Saa 192 za Lowassa, Magufuli ikulu

Saa 192 za Lowassa, Magufuli ikulu Na Mwandishi Wetu NI saa 192 tu zilizobaki kuamua nani atakayekuwa rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baina ya Dk. John Magufuli wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa wa Chadema. Vyama hivyo viwili vinaendelea na kampeni za nguvu katika siku nane za mwisho ambapo CCM inakamilisha ratiba zake visiwani Zanzibar kabla ya kuelekea Kanda ya Ziwa. Hata hivyo, gumzo kubwa katika kipindi hiki kilichosalia ni kuona hatima ya ndoto za Safari ya Matumaini ya Mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa, zilizoanza miaka 20 iliyopita kama zinafikia ukingoni. Watanzania wanasubiri kutumia haki yao ya kikatiba kuiweka madarakani serikali ya awamu ya tano kwa kuwachagua madiwani, wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mara ya kwanza uchaguzi huo umekuwa wa upinzani mkali tofauti na chaguzi zilizowahi kufanyika tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania. Ingawa wiki moja ni muda mrefu katika siasa, lakini taswira inaonyesha wazi kwamba mbio za urais katika uchaguzi wa mwaka huu zimekuwa kama za ‘farasi wawili’ – John Pombe Magufuli wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa wa Chadema ambao hatima ya nani atakaa Magogoni baada ya Rais Jakaya Kikwete itaamuliwa na masanduku ya kura Oktoba 25, 2015. Safari ya Lowassa kutaka kuwa amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama nchini Tanzania haikuanza jana, bali ilianza Jumatatu, Julai 12, 1995 wakati yeye na Jakaya Kikwete, rais anayemaliza muda wake, walipochukua fomu za kuwania urais mjini Dodoma. Lowassa ameendelea kuwa na ndoto za kuwa rais hata baada ya kupewa uwaziri mkuu ambao alijiuzulu kwa kashfa ya kuipa zabuni kifisadi kampuni ya Richmond. Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanaeleza bayana kwamba, ‘Mtandao’ ulioundwa ndani ya CCM mwaka 2005 ndio unaoendelea kumbeba Lowassa kila anakokwenda, licha ya propaganda zinazoenezwa kwamba ana nyota ya kupendwa na kwamba anakubalika. Chadema, ambao wamenufaika zaidi na ujio wa Lowassa, tayari wamejihakikishia ushindi na mara kadhaa wamekuwa wakitangaza kwamba wanasubiri mgombea wao aapishwe tu. Lakini kwa upande mwingine, Magufuli wa CCM ameweza kuvunja ukuta mnene uliokuwepo wa ‘kukataliwa kwa CCM’ na kuudhihirishia umma kwamba yeye ndiye chaguo sahihi la chama hicho na Tanzania kwa ujumla, kwani kero zote zinazotajwa na wapinzani zinaweza kumalizwa yeye akichaguliwa. Hakuna hesabu rahisi inayoweza kuthibitisha ushindi kwa CCM ama Chadema, lakini kinachoonekana katika siku nane za mwisho ni kasi kubwa ya Magufuli kurudisha imani ya Watanzania na kuongeza asilimia ya kura zake.
Post a Comment