ad

ad

HADITHI: ... RAHA YENYE MAUMIVU -05


SEHEMU: 05
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
"Punguza munkali Mr tell me, kila kitu kitakuwa sawa ila nilitaka kukueleza kuwa hali yake si mbaya ni majeraha madogo siyo makubwa ya kutisha japo la kichwani ni kubwa kidogo lakini halihitaji kushonwa bali kufungwa dawa tu."
"Ooh afadhali," Mr Tell me why alishusha pumzi ndefu kisha alisema.
"Mr Eliud naweza kwenda kumuona mgonjwa wangu?"
"Mmh mara hii ameisha kuwa mgonjwa wako wakati umemuokota njiani?"
"Hapana kwa sasa ni mgonjwa wangu mpaka hapo nitakapo mkabidhi kwa familia yake."
SASA ENDELEA…

"Ni kweli unaonyesha jinsi gani ulivyo na utu wa kuwajali wanadamu wenzio."
"Sasa naweza kwenda kumuona?"
"Hapana kwa leo itakuwa ngumu kwa kuwa muda huu amelala baada ya kumpatia dawa za maumivu zilizompa usingizi ili kumfanya apumzike hata atakapo amka atakuwa hana maumivu makali."
"Kwa hiyo mimi mnaniambiaje?"
"Wewe nenda ukaendelee na shuguli zako kama kawaida ila kesho nina imani ukija utamkuta nina imani kama hatakuwa na tatizo lingine tutamruhusu kesho."
"Daktari mbona haraka si unajua ajali kuna mambo hujificha kwa nini asikae hata wiki ili kuiangalia afya yake kwa umakini mkubwa."
"Ni kweli lakini kuna gharama zingine hazina umuhimu bora akauguzie maumivu nyumbani kwao kama atajisikia vibaya anaweza kurudi."
"Mr Eliud pesa kwangu sio tatizo la muhimu ni hali ya mgonjwa vilevile hatujui hali yake kimaisha huenda kwao hali ya kimaisha sio nzuri ambayo itasababisha apate shida ya kujitibu huoni kama tutakuwa tumemuongezea mzigo?"
"Mimi sina neno nakusikiliza wewe."
"Kama nilivyo kueleza atulie kwa muda wa wiki nzima."
"Ok, basi kesho kama kuna mabadiliko nitakujulisha kwa njia ya simu."
Waliagana na doctor Eliud na kuendelea na mambo mengine hata safari yake ya Kibaha aliiahilisha na kurudi nyumbani kwa mapumziko. Aliona mbele kuna mkosi.
****
TMJ HOSPITALI MIKOCHENI

