ad

ad

HADITHI: RAHA YENYE MAUMIVU - 08


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
"Hakika kila asimamae kwa ajili ya nafsi yake huiokoa nafsi yake."
Tell me why alimuaga Gift ambaye alimsindikiza hadi kwenye gari lake aliwaaga na kuondoka huku akimuacha Gift kwenye mtihani mzito wa moyo wake na kujiuliza ni kweli turufu aliyoitupa ni kubwa kuliko ya mpinzani wake au ndio imemezwa na kubwa zaidi kama samaki mdogo kuliwa na mkubwa.
SASA ENDELEA…
*****
Huo ndio ukawa mwanzo wa mahusiano ya karibu kati ya Tell me why na Gift. Tabia ya Gift ya msimamo na kupenda kujua mambo na muda wote alipenda kuwa muwazi. Ilimvutia Tell me why na kumuona ni msichana anayefaa kumuoa. Alimsubiri amalize masomo yake ili waweze kuwa karibu zaidi, kwa vile muda uliokuwa umebaki ni wa mtihani wa mwisho.
Alipomaliza tu mtihani alijiachia na muda wote kuwa karibu ya Tell me why.
Tabia za Gift kila dakika zilimvutia Tell me na kuamini kabisa mwanamke wa ndoto yake ni Gift. Siku moja Tell me why alimueleza ukweli Gift juu ya kuvutiwa kwake na tabia zake na kila alichokitaka kwake alikuwa nacho na zaidi.
Alimjulisha kuwa anataka kukamilisha ile hesabu ya moja na moja.
Gift aliona kama miujiza ile ndoto yake inakaribia kutimia alimuomba Mungu itimie kweli. Tell me alimuomba ndoa yake ifanyike upesi upesi kwa kuwa alikuwa na shughuli nyingi.
Kwa kuwa mama yake alikuwa nje kikazi Gift alimuomba waiahirishe mpaka hapo atakuapo rudi mama yake, kauli ile ilimfanya Tell me ahoji..
"Ina maana mzazi wako wa kiume amekwisha kufa?"
"Hapana."
"Kwani yeye hawezi kusimamia ndoa yako?"
"Anaweza lakini aliachana na mama kila mtu yupo kivyake."
"Hata kama wapo kivyao, lakini baba yako bado ana nguvu ya kusimamia ndoa yako."
"Mama lazima atakasirika ikiwezekana hata kuivunja ndoa yetu."
"Kwani akivunja wanawake wamekwisha?"
"Sivyo hivyo, nitakuwa nimeathirika mimi."
"Kauli yako imenifanya nihoji ni nani aliyevunja ndoa ya wazazi wako wawili?"
"Ni mama."
"Nilijua, kwa nini?"
"Toka alipopata pesa kwenye biashara zake na baba kumwekea mipaka hapo ndipo alipo lazimisha talaka. Japo baba alikuwa hapendi kumwacha, mama alimpeleka baba mahakamani kumdai talaka ambayo ilitolewa mbele ya Hakimu."
"Baba yako ana kazi gani?"
"Ni mtumishi wa umma aliyesitaafu."
"Ana shughuli gani?"
"Ana mashine ya kusagia unga na Heace mbili."
"Unamuheshimu baba yako?"
"Tena sana, kitendo cha mama cha kumwacha baba na kumliza mzee mzima mahakamani akimlilia mama, kiliniumiza moyo na baba aliapa hataoa maishani mwake mpaka anakufa. Japo mama yeye anapenda ujana humchukua mwanaume yoyote amtakaye kwa gharama yoyote. Kitu kinachonitisha na kama hivyo amezaa na kijana mmoja Arusha ambaye hamjui jina wala sura hamkumbuki japo amesema mdogo wangu anafanana na baba yake copy right, unajua nini Tell me kwa mfano.
"Wewe ni kijana bado unadai vilevile una matamanio ya kimwili na mama yangu ni mtu mzima anayekwenda na wakati kwa bahati mbaya wewe nawe mwanadamu unaweza kukutana naye bila kumjua kama mkweo katika biashara zenu na kumchombeza unarudi nyumbani nakutambulisha kuwa huyu ndiyo mkweo sijui hapo kutakuwa na picha gani?"
"Itakuwa mbaya tutashindwa kutazamana usoni tumuombe Mungu ayaepushe haya."
"Ndiyo maana nikaitafuta hesabu ya moja kwa moja yenye jibu ya moja yaani ndoa ya watu wawili huzaa mwili mmoja."
"Naomba twende kwa baba yako mpe heshima kama inavyo sitahili."
"Wacha niwasiliane na mama kama ataweza kuwahi ili wajumuike wazazi wangu wote."
