ad

ad

JINI LA DARAJA LA SALENDA - 10



ILIPOISHIA:
“Nina imani mmebahatika kumuona Balkis jinsi alivyo mwanamke mzuri sana, ambaye hakuna mwanaume atakayemtaka akamkataa. Mchumba’ako akaingia kichwa kichwa kumtaka kimapenzi, kana kwamba hana shida na mumeo, alipoonesha dalili za kumtaka alimuuliza maswali ya mitego, kama angekuwa na akili angetambua kuwa yule si mtu wa kawaida. SASA ENDELEA...

Lakini kutokana na kuchanganyikiwa na mapenzi, hakupata muda wa kujiuliza, Balkis alimuuliza maswali kuhusiana na uhusiano wenu, hakushangaa mtu kuonana naye mara ya kwanza kumuulizia vitu ambavyo hata watu wenu wa karibu hawajui.

Alipomuulizia kuhusu kumtaka yeye wakati wewe ni mchumba wake, mwenzio alikukana na kusema kuwa wewe ni mpenzi wake si mke wake. Alipoulizwa kama yupo tayari kuoa mwanamke mwingine na kuachana na wewe, kutokana na kiwewe cha mapenzi alikubali kuwa yupo tayari na kuusema udhaifu wako.

“Alipoulizwa tena yupo tayari kumuoa yeye Balkis alikubali. Aliutumia udhaifu wa mchumba wako kujenga uhusiano wa haraka na kutaka kuwa naye siku ile, pia alikubali. Walikubaliana kwenda nyumbani kwa mchumba wako, ili kutowagonganisha, mchumba wako alitaka kukupigia simu ili usiende, lakini Balkis alimzuia asikupigie simu na kukueleza uende na ulipokwenda ulimuona jinsi alivyobabaika baada ya kuingia na kwenda moja kwa moja chumba cha wageni alichokuwa ameingia Balkis muda ule ule. Ulishtuka baada ya kumuona ameingia ghafla chumbani, ni kweli?”

“Ni kweli,” Suzana alijibu kwa sauti ya chini huku akiwa anaona muujiza mkubwa kutokana na maneno ya mganga ambayo mwanzo aliyaona kama simulizi ya kusisimua isiyo na ukweli. Lakini swali lile lilikuwa kama kitu kilichomtoa kwenye bumbuwazi.

“Basi kitendo cha kuingia na kwenda moja kwa moja kilimtia wasiwasi mkubwa mchumba wako kwa kujua lazima utamkuta Balkis na kumfumania. Hata lugha zenu ziligongana kitu kilichokushangaza. Kingine kilichokushangaza kilikuwa kwa mpenzi wako kuwa tofauti na siku zote kukujibu kwa ukali jambo la kawaida.

Baada ya kumuona humuelewi, ulikwenda chumba cha kulala, yeye alirudi hadi chumba cha wageni  na kushangaa kumkuta Balkis akiwa amejaa tele kitandani. Alipotaka kujua alikuwa wapi alimwambia akuwahi chumbani ili akurudishe kwenye hali ya kawaida.

Baada ya kuingia chumbani, penzi alilokupa ndilo lilikuchanganya na kusahau yaliyotokea muda mfupi. Usiku jini Balkis alikuja kukuchukua ukiwa usingizini na kukurudisha kwako na yeye kulala na mchumba wako mpaka asubuhi. Wote mlipoamka mlishtuka lakini hakuna aliyejua ukweli wa tukio la usiku ni kama ndoto au kweli.

Ulipokwenda kwake asubuhi ya jana kupata uhakika kwa kilichotokea, ndani walikuwa mchumba wako na Balkis, ndiye aliyemweleza ujio wako. Ulipofika alikuwa mule mule chumbani amelala kitandani. Wewe hukumwona ila mwenzako alimwona kama kawaida, kitu kile ndicho kilichompa kigugumizi.

Hali ile ilikuchanganya na kumuona kama mtu mwenye matatizo, wakati huo Balkis alimwambia mchumba wako kwa sauti ya juu ya kumkemea kuwa akikuuliza useme hukuja jana ili ujue kilichotokea si kweli bali ni ndoto.

Lakini kwa yeye kuwepo  pembeni ya kitanda karibu na Balkis aliyekuwa amelala pembeni yako bila wewe kumuona, ilizidi kumchanganya.

Mchumba wako alipatwa na kigugumizi kwa kujua utanamuona Balkis, kubabaika kwake kulikufanya umtilie wasiwasi na kumuuliza swali ambalo lilimchanganya pale ulipotaja jina la Balkis kama jini, jina ambalo lilikuwa la mpenzi wake, kumtaja kama jini ilimuudhi sana Balkis na kukupuliza upepo uliokufanya upoteze fahamu.

