NILIISHI DUNIA YA PEKE YANGU - 8

ILIPOISHIA:
Nilipozingatia kuwa mama Martha alikuwa akiniamini kama binti mwenye heshima, niliwaza nini kitatokea kama akisikia natembea na mumewe au ajue siku niliyopiga kelele nilibakwa na mumewe.
Nilijiuliza nitaweka wapi uso wangu japo sikutakiwa kufunua kombe kabla mwanaharamu hajapita.
SASA ENDELEA...
Nilijikuta nipo njiapanda kupata jibu la nini cha kufanya kwa kuamini kabisa muonja asali huwa haonji mara moja. Kitendo cha kunibaka nilijua hakikuwa cha bahati mbaya bali alikipanga kwa kuamini umaskini wangu ungenifanya nimkubalie na kuendeleza mchezo wake mchafu ambao mwisho wake ungekuwa mbaya kama bomu lililosubiri kulipuka.
Lakini nilikumbuka kauli ya asubuhi ya mzee Sifael aliponiomba msamaha:
“Najua nimekukosea sana, naijutia nafsi yangu kwa kitendo cha kishetani nilichokutendea. Nashukuru kwa kuokoa ndoa yangu, nakuahidi sitarudia tena na Mungu shahidi yangu, kama nitafanya hivyo tena basi uchukue uhai wangu. Ester nakuahidi kukupatia kitu chochote utakachokitaka ili kurudisha furaha yako.”
Niliyarudia maneno yake akilini na kuanza kuyatafakari kabla ya kuchukua uamuzi mzito wa kuondoka pia kurudia dini yangu ya zamani. Wazo lingine liliurudisha moyo wangu kwa kuamini maneno yale yalionesha majuto na kuamini hatarudia tena. Lakini wasiwasi ulibakia kuwa, je, hajanipa ujauzito au kuniambukiza magonjwa ya zinaa?
Nilijikuta nakubaliana na wazo jipya la kuachana na mpango wa kuondoka na kuamini Binadamu anayegundua kosa lake hawezi kulirudia. Nilipiga magoti pembeni ya kitanda kumuomba Mungu anipe ujasiri niweze kuyashinda majaribu yale. Baada ya maombi, nilipanda kitandani na usingizi haukuchelewa kunichukua mpaka nilipoamshwa na mama kwa ajili ya chakula cha mchana.
Niliungana na mama kula chakula cha mchana, kila dakika aliniuliza hali yangu, ilionesha jinsi gani alivyokuwa na mapenzi ya kweli kwangu. Japo moyo wangu ulikuwa bado una kovu la kubakwa na mumewe lakini mapenzi yake yalinifariji.
Niliamua kuliacha lile lipite kwa kuamini kitendo alichotenda mzee Sifael ni kosa kama la binadamu mwingine hivyo alitakiwa kusamehewa. Niliendelea na maisha yangu huku moyo wangu ukiwa umekufa ganzi, hata kuhudhuria kanisani kulipungua tofauti na mwanzo, watu wangu wa karibu wakawa wananiulizia lakini siri ilibakia moyoni mwangu.
Siku nazo zilikatika ambapo nilianza kugundua mabadiliko mwilini mwangu. Hali ile ilinitisha sana, kwa vile nilikuwa nimeshakuwa na ufahamu nilikwenda duka la dawa na kuchukua kipimo cha ujauzito. Niliporudi nyumbani nilijifungia chumbani kwangu na kupima kwa njia ya haja ndogo.
Baada ya kuweka haja ndogo kwenye kopo niliingiza kipimo, baada ya kukitoa jibu lilikuwa lilelile... nilikuwa nimenasa ujauzito. Nilipatwa na mshtuko wa ajabu, nikajiuliza itakuwaje kama nitaulizwa ujauzito ule wa nani? Sikuelewa ningejibu nini, pia ile heshima yangu ingepotea si kwa mama Martha pekee, hata wasichana wenzangu wa kanisani.
