ad

ad

HADITHI: ... RAHA YENYE MAUMIVU SEHEMU - 06


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
"Ni ajali kama ajali zingine hata kuelezea nashindwa lakini namsifu dereva kwa kujitahidi kuokoa maisha yangu.Vilevile kuwa na roho ya kibinaadamu ya kunikimbiza hospitali."
"Huyo dereva yupo wapi?"
"Ukweli mama sijamuona ila nimeambiwa baada ya kunileta hakuondoka mpaka alipoelezwa hali yangu inaendelea vizuri lakini nasikia ameahidi kuja leo kunijulia hali yangu."
SASA ENDELEA…

"Chuoni umewajulisha amepata ajali?"
"Niwajulishe wapi simu sina."
"Na kweli simu yako ipo wapi?"
"Hata sielewi ndio namsubiri huyo kaka labda ameniwekea."
"Basi wacha niwapigie simu chuoni kwenu ili wajue upo kwenye hali gani."
"Sawa mama."
Mama Gift alimpigia simu mkuu wa chuo kumjulisha matatizo yaliyomkumba mwanaye naye mkuu wa chuo alisema atawajulisha wote. Aliamua kwenda kumuona daktari mkuu Mr Eliud ili ajue hali ya mwanaye.
Mama kubwa au mama Teddy ukipenda mwite mama Gift baada ya kutoka kwa mwanaye na kuelekea kwa daktari alipishana mlangoni na kijana mtanashati aliyekuwa amepakatia mfuko uliokuwa na vitu vingi pamoja na kadi na ua mkononi.
Hakumjali alielekea kwa daktari, yule kijana aliingia kwenye chumba cha Gift na kumkuta Gift akiwa anakula ndizi alizoletewa na mama yake. Alipomuona kijana mtanashati akiingia na chumba chote kubadilika harufu ya ndani na kunukia manukato ya gharama ambayo aliyakumbuka aliishawahi kutumia mama yake siku za nyuma na kumwambia ni matukato ya gharama nchi za Afrika hayapatikani ni wachache wa kuyanunua.
"Karibu kaka."
"Asante...nina imani wewe ni mgonjwa wangu?"
"Kwani wewe ndiye uliyenigonga?" Gift aliacha kula na kumtazama yule kujana aliyekuwa amepeneza mavazi nywele zake muonekano wake mbele za watu. Shingoni alikuwa na mkufu mnene wa dhahabu.
"Hapana sijakugonga bali gari lilikusukuma kidogo."
"Ndiyo mimi, karibu tunakula."
"Asante, kwanza pole sana, vipi hali yako?"
"Kiasi sijambo sio kama jana."
"Inaonekana jana ulikuwa umechanganyikiwa shemeji alikuwa amekuudhi nini?"
"Walaaa, matatizo ya dunia."
"Umeolewa?"
"Hapana nasoma."
"Wapi?"
"Chuo kikuu Mlimani."
"Ooh, kumbe naongea na msomi."
"Mmh,"Gift aliguna tu.
"Sasa mrembo nina imani familia yako imeshapata taarifa?"
"Ndiyo..tena mama yupo."
"Oooh kumbe mama mkwe ameisha kuja vizuri..Sasa ni hivi wacha niwahi ila kesho nitakuja na kujua nini cha muhimu ili kuhakikisha unarudi katika hali yako ya kawaida."
"Mmh, sidhani kuwepo hadi kesho nasubiri mama atakuja kuniambiaje."
"Sio mbaya chukua hii kadi yangu ya shughuli zangu tutawasiliana sawa au nitakuja kukutafuta chuoni, nakaribishwa?"
"Karibu, lakini naomba umsubiri mama akuone."
"Hapana...nani kweli?"
"Gift."
"Oooh, una jina zuri inaweza kuwa zawadi yangu," Gift hakujibu alitabasamu tu.
"Ok, Gift tutaonana msalimie sana mama kwa vile una kadi yangu nitafika nyumbani au chuoni kukujulia hali..Huna simu msomi?"
Kauli ile ilimshtua Gift wakati yeye alikuwa akijipanga kuulizia simu yake ilibidi ajibu.
"Nilitegemea labda wewe jana uliichukua hivi nilikuwa najiandaa kukuuliza."
"Oooh pole, sana inawezekana watu waliichukua baada ya ajali."
"Simu yangu ilikuwa ya gharama kubwa."
"Kwani ilikuwa shilingi ngapi?"
"Milioni moja na nusu."
"Milioni moja na nusu zote unanunua simu?"
"Alininunulia mama alipokwenda nje kibiashara."
"Usihofu nitakupa pesa sasa hivi ili akija umpe akakununulie."
Tell me alimpa Gift Milioni mbili taslimu na kumuaga huku Gift akisisitiza amsubiri mama yake arudi iliamuone. Lakini Tell me alimuomba radhi siku nyingine. Aliondoka na kumuacha nyuma Gift akimsindikiza kwa macho.
***

