ad

ad

Kamatakamata ya wagombea ubunge Chadema yafikia wanne.

agombea ubunge wengine wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa anayetetea Jimbo la Iringa Mjini na Jonas Kalinde anayegombea katika Jimbo la Mpanda, walikumbana na adha ya kutiwa mikononi mwa polisi usiku wa kuamkia jana na kushikiliwa kwa saa kadhaa kutokana na tuhuma zinazohusiana na kuvunja sheria katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 25.
 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi.
Kukamatwa kwa wagombea hao kunafanya idadi ya wagombea ubunge wote wa Chadema waliowahi kukumbana na ‘kibano’ cha polisi tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu kufikia wanne.
 
Wengine waliowahi kukumbana na adha hiyo ni Godfrey Lema anayetetea Jimbo la Arusha Mjini na Benson Kigaila anayewania Jimbo la Dodoma Mjini. Hata hivyo, Kigaila na wafuasi wengine kadhaa wa Chadema kwenye Jimbo la Dodoma wameshafikishwa mahakamani kukabiliana na mashtaka. Lema alikamatwa na kushikiliwa kwa muda kabla ya kuachiwa baada ya kuhutubia mkutano wa kampeni kwa dakika kadhaa baada ya saa 12:00 jioni.
 
 
SAKATA LA MSIGWA
Msigwa anayewakilisha pia umoja wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema,  NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF), alikamatwa juzi usiku ikiwa ni muda mfupi baada ya kukamatwa kwa wafuasi 62 wa chama chake. Wote walishikiliwa na polisi mkoani Iringa, baada ya kudaiwa kufanya vurugu na kufunga baadhi ya barabara za maeneo ya mjini (Iringa).
 
Inaelezwa kuwa vurugu hizo zilitokea jirani na Uwanja wa Samora kulikokuwa kukifanyika mkutano mkubwa wa kampeni wa mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa watuhumiwa hao walikamatwa jana jioni karibu na Kambi ya Kikosi cha Kuzuia ghasia FFU.
 
Alisema awali, wanachama hao wa Chadema walikuwa na kikao chao cha ndani kilichoanza mchana na walipomaliza saa 12: 30 jioni, walianza kufanya vurugu na kufunga barabara ya kutoka Iringa Mjini kuelekea Kihesa.
 
Alisema kulikuwa na pikipiki zaidi ya 150 zilizokuwa zimefunga barabara hiyo, hivyo kusababisha isipitike na kuwaletea usumbufu mkubwa watumiaji wengine wa barabara.
 
Kamanda Mungi alisema mkusanyiko huo ulikuwa mkubwa na wote walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kuhamasishana huku wakizuia watumiaji wa barabara hiyo.
 
“Tulipata taarifa na nikamwagiza kamanda wa FFU akawaondoe lakini katika hali isiyo ya kawaida, askari walipofika pale wale vijana walianza kuwarushia mawe na ndipo askari walipofyatua mabomu ya machozi kuwatawanya na kisha kuwakamata baadhi yao," alisema Kamanda Mungi.
 
Mungi alisema Mchungaji Msigwa hakuwapo eneo la tukio lakini alikamatwa baadaye kutokana na kuhisiwa kuwa ndiye aliyepanga njama kuwezesha kutokea kwa vurugu hizo.
 
Taarifa zaidi zilieleza baadaye kuwa Msigwa na wafuasi hao wa Chadema waliachiwa jana kwa dhamana na leo saa 2:00 asubuhi wanatakiwa kuripoti polisi huku wakitarajiwa kufikishwa mahakamani pindi taratibu za kufanya hivyo zikikamilika.
 
KUKAMATWA KALINDE
Inaelezwa kuwa mgombea ubunge wa Chadema Jimbo la Mpanda, Kalinde, alikamatwa akiwa na viongozi wenzake kadhaa wa chama hicho kwa tuhuma za kufanya maandamano bila kibali.
 
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Kalinde alisema wakati akitoka kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kata ya Shanwe, Mtaa wa Kigamboni mjini Mpanda, waliharibikiwa na gari na kuanza kutembea kwa miguu hadi katika ofisi za chama chao kabla ya kukamatwa majira ya saa 12:30 jioni.
 
“Gari langu liliharibika. Nikalazimika kuondoka kwa miguu nikiwa na viongozi wenzangu wasiozidi kumi na tukiwa njiani, tulipishana na polisi ambao hawakusema lolote. Cha kushangaza, tulipokaribia ofisi za Chadema ndipo tukakamatwa kwa kudaiwa tumeandamana. Inashangaza sana,” alisema na kuongeza kuwa walishikiliwa na polisi hadi saa saa 4:00 usiku ndipo walipoachiwa kwa dhamana.
 
Alisema ameshangazwa kuona wao wakiandamwa na polisi wakati wenzao wa CCM wamekuwa wakiachwa bila kubughudhiwa wanapokuwa kwenye misafara kuelekea au kurejea kutoka kwenye mikutano ya kampeni.
 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi hakupatikana kuzungumzia tukio hilo na hata alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi, iliita mara kadhaa bila kupokewa.
 
CHADEMA WAJA JUU
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, alilalamikia matukio ya kukamatwa kwa wagombea wao kutokana na madai mbalimbali na kudai kuwa kuna kila dalili kwamba kinachofanyika ni matokeo ya kuwapo kwa mbinu za kutaka kuwadhoofisha Chadema kwa manufaa ya chama tawala (CCM).
 
Alisema dalili za kuwapo kwa mpango huo zinadhihirishwa na ukweli kuwa juzi, Msigwa na wanachama wengine wa Chadema walikuwa kwenye mkutano wa ndani na inashangaza kusikia polisi wakidai kuwa walifanya vurugu.
 
“Watu wapo kwenye mkutano wa ndani... polisi wanakuja na kuwatembezea kipigo. Hii inaonyesha wazi kuwa CCM haijawahi kupitia wakati mgumu kama ilivyo katika uchaguzi wa mwaka huu na hivyo hofu ya kushindwa ndiyo inayotruletea adha hizi,” alisema Makene.
 
Kadhalika, alizungumzia tukio la kukamatwa kwa Kalinde na wenzake waliodaiwa kuandamana bila kibali Mpanda, akisema huo ni muendelezo wa visa wanavyofanyiwa wagombea wao wa ubunge kwani wala hawakuwa wakifanya maandamano.
 
“Hivi hawa watu hawakuwa na gari. Ina maana wanataka watembee vipi? Zote hizi ni mbinu chafu tu kutaka kutuvuruga,”  alisema.
 
*Imeandikwa na Joseph Mwendapole, Beatrice Shayo na George Tarimo
 
CHANZO: NIPASHE
Powered by Blogger.