BORA MAGURI APOKEE MSHAHARA KIDOGO MAZEMBE KULIKO KUBAKI DAR AICHEZEE YANGA
Na Saleh Ally
Mshambuliaji Elias Maguri amefanikiwa kufunga mabao 10
kwa msimu huu hadi sasa, jambo ambalo linaonyesha ana mwanga mzuri huko
aendako.
Maguri amefunga mabao 9 akiwa na klabu yake ya Stand
United, bao moja ameifungia Taifa Stars katika mechi dhidi ya Algeria ikiwa
ndiyo mechi yake ya kwanza kurejea katika kikosi hicho pia ikiwa ni mara ya
kwanza kukichezea chini ya kocha mzalendo, Charles Boniface Mkwasa.
Maguri aliondolewa Simba huku ikielezwa Kocha Dylan
Kerr raia wa Uingereza hakuwa akivutiwa naye. Hiyo ikawa imeifanya Simba kuweka
rekodi ya kuwatema washambulizi wake tegemezi kila baada ya msimu mmoja.
Ilifanya hivyo kwa kumtema Amissi Tambwe na kusema
Kocha Patrick Phiri hakuwa akimhitaji. Msimu mmoja kabla, Tambwe alikuwa ndiye
mfungaji bora.
Maguri amekuwa jasiri baada ya kuamua kwenda Stand
United. Kwa alipokuwa amefikia kutoka katika timu ya jeshi na kujiunga na
Simba, tayari alikuwa amepiga hatua.
Angekuwa muoga, huenda angeisha kabisa kisoka. Badala yake
akaamini uwezo wake na kujiunga na Stand United, sasa ana mabao mengi kuliko
washambuliaji wote waliosajiliwa na Simba msimu huu.
Juhudi za Maguri zimefanya awe lulu, tayari kuna
klabnu zimeweka wazi zinamhitaji ambazo ni Simba, Yanga na TP Mazembe pia
imeanza kumtupia jicho.
Tayari Maguri ameweka wazi msimamo wake kuhusiana na
Simba. Kwamba hawezi kujiunga na Simba kwa kuwa hawakuwa waaminifu kwake na
walimuondoa katika hali ambayo ilimshangaza na kumkatisha tamaa.
Fainali inabaki Yanga na TP Mazembe. Yanga inakuwa
lahisi kumpata kwa kuwa wako naye hapa, lakini swali moja tu. Kuna tofauti
kubwa kati ya Yanga na Simba?
Klabu kongwe zenye tabia zinazofanana, ambazo
zinaamini zinajua au bora kwa kila kitu na zisizo na uwezo mkubwa sana wa
kujali wachezaji wao.
Yanga na Simba, hazina uwezo wa kusikiliza u kufikiria
maumivu ya wengine. Sasa kunaweza kukawa kuna tofauti yoyote ya thamani au
kuamini kwamba usipoenda na utaratibu unaumiza watu.
Maguri ameishacheza Simba, kuna siku kama atakuwa na
Yanga, basi akikosa kufunga bao, watasema ana mapenzi na Yanga.
Akikosea watasema bado ana uhusiano wa kirafiki na viongozi wa Simba na kadhalika. Jambo litamtokea si baada ya muda mrefu kwa kuwa kama mchezaji, lazima iko siku atakosea tu. Unafikiri Yanga wote ni waelewa kiasi hicho?
Inawezekana mshahara wa Yanga ukawa juu, lakini bora
akipata nafasi TP Mazembe kwa mshahara ulio chini aende kama sehemu ya
kujifunza na kujipa nafasi ya kujitanua kiuwezo na fikra pia.
Kubaki Tanzania akiichezea Yanga ni kuendelea kuingia
kwenye kundi la wachezaji wa Kitanzania ambao wengi wametamba na kuishia hapa
nyumbani.
Lazima Maguri awe na hamu ya kutoka, waamini kupambana
katika sehemu ngumu ni sehemu ya kukua haraka.
Maguri akibaki Yanga tayari ni staa, lakini akiondoka
na kujiunga na TP Mazembe, atajiona hana kitu, atalazimika kupambana kupata
namba.
Wakati akipambana itakuwa chachu na changamoto kwake,
hivyo ataweza kujifunza zaidi na kuwa bora zaidi kuliko akibaki Yanga ambako
nafasi ya kupata namba ni kubwa mno kwa kuwa tayari anaongoza kwa mabao ya
kufunga.
Najua Maguri anaangalia maslahi pia, lakini bado atakuwa na nafasi ya kuangalia maslahi zaidi hapo baadaye kuliko sasa halafu iwe kwa kipindi kifupi.
Post a Comment