ad

ad

Singidani (A Story From My Heart) - 14



ILIPOISHIA...
Alikuwa akimfuata msanii mwenzake Ramsey.
SASA ENDELEA...
ALIKANYAGA mafuta kisawasawa, foleni ni kama ilikuwa hakuna kabisa usiku huo. Dakika kumi tu zilitosha kabisa kumfikisha Mzalendo Pub. Akaegesha gari lake kisha akapanda hadi ghorofa ya kwanza ilipo Pub hiyo.
Hakupata shida kujua Ramsey alipokuwa amekaa maana walikuwa na kawaida ya kukaa sehemu moja ndani ya Pub hiyo kila walipokwenda. Alimfuata akiwa ameachia tabasamu mwanana.
“Vipi kaka?” Ramsey akamsalimia.
“Poa, mambo?”
“Fresh kabisa... vipi za kijijini?”
“Daaah! Huko acha tu. Yaani habari ndefu sana kaka. Nimekutana na mengi sana huko.”
“Usiniambie umepata mwanamke wa ukweli tayari... ni Mnyiramba au Mnyaturu?” akauliza Ramsey.
“Mh! Wapi ndugu yangu? Majanga tu mzee.”
“Imekuwaje?”
“Ngoja nikusimulie.”
Chris akakaa sawasawa... ni muda huo mhudumu alifika mezani kwake na kutaka kumsikiliza. Aliagiza pombe kali. Wakati mhudumu anakwenda kaunta kumchukulia kinywaji chake, Chris alianza kumsimulia Ramsey.
Hakuna alichomficha, alimweleza yote yaliyotokea Singida Mjini. Mipango waliyopanga na baba yake mdogo, Shamakala na namna alivyozugumza na baba yake baada ya kuingia Dar usiku huo.
“Aisee una kazi kaka. Yote hayo nimekusikia lakini sasa nahisi mzee mzima unaweza kuingia kwenye skendo!”
“Skendo?” Chris akahamaki.
“Ndiyo! Kama huyo mwanamke wa Singida kweli ni mke wa mtu, tena wa polisi, kuna nini tena kaka? Utachafuka!” Ramsey akasema kwa msisitizo.
Chris akabaki kimya.
Maneno yale yalimwingia akilini. Alitulia akifikiria kwa kina, akajikuta akipoteza furaha. Ni kweli alikuwa maarufu kiasi kwamba, mtu yeyote akitaka kumpata muda wowote ingekuwa rahisi tu.
“Lakini kaka, ukweli ni kwamba sikutembea naye!” Chris akamwambia Ramsey.
“Sawa ila si ulikuwa naye chumbani?”
“Kaka kuna mambo ya kisheria hapo. Hata kama nilikuwa naye chumbani, hakuna mtu aliyenikuta nikiwa naye huko chumbani. Kama ningekuwa nimefumaniwa ingekuwa sawa, lakini maneno tu ya mtaani yanaweza kunikamatisha na kuniweka ndani?”
“Kaka tunywe tu bwana!” akasema Chris kwa sauti ya kilevi.
“Ndicho kilichobaki mkubwa. Aisee nina majukumu mengi sana wiki hii. Sijui itakuwaje lakini nitajipanga,” akasema Chris.
Pombe zikaendelea. Haikuwa rahisi kwa Chris kukaa pale muda mrefu hasa kwa sababu ndiyo kwanza alikuwa ameingia Dar. Bado mawazo juu ya Laura yaliendelea kumzonga.
Alitamani sana Laura asingekuwa mke wa mtu!
***
Laura alipoteza amani ya moyo kabisa... mwanaume aliyempenda ghafla haonekani tena mbele yake. Alifikiria sana namna ya kumpata lakini alikosa majibu.
Alijiuliza maswali mengi sana, lakini mwisho alipata wazo zuri. Lilikuwa jambo gumu sana kwake lakini alikuwa tayari mradi ampate Chris.
“Lazima niende Dar es Salaam...” akawaza Laura.
Lilikuwa wazo zuri lakini lingetumia muda mwingi sana kukamilika. Alikuwa tayari kupoteza masomo japo kwa wiki moja ili aweze kumpata Chris, mwanaume wa maisha yake.
Mara moja akaanza kupanga mipango ya safari ya kwenda Dar es Salaam.
***
Laura alikuwa amedhamiria hasa. Wiki moja baadaye alikuwa jijini Dar es Salaam. Saa 11:00 jioni  alikuwa anashuka ndani ya Basi la ABC katika kituo kikuu cha mabasi ya mikoani na nchi jirani, Ubungo jijini Dar es Salaam.
Alikuwa amechoka sana. Hakuwa mgeni wa Dar es Salaam. Alikuwa na ndugu zake wawili waliokuwa wakiishi jijini humo ambao kuna wakati huwa anakwenda kuwatembelea.
Mama yake mdogo aishiye Kurasini na mjomba wake anayeishi Gongo la Mboto ndiyo ndugu zake jijini Dar. Hakutaka kabisa wajue uwepo wake jijini Dar kwa sababu alikwenda kwa sababu maalum.
Alichukua taksi na kumwambia dereva ampeleke Manzese. Huko aliamini angepata gesti ya bei nafuu ambayo angeishi hapo kwa wiki nzima wakati akimtafuta Dk. Chris.
Wakiwa wanakaribia mataa ya Shekilango, Laura akavunja ukimya, alijua kwa kumtumia dereva yule  angepata mwanga wa wapi pa kuanzia ili aweze kumpata Chris.
“Kaka hivi nawezaje kumpata Dk. Chris, yule mcheza filamu?” Laura aliuliza kwa sauti laini, akiyalegeza macho yake na kumfanya dereva apoteze umakini barabarani.
“Vipi unataka kumwa mwigizaji au umeshampenda bibie?” dereva yule akajibu huku akiachia tabasamu, macho yake akiwa ameyatuliza kwa Laura.
Aliporudisha macho yake barabarani, alishangazwa sana na kitu kilichotokea!
“Nakufaaa....” Laura akapiga kelele.
Usikose kufuatilia kesho.

Powered by Blogger.