Kitendo kile mchumba wako alikiona na kumpandishia na kutaka kujua amekufanyia nini, Kauli ile ilimfanya Balkis kukasirika na kuondoa nguvu za kiume za mchumba wako na kutaka nawe kukutoa kizazi.”

“Mama yangu!” Suzana alishtuka na kushika mdomo kusikia vile.
“Usiogope, hakukutoa kizazi baada ya mchumba wako kumuomba msamaha na kuwa tayari kumuoa baada ya kumkataa kutokana na vitendo vyake visivyo vya kawaida. Baada ya Balkis kumsamehe aliamua kuondoka naye kwenda kuishi chini ya bahari.”

“Mamaaa!” Suzana alipiga mayowe ya mshtuko.
“Mungu wangu unataka kutuambia Brighton yupo ujinini?” Mama Sharifa aliuliza.
“Ndiyo, lakini kwa sasa yupo katika matatizo.”
“Matatizo! Matatizo gani tena jamani?” Suzana aliuliza kwa huzuni.

“Baada ya kufika katika mji wa majini, baba mzazi wa Balkis alishtuka kuona mwanaye amekwenda na mwanadamu akimsema ndiye mume wake badala kupeleka alichotumwa.
Hapo palitokea kutoelewana kati ya Balkis na baba yake, baba akitaka mwanaye arudi duniani kuendelea kutafuta vizazi zaidi vya wanawake ili apate dawa ya kuweza kupata ujauzito ili aolewe na jini mwenzake.

Lakini Balkis hakuwa tayari kuolewa na jini mwenzake baada ya kuonja penzi la mwanadamu. Yeye aliamini kuolewa na mwanadamu kusingekuwa na haja ya kuendelea kuwatoa uzazi wanawake. Kwani angekutana kimwili na mwanadamu angeweza kupata bila kutumia dawa hiyo.

Hapo ndipo palipozuka mvutano wa mtoto na baba, Balkis aliamini kwa vile anapendwa sana na baba yake atakubaliwa, lakini baba yake hakuwa tayari kuchanganya damu ya jini na mwanadamu. Baada ya kuona mtoto wake amemkosea adabu, alimuamuru mkuu wa Watwana anaitwa Kulani, Jini mweusi lakini mwenye nguvu. Kumchukua Balkis na mchumba wako kuwapeleka katika chumba cha giza.”

“Kwa hiyo ndiyo harudi tena?” Suzana aliuliza.
“Anaweza kurudi lakini mpaka atoke sehemu aliyofungwa.”
“Bila ya hivyo hawezi kutoka?” Sharifa aliuliza.

“Inategemea na uamuzi wa mfalme wa bahari kumtoa.”
Mambo yanazidi kuwa mazito. Je, Brighton atapona au atauawa katika mji wa majini? Mganga njiwa Manga atawasaidia?
“Anatakiwa njiwa mwekundu tu, kwenye mabanda yangu atapatikana.”
“Na mimi kumpata mchumba wangu utanisaidiaje?”
“Kama akitoka kwenye chumba cha giza tutampata, lakini kumtoa kule ni kazi ngumu, haonekani kila nikimtafuta.”

“Kwa hiyo utanisaidia vipi?”
“Kwa vile kazi ya mwenzako ni nyepesi ngoja tuifanye usiku wa leo, ya kwako itabidi nichimbe sana kuona kama kuna uwezekano wa kumtoa hata akiwa chumba cha giza.”
Walikubaliana kuifanya kazi ile usiku wa siku ile, mganga aliwaruhusu wakapate chakula na kupumzika ili kuvuta muda. 
                                                            ***
Majira ya saa sita usiku Sharifa alisimamisha gari lake pembeni kabisa na bahari maeneo ya pwani ya Bagamoyo, sehemu aliyoelekezwa na Mganga Njiwa Manga.  Hali ya hewa ilikuwa giza la wastani, kwa mbali ilionekana miale ya moto ya wavuvi wa usiku.
Baada ya kusimamisha gari hakuteremka walisubiri maelekezo ya mganga. Mganga Njiwa Manga alianza kuteremka kisha aliwaita, wote walitoka nje ya gari.

Baridi la ufukweni lilikuwa kali, kila aliyekuwepo pale lilimchonyota hadi kwenye mifupa. Mganga alitoa vifaa vya kufanyia kazi, njiwa wa kazi alikuwa  ameshikiliwa na Sharifa.

Wote walikuwa kimya wakimsikiliza mganga ambaye alikuwa akitembea kuelekea baharini, mawimbi muda ule hayakuwa makali sana yalipiga taratibu. Mganga aliingia majini usawa wa maji ya mafuti na kumwaga vitu huku akizungumza maneno kwa sauti ya juu.
“Ewe jini la bahari nakuletea zawadi hii ili bahari iwe tulivu, pia nimekuletea zawadi ya njiwa ili kuniruhusu niifanye kazi yangu bila kikwazo.”