Wazo la kutoa mimba sikulipa nafasi kabisa, niliapa toka nilipoponea kwenye tundu la sindano sitatoa ujauzito tena maishani mwangu. Niliamini baada ya kosa la kwanza ningekuwa makini maishani mwangu kwa kutoutoa mwili wangu kwa mwanaume kabla ya kuolewa.
Lakini ilikuwa tofauti na mipango yangu, nilijikuta nimeshika ujauzito baada ya kubakwa na mtu niliyemuheshimu kama mzazi wangu. Nilijikuta nikiwa katika wakati mgumu sana, sikujua nifanye nini. Sikutaka kufanya pupa, niliweka vitu vyangu vizuri na kutoka sebuleni nikiwa sioneshi kitu chochote usoni kwangu.
Kila nilipomuona mzee Sifael akipita, moyo ulikuwa ukinilipuka na kuona kuna umuhimu wa kumweleza siku ileile ajue atanisaidia nini japo niliamini kabisa atanishauri kutoa, kitu ambacho sikutaka kukisikia. Baada ya uzalendo kunishinda nilimwita mzee Sifael.
“Samahani baba.”
“Bila samahani mwanangu.”
“Nilikuwa na mazungumzo na wewe.”
“Hapa au pembeni?”
“Nina imani pembeni ingefaa zaidi.”
“Basi twende nje mwanangu tukazungumze,” mzee Sifael alisema huku akielekea nje, nami nilimfuata huku mama na kina Martha wakinitania.
“Mmh! Mtu na baba yake mna siri gani? Au umeshapata mchumba nini?”
Sikuwajibu, nilicheka tu huku nikimfuata baba nje, nilimkuta amesimama karibu na getini.
“Mh! Mama ulikuwa unasemaje?”
“Kuna tatizo limejitokeza.”
“Tatizo gani tena mama?” mzee Sifael aliuliza kiungwana na kunifanya niwe na wakati mgumu wa kumweleza kwani niliona kama namuonea mtu aliyeamini baada la tukio lile baya Mungu amemuepushia mbali.
“Hata nashindwa nianzie wapi unielewe.”
“Sema tu mama nitakuelewa.”
“Hivi karibuni niligundua mabadiliko mwilini mwangu na kunifanya leo niangalie afya yangu, muda si mrefu nimetoka kujipima na kujikuta nina ujauzito.”
“Ooh! Ujauzito wa nani?” mzee Sifael alishtuka.
“Wa kwako.”
“Mimi?”
“Kwani nani aliyenibaka?”
“Hata kama nilikubaka lakini ujauzito si wangu,” mzee Sifael alijifanya kuruka futi mia.
“Sikiliza baba toka nifike hapa sijawahi kukutana kimwili na mwanaume na wewe ndiye uliyeniingilia mara ya mwisho, kwa hiyo naomba uniambie utanisaidiaje kabla sijamwambia mama?”
“Ha...ha...pana usifanye hivyo.”
“Sasa niambie utanisaidiaje?”
“Mmh! Mbona mtihani mzito.”
“Sasa mimi nifanye nini?”
“Ni kweli ujauzito ni wangu?”
“Wewe unafikiri wa nani?”
“Huna rafiki wa kiume?”
“Sina.”
“Siyo kitu, kesho tutafanya zoezi la kutoa hiyo mimba.”
“Hapana suala la kutoa ujauzito wangu sahau.”
“Una maana gani kusema hivyo?”
“Katika kitu ambacho sitakifanya maishani mwangu ni kutoa mimba.”
“Sasa tutafanyaje? Njia nzuri ni kuitoa tu bila hivyo tutaharibu kila kitu.”
“Tafuta njia yoyote ya kutatua tatizo hili, lakini mimba sitoi hata kwa mtutu.”
“Lakini kwa nini Ester, huoni kama inaweza kuleta tafrani nzito ndani.”
“Najua lakini katu sitatoa mimba,” nilisimamia msimamo wangu.
“Kwa nini Ester hutaki kutoa mimba?”
