DIRISHA LINAFUNGULIWA, SIJUI YANGA, SIMBA, WENGINE WANAKUMBUKA WALIBORONGA
Na Saleh Ally
DIRISHA la usajili limefunguliwa kutokea
Novemba 15 hadi Desemba 15 na kila timu inayotaka kufanya usajili inatakiwa
kuwa imekamilisha kila kinachotakiwa.
Usajili ni sehemu mpya kwa timu kujirekebisha
na kufanya kile ambacho inaona kimepungua katika kikosi chake kwa ajili ya
kumalizia ligi.
Kwangu nimekuwa ninaona kama kuna kitu
ambacho hakipo sawa. Kwamba dirisha dogo la usajili linafunguliwa mapema sana.
Kweli
karibu kila timu inakuwa imeona upungufu ambao inaweza kuufanyia kazi. Lakini
angalau kungekuwa na idadi ya kutosha ya timu huenda kungeweza kuwa na
mabadiliko bila ya kuingia gharama.
Wakongwe Simba na Yanga, katika misimu miwili
wameingia kwenye rekodi ya timu ambazo zimefanya usajili wake kwa kukurupuka,
tena kwa kiasi kikubwa na mara nyingi wamekuwa ni wagumu kukubali.
Yanga wanaweza kuwa na angalau, Simba wakawa
walivurunda zaidi lakini hakuna anayeweza kukwepa kwamba kuna mambo mengi sana
hayakuwa sawa katika suala la usajili.
Beki Vincent Bossou, raia wa Togo, amejiunga
na Yanga lakini alijikuta akikaa benchi zaidi ya mechi tano akiangalia
Watanzania wakiendelea kucheza, jambo ambalo halikuwa sawa hata kidogo.
Hali kadhalika Simba tuliona, mshambuliaji
Pape N’daw kutoka Senegal, naye alilazimika kusubiri katika benchi la Simba na
hata siku alipopewa nafasi ya kuingia, ikawa ni sawa na uigizaji wa kipindi cha
komedi.
Maana
aliingia na viatu vikuukuu na mwisho akasema ni bahati, siku chache baadaye
akakamatwa akiwa na hirizi ambayo tuliibandika jina la Power Bank. Hakuna
alichoifanyia Simba ambayo imeishia kumlipa dola 3,000 (zaidi ya Sh milioni 6)
ili aondoke.
Utakumbuka msimu mmoja kabla, Simba
iliwasajili wachezaji wa kigeni na kuwaacha ndani ya msimu mmoja. Sasa imewaacha
wachezaji hata kabla ya nusu msimu kufika. Hili si jambo zuri kwa wanaohusika
na usajili na lazima wakubali kutuacha tuseme kwa kuwa vitu walivyofanya si
sahihi.
Inawezekana ni kosa la kocha, kosa la mjumbe
wa kamati ya usajili au vinginevyo. Lakini ukweli ni kwamba, kosa limefanywa na
Simba na kamwe hawawezi kulikimbia.
Makosa yamekuwa mengi, hakuna sababu ya
kusajili mchezaji wa kigeni anayelipwa kwa dola halafu anaendelea kukaa benchi,
si sahihi.
Mbrazili, Coutinho wa Yanga, bado hana faida
kubwa kwa kuwa kocha anaonekana hamkubali katika programu zake. Anatumia muda
mwingi benchi huku akichota mamilioni ya fedha kuliko wale wanaocheza, hakika
bado hili si jambo zuri na lazima liangaliwe.
Wachezaji wa kizalendo wengi wanaumia,
tatizo lao ni moja. Waoga, hivyo hawawezi au hawako tayari kuanika ukweli
kwamba wanaona wanatumika, wanapambana kwa ajili ya klabu na timu kwa ujumla
lakini wanaolipwa zaidi wanaonekana hawana msaada kama walionao wao.
Kuna mengi yanawezekana kushindana kuepushwa
yasitokee katika kipindi hiki cha usajili hasa kama Simba, Yanga, Azam FC na
klabu nyingine zitafanya usajili. Hauwezi kuepusha wachezaji kukaa benchi kwa
kuwa wote hawawezi kucheza.
Lakini vigezo vinabaki palepale, wachezaji
wa kigeni lazima wawe na ubora ulio juu zaidi, msaada wa juu ni funzo au
changamoto kwa wachezaji wengine wazalendo. Lakini si waje hapa nyumbani kuuza
sura kwenye benchi huku wakichota mamilioni ya fedha kuliko wazalendo tena
wanaoonekana wana msaada mkubwa zaidi katika vikosi vyao.
Najua
kusema maneno ya kukosoa inauma sana, lakini tukubaliane jambo hili. Kama klabu
zitaendelea kusajili wachezaji wa kubahatisha, basi hofu ya kwamba kuna “dili”
zinapigwa kufaidisha mifuko ya watu, zitakuwa ni sehemu ya hoja.
Post a Comment