HADITHI: RAHA YENYE MAUMIVU - 09
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’ILIPOISHIA:
"Mmh! Wengi wawili tu."
"Lazima wawe wanne yaani wawili kwenu na wawili kwetu."
"Mmh, haya kazi kwako kulima kwa bidii."
Mara simu ililia wote walishtuka kwa uchovu Gift aliichukua na kuongea ilikuwa inatoka kwa mama yake.
SASA ENDELEA…
"Haloo mama Shikamoo."
“Marahaba.”
“Leo umetukumbuka, za siku?”
"Nzuri vipi hali yako?"
"Mimi sijambo sijui wewe?"
"Kwa kweli mimi mzima wa afya japo mambo yangu ni mengi lakini nakuja mara moja wiki ijayo kusimamia harusi ili nirudi kwenye shughuli zangu."
"Hamna tatizo mama."
Gift alimficha mama kuwa amekwisha olewa na sasa hivi ni mke wa mtu. Aliogopa malumbano ya ndani ya simu, vile vile mama yake angeweza kughaili kuja Tanzania. Aliamua amuache ili aje ajionee mwenyewe mkwewe ambaye anashida naye ya kumuona kama mwanga kwa kipofu.
Baada ya mazungumzo Gift alimgeukia mumewe.
"Honey mama anakuja wiki ijayo."
"Oooh vizuri hata mimi nina hamu naye."
WIKI MOJA BAADAYE
Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mwalimu J.K.Nyerere majira ya saa nne Gift akiwa na mumewe waliwasiri uwanja pake kumsubiri mama Gift ambaye alikuwa akiwasiri siku ile. Waliwahi nusu saa kabla ndege ya shirika la ndege la Swiss air kuwasiri. Wakiwa wametulia sehemu ya kupokelewa wageni tangazo liliwajulisha kuwa wakati wowote ndege ya shirika la Swiss air itawasiri.
Wote waliokuja kupokea wageni wao walikaa tayari kuwapokea wageni wao. Gift na mumewe Tell me why nao walijitayalisha kumpokea mgeni. Saa nne juu ya alama ndege iliwasiri na abiria walianza kushuka mmoja mmoja. Kila aliyekuja kupokea mgeni wake alipepesa macho ili amuone.
Gift alipepesa macho kwenye foleni ya wageni waliokuwa wakitoka kwenye msafara mmoja. Mara alimuona mama yake alijikuta akipiga ukelele
“Mamaaa.”
"Wawooooo mwanangu."
Mama yake na yeye alijikuta akiachia kigari cha mizigo na kumkumbatia mwanaye.
"Jamani mwanangu."
Wakiwa wamekumbatiana Tell me why alikuwa pembeni akiangalia furaha ya mama na mtoto, baada ya kuachiana Gift alimtambulisha mumewe kwa mama yake.
"Mama kutana na mkweo ambaye ulikuwa na hamu ya kumuona lakini sasa ni mume wangu."
"Oooh baba nimefurahi kukuona," alisema huku akijitoa kwa Gift na kumkumbatia.
"Hata mimi."
Waliongozana hadi kwenye gari na kurudi mjini, wakiwa njiani mama Gift alitaka kujua ile hali ya mwanaye kuwa katika ujauzito bila kufunga ndoa.
"Haya mama tutayaongelea nyumbani humu sio pahala pake."
Mama Gift hakutaka kuongeza neno akilini mwake alijua mwanaye bado hajafunga ndoa na haikuwa vizuri mtu akiwa akisubiri ndoa akubali kubeba mimba.
Baada ya kufika nyumbani walimwacha mama yao ajipumzishe ili jioni wapate muda wa kuongea naye. Kwa upande wa mama Gift alikuwa amempotea kabisa Tell me why kwa kuwa hata kimawazo asingeamini mchoma nyama kuwa tajiri mkubwa namna ile.
Hata Tell me naye hakumtilia maanani mama Gift siku waliyokutana kwa mara ya kwanza kwa hiyo sura yake haikuwa kwenye kumbukumbu kabisa alimwona mtu kama mtu. Na kwa muda ule alimchukulia kama mama mkwe.