“Siwezi kupona mara mbili, mara ya kwanza nilichungulia kaburi, nikirudia nitakufa.”
“Nitakupeleka kwa wataalamu.”
“Hata kwa Mungu sikubali.”
“Kwa hiyo tutafanyaje?”
“Tafuta njia yoyote lakini si kutoa.”
“Fanya hivi...hili suala njoo kesho kazini tuzungumze vizuri hapa si pazuri.”
Kabla ya kuingia ndani mzee Sifael alinirudisha nyuma na kuniambia.
“Sikiliza Ester ukiulizwa na mama yako mwambie umepata mchumba Muislam, sawa?”
“Sawa.”
Baada ya kukubaliana tuliingia ndani, walipotuona walisema kwa pamoja.
“Mmh! Mtu na mtoto wake mna siri gani?”
“Siyo lazima kuijua ndiyo maana tumezungumza wawili,” mzee Sifael aliwajibu.
Sikujibu kitu, nilifika na kukaa pembeni ya mama.
Muda wote niliokaa na mama sikuulizwa swali lolote mpaka muda ulipofika wa maombi ili kila mmoja aende chumbani kwake. Kama kawaida baba aliongoza maombi kuonesha kweli roho mtakatifu kamuingia kumbe alikuwa shetani mkubwa. Nilimuona muongo mkubwa aliyenifanya niichukue dini kwa kuamini mashetani kama wale ndiyo wachafuzi wa dini za watu huku wakionekana wapo mbele kumtukuza Bwana kwa midomo yao kumbe wachafu mioyoni.
Tokea nilipobakwa na jinsi tabia ya mzee Sifael aliyokuwa akijionesha mbele za watu, moyo uliniuma na kufikia hata kuiona ibada yote aliyokuwa akiongoza ni ya kinafiki tofauti na mwanzo nilikuwa nikimwamini.
Baada ya maombi ambayo kwa upande wangu niliyaona ya kinafiki tulikwenda kulala, usiku ulikuwa mrefu kwangu niliwaza hiyo kesho angeniambia kitu gani tofauti na utoaji wa ujauzito. Pamoja na kuwa na mawazo mengi usingizi ulinipitia na kushtuliwa alfajiri kwa ajili ya maombi ya asubuhi ya kumshukuru Mungu kutulaza salama pia kumuomba atuvushe siku salama.
Baada ya maombi kabla ya kuondoka baba alimueleza mama:
“Baadaye Ester aje kazini.”
“Saa ngapi?”
“Kuanzia saa tano.”
“Nina imani amekusikia.”
Baada ya kusema vile aliondoka na kuniacha na mama nikifanya usafi na kazi zote muhimu kabla ya kwenda kuonana na baba.
Saa tatu na nusu mama aliniomba nijiandae kwenda kwa baba, baada ya matayarisho yote nilikwenda kazini kwa baba.
Nilipofika hakutaka tuzungumzie pale, alinipeleka kwenye hoteli moja iliyokuwa tulivu na kuagiza vinywaji kabla ya mazungumzo. Siku hiyo alikuwa mpole kupindukia, nami nilikuwa kimya muda wote nimsikie anataka kuniambia nini.
Kabla ya kusema nilishangaa kumuona mzee mzima akitokwa machozi na midomo ikimcheza kuonesha alikuwa na wakati mgumu mbele yangu kitu ambacho sikutaka kukipa nafasi kwa kuamini kosa langu lolote ni kifo changu.
Niliendelea kujiapiza sitakubali hata kwa mtutu wa bunduki kutoa mimba kwa vile yaliyonikuta sitayasahau mpaka naingia kaburini. Baada ya kujifuta machozi aliniita jina langu kwa sauti ya chini.
“E..e..ster.”
“Abee baba.”
“Kwanza samahani.”
“Bila samahani baba.”
“Najua nililolifanya kwa kweli halikukufurahisha.”
“Ni kweli, lakini lilishapita.”
