ad

ad

AZIZA WA FACEBOOK - 1 & 2


AZIZA WA FACEBOOK - 01
www.facebook.com/2jiachie
Mtunzi: Nyemo the Prince ‪#‎2jiachie‬
NAJISIKIA nimechoka sana, nimechoka sana kwa sababu nilikuwa nimetoka kucheza mpira uwanjani huku nikiwa nimechafuka kupita kawaida.
Ninapofika nyumbani, ninaoga na kisha kuchukua simu yangu kwa ajili ya kuangalia updates za facebook, sikukuta hata meseji moja zaidi ya notification tu, tena wala hazikuwa nyingi. Nilichokifanya ni kuanza kuzugazuga hapa na pale na kisha kutulia. Mara ghafla nikaona namba moja nyekundu kwenye sehemu ya meseji, kulikuwa na meseji imeingia, nilichokifanya, nikaifungua na kuanza kuchati na mtu huyo huyo.
EDUADO: Mambo vipi Shahruk Khan.
MIMI: Hahaha! Poa. Inakuwaje wewe mtu?
EDUADO: Kama kawa. Nilikuwa nakusubiri sana hewani. Nilikuwa na mzuka na wewe ile mbaya.
MIMI: Duh! Mzuka na mimi! Kuna nini tena?
EDUADO: Kuna bonge la kazi hapa. Unataka?
MIMI: Kwa nini nisitake? Nipe mawasiliano yao niandike barua ya kuomba kazi fasta.
EDUADO: Hahahaha! Kaka unakosea. Niliposema kazi sikumaanisha hiyo.
MIMI: Wewe ulimaanisha ipi sasa?
EDUADO: Kazi moja hivi. Kazi ambayo watu wengi wameishindwa hasa masharobaro.
MIMI: Hahahaha! Itakuwa kubeba zege hiyo watoto wa mama hawaiwezi. Mimi naiweza, hebu niambie ni jengo gani?
EDUADO: Siyo kazi ya kubeba zege. Kuna mtu nataka umfanyie kazi.
MIMI: Mtu gani?
EDUADO: Kuna mrembo fulani nipo naye hapa UDSM ni mkali ile mbaya. Yaani mkali mpaka nashindwa kusema ukali wake unafanana na nini.
MIMI: Hebu acha masihara kaka. Kwa hiyo kama mkali mimi nifanye nini?
EDUADO: Huyu mrembo anaringa mbaya. Yaani mrembo ananata utafikiri akanyagi ardhi hii tunayochimbia vyoo.
MIMI: Oke! Wazuri wapo wengi na hata wenye maringo wapo wengi pia. Hebu niambie kuhusu huyo. Kwanza anaitwa nani? Nipe maelezo ya kujitosheleza na siyo naanza kumtengeneza mrembo mkali kichwani mwangu ikawa ndivyo sivyo.
EDUADO: Huyu mrembo anaitwa Aziza Moddy, anaishi Msasani, baba yake ni mfanyabiashara mkubwa sana aisee. Ni mrembo fulani pini…yaani ni pini sana.
MIMI: Hebu acha masihara. Sasa inakuwaje watoto wa kisharobaro wamemshindwa?
