ad

ad

HADITHI: RAHA YENYE MAUMIVU - 07


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Baada ya kusema yale Eliza alianza kulia kitu kilichofanya Gift anyanyuke kitandani na kwenda kumbembeleza.
“Pole sana rafiki yangu.”
“Gift inauma umasikini huu utaendelea kutudhalilisha mpaka lini?”
“Najua nakuahidi kukusaidia rafiki yangu najua mimi nimeumia lakini wewe umeumia mara mbili kwa vile hukufanya kwa ridhaa yako tofauti na mimi.”
Gift alisahau yake na kumtia moyo Eliza aliyekuwa akilia kwa majuto.
SASA ENDELEA…
***************

Ilikuwa siku ya jumapili Gift akiwa na shoga yake ambaye shuleni wapambe waliwabatika kama wake wenza kwa ajili ya kutembea na mwanaume mmoja. Kwa vile msimamo wao ulikuwa mmoja wa kumkomoa Kanuth hilo halikuwashtua walikuwa na siri yao nzito.
Wakiwa wanajisomea chini ya mti kwa mbali lilisimama gari moja la kifahari aina ya Lange lover Vogue ya rangi ya nyeusi. Hawakuijali baada ya kuisifia tu kuwa gari zuri waliendelea na masomo yao. Sauti ya juu iliyokuwa ikimwita Gift ilimfabya aache kusoma na kuangalia ni nani.
"Gift mgeni wako huyo," Eliza alisema huku alimuangalia vizuri mgeni wa kiume ambaye alikuwa mgeni machoni mwake.
Kila alivyokuwa akisogea naye alimwangalia vizuri, alikuwa kijana mmoja mtanashati aliyekuwa kwenye suti nzito alijiuza ni nani. Macho yalipotulia alimkumbuka lakini jina alikuwa amemsahau.
Bila kijielewa alijikuta ametupa vitabu na kukimbia kumpokea kwa kumkumbatia.
"Oooh! Kaka karibu."
"Asante, upo sawa?"
"Kama chuma si unaniona!"
"Vizuri, mrembo hujambo?" alimgeukia Eliza aliyekuwa bado amepigwa butwaa.
"Sijambo shemeji."
"Eliza tabia gani mtu hujatambulishwa unapayuka."
"Samahani shoga...karibu kaka..nani sijui?"
"Gift atakutambulisha."
"Huwezi amini jina lako nimelisahau.. hebu ngoja nikumbuke Mr listen kama sikosei..oooh nimekumbuka talk to me."
"Ngoja nikukumbushe naitwa Niambie kwa nini umelisahau jina langu wakati hata kadi nilikupa."
"Oooh nimekumbuka Tell me why....Oooh karibu sana kaka tell me why ni kweli nilikuwa na kadi ambayo nilimpa mama ili siku nitayotoka tukualike tujumuike pamoja kwa chakula cha usiku mama alikuwa na hamu ya kukuona.
"Lakini aliondoka siku moja baada ya mimi kutoka hospitali na kupanga tutakualika, kibaya hata kadi yako aliondoka nayo na mimi sikuwa nimeiandika pembeni. Nilikuwa na hamu ya kukuona lakini ndivyo hivyo ilibidi namsubiri mpaka mama arudi."
"Mmh! Tuachane na hayo, vipi hali yako unajua sikujisikia vizuri kutokujua maendeleo yako kibaya zaidi msomi ambaye ni tegemeo la taifa," Tell me alisema huku akichanua tabasamu mwanana.
"Tegemeo wapi kila kukicha tunanyanyapaliwa na serikali."
"Lakini si mambo yametulia."
"Sawa yametulia lakini jasho limetutoka kila siku mpaka mishipa ya shingo itusimame. Wao mbona huwa hawaandamani kuongezana posho wamesahau na wao wamesoma bure lakini wenzao ndio watukamue."
"Hata nyinyi mkifika juu mtakuwa hivyohivyo, wangapi walisema lakini wamepata wamesahau ahadi zao njaa mbaya ukiwa na njaa utatoa ahadi za ajabu hata kuvuta meli kwa mkono ili upate chakula ukishiba unawageuka kwa kuwauliza ni nani mwenye uwezo wa kuvuta meli kwa mkono wewe atakuwa wa pili."
"Mr Tell me why mbona unatetea au una mpango wa kugombania Ubunge?"
"Siku zote kweli utafutiwa sababu ili kuonekana si kweli."
"Umeshinda, tuachane na hayo karibu kazini kwetu hapa ndipo tunapo itafuta sembe."