Jioni walikwenda kwa mama Gift kwa mazungumzo ya safari na mipangilio aliyokuja nayo mama Gift. Ilikuwa baada ya chakula cha usiku majira ya saa tatu na nusu wakiwa sebuleni Mama Gift alitaka kujua mpaka sasa matayalisho ya harusi yamefikia wapi.
Tell me alishtuka kusikia kauli ile ilibidi amgeukie Gift kwa kumuuliza kwa macho kuwa mama ana maana gani.
"Mama sina budi kwanza nikuombe msamaha kwa kukiuka kauli yako, pili kusema uongo kwa baba nilikuwa sina jinsi. Ukweli nimeisha olewa huu ni mwezi wa pili na sasa hivi mimi ni mzazi mtarajiwa."
"Atiii..unasemaje Gift umeolewa kwa idhini ya nani?"
"Ya baba."
"Nilikwambiaje?"
"Kumbuka mimi ni mtoto wa pande mbili na mwenye madaraka ni baba yangu siwezi kumdharau baba yangu bila yeye mimi nisingekuwepo," Gift alijibu kwa kujiamini.
"Baba yako ni nani mbona mdogo wako amepatikana bila baba yako hata wewe ungepatikana bila yeye. Kwanza nilifanya makosa kuolewa na mtu maskini kama yule."
"Mama bila baba nisingezaliwa mimi, angezaliwa mwingine kaa ukielewa namheshimu baba na nitaendelea kumheshimu sioni kosa lake kwako zaidi ya kumdhalilisha kwa umasikini wake."
"Gift unanivunjia adabu mbele ya mumeo lakini amini ndoa mliyofunga ni batili mimi siitambui."
"Kama huitambui sio juu yako mimi sasa hivi ni mke wa mtu na baba yangu ndiye msimamizi mkuu."
"Na huyo baba yako atanitambua atatoaje idhini anajua gharama za malezi yako?"
"Hakushindwa bali ulining'ang'ania," Gift alimpasulia mama yake.
"Gift leo umenigeuka?"
"Kwa mtindo huo sipo pamoja nawe," Tell me aliyekuwa kimya ilibidi aingilie kati.
"Samahanini japo sijui kwa undani, sidhani kama mmeachana ifikie hatua ya kuchukiana kiasi hicho. Siku zote kiunganisho cha familia ni watoto nakuomba mama mkwe tuliza munkari, tumieni ndoa yetu ili kurudisha mahusiano."
"Itakuwa ngumu."
"Hata kama kwako ni ngumu lakini baba yangu nampenda tena kwa taarifa yako kila siku ilikuwa lazima nionane naye mawazo yake ndiyo leo yamenipa muongozo na kuwa mke mwema kwa mume wangu. Kama ningefuata tabia zako siwezi kukaa na mwanaume.
“Mama tabia yako hainifurahishi naogopa kuishi maisha unayoishi ni madhara makubwa wala hayana mafunzo kwetu sisi wanao. Nikikufuata siwezi kujenga nyumba yangu pesa si kitu kama utu wa mtu," Gift alizungumza huku akilia kwa kutoa machungu ya muda mrefu ya tabia ya mama yake.
"Nini kilichopunguka kwangu?" Mama Gift alihoji.
"Hukioni mdogo wangu baba yake ni nani?"
"Baba siyo muhimu, cha muhimu malezi anawazidi hata hao wenye baba."
"Siku akimtaka baba yake utamwambia nini?"
"Gift hujakuwa,wewe huwezi kunihikumu."
"Nikuhukumu kwa lipi zaidi ya kukueleza ukweli, isifikiri nafurahia kitendo cha kumuacha baba roho inaniuma. Umasikini sio sababu ya kumuacha mtu, mangapi baba alikufanyia mpaka ukawa hapo na chanzo chote cha baba kuwa kwenye hali ile ni wewe kwa kumtapeli pesa zake," Gigt kwa uchungu aliamua kumvua nguo mama yake mbele ya mumewe.
"Gift hapa sio wakati wake," Tell me aliingilia kati kwa kuona marumbano yamekuwa makubwa na mwelekeo wake ni mbaya.
Nini kitaendelea? Kuyajua yote endelea kufuatilia.
Post a Comment