"Itakuwa vizuri basi tuonane baadaye kujua umefikia wapi...sitaki uifute shauku ya moyo wangu, elewa wewe ndiye uliye ushawishi naogopa usije uudhi."
Waliagana Tell me why na Gift, jioni ya siku ile aliwasiliana na mama yake ambaye alimjulisha atachelewa kurudi na kuomba radhi kwa kuwa tayari kulipa gharama yote ya harusi. Alimuomba baba yake awe msimamizi wake, lakini mama yake alikataa katakata kwa kusema gharama za maisha ya Gift anazijua yeye umiliki wa Gift uliishia pale walipoachana tu siku alipotoa talaka mahakamani.
Gift alijua kama atamweleza Tell me why, yale aliyoongea na mama yake mume atamkosa. Aliamua kutunga uongo pale alipokutana na Tell me why kwa kumwambia kuwa mama yake amekubali baba yake awe msimamizi wake. Kauli ile ilimfanya Tell me why afurahi sana na kupanga siku ya pili kwenda kwa baba yake mzee Edgar Bilikila
Siku ya pili waliongozana hadi kwa mzee Bilikila ambako walipokelewa kwa furaha na bashasha. Gift baada ya kumtambulisha mchumba wake alieleza sababu kubwa iliyowapeleka pale. Mzee Bilikila alishangaa na kuhoji.
“Leo mtoto wa mama umekuja mimi baba yako maskini nikuoze na mama yako je?"
"Mama hayuko ila amesema wewe uendelee na shughuli zote bado mizunguko yake haijaisha."
"Sipendi kuongea mengi kwa vile wewe mwanangu upo peke yako nilikuwa na haki ya kukataa. Lakini nitakuwa sikukutendea haki, kingine ni mtoto uliyeonyesha mapenzi ya dhati kwa mimi baba yako pamoja na mama yako kukukataza."
"Baba wewe ndiye baba yangu sina mwingine, baba huwa najisikia uchungu kwa kitendo cha mama cha kukuacha kwa ajili ya pesa namuomba Mungu nisifuate nyayo za mama ili niwe mtiifu kwa mume wangu nimpende kwa shida na raha kwa kuwa fedha ni matokeo fedha zinaweza kukupa sifa pia hizohizo zikakudhalilisha."
"Ni kweli mwanangu kauli yako inaonyesha ni kiasi gani ulivyopevuka na pesa si msingi wa maisha pale unapozitumia vibaya...mwanangu ninakupa baraka zote ili uolewe na mumeo. Na wewe baba nakuomba uwe mume mwema lakini uwe makini kwa hawa wanawake japo mwanangu sipendi awe na tabia kama za mama yake."
"Nashukuru kwa nasaha zako baba namuomba Mungu ampe mke wangu mtalajiwa akili na upendo ili ndoa yetu itenganishwe na kifo."
"Amen."
Baada ya kupata idhini ya kumuoa Gift Tell me alirudi mjini kufanya taratibu zote za ndoa ambazo nazo zilikwenda kwa haraka sana. Ndani ya wiki mbili ndoa ilifungwa rasmi na Gift kuwa mke wa Tell me why.
Gift alikuwa na siri moyoni juu ya kauli ya mama yake alijua akirudi lazima kutakuwa na matatizo hata kufikia hatua ya kutoitambua ndoa yao. Lakini alijipanga kwa ajili ya kukabiliana na mama yake na kuwa tayari kwa lolote, wala hakumtaarifu kuwa ameisha funga ndoa.
***
Tell me why alianza maisha kwa mafanikio makubwa na kujilaumu kwa kuchelewa kuoa, lakini alijua kama angewahi kuoa asingepata mwanamke kama Gift alijua ni zawadi aliyopewa na Mungu. Ndani ya wiki mbili alikuwa tayari ameisha cheka na nyavu, mwezi ulikatika Gift akiwa mjamzito. Mimba nayo ilimpenda alizidi kunawili na kupendeza. Wakiwa wamekaa sebuleni Gift alimtania Tell me.
"Mmh sikuwezi."
"Kwa vipi mpenzi?"
"Yaani kugusa tu bao.”
"Siku zote biashara mapema na mshambuliaji mzuri si mpiga cheka bali mpiga mabao.”
"Siyo unizalishe kama mlea kambi ya yatima."
"Wanne wanatosha."
"Mmh! Wengi wawili tu."
"Lazima wawe wanne yaani wawili kwenu na wawili kwetu."
"Mmh, haya kazi kwako kulima kwa bidii."
Mara simu ililia wote walishtuka kwa uchovu Gift aliichukua na kuongeam ilikuwa inatoka kwa mama yake.

Nini Kitaendelea? Ili kuyajua yote endelea kufuatulia
Powered by Blogger.