HADITHI: RAHA YENYE MAUMIVU - 10
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’.ILIPOISHIA:
"Gift hapa sio wakati wake," Tell me aliingilia kati kwa kuona marumbano yamekuwa makubwa na mwelekeo wake ni mbaya.
SASA ENDELEA…
Tell me alimuondoa mkewe ambaye alionekana kughadhibika na tabia za mama yake. Alimuondoa huku Gift akiwa analia na mama yake akiwa amepingwa na bumbuwazi asiamini aliyokuwa akizungumza mwanaye na kujiuliza ujasili ule kautoa wapi.
Hata walipofika nyumbani Gift alikuwa bado analia kitu kilichomfanya Tell me aingie kazi ya kumbembeleza mkewe.
"Basi Honey yameisha si tumeisharudi?"
"Yaani wewe hujui basi tu mama yangu amenizaa lakini sina haja naye kwanza malezi gani anayonilea muda mwingi yupo kwenye biashara zake bila baba sijui ningekuwa kwenye hali gani?"
"Kwani nini kilichofanya mama na baba yako watengane?"
"Ni hadithi ndefu, mama yangu kabla ya kuolewa na baba alikuwa akifanya biashara ndogo ndogo. Wakati huo baba alikuwa ni mfanyakazi serikalini. Sielewi kama mama wakati ule alimkubali baba kwa kuwa alikuwa na pesa nyingi.
“Kwa maelezo ya baba, mama alipewa kila alichotaka kwa vile baba alikuwa akimpenda sana mama alijikuta akiiba vitu vingi na kuviuza na pesa zote alimpa mama. Baba alikiri ndoa yao ulitawaliwa na matumizi makubwa yaliyofanya baba awe na kazi ya ziada kuhakikisha nyumba haiteteleki.
“Lakini kama hujuavyo kila kitu chenye mwanzo hakikosi mwisho, serikali iliposhtuka mirija ya pesa ya baba ilizibwa na kujikuta akitegemea mshahara tu. Hapo ndio ukawa mwanzo wa matatizo ya mama kutaka vitu vya bei ya juu na matumizi makubwa wakati akijua hali ya baba...
“Hapo ndiyo ukawa mwanzo wa dharau na kujiamulia vitu anavyotaka, baada ya baba kustaafu alilipwa malipo yake hapo mama aliomba nusu ya malipo ili afanyie biashara. Pamoja na dharau baba bado alikuwa na mapenzi na mama alimpa kiasi anachotaka.
“Mama alianza biashara za nje ya mkoa ambazo siku nyingine zilitumia wiki hadi mwezi. Kumbe mama alikuwa na biashara mbili ya kununua vitu na kuuza na ya mwili. Kwa muda mfupi mama alijulikana na kuwa na pesa nyingi kwa kuwa alihujumu ndoa yake na matajiri.
“Hapo ndipo alipoanza biashara za kusafiri nje ya nchi, wingi wa pesa uliongeza kiburi na dharau kwa baba wakati huo baba hela yake ilikuwa ndogo kwa kutegemea mashine yake ya kusaga na gari zake mbili za kubeba abiria. Taarifa za mama kutokuwa muaminifu kwenye ndoa yake ilimfanya baba ampige marufuku kufanya biashara ile.
Hapo ndipo mama alipoota mapembe na kulazimisha talaka baba alipokataa mama alifungua kesi mahakamani na kufanikiwa kuivunja ndoa yake bila malipo yoyote. Wakati huo nilikuwa na miaka kumi na tano mama alinichukua na kunikataza nisiende kwa baba. Jambo ambalo kwangu lilikuwa gumu baba yangu nilikuwa nampenda muda mwingi nilikuwa naye karibu.
“Nilimkubalia mama kwa mdomo lakini muda mwingi mama akiwa hayupo nilikwenda kwa baba na kushinda siku nyingine hulala huko huko. Toka mama aachane na baba amekuwa na tabia mbaya ambazo kwa upande wangu sikupaswa kuziona wala kuzisikia lakini kwa mama yangu aliona ni jambo la kawaida.
“Tabia mbaya ambayo ilibidi hata mimi mwanaye nimkemee ni tabia ya kukosa ustaarabu kwa kutembea ovyo na wanaume bila kijali lika wala umri. Kibaya zaidi toka awe na pesa amekuwa akiwahonga wanaume nilimweleza mama kuwa tabia kama ile ni mbaya sana anaweza kuchangia mwanaume na mimi mwanaye tutaangalianaje.
Nilimuomba atafute mwanaume mmoja ambaye atamfaa na kuwa mumewe japo nilimuomba amrudie baba bila mafanikio kwa upande wa baba kutokana na mapenzi na mama alikubali wakati wowote. Ninachoshukuru kitu kama hicho hakijatokea nimeweza kuolewa bila kutokewa na kitu cha aibu. Hebu fikiria mama yangu kila sehemu akifika anatafuta bwana kwa hela zake.