EDUADO: Huyu mrembo hafagilii muonekano, ni mrembo fulani ambaye anapenda mtu amfuate kama jinsi alivyo. Yaani kama wewe ni mtu wa chini, mfuate hivyohivyo ila tatizo watoto wa hapa chuo wanapenda kumfuata kisharobaro kaka.
MIMI: Dah! Kwa hiyo kazi unayotaka kunipa ni ipi?
EDUADO: Umchukue huyu mtoto. Yaani ukifanikiwa, moyo wangu utakuwa mweupeee kama theluji.
MIMI: Hahaha! Usitake kunichekesha Eduado, hivi unamkumbuka Sikitu?
EDUADO: Sikitu yupi?
MIMI: Si yule mrembo wa mwaka jana ambaye ulikuwa unamsifia sanaaa kwamba mkali kumbe wala hakuwa mkali kama ulivyokuwa ukimsifia, mbaya zaidi alikuwa anakaa mbali, Musomaaa.
EDUADO: Achana na hayo, yule msahau kwani mimi mwenyewe alinitumia picha ambayo siyo yake. Ila kaka kiukweli Aziza ni mrembo mmoja mkali sana. Hapa chuo amekuwa gumzo kila kona, vijana wengi wamechemka.
MIMI: Sasa kama wengine wamechemka mimi nitaweza vipi?
EDUADO: Hahahaha! Kaka ninakuamini sanaaa, wewe mtu unaweza sana kuongea, unaweza sana kuandika. Endapo nitakupa kazi hii na ukishindwa, hakika nitajua kweli duniani kuna wasichana wagumu.
MIMI: Kwa hiyo kazi yako ina malipo au?
EDUADO: Ikitokea umempata, nitakupa zawadi kaka. Yaani ninachokitaka huyu mrembo umchukue tu, basiii. Anaringa sana, ananata sana, yaani sijui niseme vipi.
MIMI: Ila si anaringa kwa sababu mzuri?
EDUADO: Ndiyo. Ila yeye kazidi.
MIMI: Ila kwa sasa aisee nahisi nimepoteza kumbukumbu zangu za kuongea na hawa watoto wa kike, sijui kama nitaweza.
EDUADO: Acha kunitania kaka. Nakuamini sana kwamba unaweza kuliko mtu yeyote na ndiyo maana nikakufuata wewe. Hivi haujiulizi kwa nini sikumfuata Thomas? Thomas kwenye kuongea mkali sana ila kwenye kuandika hakuna kitu, ila wewe, aisee una kipaji kila kona, sidhani kama kuna demu ambaye utamtokea asikukubali!
MIMI: Hahaha! Hebu acha kunipamba. Hebu niambie, huyo mrembo yupo Facebook?
EDUADO: Amejaa teleee…yaani kajaa teleee. Anajiita Aziza M Aziza. Ni mrembo mkali sana. Hebu mcheki kwanza.
MIMI: Sawa.
Sikutaka kuchelewa, tayari kichwa changu kikaanza kujazwa na sura nyingi za wasichana wazuri huku nikianza kuzigawanya kimakundi kwamba huyu alikuwa Aziza mwenyewe huyu hakuwa mwenyewe. Nilikuwa namfahamu Eduado tangu tukiwa sekondari alipokuwa akisema msichana fulani ni mzuri, mzuri kweli japokuwa kwa Sikitu alikuwa ameniingiza choo cha kike.

