ad

ad

Diamond Kufulia, Tutasubiri Sana!

EDSON Arantes do Nescemento maarufu kama Pele ndiye mwanasoka anayetajwa kuwa na kipaji halisi cha kucheza kandanda kuliko wengine wote, ingawa Diego Amando Maradona amekuwa akiipinga dhana hiyo, akitaka dunia imtambue yeye kuwa ndiyo mwanasoka mwenye sifa hiyo.

Hata hivyo, soka ni mchezo wa kudumu na wachezaji ni watu wa kupita. Baada ya Pele kuitawala dunia enzi zake, alifuata Maradona, akaja Ronaldinho na Zinadine Zidane na sasa ni wakati wa Lionel Messi.
Hawa ni miongoni mwa binadamu wachache waliowahi kuamua waufanye nini mpira na kwa wakati gani. Ungeweza kuwa shabiki wa timu pinzani, lakini ukajikuta unainuka kushangilia wakati Ronaldinho Gaucho anapoamua kubadili uelekeo wa mpira katika namna isiyoelezeka.
Pamoja na upinzani unaotajwa kuwepo hivi sasa baina ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, lakini katika ukweli halisi, raia huyo wa Argentina anakosa mpinzani wanapozungumza kuhusu mtu mwenye mamlaka ya kuuamrisha mpira uwe vile anavyotaka mbele ya wapinzani wake.

diamondUtangulizi huu unamhusu Diamond Platnumz, kama tutaamua kuzungumzia Bongo Fleva. Kuna watu waliutawala kabla yake. Sugu pengine ndiye wa kwanza kuitawala Bongo Fleva kama solo artist, akaja Juma Nature, Afande Sele (kumbuka aliibuka kinara wa mkali wa Rhymes Bongo), Mr Nice na Ali Kiba.
Si kwamba hakukuwa na wasanii wengine waliosumbua kipindi chao, lakini wao ndiyo walikuwa alama ya Bongo Fleva. Na bahati mbaya, wengi wao hawakuweza kukitumia vizuri kipindi chao. Walitumia umaarufu wao kupata pesa nyingi kupitia shoo za majukwaani.
Wapo walioishia hapo, lakini kuna watu walitumia nyakati zao kutengeneza ‘connection’ zilizowawezesha kurekebisha maisha yao kiasi kwamba hata kama hawafanyi tena muziki wa kutegemea shoo, lakini maisha yao yapo ‘under control’.
Wakati Afande Sele akitwaa Taji la Mfalme wa Rhymes 2004, alikuwa hot cake, kila mtu alitaka afanye naye kazi na shoo zake zote zilijaza mashabiki kupita maelezo. Hakuna maneno yanayofaa kumzungumzia Mr Nice juu ya namna gani alikuwa ameiteka Bongo Fleva.
Ninapomtazama Diamond kama msanii, ninamuona ni mtu ambaye ametumia vyema wakati wake akiitawala Bongo Fleva kwa kujitengenezea msingi ambao utamfanya aingize mamilioni ya fedha, hata akiacha kukamata mic. Kwanza alijitahidi kulifanya jina lake liwe brand barani Afrika, kitu ambacho amekimudu kwa ufanisi mkubwa.
Leo hii, siyo rahisi kuifikia Afrika ya burudani ambayo haimjui Diamond. Baadhi ya wasanii wetu wanafahamika huko nje kwa sababu sasa muziki wetu unafuatiliwa kwa sababu yake.
Amesajili lebo ambayo hivi sasa ndiyo kubwa hapa nchini, WCB. Kuna lebo nyingi, lakini bila shaka, licha ya uchanga wake, hii iko ‘active’ na ndiyo maarufu zaidi. Ina wasanii wanne, Rich Mavoko, Harmonize, Raymond na Queen Darleen.
Ametumia mamilioni ya shilingi kununua vifaa vya muziki vya kisasa kabisa. Hivi sasa ana bendi yake ambayo akipanda nayo jukwaani, nyimbo zake zinapigwa katika ubora uleule ambao unakuwepo kama ataweka CD.
Amewatengeneza wasanii wake. Ukimuacha Mavoko, ambaye ni msanii mkubwa hata kabla hayupo WCB, wengine wote wamekuzwa na Diamond na leo hii, wanaweza kufanya shoo ya peke yao na kujiingizia mamilioni.
Haufanyi muziki kama kitu cha kumpatia sifa ili awapate wasichana kirahisi, bali anaufanya kama kazi nyingine zilivyo. Ndiyo maana anakesha studio, akijaribu kufanya kila aina ya muziki na kote amefaulu.
Zipo tetesi kuwa Vodacom wameingia mkataba na Diamond ili kufanya Wasafi Tour katika mikoa 10. Endapo itafanikiwa, yeye ataingiza fedha mara mbili, kwanza kama msanii lakini pia kama bosi wa kampuni yake.

Kama hili litakuwa ni tetesi sawa, lakini namuona Diamond akiingia mkataba na kampuni moja kubwa kwa ajili ya kitu kama hiki miezi si mingi ijayo. Ikifanyika hivi, maana yake ni kuwa atakuwa amebuni kitu cha kudumu, ambacho kinaweza kufanyika kila mwaka.
Katika dunia inayobadilika kuhusu haki za wasanii, kama kasi yake itaendelea kama dalili zinavyojionyesha, uhai wa Diamond kimapato ni wa milele.


Badala ya mashabiki pinzani kumuombea mabaya, wakimtolea mfano wa waliowahi kuwika na kupotea, Diamond awe mfano wa jinsi wasanii wa Tanzania wanavyoweza kufanikiwa na kuzalisha ajira kwa ustawi wa taifa letu. Kupitia muziki, kijana huyu ameajiri vijana watanzania 42, wakiwemo wa kudumu na part time, vipi tukiwa na wasanii kumi kama yeye?


Makala: Risasi Vibes; Risasi Mchanganyiko, Jan 4-6, 2017, Toleo 1388

No comments

Powered by Blogger.