AZIZA WA FACEBOOK - 7

BONYEZA==> #2jiachie
ILIPOISHIA : www.facebook.com/2jiachie
ILIPOISHIA
AZIZA: Hahahah! Utaweza kunilipa?
MIMI: Kwa nini nisiweze? Nitakuwa na fedha mbayaaa....nitamiliki magari ya kifahari na majumba makubwa sana....lol! sasa endelea...
AZIZA: Yote ni mipango ya Mungu ila napenda ulivyoongea kwa sababu unaonekana una imani ya kupata hivyo, cha msingi yakupasa kujituma tu na kumtanguliza Allah kwa kila kitu. Naomba nikuulize swali.
MIMI: Usijali. Uliza.
AZIZA: Unaishi wapi?
MIMI: Tandale kwa Mtogole.
AZIZA: Kule kwenye wezi wengi na wakabaji?
MIMI: Si wezi wengi tu, kule kunapodharaulika na watu wenye fedha kama nyie.
AZIZA: Hahaha! Usiseme hivyo bwana. Ila mbona umedanganya?
MIMI: Nimedanganya nini?
AZIZA: Kwenye profile lako. Umeandika unaishi Romania. Ulikuwa unataka kujipaisha nini upate wanawake?
MIMI: Hapana Aziza. Hiyo imekuja yenyewe tu.
AZIZA: Kivipi?
MIMI: Nilikuwa nataka kupatambulisha kama home kwetu ni Tandale. Ila nilipokuwa nikiandika Tandale, haikuwa ikitambulika kama ilivyokuwa sehemu nyingine. Matokeo yao wao kama facebook wakaniletea Tandalesti mji fulani kutoka Romania, nikaona sio kesi, nikakubaliana nao, ila ukiangalia kwa makini, Tandale imetokeza katika jina hilo.
AZIZA: Yeah! Nimeona. Hebu naomba uniambie mengi kuhusu Tandale.
MIMI: Kama yapi unataka kufahamu?
AZIZA: Mazingira, watu wa huko na mambo mengine.
MIMI: Tandale kama Tandale mazingira yake mazuri sana, watu full kuyafurahia maisha kama kawa. Kuna watoto wazuri, watoto ambao wanajitambua wao ni nani na kipi cha kufanya maishani mwao. Kuna mambo ya Rusha Roho usiku, yaani kwa kifupi kuhusu maisha, huku tunakula sana bata kuliko kwenu pa kulala saa moja.
AZIZA: Hahaha! Kwani huko kwenu huwa mnalala saa ngapi?
MIMI: Huwa nikiwa mgonjwa sana, nawahi kulala kama saa saba hivi.
AZIZA: Saa saba?
MIMI: Yeah! Ila nikiwa si mgonjwa, mpaka adhana iadhiniwe. Watu tunatransform usiku kuwa mchana na maisha yanasonga.
AZIZA: U must be kidding me Ibra.
MIMI: Huo ndio ukweli Aziza. Siwezi kukutania.
Unaona jinsi mawasiliano yetu yalivyokuwa yakienda? Hapo ndipo nilipokuwa napataka sasa. Nilikuwa namletea sana ucheshi lakini mwisho wa siku kuna kitu nilikuwa nakihitaji kutoka kwake, namba ya simu tu. Unajua katika maisha ya kuchati facebook huwa yanachosha sana, kuna kipindi fulani automatically unatokea kummisi mtu fulani na ungependa sana awe hewani lakini hayupo hewani, unapokuwa na namba ya simu, inakupa wakati mzuri wa kumsikia na kumjulia hali katika kipindi chochote ambacho ungependa kumsikia.
Ucheshi ndio ulikuwa kawaida yangu ila katika kipindi hiki nilikuwa nataka kuuleta ucheshi mpaka katika maandishi. Aziza akaonekana kulifurahia hilo, akaonekana kuanza kunikubali japokuwa hatujawahi kuonana hata siku moja. Nilikuwa bize na chatting na Aziza, sikutaka kuwasiliana na mtu mwingine katika kipindi hicho japokuwa nilimuona Eduado, Ibra Akilimia na Emmanuel Solo walikuwa wamenitumia meseji.
Nilikuwa nikijitahidi sana kumuingiza Aziza kwenye himaya yangu, yaani aingie bila kupenda na mwisho wa siku kila kitu kiwe poa sana. Sikujali alikuwa akiishi wapi, sikujali na mimi nilikuwa nikiishi wapi, kitu ambacho nilikuwa nikikiamini ni kwamba mapenzi wala hayakuwa na hiyana, yalikuwa hayabagui watu kama tulivyo wanadamu.
AZIZA: Nikuulize kitu.
MIMI: Niulize tu.
AZIZA: Unasoma?
MIMI: Hapana.
AZIZA: Unafanya kazi?
MIMI: Hapana.
AZIZA: Sasa unafanya nini?
MIMI: Niponipo nyumbani. Nilisoma kidato cha kwanza, sikuwa na fedha za kuniendesha kielimu, nikaachana nayo mpaka sasa hivi. Kuna kipindi nilipata vijisenti mara baada ya kubeba sana mizigo Tandale sokoni, nikaenda kusoma English Course.
AZIZA: Kwa hiyo haufanyi kazi?
MIMI: Yeah! Sifanyi kazi.
AZIZA: Unafanya kitu gani kingine?
MIMI: Sifanyi chochote kile.
AZIZA: Ila niliona kama unaandika hadithi! Au majina yamefanana?
MIMI: Yeah! Huwa ninazipost tu.
AZIZA: Hadithi zile huwa unaandika wewe?
MIMI: Hapana.
AZIZA: Sasa huwa anaandika nani?
MIMI: Anaandika baba na kisha mimi kuzichukua na kuziweka facebook.
AZIZA: Unanidanganya Ibra.
MIMI: Nikudanganye ili iweje? Kuna tuzo ya uongo wanapewa waongo? Huo ndio ukweli.
AZIZA: Mmmh! Basi mpe hongera baba yako.
Mimi: Zimefika.
Wakati mwingine haitakiwi kuwa mkweli kwa kila kitu. Tayari nilikwishaona kwamba kagundua kwamba sisi ni watu tunaoishi sehemu mbili tofauti, madaraja mawili tofauti na katika kichwa chake aliamini kwamba Tandale wanaishi watu masikini japo haikuwa hivyo. Nilichokuwa nikikifanya ni kuendana na akili yake alivyokuwa ameiweka, nami nikaanza kujifanya masikini ambaye sikubahatika kusoma kwa kuwa sikuwa na fedha ya kuniendeleza kielimu.
Nikafanikiwa, kwa kiasi fulani aina ya maisha ambayo nilimpa yalimfanya kuamini kwamba kweli nilikuwa mtoto wa uswahilini, nilijivunia kuishi Tandale katika uwepo wake.
Maisha yalikuwa yakiendelea kama kawaida, kuhusu Aziza, wala sikuwa na wasiwasi kwa kuamini kwamba piga ua huyu mtoto ni lazima ningemchukua bila tatizo lolote lile.
Itaendelea siku ya kesho.
Post a Comment