Gift baada ya kuzinduka alishangaa kujikuta akiwa hospitali amelazwa kitandani, alijiuliza pale amefikaje na alipojaribu kujigeuza alihisi maumivu makali sehemu za mbavu na mwili wote ulikuwa ukimuuma. Alipopeleka mkono kichwani alikutana na jeraha lililokuwa limefungwa.
Gift alitahayali na kujiuliza nini kilichomsibu mpaka kuwa pale katika hali ile, alipojaribu kurudisha kumbukumbu alikumbuka kitendo alichotendewa na Kanuth na shoga yake mpenzi Eliza cha kumsaliti.
Lakini kumbukumbu zake zilimjulisha kuwa baada ya tukio lile alidondoka chini na kilichoendelea hakujua na alipozinduka alijikuta akiwa chumbani peke yake na wasaliti wake hakuwaona walikuwa wameisha ondoka na kumwacha ndani peke yake.
Lakini baada ya hapo hakumbuki nini kilichoendelea mpaka kujikuta pale.
Wazo lilimuijia huenda Kanuth alimpigaa.
"Mmh, huenda nilifanya fujo zilizopelekea wanipige...Mmh, lakini mbona sikumbuki kama nilifanya fujo zilizopelekea mimi kupigwa au..haa.. pana... lakini... hapana, nina uhakika sikufanya lolote zaidi ya mimi kuanguka chini au nilipata nguvu kuamka tena na kuanzisha fujo ...ni jambo la ajabu sijawahi wala sintawahi kupigania mapenzi japokuwa huwa naumia moyoni...basi itakuwa mara yangu ya kwanza...
"Mmh, na.. na.. nani aliye nileta hosipitali na hii ni hospitali gani ...ooh TMJ," alisema vile baada ya kuona nembo yake kwenye pazia za madirishani.
Akiwa katikati ya lindi la mawazo alishtushwa na sauti ya mlango wa chumba alicholazwa ukifunguliwa na kuingia muuguzi akiwa na trey iliyokuwa na dawa, aliachia tabasamu pana baada ya kuona mgonjwa amepata fahamu alimsogelea na kumjulia hali.
"Pole sana dada."
"Asante," Gift alijibu kwa sauti ya chini.
"Unaendeleaje?"
"Mmh, bado."
"Pole sana, lakini una mabadiliko makubwa na ulipoletwa."
"Kwani nilikuwa kwenye hali gani?"
"Ulikuwa hujitambui na damu zilikuwa ni nyingi zilizotushtua lakini baada ya kukupa matibabu ya haraka na vipimo vya awali ilionyesha hukuwana jeraha kubwa na vipimo vilionyesha ujaumia sana."
"Dada yangu sijaumia sana wakati mwili wote unaniuma kama kidonda?"
"Huo ni msukumo wa gari una bahati hukugongwa na gari bali ni msukumo. Inavyoonesha dereva alijitahidi kufunga breki lakini kwa vile ilikuwa kwenye kasi utelezi ulisababisha gari likukumbe na kukutupa kwenye mtalo."
"Yaani nesi unataka kuniambia nimegongwa na gari?" Gift alishtuka.
"Ina maana hukujua kilichokuleta hapa?"
"Hata moja sina nashangaa kujiona nipo hapa."
"Kwani wewe ulikuwa wapi mpaka ajali hii inakupata?"
"Sikumbuki ila...Oooh wacha aina muhimu...Ni nani aliyenileta hapa?"
"Kuna kaka mmoja mfanya biashara maarufu jijini ndiye aliye kugonga na ndiye aliyekuleta."
"Yeye yupo wapi lazima nimshtaki."
"Unachekesha yaani badala ya kumshukuru mtu kukugonga na kukukimbizia hospitali tena ya gharama. Tofauti na madereva wengi wakishagonga hukimbia au hukupeleka hospitali ya wilaya na kukuacha lakini kaka huyo.
"Alionyesha kuchanganyikiwa na hakuwa tayari kuondoka mpaka ajue hatma ya hali yako. Mpaka alipoelezwa kuwa unaendelea vizuri ndipo aliporuhusiwa kuondoka na kuelezwa arudi kesho."
"Simu yangu ipo wapi?"
"Kwa kweli hatujui tulikupokea hukuwa na kitu chochote."
"Inawezekana aliyenigonga ameniibia?"
"Sidhani mtu mwenyewe hujamuona sio mtu wa njaa hawezi kuchukua simu yako."
"Simu yenyewe unaijua nimeinunua milioni moja na nusu."
"Hata tatu si kwa Tell me why."
"Tell me why una maana gani?"
"Ndio jina la mfanya biashara huyo ni maarufu nashangaa wewe humjui."
" Una simu?"
"Ndio."
"Naomba nimtaarifu mama."
"Kwani mama yako ni nani?"
"Mama Tedy au mam’ kubwa."
"Yule mfanya biashara maarufu?"
"Ndiye huyohuyo."
"Ok, simu hii mpigie," Gift aliipokea ile simu na kumpigia mama yake.
"Haloo mama nipo hospitali nimepata ajali."
"My God hospitali gani...una hali gani mwanagu?" Mam’ kubwa alichanganyikiwa.
"Mama punguza presha nipo TMJ lakini hali yangu sio mbaya ni majeraha madogo madogo."
"Ok, nakuja sasa hivi," mama Teddy alikata simu.
"Asante anti kwa msaada wako," Gift alimshukuru muuguzi kwa msaada wa simu.
"Ni kawaida yetu wanadamu kusaidiana usihofu kwa hilo."
“Nashukuru.”
"Naomba basi nikuchome sindano."
Gift alijitayalisha kuchomwa sindano baada ya kuchomwa sindano muuguzi aliondoka ili kumuacha apumzike. Kabla hajapumzisha mwili baada ya kundungwa sindano mama yake aliingia huku akitweta.
"Vipi mwanangu upo salama?"
"Nipo salama mama."
"Ilikuwaje?"
"Ni ajali kama ajali zingine hata kuelezea nashindwa lakini namsifu dereva kwa kujitahidi kuokoa maisha yangu.Vilevile kuwa na roho ya kibinaadamu ya kunikimbiza hospitali."
"Huyo dereva yupo wapi?"
"Ukweli mama sijamuona ila nimeambiwa baada ya kunileta hakuondoka mpaka alipoelezwa hali yangu inaendelea vizuri lakini nasikia ameahidi kuja leo kunijulia hali yangu."

Nini Kitaendelea? Ili kuyajua yote endelea kufuatulia
Powered by Blogger.