"Ninashukuru huwezi kuamini kukaa kwangu kote jijini sijawahi kufika chuoni hapa."
"Muongo mtu maarufu kama wewe usifike sehemu kama hii."
"Gift yaweza kuwa kweli pengine hana shida napo aje afanye nini?" Eliza alimuunga mkono Mr Tell me.
"Kwanza mimi si maarufu kama anavyosema, ningekuwa maarufu angepoteza kadi yangu na kushindwa kunipata."
"Mmh! Tell me imekuwa sababu..basi nisamehe leo simu ninayo najua sasa kesi itaisha."
"Kuwa na simu siyo sababu muhimu mawasiliano."
"Sasa utanichoka usijesema karaha au kumuudhi wifi."
"Ni hapo nitakapokuwa naye....Sasa Gift nina imani kidogo moyo wangu utaridhika au kutulia baada ya kupata kujua hali yako. Nimefarijika sana kukuta mzima wa afya tena ukibukua."
"Hata mimi nimefurahi huwezi kuamini siri ipo moyoni mwangu ipo siku nitakwambia. Tell me why kila dakika unanifanya niwe mwanafunzi wako wa kujifunza tabia za watu na kufuta dhana kuwa baadhi ya viumbe si wabaya ila kiumbe mmoja ndiye anayeweza kutia doa na kusababisha kuona wote ni wabaya....wewe ni mfano wa kuigwa."
"Kwa nini unasema hivyo?"
"Ni vigumu kuamini japo ni muda mrefu nashangaa kuona kama nilikuwa nawe siku zote na kujiona mpweke pale utakapo niaga na kujuta kwa nini nimekufahamu."
"Gift una maana gani?" Maneno ya Gift yalimchanganya kidogo Tell me.
"Ni vigumu kuwa wakili wa moyo wako, hasa sisi wanawake pale moyo unapoingia gerezani pasipo kosa wakati mtetezi yupo ambaye ni muoga kuutetea moyo ambao huteseka bila kosa."
"Ninaweza kuwa nimekuelewa lakini huenda vilevile sijakuelewa hebu niweke wazi una maana gani kama sivyo nifikiliavyo?" Maneno ya mafumbo yalizidi kumwweka njia panda.
"Sio siri kila muda kila dakika kila nikikufikiria nakosa jibu kuwa wewe ni kiumbe wa aina gani hata mama yangu mzazi alikusifia kwa yote uliyonitendea nashindwa nikilipe nini...ili isiweze kukupoteza ili nami uuone ukarimu wangu."
"Sihitaji malipo yoyote kutoka kwako...ilikuwa ni wajibu wangu kama mwanadamu kuonyesha ubinaadamu hasa pale unaposababisha maumivu kwa mwenzio japo ilikuwa bahati mbaya."
"Lakini elewa Tell me why siku zote hesabu huanzia moja, lakini kwa upande wangu naomba ifike kumi na moja nina imani unaijua hesabu hii hutumika hasa kanisani, moja na moja huwa moja kibinaadamu huwa kumi na moja naomba hesabu yetu iende kikanisa ili tupate moja."
"Nimekuelewa kuliko ulivyozungumza nipe muda."
"Umenielewa nini Tell me why?"
"Nina imani mzigo ulionipa umeufunga hukutaka kila mtu aujue kwa mimi muungwana nimekuelewa kwa hiyo wacha nikauangalie kama unapendeza hauna kipingamizi."
"Nitafurahi kama kile nilichokiota mchana kinakuwa kweli nimeamini unaweza kuota huku ukiwa macho."
"Umeota nini tena Gift?"
"Nimeota moja na moja ni moja wala si mbili wala kumi na moja."
"Mmmh kweli wewe msomi unayeongea kwa mifano isiyoonekana kwa macho wala kwa akili nyepesi bali kwa yule aliyezama chini ya maji ndiye hugusa mchanga mweupe."
"Hakika kila asimamae kwa ajili ya nafsi yake huiokoa nafsi yake."
Tell me why alimuaga Gift ambaye alimsindikiza hadi kwenye gari lake aliwaaga na kuondoka huku akimuacha Gift kwenye mtihani mzito wa moyo wake na kujiuliza ni kweli turufu aliyoitupa ni kubwa kuliko ya mpinzani wake au ndio imemezwa na kubwa zaidi kama samaki mdogo kuliwa na mkubwa.

Nini Kitaendelea? Ili kuyajua yote endelea kufuatulia
Powered by Blogger.