“Bado mwanangu, lililopita lilikuwa dogo lakini hili ni kubwa sana.”
“Sasa tutafanyaje na imeshatokea?”
“Kwa nini hutaki tuitoe hiyo mimba?”
“Baba nimekueleza hata kwa mtutu wa bunduki siitoi.”
“Kwa nini Ester?”
“Nilikueleza niliujaribu mchezo huu mpaka leo nazungumza na wewe ni Mungu tu, nilikuwa nimekwishapelekwa mochwari.”
“Kwa sababu gani?”
Sikutaka kumficha, nilimweleza maisha yangu ya uhusiano na mpenzi wangu wa kwanza mpaka aliponipa ujauzito na kisha kunishauri kama yeye kuutoa ujauzito na matokeo yake. Baada ya kunisikiliza alitulia kwa muda na kushusha pumzi nzito. Alitulia akiangalia juu akigongesha vidole kwenye meno kisha aliniita tena.
“Ester.”
“Abee.”
“Inaonekana mlikwenda kwenye hospitali za uchochoroni.”
“Nimekwambia hivi, hata kama zingekuwa hospitali za barabarani, sikubali yaliyonikuta nayajua, ungekuwa ni wewe ndiye yamekukuta usingethubutu kunishauri nitoe mimba.”
“Sasa ukiulizwa mimba ya nani utasemaje?”
“Ya kwako.”
“Ha!” Alishtuka mpaka akasababisha vinywaji kumwagika.
“Unashtuka nini, unataka niseme ya nani wakati baba wa mtoto ni wewe?”
“Ester, chondechonde, utaharibu sifa yangu kuanzia ndani mpaka kanisani, si unajua kabisa mimi ni kiongozi wa kanisa?”
“Huo uongozi wa kiroho au ushetani?”
“Wa kiroho Ester, nilichokifanya hata mitume waliotangulia wapo waliofanya makosa kama mimi lakini walisamehewa.”
“Hata mimi nilikusamehe, lakini bado roho mchafu yupo ndani yako kwa kutaka kukiua kiumbe kisicho na hatia. Umefanya dhambi ya kuzini, tena kwa kunibaka, dhambi hiyo hujatubu unataka kuua, wewe ni mtu wa aina gani?” nilimuuliza nikiwa nimemkazia macho.
“Unafikiri ukisema hii mimba ni yangu nitaweka wapi sura yangu?”
“Kwani uliponibaka ulitegemea nini?”
“Nikwambie mara ngapi shetani alinipitia?”
“Acha kunichekesha ina maana huyo shetani kazi yake kukupitia wewe tu kila siku?”
“Sijawahi kufanya kitendo kama hiki ndiyo maana nina wasiwasi kuna mkono wa mtu, siwezi kumbaka binti yangu niliyemlea mwenyewe,” mzee Sifael alizungumza akiamini kabisa sijui historia ya uchafu wake wa nyuma.
“Baba unajua unazungumza na mtu mzima, sasa kama nisingemuua mwanangu kutokana na akili za kitoto sasa hivi ningekuwa mama fulani hivyo usizungumze kama unazungumza na mtoto mdogo.”
“Kwa nini?”
“Hii tabia yako ya asili ya kubaka wasichana wanaokaa ndani mwako na kujificha kwenye kivuli cha ucha Mungu kama mzee wa kanisa naijua vizuri.”
“Ester ni maneno gani hayo, mimi nimekuona mtoto kivipi?”
“Unajua najua kila uchafu wako uliosababisha mama akimbie nyumbani, kwa hili ulilonifanyia si geni ni kawaida yako.”
“Estaaa! Nani kakwambia uongo huo?”
“Si kujua nani kaniambia, jua naelewa kila kitu juu ya uchafu chako.”
Kauli yangu ilimfanya aone aibu na kuwa na kazi nzito mbele yangu, niliamini utapeli aliokuwa akiutumia kwa wasichana waliotangulia kwangu ulikuwa umejulikana.
Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya kesho hapa
Post a Comment