ad

ad

Singidani (A Story From My Heart) - 8


www.facebook.com/2jiachie ‪#‎2jiachie‬
ILIPOISHIA...
“Tafadhali naomba unisaidie kwa hilo. Nipe nafasi moyoni mwako. Nakupenda sana Laura,” Chris akasema kwa hisia kali sana.
SASA ENDELEA...
HUMBA kilikuwa kikubwa chenye kila kitu. Giza jepesi la jioni lilianza kuchukua nafasi chumbani mle. Taratibu jua liliendelea kuzama na kufanya ukimya wa jioni uanze kuingia taratibu.
Ndani ya chumba hiki, watu wawili walikuwa wamezama katika mazungumzo muhimu sana. Dk. Chris anajaribu kueleza namna anavyougulia mapenzini kwa msichana mrembo Laura.
Kwa hakika Chris aliamua kujitutumua. Alijihisi mpweke na hakutaka kabisa kumkosa. Tayari alishakatisha safari yake ya kijijini kwao ambako alitakiwa aende kutafuka mke huko.
Laura alimtosha kabisa.
Laura ni kama hakusikia vizuri kauli ya Chris. Kama alisikia basi alikuwa hajaamini maneno ya kijana huyo ambaye anasumbua katika ulimwengu wa filamu za Kibongo.
“Chris una hakika na unachokizungumza?” Laura aliuliza kwa sauti laini, tamu ambayo ilikuwa burudani tosha kwa Chris.
Jibu lilikuwa rahisi sana: “Nina zaidi ya hakika Laura. Nipe nafasi. Nitaumia sana nikikukosa. Moyo wangu umeniambia unakupenda wewe tu. Tafadhali usiniumize wala kuniadhibu.”
“Siamini maneno yako Chris.”
“Kwa nini mama?”
“Sikuamini tu. Nyie wanaume maneno mengi sana, hasa ninyi wasanii. Mh! Hapo utasema maneno yote lakini ukinipata tu, mapenzi yanaishia hapo. Kwa kweli nimeondoa kabisa imani na wanaume.”
“Kuna tofuati kubwa sana kati ya wanaume na Chris. Mimi ni tofauti na wengine wote unaowajua au uliowahi kukutana nao. Mimi ni kweli ni mwanaume, lakini ni Chris. Nipe nafasi tafadhali.”
Kama ni filamu basi Chris alikuwa kwenye kipande cha mapenzi na aliweza kuvaa uhusika wake kisawasawa. Unaweza kudhani hivyo, lakini safari hii Chris hakuwa mbele ya kamera.
Alikuwa akizungumza kutoka ndani na kueleza hisia za kweli za moyoni mwake. Laura alimteka kwa hakika.
“Hata kama nikikubali Chris, kumbuka baba yako ameshasema anataka mke wako atoke kijijini. Angalia... kwanza mimi siishi kijijini, pia siyo Mnyiramba kama baba yako anavyotaka. Mimi ni Msukuma. Itakuwaje?”
“Najua cha kufanya Laura. Ninalo wazo.”
“Wazo gani?” Laura akauliza harakaharaka.
“Lipo lakini nataka kujua kwanza kutoka kwako. Wewe unanipenda?” Chris akamwuliza Laura.
“Ndiyo... kwa nini nimchukie binadamu mwenzangu? Nawapenda watu wote.”
“Tafadhali Laura, usiniumize hisia zangu. Usiutese moyo wangu tafadhali. Nazungumzia mapenzi hapa. Tunajadiliana kuhusu maisha mama. Tafadhali chukulia kwa uzito huohuo Laura.”
“Nakupenda Chris,” Laura akasema mara moja tu, akanyamaza.
“Kweli?”
“Ndiyo... lakini bado kuna mambo nahitaji kuzungumza kidogo na wewe. Kuna vitu nataka kujua zaidi kuhusu wewe. Nadhani tukutane Club jioni, tuzungumze zaidi.”
Chris alisimama alipokuwa amekaa, akapiga hatua fupi nne, akamfikia Laura. Akamnyooshea mikono yake miwili kama ambaye alitaka kupokewa. Laura akaipokea.
Taratibu Chris akamwinua Laura, akasogea mzimamzima. Akamlaza kifuani mwake. Miili yao ikakutana. Wote kwa pamoja wakapata msisimko mkali sana.
“Nakupenda sana Laura,” Chris akatokwa na maneno hayo huku akimwaga machozi.
“Nakupenda pia Chris, sikutegemea kama ningekupenda kwa kiwango hiki. Ngoja niwe mkweli... sikukupenda hata kidogo lakini sasa naona ni kwa namna gani ningepoteza mtu muhimu sana maishani mwangu.
“Nimekupa kila kitu mpenzi wangu. Nakupa moyo wangu. Chukua mwili wangu. Nichukue baba. Nichukue mpenzi. Mimi ni wako kwa kila kitu. Nifanye upendavyo!”
Chris akasisimka!
Sheria yake ilikuwa ileile. Ndani ya nafsi yake, huba zito lilimlemea. Kamwe hakutaka kuonekana mhuni. Pamoja na maneno yale ya Laura kuashiria kwamba alikuwa tayari kwa lolote, moyoni Chris alikataa!
“Ahsante dear. Nami nimekukabidhi kila kitu mpenzi wangu. Nakupenda sana.”
“Nitoe baba niondoke, jioni tukutane Club sawa?”
“Sawa mama.”
Wakatoka nje wakiwa wameshikana mikono. Laura akaingia kwenye taksi na kuondoka zake. Ahadi ilikuwa kukutana Club usiku.
***
Ni saa nne na dakika zake usiku. Chris alikuwa anatoka kwenye Baa ya G8, Kibaoni. Kutoka hapo hadi ilipo hoteli yake ni jirani mno, ni mwendo wa dakika mbili tu kwa miguu. Njiani akakutana na mmoja wa wahudumu wa hoteli aliyofikia.
Akamwambia: “Kaka unatafutwa na maaskari. Kumbe yule mwanamke uliyekuwa naye chumbani ni mke wa polisi, tena ni mkuu pale Central. Wamekuja maaskari wanne na silaha wanakutafuta. Mimi nakushauri usirudi tena. Tafuta mahali ulale mpaka asubuhi wakati tukitafuta ufumbuzi wa hili jambo,” alisema akionekana kujawa na wasiwasi mwingi.
Itaendelea siku ya kesho
TOA MAONI yako hapa na share kama unataka iendeleee ukishare utatumiwa sehemu inayofuata kabla ya kesho.
UKIWA UMEPITWA SEHEMU YA NYUMA BONYEZA HII TAG #2JIACHIE
Powered by Blogger.