Kibaya hata aogopi gonjwa la ukimwi ukimuuliza anasema anajali kama angekuwa anajali mtoto amempataje.
"Kingine kibaya hata aliyempa mimba amemsahau alikutana naye siku moja usiku akiwa kwenye safari zake na hata alipomfuata alikuta ameacha kazi."
"Ni wapi huko?" Tell me aliuliza.
"Hata najua, ukimuhoji sana unaonekana umekosa adabu."
Kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda waliamua kupumzika na kulala mpaka siku ya pili.
****
Mama Gift hakuamini maneno ya mwanaye yaliyokuwa na ukweli mtupu. Aliamua siku ya pili kwenda kwa mwanaye kumuomba msamaha na kuwaacha ndoa waendelee yao.
Aliwasiri kwa mwanaye majira ya saa nne asubuhi na kuwakuta Gift na mumewe akiwa wametulia sebuleni, Gift akiwa amemwegemea mumewe kifuani kwenye sofa.Walipomuona walimkaribisha kwa furaha kama jana hapakuwa na malumbano yoyote.
Mama Gift akiwa ameongozana na Mwanaye ambaye alifanana sana na Tell me Why, lakini hakuwa na wazo kuwa atakuwa baba yake hakuamini kama mchoma nyama anaweza kuwa siku moja tajiri mkubwa.
Tell me alimpokea shemeji yake na kukaa naye karibu, naye mama Gift alitumia muda ule kumuomba msamaha mwanaye na kukubaliana na kile kilichotokea bila idhini yake.
"Mama mimi sina kinyongo na wewe kwa kuwa nilichokifanya nilikuwa na haki kufanya vile."
"Nimefurahi kusikia hivyo la muhimu ni kurudisha mapenzi yetu ya awali."
"Mama kama nilivyokueleza mimi sina kinyongo na wewe jisikie amani moyoni mwako."
Wakati wakiongea Gift aliponyanyua macho alikuta na kitu ambacho kilimfanya aongee kwa sauti.
"Mume wangu yaani mlivyofanana na mdogo wangu mtu akiingia atajua wewe ndiye baba yake."
"Duniani wawili wawili huenda baba yake tunafanana."
Kauli ile ilimfanya mama Gift kunyanyua macho kuangalia kile alichokuwa akikisema mwanaye. Alimwangalia mwanaye kisha Tell me ilijikuta moyo ukimshtuka baada ya kugundua mwanaye anafana sana na Tell me kwa kiwango kikubwa.
Picha ya Tell me ilionekana si ngeni kwenye ubongo wa mama Gitf, alijikuta akimuuliza Tell me labda anaweza kuwa na mahusiano na mtu ambaye ni mzazi mwenzie.
"Samahani baba sijui umeishawahi kukaa Arusha?"
"Ndiko nilipozaliwa."
"Mmh! Hotel ya New Arusha Hotel unaijua?"
"Aah, mbona pale nimefanya kazi sana."
"Kipindi gani?"
"Mwaka wa tano sasa."
"Wa tano?" Mama Gift aliuliza kwa mshangao.
"Ndio mama."
"Ulikuwa unafanya kazi gani?"
"Unajua mama maisha haya huwezi kuamini hatua mtu alizopitia hata leo kuwa kwenye maisha haya. Hata mke wangu niilisha mweleza kuwa siku zote mwanadamu usikate tama, hujui Mungu mbele amekupangia nini. Maisha niliyokuwa nikiishi siamini.
“Lakini ukweli utabakia pale pale yalikuwa maisha ya kubahatisha, pale nilikuwa nafanya kazi upande wa jikoni nilikuwa mtaalamu wa kuchoma nyama. Mshahara tuliokuwa tukipata mdogo sana ilikuwa laki moja kwa mwezi.
“Lakini siku zote malengo ndio njia pekee ya kukukomboa pale upatapo kidogo. Nilipanga kama nitapata pesa basi ningekuja hapa jijini kufanya kazi ya kuuza mitumba rafiki yangu mmoja alinieleza nitafute laki moja. Lakini siku moja nilipata zali la kupata laki tano. Nikaona nasubiri nini? Kesho yake nikatimkia Dar. Mungu akaniangazia mpaka leo hii nipo hivi."
Ilikuwa simulizi iliyoushitua moyo wa mama Gift na kujikuta akitafuta ukweli zaidi kwa kumchimba Tell me.
"Kwa hiyo baba ulipoondoka hukuwaaga wenzako?"
"Sikumuaga yoyote sikupenda mtu ajue mipango yangu, labda rafiki yangu mmoja wa karibu ambaye kwa sasa ni marehemu."
Nini kitaendelea? Kuyajua yote endelea kufuatilia.
Post a Comment