Gift alikuwa anaona kama njozi ya mchana na kuona watu wana pesa za mchezo mtu kumwambia kiasi kikubwa cha pesa kiasi kile lakini hakuteteleka wala kuguna. Alijiona mpumbavu pale alipomkisia kamchulia simu yake. Akiwa bado akizihakiki zile pesa mara mama yake aliingia na kumkuta akiwa bado amezishikilia mkononi alishangaa kazitoa wapi ulibidi amhoji mwanaye.
"He! Mwenzetu pesa zote hizo umezitoa wapi?"
"Kanipa yule kaka aliyenigonga."
"Za nini?"
"Za simu yangu."
"Ulimdai?"
"Hapana ila alipokuja aliniuliza kama nina simu ili tuweze kuwasiliana kujua hali yangu, ndipo nilipomweleza kuwa simu yangu imepotea siku ya ajali."
"Ehe ikawaje?"
"Basi aliniuliza simu ya aina gani na dukani unauzwa kiasi gani? Nilimwambia milioni moja na nusu nilishangaa anafungua mkoba wake na kunipa hela hii."
"Kwa nini usiikatae?"
"Mama kuna mtu anakataa pesa wewe hutulii nyumbani kwa ajili ya pesa, tena siyo ananihonga bali ananilipa simu yangu."
"Sio hivyo mwanangu unajua mtu aliyejitolea kuokoa maisha yako kukuleta hospitali ya gharama kama hii.Kitu kingine cha ajabu bado amekuja kukujulia hali na kadi ya pole na maua amekuletea pamoja na matunda....pesa nini mwanangu kwani mimi ningeshindwa kukunulia simu nyingine?" Mama Gift hakufurahishwa na kitendo cha mwanaye kumlipisha simu.
"Lakini mama mimi sikimdai amenipa mwenyewe."
"Oooh, tuachane na hayo, haya huyo kijana yupo wapi?"
"Nina imani umepishana naye alikuwa na haraka amepigiwa simu."
"Kwa nini hukuniita nikaja kumjua inaonyesha ni kijana mwema mwenye roho ya huruma."
"Mama nimemsihi akusubiri alikubali lakini kuna simu amemfanya aondoke haraka lakini kanipa bussines card kama nikinunua simu nimjulishe."
"Itakuwa vizuri nitamualika chakula cha jioni utakapotoka hospitali."
"Itakuwa vizuri mama yule kijana wa ajabu sana ni mpole na mcheshi vilevile nimeambiwa ni mmoja wa wafabiashara maarufu."
"Pesa sio kigezo tabia ni moyo wa mtu...," mama Teddy alikatishwa na hodi iliyokuwa ikigongwa.
"Karibu ingia." mama Teddy alikaribisha, mlango ulifunguliwa alikuwa ni Mkuu wa chuo aliyeongozana na baadhi ya wanafunzi miongoni ya wanafunzi alikuwepo shoga yake Eliza.
Gift alipomuona moyo ulimpasuka alitamani ammeze kwa kumuona ni adui yake namba moja. Lakini aliificha hasira yake angekuwa peke yake angemfukuza kama mbwa mwizi. Lakini ndiyo hivyo yupo mbele ya mkuu wa chuo na mama yake na wanafunzi wenzie pia hakutaka siri yao kila mtu aijue.
Baada ya kumpa pole Mkuu wa chuo na wanafunzi waliaga na kuondoka na kumwacha mama Gift na mwanaye. Naye mama Gift aliingia mjini kwa ajili ya shughuli zake za kibiashara na kumwacha mwanaye akiwa amepumzika.
Gift akiwa amefura kwa hasira baada ya Eliza kuja kumsanifu alijikuta akijiapiza moyoni kuwa akitoka salama atahakikisha anamshikisha adabu. Akiwa katikati ya mawazo mlango uligongwa aliacha kuwaza kukalibisha.
"Pita ndani"
Mlango ulifunguliwa aliyeingia alimfanya Gift azidishe hasira na kujikuta akibwata kwa hasira kwa sauti ya juu.
"We mbwa umerudi kufanya nini?" Alimfokea Eliza aliyerudi kuomba msamaha.

Nini Kitaendelea? Ili kuyajua yote endelea kufuatulia
Powered by Blogger.