Sawa mama," wauguzi aliipokea ile barua na kuendelea na shughuli zao hawakumtilia maanani.

Nini kitaendelea? Kuyajua yote endelea kufuatilia.
Powered by Blogger.