AZIZA WA FACEBOOK - 2

ILIPOISHIA;
Sikutaka kuchelewa, tayari kichwa changu kikaanza kujazwa na sura nyingi za wasichana wazuri huku nikianza kuzigawanya kimakundi kwamba huyu alikuwa Aziza mwenyewe huyu hakuwa mwenyewe.
Nilikuwa namfahamu Eduado tangu tukiwa sekondari alipokuwa akisema msichana fulani ni mzuri, mzuri kweli japokuwa kwa Sikitu alikuwa ameniingiza choo cha kike.
SASA ENDELEA:
Sikutaka kuremba, mara baada ya kuona majina kadhaa, nikamfuata Eduado inbox.
MIMI: Oyaa Akshey.
EDUADO: Vipi ushampata?
MIMI: Wamekuja akina Aziza wengi hao, mpaka wengine wanakaa India.
EDUADO: Hebu subiri.
Sikujua alikuwa akifanya nini, kwa sababu aliniambia kwamba nisubiri, wala sikuwa na presha, nikamsubiri nione angeniambia kitu gani baada ya hapo. Nilimsubiri kwa kipindi kama cha dakika moja hivi, akanijia tena inbox.
EDUADO: Umeiona hiyo picha yenye mdoli wa Barbie?
MIMI: Yeah!
EDUADO: Ndiye yeye huyo. Ibra huyo ni mrembo mkali ambaye sijawahi kuona.
MIMI: Acha utani.
EDUADO: Shua. Unamkumbuka Silvia tuliyesoma naye? Sasa Silvia haingii kwa Aziza.
MIMI: Acha utani kaka. Silvia haingii?
EDUADO: Kweli tena. Tena hagusi hata robo.
MIMI: Sasa mbona hajaweka picha yake, nitamjua vipi kama ni mkali. Hebu nimpe sifa kwanza manake naona picha zake kazipiga pini watu wasio marafiki zake wasizione.
EDUADO: Kwanza mrembo ni pini sana, mrembo kwao wana mahela ya kumwaga, chuo anakuja na gari, Verrosa moja nyeusi, mtoto anamiliki laptop aina ya Apple ile inaayouzwa milioni tatu, mtoto anamiliki anamiliki iPhone 5 huku akisema kwamba iPhone 6 ikianza kuuzwa atataka kuanza kuitumia kwani anapenda kwenda na wakati.
MIMI: Kaka utakuwa unanitania tu.
EDUADO:  Kweli tena. Halafu kuna cha zaidi.
MIMI: Kipi?
EDUADO: Otea.
MIMI: Hebu niambie kipi?
EDUADO: Ugonjwa wako.
MIMI: Unamaanisha nini?
EDUADO: Mtoto Mpemba.
MIMI: Hahahaha! Kaka acha utani, utanifanya nimfuate sasa hivi.
EDUADO: Ndiyo hivyo. Mtoto ni pini sana, pini ile iliyosimama.
MIMI: Hahaha! Pini kama ya Blackberry vile.
EDUADO: Acha kaka. Mtoto ni pini zaidi ya zile za Blackberry. Kwanza ukimuona tu, mtoto utampenda. Mavazi yake sasa…weeeeee.
MIMI: Hebu nipe sifa zake kwa ujumla.
EDUADO: Nisikilize. Mtoto ni wa Kipemba. Ana nywele ndefu zinazomfikia chini ya mabega yake, mtoto ana hipsi zilizopangika, hapa mashavuni mwake ana vijishimo viwili, lipsi lainiiiii kila wakati zinang’aaa.
MIMI: Kingine?
EDUADO: Mtoto ana sura nyembamba, masikio hayaonekani sana, kifuani hapa kumesimama vizuri sana, mavazi yake huwa ni suruali za jinsi kwa sana.
MIMI: Umesema anaishi wapi?
EDUADO: Anaishi Masaki.
MIMI: Halafu mimi naishi uswahilini Tandale. Umesema anamiliki simu gani?
EDUADO: Anamiliki iPhone 5.
MIMI: Halafu mimi namiliki Nokia ya Tochi. Umesema baba yake ana gari?
EDUADO: Yeah! Yeye mwenyewe analo.
MIMI: Mimi sina gari na baba yangu hana hata gari.
EDUADO: Acha kujidharau Ibra. Mtoto unang’oa huyu.
MIMI: Usijali. Ushawahi kufika kwao?
EDUADO: Yeah kaka. Kwanza hiyo nyumba yao….duh! Kuna watu wanakufuru. Kwanza bonge la nyumba. Limezungushiwa ukuta, jumba lina fensi kwa juu, ndani kuna kamera, nyumba vigae, ukiingia ndani unakutana na bwawa la kuogelea. Kuna ungo wa Dstv, kuna bustani kali ya maua mbalimbali, kuna walinzi wawili ambao wanalinda kwa silaha za moto. Yaani wapo full.
MIMI: Oke! Mimi naishi Tandale. Nyumba yetu ndogo, haina ukuta wala fensi, haina mlinzi na kama kuogea, tunaogea bafuni na si kwenye bwawa. Mpaka hapo, nimeshamkosa.
EDUADO: Ibra. Usiniangushe. Yaani mimi lengo langu umchukue huyu mtoto tu.
MIMI: Una namba zake za simu?
EDUADO: Hapana.
MIMI: Basi ngoja nifanye mishe halafu nione itakuwaje. Ila wasiwasi wangu uleule tu, itakuwa kama Sikitu.
EDUADO:  Usijali kaka. Huyu siyo kama Sikitu. Kwanza yule demu mwenyewe alinitaka nikaamua kukurushia wewe. Mimi na mrembo wa mkoa wapi na wapi. Ishi Dar tuwe tunamalizana, mambo ya mikoani wapi na wapi? Hapa hapa Bongo ndiyo pazuri, ukimtaka tu demu, nauli yako sh 400 kwenda, 400 kurudi. 600 soda yako, 600 soda yake. Mwisho wa siku kwa gharama zote ukitoa buku tano, michenji inarudi kibao na kusababisha usumbufu mfukoni.
MIMI: Hahaha! Umeonaeee. Hakuna gharama kabisa. Ila poa, usijali. Ngoja nimtumie friend request halafu nianze kumfanyia uninja. Ila niandalie zawadi yangu.
Itaendelea siku ya kesho!

Powered by Blogger.