Baada ya kusema vile aligeuka bila kutoka ndani ya maji na kumwita Sharifa.
“Kavue nguo zote kisha ujifunge upande wa kanga halafu uingie ndani ya maji na njiwa wako.” 

Sharifa alifanya kama alivyoelekezwa na mganga, aliingia ndani ya maji na kuwaacha mama yake na Suzana wakiwa wamesimama huku wakiendelea kupigwa na baridi kali ya upepo utokao baharini. Aliingia ndani ya maji ya baridi huku akiwa na hofu ya kutojua mganga anataka kumfanya nini hasa akiwa amejifunga upande wa kanga bila kitu chochote mwilini.

Alipomfikia mganga alisogea naye mbele hadi maji ya shingo njiwa wake akiwa amemnyanyua juu. Baada ya kufika kimo kile cha maji, mganga alimwambia Sharifa amuweke kichwani, naye alifanya vile. Mganga alimshika sikio la kushoto na kuanza kuomba kwa lugha ya kiganga.

Aliomba kwa kuzungumza maneno haraka haraka bila kumeza mate kwa zaidi ya nusu saa. Baada ya robo saa Sharifa alianza kusikia vitu vikikoroga tumboni, Sharifa alishindwa kufanya kitu kutokana na mikono kuwa kichwani amemshikilia njiwa.

Mganga aliendelea kuzungumza maneno ya kiganga akiwa bado amemshikilia sikio, tumbo nalo liliendelea kumkoroga huku mwili ukizidi kupungua nguvu. Mara alianza kuona kiza mbele na kuangukia ndani ya maji na njiwa wake mkononi.

Mganga aliwahi kumdaka na kujitahidi kumsimamisha lakini miguu haikuwa na nguvu, alipiga kelele kuomba msaada kwa mama Sharifa na Suzana waliokuwa nje ya maji. Nao walijikuta wakiingia kwenye maji na nguo zao bila kujijua kuwahi kutoa msaada kwa mganga.

Walipofika ndani ya maji ya shingo walimsaidia mganga kumsogeza ufukweni, walipofika ilionesha kama Sharifa amepoteza fahamu.
“Mganga mbona hivi?” Mama Sharifa aliuliza.
“Ni kawaida kuna kitu kilikuwa mwilini mwake kimetoka lakini baada ya muda atakuwa katika hali ya kawaida.”

Pamoja na Sharifa kupoteza fahamu mganga aliwaomba wambebe hadi ndani ya maji ili aendelee na tiba yake.
“Sasa baba si unamuona alivyo kwa nini tusisubiri arudiwe na fahamu kisha uendelee na tiba?” Mama Sharifa aliuliza akiwa amejawa na wasiwasi juu ya hali ya mwanaye.
“Mama unanifundisha kazi?” Mganga alimuuliza kwa sauti ya ukali.
“Samahani baba.”

“Sipendi kufundishwa kazi kama ulikuwa unajua kwa nini mlimleta kwangu?”
“Nisamehe baba yangu.”
“Basi naomba kila utakachokiona hapa ukae kimya.”
“Nimekuelewa baba yangu nisamehe sana.”
“Haya mbebeni muda unakwenda.”

Mama Sharifa na Suzana walimbeba Sharifa mpaka maji ya chini ya mafuti  mganga alimuomba Suzana akae chini ili ampakate mgonjwa. Suzana alifanya kama alivyoelezwa na mganga kisha Sharifa alilazwa chali juu ya Suzana. Mama yake alimshika sehemu ya kichwani ili kisiingie kwenye maji. Baada ya kulazwa mganga aliendelea na tiba yake kwa kuendelea kusema maneno ya kiganga kwa zaidi ya nusu saa. Huku njiwa aliyekuwa amelowana akimshikilia kwenye tumbo la Sharifa.

Baada ya muda mganga alinyamaza ghafla na kupita kimya kizito kikifuatiwa na upepo mkali. Baada ya muda upepo ulikoma. Suzana na mama Sharifa kila mmoja aliingiwa na wasiwasi kutokana na hali iliyojitokeza mle baharini. Kila moja alimuomba Mungu kimoyomoyo.

Baada ya upepo kutulia ilisikika sauti ya Sharifa ikiita.
“Mama...mama...mama.”
Mama Sharifa hakuitikia alimuangalia mganga aliyekuwa bado akitazama upepo ulipotokea na kunyanyua mkono.
TUKUTANE SIKU YAKESHOOOOOOOOOOOOOO

No comments

Powered by Blogger.